Tunakuja sasa kwenye makosa makubwa ya
viongozi wanaoshindwa, kwasababu ni muhimu pia kufahamu ni nini cha kutokufanya kama ilivyokuwa muhimu pia
kujua ni nini cha kufanya.
1. KUSHINDWA
KUPANGA MAMBO KWA KINA. Uongozi wenye ufanisi unahitaji uwezo wa kupanga na
kufahamu kwa undani mambo. Kamwe hakuna kiongozi wa kweli anayekosa muda wa
kufanya kitu chochote anachotakiwa kufanya kama kiongozi. Kiongozi ama mfuasi
anapokosa muda wa kupanga au kuwa makini na dharura yeyote, ni ishara ya
kutokuwa na ufanisi. Kiongozi mwenye mafanikio ni lazima afahamu majukumu yote
yanayohusiana na nafasi hiyo. Bila shaka, ina maana kwamba tabia ya kugawa
majukumu kwa wasaidizi waliokuwa na uwezo ni lazima iwepo.
2. KUTOKUWA
TAYARI KUTOA HUDUMA KWA UNYENYEKEVU. Ukweli viongozi wakubwa huwa tayari wanapohitajika
kufanya jukumu lolote ambalo wangeweza kumwambia mwingine afanye. “ Aliye mkubwa zaidi miongoni mwenu,
atakuwa mtumwa wa wote” ni ukweli
ambao viongozi wote wanaojiweza huzingatia na kuheshimu.
3. MATAZAMIO
YA MALIPO KWA KILE ‘WANACHOKIJUA’ BADALA YA KILE WAKIFANYACHO KWA KILE
WANACHOKIJUA. Dunia hailipi kwa kile watu ‘wanachokijua’, Huwalipa kwa kile wanachofanya au kile wanachohimiza
wengine kufanya.
4. WOGA
WA USHINDANI KUTOKA KWA WAFUASI. Kiongozi anayehofia kwamba mmoja wa wafuasi
wake anaweza akachukua nafasi yake ana uhakika wa hofu hiyo kuwa kweli muda
wowote. Viongozi wanaojiweza huwafunza wasaidizi wanaoweza kukaimu madaraka muda
wowote. Ni kwa njia hii pekee viongozi hujiongeza wenyewe na kujitayarisha kuwa
sehemu nyingi kwa wakati mmoja. Ni ukweli wa milele kwamba watu hupata malipo
zaidi kutokana na uwezo wao wa kusababisha watu wengine kufanya kazi kuliko
ambavyo wangeweza kupata kwa kutumia nguvu zao wenyewe. Viongozi wenye ufanisi
wanaweza kupitia uelewa wa kazi zao na mvuto wa haiba zao, kuongeza kwa kiwango
kikubwa ufanisi wa watu wengine na kuwahamasisha kutoa huduma zaidi na bora kuliko vile
wangeweza kufanya wenyewe.
5. KUKOSA
UBUNIFU. Bila ubunifu viongozi hawawezi kukabiliana na dharura, na kutengeneza
mipango itakayowaongoza wafuasi kwa ufanisi.
6. UBINAFSI.
Viongozi wanaotaka heshima yote kwa kazi ya wafuasi wao wanajihakikishia
kukutwa na maudhi. Ukweli viongozi wakubwa huwa hawatadai kutukuzwa.
Wanaridhika kuona heshima inawaendea wafuasi wao kwasababu wanajua kwamba watu
wengi watafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya pongezi na kutambuliwa kuliko
kufanya kwa ajili ya pesa peke yake.
7. KUTOKURIDHIKA.
Wafuasi hawamuheshimu kiongozi asiyetosheka(mlafi). Zaidi ya hayo kutokutosheka
katika aina zake mbalimbali huharibu uvumilivu na nguvu ya wale wote
wanaoiendekeza.
