SURA YA 7
MIPANGO MADHUBUTI
Kubadilisha
Shauku kuwa Vitendo
(Hatua ya sita Kuelekea Utajiri)
Umeshajifunza kuwa kila kitu kinachoumbwa au
kumilikiwa huanza katika mfumo wa shauku. Shauku hiyo huchukua safari yake ya
mwanzo pasipo kuwa na kitu chochote mpaka kwenye kitu kinachoweza kushikika
katika karakana ya Ubunifu mahali
ambapo mipango kwa ajili ya mabadiliko yake hutengenezwa na kupangiliwa.
Katika sura ya 2 ulielekezwa kuchukua hatua
kamili sita za kivitendo kama hatua ya kwanza katika kutafsiri shauku kuwa
pesa. Moja ya hatua hizo ni kutengeneza mipango kamili ya kivitendo ambayo
kupitia hiyo, mageuzi haya yanaweza kufanyika.
Sasa utaelekezwa juu ya namna ya kutengeneza
mipango ya kivitendo.
(1)
Shirikiana wewe mwenyewe na kundi la watu wengi kwa kadiri
utakavyohitaji kwa ajili ya kutengeneza na kutekeleza mpango wako au mipango
yako ya kujichumia fedha, ukitumia kanuni
ya “Ushirika
wa kushauriana maendeleo”(Mastermind Group)
iliyoelezwa katika Sura ya 9. (Kukubaliana na
maelekezo haya ni muhimu kabisa. Usije ukayapuuza.)
(2)
Kabla hujaunda “Ushirika wako wa kushauriana” amua ni faida zipi na
manufaa unayoweza kuyatoa kwa wanachama mmojammoja wa kundi lako kama malipo
kwa ushirikiano wao. Hakuna mtu atakayefanya kazi milele pasipokuwa na aina
fulani ya malipo. Wala hakuna mtu mwenye akili atakayemuomba ama kumtegemea
mwingine afanye kazi pasipokuwa na malipo yanayofaa, ingawaje siyo kila mara
malipo hayo yanaweza yakawa katika mfumo wa pesa.
(3)
Panga kukutana na wanachama wa Kundi lako la kushauriana angalao mara
mbili kila juma, na mara nyingi zaidi kama itawezekana mpaka wote kwa pamoja
mmekamilisha mpango au mipango kwa ajili ya kujichumia fedha.
(4)
Dumisha masikilizano kamili
kati yako mwenyewe na kila mwanachama wa “Kundi lako la kushauriana”. Ikiwa
utashindwa kutekeleza sharti hili kwa umakini unaweza ukakutana na kikwazo.
Kanuni ya “Ushirika wa Kushauriana” haiwezi kufanya kazi mahali pasipokuwa na
masikilizano kamili.
Zingatia ukweli ufuatao;
(a)
Unajiingiza katika jukumu lenye umuhimu
mkubwa kwako. Kuwa na uhakika wa mafanikio, ni lazima uwe na mipango isiyokuwa
na makosa.
(b)
Ni lazima uwe na faida ya uzoefu, elimu,
uwezo wa asili na ubunifu wa akili za watu wengine. Hili linakubaliana na njia
zilizofuatwa na kila mtu aliyewahi kujikusanyia utajiri mkubwa.
Hakuna mtu mwenye uzoefu wa kutosha, elimu,
uwezo wa asili na ujuzi kuhakikisha anajikusanyia utajiri mkubwa pasipokuwa na
ushirikiano wa watu wengine. Kila mpango unaotumia katika shughuli zako za
kujipatia utajiri unatakiwa uwe wa pamoja, wewe mwenyewe na kila mwanachama
mwingine wa Kundi Lako la Kushauriana. Unaweza ukaanzisha mipango yako
mwenyewe, aidha mipango mizima au sehemu yake, lakini ona kwamba mipango hiyo inaangaliwa na kupitishwa na wanachama wa
‘Kundi lako La Kushauriana.’
Ikiwa mpango wa kwanza utakaotumia hautafanya
kazi kwa mafanikio, ubadilishe na mpango mwingine mpya. Ikiwa mpango huo mpya
utashindwa kufanya kazi, ubadilishe badala yake weka mwingine tena, hivyo hivyo
mpaka unapata mpango utakaofanya kazi. Mahali hapa hasa ndipo kituo ambapo watu wengi
hukutana na maanguko kutokana na kukosa kwao msimamo katika kuunda mipango
mipya kuchukua mahali pa ile ambayo imeshindwa.
