NI BIASHARA NDOGO YENYE MTAJI MDOGO FAIDA NDOGO LAKINI INAYOKUA UPESI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NI BIASHARA NDOGO YENYE MTAJI MDOGO FAIDA NDOGO LAKINI INAYOKUA UPESI

BIASHARA NDOGO YENYE MTAJI KIDOGO
Kwenye kipengele cha BIASHARA ZILIZOSAHAULIKA leo hii tutajibu pia swali la msomaji mmoja alilotuma kwa njia ya meseji ya simu akitaka ushauri katika biashara anayotarajia kuianzisha hivi karibuni. Hivi ndiyo kusema kwamba, makala hii ya leo itavaa kofia mbili, moja ni ya biashara zilizosahaulika au zisizopewa kipaumbele na ya pili ni ile ya USHAURI au Ongea na mshauri.


Kwenye swali la msomaji wetu huyu nitakayempa jina la “Anita”(Huwa hatutaji majina ya watu pasipo ridhaa yao) aliuliza kama ifuatavyo;

“Poleni na majukumu ya kila siku,Mimi naitwa ‘Anita’ naishi hapa hapa Dar, naomba ushauri wenu juu ya biashara ya kuuza uji wa ulezi maeneo ya (pia eneo hatuwezi kutaja kwani ni siri ya biashara ya muuliza swali), nategemea pia kuuza na uji wa mchele, chai na vitafunio kama mandazi, karanga na sambusa kama nitapata baraza nzuri au kandokando ya duka la mtu. Je biashara hii inaweza kulipa?”

Majibu kwa swali alilouliza Anita;
Asante sana Anita, kwanza napenda nikupongeze kwa uamuzi wako mzuri wa kutaka kuanzisha biashara bila ya kujali kwamba biashara unayoanzisha ni ndogo kiasi gani, ni watu wengi huona aibu kuomba ushauri wakidhani watachekwa kwa kuwa biashara wanayotaka kuanzisha ni ndogo, mama lishe, umachinga, genge, kuuza karanga, kuuza mihogo kwa kutembeza barabarani, kuuza kahawa, kuokota chupa na vyuma chakavu au vitu vya zamani na kwenda kuviuza nk.

Ninachotaka kukutia wewe moyo na wasomaji wengine wote wanaosoma hapa na walio katika hatua ya kuanza biashara kama wewe(startups) ni kwamba, biashara za namna hii ni aina ya biashara ambazo watu wengi wamekuwa wakizipa uzito wa chini ili hali ndiyo injini ya uchumi wa  nchi nyingi zilizokuwa katika ulimwengu wa tatu na hata baadhi ya zile zilizoendelea pia.


Ndiyo maana ukaona mimi nikiziita, biashara zilizosahaulika au biashara zisizojulikana na watu wengi bado. Ina maanisha kuwa watu bado hawajagundua fursa kubwa zilizojificha nyuma ya biashara hizo, na wale wachache waliogundua basi wanatamani wala wengine wasije wakagutuka kusudi waendelee kupiga hela kama watoto wa mjini walivyozoea kusema.

Kwanini isilipe Anita? Kwanza nataka nikuibie siri moja ambayo mimi binafsi nimeigundua hivi majuzi tu nilipokuwa ziarani maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na vitongoji vyake nikisaka fursa mbalimbali kwa ajili ya kuwajuza wasomaji wangu katika blogu hii na mitandao mingine ya kijamii ninayoandikia. Nasema nakuibia kwani siri hii mamlaka nyingi za miji na majiji hapa Tanzania na nadhani hata Mkuu wa nchi mwenyewe asingependelea sana watu wengi waigundue fursa hiyo, inaweza kuleta balaa.

Lakini kwa kuwa naamini blogu hii wasomaji wake wengi ni wajasiriamali wadogo wanaotafuta mbinu zozote zile halali ili waweze kutoka kimaisha hasa kupata mitaji ya uhakika ya kuendeshea biashara kubwa, nitaisema fursa hiyo adimu. Mpaka mamlaka zije kushtuka, kama wewe ni mjasiriamali makini nadhani utakuwa umeshapiga hatua nyingine mbele, pengine umeshaandaa mazingira mazuri zaidi kibiashara.

Nadhani utakubaliana na mimi kabisa kwamba wakati wa kuanzisha biashara mpya hakuna kitu kigumu kama changamoto ya kupata mtaji. Umeshafanya utafiti wako wa kutosha, umeshaandaa mpango wako wa biashara au mchanganuo wa biashara, vyovyote vile utakavyouita na mpango huo umeshauandika mahali au umeamua tu kuuhifadhi kichwani, hamna tatizo kwani utafanya kazi tu kama kawaida.

Sasa ugumu unakwenda kuonekana kwenye, ni wapi utakakokwenda kupata mtaji au msingi wa kuendeshea biashara yako hiyo mpya. Unaweza ukawa mfukoni pengine unazo pesa kidogo lakini mara nyingi watu hukuta haziwezi kutosha mahitaji yote ya biashara iweze kuanza na kupaa vizuri.


Hii ndiyo sababu kubwa sana inayowafanya wajasiriamali wengi wadogo kukimbilia kuanzisha biashara ndogo ndogo kama zile nilizozitaja pale juu kutokana na urahisi wake wa kuzianzisha kimtajii. Mara nyingi biashara hizo mtu hahitaji kulipa pango wala kununua mali za fedha nyingi sana.

Ni Biashara ndogo zenye mitaji midogo, Faida kidogo, lakini zilizokuwa na uwezo wa kukua haraka sana na hatimaye kumfanya mtu aweze kupata mtaji mkubwa wa uhakika wa kufungua biashara ya maana.