8. KUKOSA
UAMINIFU. Pengine hii ingepaswa kuja mwanzoni mwa hii orodha. Viongozi
wasiokuwa waaminifu kwa kampuni na kwa washirika wao – waliokuwa juu na chini yao - hawawezi kudumisha uongozi
wao kwa muda mrefu. Ukosefu wa uaminifu huwatia watu alama ya kuwa wadogo
kuliko vumbi la mchanga na kushusha chini juu ya vichwa vyao dharau
wanayostahili. Ukosefu wa uaminifu ni moja kati ya sababu kubwa za kufeli
katika kila nyanja ya maisha.
9. MSISITIZO
WA “MADARAKA” YA UONGOZI. Viongozi wenye ufanisi huongoza kwa kutia moyo na
siyo kwa kujaribu kupandikiza hofu katika nyoyo za wafuasi wao. Viongozi
wanaojaribu kuwavutia wafuasi kwa madaraka yao huja katika kundi la uongozi
kupitia nguvu. Viongozi wa kweli
hawana haja ya kutangaza ukweli huo isipokuwa kwa njia ya uendeshaji wao,
huruma, ufahamu, usawa na kuonyesha kwa vitendo maarifa ya kazi.
10.
MKAZO WA CHEO. Viongozi wenye uwezo
hawahitaji ‘cheo’ kupata heshima ya wafuasi wao. Viongozi wanaoendekeza sana
vyeo vyao kwa ujumla hawana kitu cha zaidi wanachoweka msisitizo. Milango
kuelekea ofisi ya viongozi wa kweli ipo wazi kwa wale wote wanaotamani kuingia
na maeneo yao ya kazi hayana urasimu wala majivuno.
Hizi ni miongoni mwa sababu kubwa zaidi za
kushindwa katika uongozi. Sababu yeyote kati ya hizi inatosha kusababisha
kuanguka. Isome orodha hiyo kwa umakini kama unataka kuwa kiongozi, na
hakikisha haufanyi makosa haya.
Baadhi
ya Sekta zenye fursa ambazo ‘Uongozi mpya’ utahitajika.
Kabla ya kumaliza sura hii, umakini wako
unahitajika katika sekta chache zilizo na rutuba ambazo kumekuwa na mapungufu
ya uongozi na ambazo aina mpya ya uongozi inaweza ikapata fursa kubwa.
1. Katika tasnia ya siasa kuna uhitaji mkubwa sana kwa uongozi mpya, uhitaji ambao hauashirii kitu kingine zaidi ya dharura. Wanasiasa wengi mno wameonekana kuwa walanguzi wa kiwango cha juu kabisa waliohalalishwa. Wameongeza kodi na kuharibu mfumo wa viwanda na biashara mpaka watu kushindwa tena kuhimili mzigo.
2. Sekta
ya fedha ipo katika mageuzi. Viongozi katika sekta hii karibu wanapoteza kabisa
uaminifu wao kwa umma. Tayari watendaji katika sekta ya fedha wameshahisi
uhitaji wa mabadiliko na wamekwishaanza.
3. Viwanda
vinahitaji viongozi wapya. Aina ya zamani ya viongozi walifikiria kwenda kwa
mtindo wa kugawana faida badala ya kufikiri na kwenda katika mtindo wa kanuni
za kibinadamu! Viongozi wa baadae wa kwenye viwanda ili wadumu ni lazima
wajihesabu wenyewe kama maofisa wa umma ambao jukumu lao ni kuongoza kampuni
zao kwa namna isiyosababisha ugumu kwa mtu mmojammoja au kikundi. Utumikishaji
wa wafanyakazi ni kitu kilichopitwa na wakati. Waache wale wanaotamani kuingia
kwenye uongozi katika sekta ya biashara, viwanda na ajira wakumbuke hili.
4. Viongozi
wa dini wa baadae watalazimishwa kuweka umakini mkubwa katika mahitaji ya muda
mfupi ya wafuasi wao katika utatuzi wa matatizo yao binafsi na ya kiuchumi ya
sasa, na kupunguza umakini katika wakati ‘mfu’ uliopita na wakati ujao ambao
bado ‘haujazaliwa’
5. Katika
taaluma za sheria, dawa na elimu, aina mpya ya uongozi na kwa kiasi fulani viongozi
wapya litakuwa ni hitaji muhimu. Hii sanasana ni kweli katika sekta ya elimu.
