BIASHARA NDOGONDOGO ZENYE FAIDA YA HARAKA TANZANIA NI HIZI HAPA, ZIPO NNE(4) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA NDOGONDOGO ZENYE FAIDA YA HARAKA TANZANIA NI HIZI HAPA, ZIPO NNE(4)

Biashara ndogondogo yenye faida ya haraka
Katika  blogu hii niliwahi kuandika kuhusiana na hii biashara yenye faida kubwa na ya haraka mara 2 ya mtaji utakaowekeza. Tuliweza kuona kwa ujumla wake biashara hizo ni za namna gani na hata tukazitaja baadhi ya biashara hizo. Lakini tofauti na makala hiyo leo hii katika kipengele cha BIASHARA NDOGONDOGO ZILIZOSAHAULIKA tutaweza kuona aina za biashara nyingine tena ambazo kwa hapa kwetu Tanzania, japo ni biashara ndogondogo lakini zina uwezo mkubwa wa kumuingizia mjasiriamali faida haraka.

Ndugu msomaji wangu najua leo hii inawezekana kabisa nikawakwaza baadhi ya wasomaji na wapenzi wa mtandao huu, lakini natanguliza kuomba radhi, sijakusudia kuvunja maadili bali kuelezea hali halisi kwani pia wasomaji hapa ni watu wa aina mbalimbali na waliokuwa na imani tofauti tofauti. Kimsingi sishabikii vileo wala biashara yeyote ile haramu kwa baadhi ya makundi ya watu.

Unapotaja biashara zilizokuwa na faida kubwa na ya haraka haraka, huwezi ukaziacha biashara zifuatazo;

1. Biashara ya vifaa vya ujenzi, hardware.
Mpenzi msomaji, hakuna ubishi wowote ule kwamba, kila binadamu anayezaliwa baada ya kuwa na akili timamu kitu cha kwanza kufikiria akilini kama ni mvulana ni, “Nikiwa mkubwa nitajenga nyumba yangu nzuri ya kuishi mimi, mke wangu na watoto”. Hapo pengine hata hajaanza darasa la kwanza. Kwa upande wa watoto wa kike nao, huanza kuwaza akilini kuja kuwa na maisha bora ya familia ndani ya mjengo mzuri. Hii ni kumaanisha kwamba kwa asili binadamu wote ni wapenzi wa kumiliki nyumba nzuri au majengo yanayopendeza.


Cha ajabu hapa ni kwamba kila mtu anapenda jengo alimiliki yeye mwenyewe ndiyo maana utakuta mtu hata ikiwa wazazi wake wana mali nyingi, ni matajiri lakini bado atatamani kujenga nyumba yake nzuri kwa pesa zake mwenyewe.


Maajabu mengine ni kwamba majengo yote hata yale ya serikali, madaraja, nyumba za ibada, Makanisa na Msikiti, reli, barabara na hata viwanja vya michezo kama soka, baada ya miaka kadhaa huhitaji matengenezo makubwa au kubomolewa na kujengwa tena upya kisasa jambo linalosababisha vifaa vya kujengea kuendelea kuhitajika kila mara miaka yote.

Nyumba aliyojenga babu enzi hizo kwa gharama kubwa leo hii mjukuu utatamani kuibomoa na kujenga jumba la kisasa zaidi. Reli aliyojenga Mjerumani leo hii Mheshimiwa Rais Magu anaweza kuamua ibomolewe na kujengwa upya, Barabara ya Morogoro aliyojenga Hayati Mwalimu Nyerere unaweza kuona leo hii kuna watu wanaobomolewa nyumba zao kupisha ujenzi upya wa barabara hiyo.