Mtu mwenye akili zaidi anayeishi hawezi akafanikiwa kupata
utajiri wala katika shughuli nyingine yeyote – pasipo mipango inayotekelezeka
na inayofanya kazi. Weka ukweli huu akilini
na kumbuka wakati mipango yako inapoanguka, kuanguka huko kwa muda siyo
anguko la kudumu. Inaweza tu ikamaanisha kwamba mipango yako haikuwa mizuri.
Tengeneza mipango mingine. Anza tena upya.
Thomas A. Edison “alifeli” mara 10,000 kabla hajakamilisha
kikamilifu kuunda balbu ya umeme. Ina
maana kwamba alikutana na vikwazo vya muda mfupi mara 10,000 kabla juhudi zake
hazijazaa matunda.
Anguko la muda linatakiwa limaanishe kitu
kimoja tu, - ujuzi fulani kwamba kuna kitu fulani kisichokuwa sahihi kuhusiana
na mipango yako. Mamilioni ya watu hupitia maisha ya mateso na umasikini
kwasababu ya kukosa mipango imara ya kuwawezesha kujipatia utajiri.
Henry Ford alipata utajiri, siyo kwa sababu
ya kuwa na akili ya kipekee, lakini ni kwa sababu alikubali na kufuata Mpango
uliothibitika kuwa timamu. Maelfu ya watu waliweza kupewa elimu bora
kuliko ile ya Ford lakini bado wameishia katika umasikini kwa sababu hawana
mpango sahihi kwa ajili ya kujipatia
utajiri.
James J. Hill alikutana na kikwazo cha muda
mwanzoni wakati alipoanzisha shughuli ya kukusanya mtaji uliohitajika kujenga
barabara ya treni kutoka Mashariki kwenda Magharibi, lakini aligeuza kikwazo
kuwa ushindi kupitia mipango mipya.
Henry Ford alikutana na anguko la muda siyo
tu mwanzoni mwa biashara zake, lakini hata baada ya kuwa alikuwa amekwenda
mbali kufika kileleni. Alitengeneza mipango mipya na kusonga mbele kwenye
ushindi kifedha.
Tumewaona watu waliojikusanyia utajiri
mkubwa, lakini tunatambua tu ushindi wao, hatutazami vikwazo vya muda
walivyopaswa kuvishinda kabla “hawajafika.”
HAKUNA MFUASI WA FILOSOFIA HII ANAYEWEZA KWA
MAKUSUDI KUTEGEMEA KUPATA UTAJIRI PASIPO KUKUTANA NA ANGUKO LA MUDA MFUPI.
Anguko linapokuja, likubali kama ishara
kwamba mipango yako siyo mizuri, tengeneza tena upya mipango hiyo na anza
safari kwa mara nyingine tena kuelekea lengo lako ulilotamani. Kama utakata
tamaa kabla lengo lako halijafikiwa, wewe ni “muachaji”
MUACHAJI KAMWE HAWEZI KUSHINDA - NA MSHINDI
KAMWE HAACHI
Ichukue sentensi hii, iandike juu ya kipande
cha karatasi kwa herufi zenye urefu wa nchi moja kwenda juu, na uiweke mahali
ambapo utaiona kila usiku kabla hujakwenda kulala,na kila asubuhi kabla
hujakwenda kazini.
Wakati unapoanza kuchagua wanachama wa Kundi
lako la Ushirika wa Kushauriana,(Master
Mind group) jitahidi kuchagua wale wasiojali sana kuanguka. Baadhi ya watu
huamini kwa ujinga kwamba pesa pekee inaweza kutengeneza pesa. Hii siyo kweli! Shauku iliyobadilishwa kuwa katika
kipimo chake cha fedha kupitia kanuni zilizotajwa hapa ndiyo wakala ambaye
kupitia yeye fedha ‘hutengenezwa’. Fedha, yenyewe siyo kitu bali nguvu
iliyolala. Haiwezi kusogea, kufikiri, au kuongea, lakini inaweza “ikasikia”
wakati mtu anayeihitaji anapoiita
ije!
Kupanga
Mauzo ya Huduma
Sehemu iliyobakia ya Sura hii imepewa maelezo
ya njia na namna ya kutafuta soko la huduma. Taarifa iliyotolewa hapa itakuwa
ni ya msaada wa kivitendo kwa mtu yeyote aliye na aina yeyote ya huduma za
kutafutia soko, lakini litakuwa jambo la faida isiyopimika kwa wale wanaotamani
kuwa viongozi katika shughuli zao walizochagua.
Kupanga kwa weledi ni muhimu kwa mafanikio
katika shughuli yeyote iliyobuniwa kuleta utajiri. Hapa yatapatikana maelezo ya
kina kwa wale ambao ni lazima waanze kutafuta utajiri kwa kuuza huduma zao.