Viongozi katika sekta hiyo wakati ujao ni lazima watafute njia na namna ya
kufundisha watu jinsi ya kutumia
ujuzi walioupata shuleni. Ni lazima washughulike zaidi na vitendo kuliko nadharia.
6. Viongozi
wapya watahitajika katika sekta ya uandishi wa habari. Vyombo vya habari vya
wakati ujao ili viendeshwe kwa mafanikio ni lazima viondolewe ‘upendeleo
maalumu’ na ruzuku inayotokana na matangazo.
Hizi ndizo baadhi ya sekta chache ambazo
fursa kwa ajili ya viongozi wapya na aina mpya ya uongozi sasa zinapatikana.
Dunia inapitia mabadiliko ya haraka. Hii inamaanisha kwamba njia ambayo
mabadiliko katika tabia za binadamu zimekuwa zikitengenezwa ni lazima ziendane
na mabadiliko hayo. Njia zilizoelezwa hapa ni zile zinazobainisha muelekeo wa
ustaarabu zaidi ya nyingine zozote zile.
Lini,
na ni jinsi gani ya kuomba nafasi.
Taarifa zilizoelezwa hapa ni jumla ya matokeo
ya uzoefu wa miaka mingi ambayo maelfu ya wanaume na wanawake walisaidiwa
kutafuta soko la huduma zao(kazi) kikamilifu. Kwa hiyo inaweza ikategemewa kama
njia inayofaa na yenye kufanya kazi.
Njia ambazo huduma zinaweza zikatafutiwa
soko.
Uzoefu umethibitisha kwamba vyombo vifuatavyo
vinatoa njia bora na za moja kwa moja zaidi za kuwaleta pamoja mnunuzi na
muuzaji wa huduma.
1. MAWAKALA
WA AJIRA. Uangalifu ni lazima uchukuliwe kuchagua mawakala wale wenye sifa nzuri tu, uongozi unaoweza kuonyesha
kumbukumbu za kutosha za utendaji wenye matokeo yanayoridhisha.
2. KUTANGAZA
kwenye magazeti, majarida ya kibiashara, majarida, na redio. Matangazo
madogomadogo yanaweza kutegemewa kutoa matokeo ya kuridhisha kwa upande wa wale
wanaotafuta nafasi za kiutendaji, nakala kuonekana katika sehemu ya gazeti
iliyo na uwezekano mkubwa zaidi wa kusomwa na daraja la waajiri wanaohitajika.
Wakati wa kuandaa tangazo ni jambo lenye faida kupata ushauri kutoka kwa
mtaalamu anayefahamu jinsi ya kutoa sifa za kutosha za mauzo ili kuleta majibu.
3. BARUA
BINAFSI YA MAOMBI, huelekezwa kwa kampuni fulani au mtu binafsi aliye na
uwezekano mkubwa zaidi wa kuhitaji huduma zinazotangazwa. Barua zinatakiwa
kuchapwa kwa unadhifu KILA MARA, na kusainiwa kwa mkono. Pamoja na barua
inatakiwa pia itumwe na CV kamili au maelezo kwa ufupi ya sifa za mwombaji.
Vyote barua ya mwombaji na CV vinatakiwa viandaliwe kwa ushauri kutoka kwa
mtaalamu(angalia maelekezo chini)
4. MAOMBI
KUPITIA KUFAHAMIANA NA MTU. Ikiwezekana muombaji anatakiwa ajitahidi kumfikia
mwajiri mtarajiwa kwa kupitia kufahamiana pande zote mbili . Njia hii ya kukaribiana
ina faida zaidi kwa wale wanaotafuta nafasi za kiutawala na wasingependelea kuonekana kama wenyewe
wanajipigia debe.
5. MAOMBI
YA MTU MWENYEWE
Katika
hali fulani inaweza ikawa bora zaidi ikiwa waombaji watatoa huduma zao wenyewe
kwa waajiri . Katika hali hiyo kauli kamili ya maandishi ya sifa kwa ajili ya
nafasi hiyo inatakiwa kuwasilishwa kusudi waajiri watarajiwa waweze kujadili na
washirika rekodi za mwombaji.