Kwa kifupi tu nataka kuonyesha jinsi ambavyo suala la ujenzi na vifaa vya ujenzi lilivyokuwa nyeti na endelevu na ambalo huwezi hata siku moja ukadai eti itapitwa na wakati. Watu watapita lakini ujenzi utakuwa palepale miaka yoye pengine mpaka mwisho wa dunia. Toka kujengwa Mapiramidi ya Misri na Mafarao kule Misri ya Kale, Mfereji wa Suez, Kuta kuu za China na Berlin na sasa Jengo refu kupita yote duniani kule Dubay, ujenzi haujakoma, ndiyo kwanza unashika kasi duniani kote.

Kwanini nimeitia biashara ya vifaa vya ujenzi kwenye kundi la biashara ndogondogo?
Kimsingi kabisa ungetegemea makala hii kukutana na biashara zile ndogondogo kabisa lakini bila shaka unaweza kushangaa kwanini nimeamua kuiweka biashara ya vifaa vya ujenzi. Vifaa vya ujenzi mtu anao uwezo wa kuanza na kiasi chochote kile cha mtaji na wakati mwingine bila ya mtaji kabisa. Kivipi?


Kuna jamaa mmoja namfahamu yeye alianza biashara hii kama dalali, akaweka sampuli za baadhi ya vifaa hivyo kama vile tofali, baluster, nguzo za fence, paving blocks nk. katika ukuta wa nyumba yake iliyokuwa kandokando ya barabara ya Morogoro maeneo fulani pale Kimara, akaweka na mawasiliano yake ya simu pale. Wateja walipompigia simu wakihitaji vifaa vile, aliwapa bei na kwenda kuwachukulia kutoka kwa watengenezaji wengine waliokuwa na site zao.

Unaweza pia kuanzisha uuzajiwa vifaa vya ujenzi vilivyokwisha tumika au “used”. Unanunua kwa bei ya chini kutoka kwa watu wanaobomoa majumba yao na kwenda kuuza kwa beiya juu kidogo lakini isiyofika sawa na ya vifaa vipya. Vitu hivyo used vyaweza kuwa nondo, mabati, mabomba, misumari, mbao, tofali, nk. Vile vile unaweza kuanza na kitu kimoja tu, mfano kuuza sementi, ukaanza hata na mfuko mmoja kwa kupima kwa kilo kisha kidogokidogo ukaweka vitu vingine. Mchanga na kokoto unaweza pia ukanunua kiasi kidogokidogo na kuuza kwa kupima na ndoo au viroba. Kwa Tanzania inasemekana bado ujenzi umefikia asilimia ndogo sana mpaka sasa hivi.

Biashara ya vileo(pombe), bia, viroba, wine, spirit, sigara na tumbaku.
Hapo ndipo naomba radhi kwa wale ambao imani au maadili yao hayawaruhusu kutumia wala kuuza. Kwa kweli nimetaja tu pombe aina ya viroba nikimaanisha spirit au wine iliyokuwa ikifungashwa katika paketi za nailoni lakini kila mtu anafahamu kuwa kwa sasa paketi hizo hazipo tena baada ya serikali kuzipiga marufuku.

Vitu hivi vinapouzwa licha ya kuwa na wateja wengi faida yake pia ni kubwa sana ukilinganisha pengine na bidhaa za aina nyingine kama soda au maji. Watu wengi wanaofungua biashara hizi mitaji yao hukua haraka huku wakifungua matawi ya biashara hizo. Unaweza kupata ushahidi wa kile ninachokizungumza kama siku chache zilizopita kabla viroba havijapigwa marufuku ulikuwa ukitembea maeneo mbalimbali ya stendi na kujionea jinsi wenye vioski na meza za kuuza bidhaa ndogondogo walivyokuwa wakiuza pombe hizo.