Inatia moyo kufahamu kwamba karibu utajiri
wote mkubwa ulianza katika hali ya kubadilishana na huduma, au kutokana na
mauzo ya mawazo. Ni kipi kingine
isipokuwa mawazo na huduma ambacho mtu angepaswa kutoa kubadilishana na
utajiri?
Kusema ukweli, kuna aina mbili za watu
duniani, Viongozi na Wafuasi. Amua mwanzoni kabisa ikiwa
unapanga kuwa kiongozi katika taaluma yako uliyochagua au kubakia kuwa mfuasi.
Tofauti katika malipo ni kubwa. Mfuasi hawezi kwa makusudi kutegemea malipo
ambayo kiongozi anastahili, ingawa wafuasi wengi hufanya kosa la kutegemea
malipo ya namna hiyo.
Siyo aibu kuwa mfuasi. Kwa upande mwingine, siyo
sifa kubakia kuwa mfuasi. Viongozi wengi wakubwa walianzia katika kiwango cha
wafuasi. Walikuwa viongozi wakubwa kwa sababu walikuwa wafuasi werevu. Isipokuwa mifano michache, watu
wasioweza kumfuata kiogozi kwa werevu hawawezi kuwa viongozi wenye ufanisi.
Watu wanaoweza kumfuata kiongozi kwa ufanisi zaidi mara nyingi ni wale
wanaoibuka kuwa katika uongozi haraka zaidi. Mfuasi mwerevu anazo faida nyingi,
miongoni mwazo ni fursa ya kupata maarifa kutoka kwa kiongozi.
Sifa
Kubwa Za Uongozi
Zifuatazo ni sifa muhimu za uongozi:
1. UJASIRI
USIOYUMBA uliojengeka juu ya msingi wa maarifa binafsi na kujitambua
binafsi na shughuli aifanyayo. Hakuna
mfuasi anayependa kutawaliwa na kiongozi asiyejiamini wala kuwa na ujasiri.
Hakuna mfuasi mwerevu atakayetawaliwa na kiongozi wa namna hiyo kwa muda mrefu.
2. KUJIZUIA
BINAFSI: Watu wasioweza kujidhibiti binafsi kamwe hawawezi kuwaongoza wenzao.
Kujizuia binafsi hutoa mfano wenye nguvu kwa wafuasi wa kiongozi ambao kwa wale
waliokuwa werevu hujifunza.
3. MTAZAMO
THABITI WA HAKI: Bila hali ya usawa na haki hakuna kiongozi anayeweza kuamrisha
na kuendelea kutunza heshima ya wafuasi wake.
4. UKAMILIFU
WA MAAMUZI: Watu wanaoyumba kwenye maamuzi huonyesha kwamba hawajiamini
wenyewe.
5. UKAMILIFU
WA MIPANGO: Kiongozi mwenye mafanikio ni lazima apange kazi, na kufanyia kazi
mpango. Kiongozi anayejiendesha kwa kubahatisha bila mpango kamili
unaotekelezeka ni sawa na meli isiyokuwa na usukani. Muda wowote ule itagonga
juu ya miamba.
6. TABIA
YA KUFANYA KAZI ZAIDI KULIKO MALIPO: Moja kati ya penati za uongozi ni umakini
na utayari juu ya sehemu ya uongozi kufanya mengi zaidi ya yale wanayowataka
wafuasi wao kufanya.
7. HAIBA
INAYORIDHISHA: Hakuna mtu mchafu, asiyekuwa makini anayeweza kuwa kiongozi
mwenye mafanikio. Uongozi unataka heshima. Wafuasi hawatawaheshimu viongozi
ambao hawatapata alama za juu katika vigezo vyote vya haiba inayovutia.
8. HURUMA
NA UELEWA: Viongozi wenye mafanikio ni lazima wawe na huruma kwa wafuasi wao.
Zaidi ya hayo, ni lazima wawaelewe pamoja na matatizo yao.
9. UFAHAMU
WA KINA: Uongozi wenye mafanikio unahitaji ufahamu wa kina juu ya nafasi ya
uongozi.
10.
UTAYARI WA KUBEBA WAJIBU WOTE: Viongozi wenye
mafanikio ni lazima wakubali kuwajibika kwa makosa na kasoro za wafuasi wao.
Ikiwa watajaribu kubadilisha wajibu huu, hawataendelea kubakia kuwa viongozi.
Kama wafuasi watafanya makosa na kushindwa, ni viongozi walioshindwa.
11.
