Biashara ndogondogo nyingi huku mitaani huendeshwa
kwa mazoea kiasi kwamba kuna wakati mteja unalazimika kujiuliza ikiwa mjasiriamali
huyu mdogo anafahamu kweli jinsi ya kutoa huduma bora kwa mteja(good customer
care) au anachotoa yeye ni customer kero kwa mteja.
Kama kawaida yangu ninapopita mitaani nikiwa
kwenye shughuli zangu za kawaida siachi pia kuchunguza mienendo ya biashara
nyingi ndogondogo kwa faida ya wasomaji wangu katika blogu hii ya
JIFUNZEUJASIRIAMALI, na safari hii nilikuwa maeneo fulani ya Mbezi mwisho baada
ya kushuka kwenye mwendokasi nikawa nawaza nikanunue kapaja ka kuku mahali
fulani walipoweka kibanda cha kukaangia nyama za kuku, mapaja, vidari,
firigisi, shingo za kuku, na hata miguu na vichwa vya kuku.
Nilikuta hamna paja nikaamua kumwambia mchoma
kuku yule anipe tu kidari cha kuku lakini anikaushie vizuri, atie chumvi,
pilipili na mazagazaga yote yaliyokuwepo pale nibebe nikalie nyumbani. Lakini
kwa mshangao yule muuzaji nyama za kuku alinijibu “Aisee nyama zimeshakaushwa
tayari, unachukua tu hamna haja tena ya kutia kwenye mafuta ya moto”
Nilipozitazama zile nyama, naona kabisa zimepoa na pengine huenda hata hazikuwa
zimewiva sawasawa.
Tulibishana kidogo huku akionekana mtu mwenye
haraka sana manake ilikuwa jioni na alikuwa akikazani kuandaa nyama mbichi
ambazo hazikuwa zimetiwa kwenye mafuta ya moto bado. Baada ya kumlazimisha,
akaiweka ile nyama kwenye mafuta kwa shingo upande huku akinung’unikanung’unika.
Ile kufumba na kufumbua tu alikitoa kile kidari kwenye mafuta na kudai tayari
kimewiva akaanza kukifungia harakaharaka, na mimi sikuona tena sababu ya
kuendelea kubishana naye, akaweka kila kitu nikaondoka zangu.
Kufika nyumbani, nyama ikawekwa mezani, nyama
kwa juu ina moto kidogo lakini ndani nyama ilikuwa baridi utadhani imetoka
kwenye friji muda uleule. Nikagundua pia kwamba nyama zile wala hazikuwa za
siku ileile bali zilikuwa za jana yake na yule muuzaji alichofanya ni kuzitoa
kwenye friji na kuziweka pale mezani. Sasa nikajiuliza alivyokuwa akiniambia
zimeshakuwa tayari alikuwa akimaanisha nikifika nyumbani nikaitie tena kwenye
mafuta ya moto? au basi yeye lengo lake
ni kuuza tu nyama, mteja utajijua mwenyewe mbele ya safari?
Lakini niliendelea kujiuliza maswali ikiwa
muuzaji yule kweli yupo ‘serious’ na biashara anayofanya kwani kwa mfano mimi
binafsi sidhani kama itatokea tena siku nyingine nikanyage pale kwake kununua
nyama ya kuku. Alinifanya hata nianze kutilia mashaka wauzaji wengine wote wa
nyama za kuku wanaoweka vibanda na meza zao maeneo ya stendi au kandokando ya
barabara. Kwa kweli ni kama aliniharibia jioni yangu ile yote niliyopanga
kwenda kutafuna kidari cha kuku kilichotiwa pilipili na limao.
Kijana akichoma kuku barabarani tayari kwa kuuza kwa wateja. |
Mfanyabiashara katika kutoa huduma nzuri kwa
wateja wako hakikisha kwanza unafahamu kwa uhakika mteja ni nani na maana ya
huduma bora kwa mteja ni nini. Mteja unatakiwa umchukulie kama mtoto mdogo
anayejifunza, hupaswi kujifanya wewe unajua zaidi yake hata ikiwa unaona kabisa
yeye anachosema ni pumba, wewe jifanye mjinga huku ukifahamu unachohitaji
kutoka kwake ni kitu gani. Kwa mteja wewe hauhitaji kingine zaidi ya pesa yake na
yeye hahitaji kitu kingine zaidi ya huduma nzuri itakayotatua shida yake
iliyomleta pale kwako, kwa hiyo jitahidi sana kuhakikisha unafahamu kikamilifu
ni kitu gani au shida gani iliyomleta mteja kwako na uhakikishe pia unampa
huduma kupita matarajio yake.
Kama yeye alijua atapata paja la kuku kwako
likiwa la moto basi na wewe muongezee hapo vikorombwezo vingine kibao, mfungie
kwa foil safi, mwekee kalimao kidogo, kachumbari kama anapenda, pilipili,
viungo vya kunukia na hata mayonnaise kama ipo, vitu ambavyo wala hakufikiria
kabisa kuvipata kutoka kwako.
Na vikorombwezo vingine hivyo wala hata
havina gharama kubwa sana, lakini hapo unakuwa umeshajihakikishia mteja wa
kudumu, maana yake mteja huyo atakuwa akijisemea, “kesho itafika lini
nikikitoka kazini nipite tena pale kwa yule Mpemba nikajichukulie hapo firigisi
na kidari” ‘Umeshamloga’ tayari badala ya
wewe kwenda kuhangaika kwa Masangoma matapeli watakaofilisi mpaka na kamtaji
kenyewe ulikokapata kwa shida.
………………………………………………………………………..
Mpenzi
msomaji na mfuatiliaji wa makala hizi juu ya biashara ndogondogo zinazolipa,
usikose kila siku kujifunza kitu kipya ndani ya blogu yako hii na pia ikiwa
utataka kujifunza mambo mengine makubwa na mengi zaidi, basi usiache kujipatia
vitabu vyako bora kutoka SELF HELP BOOKS TANZANIA chini ya SMART BOOKS TZ.
Vitabu hivi kuna vya bure na vya malipo pia unaweza kuvipata katika mifumo yote
ya SOFTCOPY kwa njia ya email au HARDCOPY ofisini kwetu au kuletewa ulipo.
Namba zetu za simu ni;
0712202244 au
0765553030
Jina
linalotokea ni;
Peter
Augustino Tarimo
Tupo Mbezi Kwa Msuguri jirani na Stendi au Bochi Hospital
SOFTCOPY SH. 10,000/=
HARDCOPY SH. 20,000/=
SOFTCOPY SH. 5,000/=
HARDCOPY SH. 10,000/=
SOFTCOPY SH. 3,000/=
HARDCOPY SH. 5,000/=
0 Response to "HUDUMA BORA KWA WATEJA KWELI HII, CUSTOMER CARE AU CUSTOMER KERO?"
Post a Comment