Sigara nazo, halikadhalika ni biashara ambayo japo faida yake ni ndogondogo, lakini kutokana na wingi wa wavutaji na uvutaji wao wa mara kwa mara katika siku moja, utakuta muuzaji wa sigara akiuza paketi nyingi na kutengeneza faida kubwa kwa siku. Kuna wanaouza pia Tumbaku yenyewe iliyosagwa au ugoro, tumbaku zinazoletwa kutoka Asia nk.ijapokuwa nazo nyingi zimekwishapigwa marufuku hapa Tanzania baada ya kuonekana ni baa kubwa kwa vijana wa Kitanzania hasa wanafunzi walioanza kuzitumia kwa wingi, jambo ambalo lingeweza kuwasababishia maradhi mbalimbali ikiwemo kansa ya koo, mapafu na nyinginezo.

3. Biashara zote ndogo ndogo za vitu vya kula na kunywa.
Tunapozungumzia biashara hizi, si suala tu la kuuza biashara ndogondogo za vitu vya kula na vinywaji, bali pia ili kuweza kupata faida ya haraka na kubwa, basi ubunifu unahitajika. Kwa kuwa biashara hizi ni rahisi kuanzisha na kila mtu anao uwezo wa kuanzisha, wale wanaoweza kuiona faida kubwa ya haraka ni wale tu wanaofanya ubunifu na kuwa wavumilivu.

Nimefurahishwa na jamaa fulani pale Mbezi, wao wameanzisha biashara  ya kuuza juisi ya miwa lakini staili yao ilinivutia. Wanatumia pikipiki iliyofanyiwa ‘modification’, ijnini yake hiyohiyo huzungusha kinu cha kukamulia miwa wakati ikiwa imesimama stendi na wateja huja kunuua juisi.


Kiduka hicho cha aina yake kimejengewa juu ya hiyo pikipiki, huku pakiwa na sehemu ya kuwekea vitafunwa mbalimbali, vyombo na sehemu ya kukaa dereva na muuzaji wakati wanapofunga biashara kurudi nyumbani. Ni kama vile kiwanda kidogo kinachotembea. Wana uwezo wa kwenda eneo au stendi yeyote ile hasa hasa nyakati za jioni palipo na wateja wengi.

4. Biashara zote ndogo ndogo za utoaji wa huduma.
Tofauti ya hizi na zile nilizozitaja katika makala nyingine ya biashara zilizokuwa na faida kubwa na ya haraka mara mbili ya faida utakayowekeza ni kwamba, hizi zipo katika kundi la biashara ndogondogo tu wakati hizo nyingine zinajumuisha biashara zote kwa ujumla.

Biashara ndogo za utoaji wa huduma ni kama vile, ususi wa nywele majumbani kwa wakina mama na kina dada, Uzibuaji wa mitaro ya maji machafu, usafi wa majumbani(fumigation), biashara za kwenye mitandao(blogging) kama hii ninayofanya, Kufundisha masomo ya ziada kwa wanafunzi wa shule za msingi au sekondari, kufundisha semina mbalimbali kama ujasiriamali, muziki, nk. kwa watu au makundi ya watu walio na mapenzi na kile unachofundisha.

Ndugu msomaji, kwa leo makala hii imeishia hapa, siku zijazo nitaendelea kukuletea makala zaidi juu ya uanzishaji na uendelezaji wa biashara ndogondogo zilizosahaulika au biashara ambazo watu wengi wanazichukulia poa(kuzipauzito mdogo)

Kama ulikuwa hujasoma kitabu hiki tulichokupa bure kabisa usome, basi JIUNGE NA BLOGU HII HAPA KUKIPAKUA au bonyeza picha ya jalada unayoiona hapo chini. 

kitabu cha bure (free book)

Ni free hutachajiwa senti tano! Pamoja na vitabu vingine zaidi ya 20 katika lugha ya kiingereza.

Kwa vitabu zaidi vya Biashara na Ujasiriamali katika lughaya kiswahili fungua, SMART BOOKS TANZANIA.



10 Responses to "BIASHARA NDOGONDOGO ZENYE FAIDA YA HARAKA TANZANIA NI HIZI HAPA, ZIPO NNE(4)"