USHIRIKIANO: Viongozi wenye mafanikio ni
lazima waelewe na kutumia kanuni ya nguvu za ushirikiano na kuwa na uwezo wa
kuwahamasisha wafuasi kufanya hivyo. Uongozi unahitaji nguvu, na nguvu huhitaji ushirikiano.
Kuna aina mbili za uongozi. Ya kwanza na
ambayo ndiyo inayofanya kazi vizuri zaidi, ni uongozi kwa hiyari ya, na
kwa ridhaa ya wafuasi. Ya pili ni uongozi kwa nguvu bila ya hiyari na
ridhaa ya wafuasi.
Historia imejaa mifano kwamba uongozi kwa
nguvu hauwezi ukadumu. Kuanguka na kutoweka kwa “Madikteta” na Wafalme ni jambo
lililokuwa wazi. Ina maana kwamba watu hawatafuata utawala wa nguvu milele.
Dunia imeingia zama mpya za mahusiano kati ya
viongozi na wafuasi, ambazo kwa uwazi kabisa zinawataka viongozi wapya na aina
mpya ya uongozi katika biashara na viwanda. Wale walio katika mtindo wa zamani
wa uongozi wa nguvu ni lazima wapate uelewa wa aina mpya ya
uongozi(Ushirikiano) au kushushwa vyeo na kuwa wafuasi. Hakuna njia nyingine
kwao.
Mahusianao ya mwajiri na mwajiriwa au ya
kiongozi na mfuasi kwa nyakati zijazo yatakuwa ni ya ushirikiano, unaozingatia
mgawanyo uliokuwa sawa wa faida ya biashara. Wakati ujao, uhusiano wa mwajiri
na mwajiriwa utakuwa zaidi kama ubia kuliko kama ilivyokuwa hapo zamani. Hitler
na Stalin ni mifano ya viongozi waliotawala kwa nguvu. Utawala wao ulipita.
Watu wanaweza wakafuata utawala wa nguvu kwa muda mfupi, lakini hawatafanya
hivyo kwa hiyari. Uongozi kwa hiyari
ya wafuasi ndiyo aina pekee inayoweza kudumu.
Aina mpya ya uongozi itakumbatia zile sifa 11
tulizoelezwa kabla katika sura hii, pia na sifa nyinginezo. Watu wanaozifanya
sifa hizi kuwa msingi wa uongozi wao watapata fursa nyingi ya kuongoza katika
nyanja yeyote ile ya kimaisha.
…………………………………………………………………………
Tukutane tena
wakati ujao katika sehemu ya (ii) ya Sura hii ya 7 ya kitabu chako, FIKIRI
UTAJIRIKE(Think & Grow Rich). Kumbuka kuanzia sasa tafsiri hii itakuwa
ikichapishwa mara kwa mara kusudi kuendana na dhamira yetu kuu ya kuhakikisha
kitabu hiki kinakamilika mwaka huu wa 2017 na wasomaji wetu mnapata fursa ya
kukisoma chote hapa, bure kabisa katika blogu hii.
Nakusihi
msomaji na mfuatiliaji wa ile kampeni yetu ya mwaka huu ya #jirudishieukuuwakotena au #makeyourselfgreatagain
kwamba hakuna lisilowezekana chini ya jua, na unaweza kutimiza malengo yako
uliyojiwekea mwanzoni mwa mwaka huu hata ikiwa imebakia miezi 2 tu.
Sisi tunaamini
hivyo na ndiyo maana hata unaona tumeahidi kukamilisha shughuli hii ya
kuhakikisha kitabu hiki unakisoma chote katika lugha ya kiswahili hapa mwaka huu huu. Haikuwa kazi
rahisi, mwaka karibu wote huu lengo letu kuu lilikuwa ni kutimiza kazi hii ya
kutafsiri na tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumeshaimaliza kazi hiyo, kilichobakia
ni wewe tu kusoma Sura zote kwa Kiswahili hapa ili uyafanyie kazi yote
uliyojifunza.
Tunatambua
kitabu hiki siyo kigeni, wapo watu wengi waliokwisha kisoma, lakini pia wapo
wengine wengi hawajakisoma kwa ukamilifu wake kutokana na changamoto mbalimbali
zikiwemo lugha nk. Sasa ni wakati muafaka wa kufaidi kila kitu kilichoandikwa
humo bila kujali tena changamoto hizo.
Usikose pia
kujipatia vitabu vingine kutoka Self Help Books Tanzania, na unaweza kuviona au
kupata maelezo yake zaidi kupitia ukurasa huu wa, SMART BOOKS TANZANIA
0 Response to "KIONGOZI BORA MWENYE MAFANIKIO HUTENDA HAKI USAWA NA AMANI ILI KUENDELEA KUTAWALA"
Post a Comment