Sasa nilikuahidi kukupa siri au fursa niliyomdokezea Anita, fursa ambayo mamlaka nyingi hapa Tanzania zisingependa kabisa watu wengi waishitukie kwani wanaamini inaweza ikaleta usumbufu mkubwa katika mipango yao ya miji na majiji.

Kama utakumbuka kipindi cha nyuma kidogo katika miji mingi nchini hususani katika jiji la Dar es salaam, wafanyabiashara wadogo wengi wakiwemo wamachinga, mama na baba lishe(mama ntilie na baba ntilie) na hata wauza vitu mbalimbali kama nguo nk. waliofanyia shughuli hizo katika maeneo yasiyokuwa rasmi, walisumbuliwa sana ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa na mgambo wa jiji/manispaa mali na bidhaa zao.


Binafsi namkumbuka mgambo mmoja wa jiji aliyekuwa jirani yangu eneo fulani, aliishi maisha ya ‘kula bata’ kiasi ambacho usingeweza hata kidogo kuamini kama alikuwa akifanya kazi ile. Nyumbani mwake mkewe alifungua kiduka cha kuuza nguo na vifaa mbalimbali mumewe alivyoleta kila siku jioni baada ya kutoka kazini, vitu ambavyo inasadikiwa alinyang’anya kutoka kwa wafanyabiashara waliouzia maeneo wasiyostahili.

Hivi karibuni kama wewe ni mdadisi wa mambo utagundua kuwa hali hiyo imebadilika. Nadhani ni kutokana na kubadilika pia kwa sera za Serikali au viongozi waliopo madarakani, au inaweza ikawa ni sababu nyingine yeyote ile, mimi sijui na wala sina ‘interest’ kubwa sana na maswala ya kisiasa bali ninachotaka tu kuonyesha hapa ni kwamba, kwa muda sasa wafanyabiashara wadogo hasahasa wamachinga na wale wasiokuwa rasmi mijini na katika majiji mbalimbali wana FURSA kubwa tofauti na siku zilizopita.

Kuna madai kwamba wakuu wa nchi wametoa maagizo wasibugudhiwe mpaka pale watakapotafutiwa maeneo muafaka. Sina uhakika na hilo lakini vyovyote vile iwavyo hiyo ni FURSA kubwa kwa mtu yeyote anayehangaika na mtaji mdogo.

Kwa mjasiriamali, hahitaji muda mwingi sana kufanya mabadiliko, hata ikiwa fursa hiyo ni ya muda mfupi kiasi gani, kama mjasiriamali nafikiri muda huo unatosha kabisa kutengeneza mtaji kwa ajili ya shughuli yake ya uhakika hapo baadae, biashara yenye mtaji wa kutosha tofauti na sasa.

Wamachinga hawataruhusiwa kufanya biashara maeneo ya wazi milele, lakini kwa muda wa mpito uliopo nimemshauri Anita kuitumia fursa hiyo kikamilifu kuuza chochote kile halali anachofikiria kitamlipa katika eneo alilochagua kutokana na unafuu wa kuanza biashara ndogo uliokuwepo sasa. Si kama nahamasisha watu kufanya biashara holela, la hasha bali ninachosisitiza hapa ni fursa ya muda wa mpito iliyokuwepo.


Na isitoshe kama kweli mpango unaosemwa wa kuwaandalia wamachinga na wafanyabiashara zisizokuwa rasmi maeneo maalumu upo, bado itakuwa ni faida kwani utakuwa pengine umekwishaorodheshwa miongoni mwa wamachinga wengine watakaokwenda kupangiwa maeneo rasmi. “Kwa hiyo Anita ninachokushauri, wewe anza kidogo halafu polepole uangalie ni kitu gani wateja wako watakachokuwa wanapendelea zaidi. Kama ni uji wa ulezi, uji wa ngano, mchele, vyovyote vile. Unaweza hata ukauza chai, maziwa au hata tangawizi ya kuchemsha, ni uamuzi wako.

Kuhusiana na eneo, usisubiri mpaka upate barazani mwa duka la mtu, hata ukiamua kuanza na chupa yako ya chai mkononi na kikapu cha vitafunwa huku ukitafuta kituo cha kudumu ni sawa, cha msingi pata wateja kwanza na masuala mengine yatajiseti yenyewe baadae.”

KILA LA KHERI ANITA!  
…………………………………………………………………....

My Dear Reader, you can MAKE YOUR SELF GREAT AGAIN, reinventing your life once again no matter how bad situation you are now experiencing with. Do you remember how strong were you? How rich, how healthy, how spiritual…how ‘good times’ you were enjoying at that time?

Make a decision today, transform your life starting with your BUSINESS. Yes it’s true that money is not a prerequisite of joy but it can simplify many things that makes our life more joyful. Transformation starts with your brain through learning new ways of doing things. So to start transforming your business, read these self help books.

 22,000/= Hardcopy
10,000/= Softcopy

 16,000/= Hardcopy
 6,000/= Softcopy




 5,000/= Hardcopy
3,000/= Softcopy


Kupata vitabu vilivyoorodheshwa hapo juu softcopy mawasiliano ni; 0712202244  au  0765553030
 



  

1 Response to "NI BIASHARA NDOGO YENYE MTAJI MDOGO FAIDA NDOGO LAKINI INAYOKUA UPESI"

  1. My name is EMMANUEL, ningependa kununua on-line kitabu cha "MICHANGANUO ya UJASIRIAMALI na BIASHARA" lakini naomba nijiridhishe na contents zake kwa kujua TOPICS zilizomo ndani.

    immaswai@hotmail.com

    ReplyDelete