Taarifa zinazotakiwa kuwasilishwa katika
CV iliyoandikwa.
CV hii
inapaswa kuandaliwa kwa uangalifu kama vile ambavyo mwanasheria angeandaa
muhtasari wa kesi itakayosomwa mahakamani. Ikiwa kama mwombaji hana uzoefu na
uandaaji wa CV, mtaalamu anatakiwa atafutwe . Wafanyabiashara wenye mafanikio
huajiri wanaume na wanawake wanaofahamu sanaa na saikolojia ya kutangaza ili
kuleta faida katika bidhaa zao. Aliye na biashara ya kuuza huduma naye anapaswa
kufanya hivyo hivyo. Taarifa zifuatazo zinatakiwa zionekane kwenye CV,
1. Elimu: Eleza kwa kifupi, lakini kwa
ukamilifu, elimu uliyokuwa nayo, na ni katika masomo gani umebobea, ukitoa
sababu za kubobea huko.
2. Uzoefu: Kama umekuwa na uzoefu kuhusiana
na nafasi inayofanana na ile unayoomba, elezea kikamilifu ukitaja majina na
anuani za waajiri wa zamani. Hakikisha unaweka wazi uzoefu wowote ule maalumu
ambao inawezekana ulikuwa nao na ambao unaweza kukufanya ujaze nafasi
unayoiomba.
3. Udhamini: Karibu kila kampuni ya biashara hutamani kufahamu kila kitu
kuhusiana na taarifa za nyuma za waajiriwa wake watarajiwa wanaoomba nafasi za
kazi. Jiandae kuwasilisha kwa mwajiri, ilkiwa utaulizwa, majina ya watu
watakaoweza kutoa taarifa kuhusiana na uzoefu na uwezo wako kama vile:
(a)Mwajiri
wa zamani
(b)Walimu
ambao ulisoma chini yao
(c)Watu
mashuhuri ambao maamuzi yao yanaweza yakaaminiwa.
4. Picha yako binafsi, ambatanisha na CV yako
picha yako mwenyewe ya karibuni.
5. Omba nafasi maalumu. Epuka maombi kwa
nafasi pasipo kuelezea hasa ni nafasi gani unayotaka. Kamwe usiombe nafasi,
“Ilimradi ni nafasi tu” Hiyo inaashiria huna sifa za kipekee.
6. Eleza sifa zako kwa nafasi hiyo unayoomba,
toa undani wote kama sababu inayokufanya uamini unafaa katika nafasi hiyo
unayoomba. Haya ndiyo MAEEZO MUHIMU ZAIDI YA MAOMBI YAKO. Ndiyo yatakayoamua,
kuliko kitu kingine chochote kile, ni majibu gani utakayoyapata.
7. Jitoe kwenda kufanya kazi kwa majaribio.
Katika hali nyingi, kama umeamua kwa dhati kuipata nafasi unayoomba , itakuwa
vizuri zaidi kama utafanya kazi bure kwa juma moja, au mwezi au kwa muda mrefu
unaotosha kumwezesha mwajiri wako
mtarajiwa kuamua thamani yako BILA MALIPO. Huu unaweza kuonekana kuwa ni uamuzi
mgumu, lakini uzoefu umethibitisha kwamba ni mara chache hushindwa kufanya vizuri angalao kwenye
majaribio.
Kama
una uhakika na sifa ulizokuwa nazo, majaribio ndiyo kitu pekee unachohitaji.
Kwa bahati njema kujitolea huko kunaonyesha kwamba unajiamini katika uwezo wako
wa kujaza nafasi unayoomba. Inashawishi zaidi ikiwa kujitolea kwako
kutakubalika na ukafanya vizuri zaidi ya vile ambavyo ungelilipwa kipindi chako
cha majaribio. Hakikisha ukweli kwamba kujitolea kwako kunazingatia yafuatayo,
(a)Imani yako katika uwezo wako kujaza nafasi
hiyo
(b)Imani yako kwa maamuzi ya mwajiri wako
mtarajiwa kukuajiri baada ya majaribio.
(c)Shauku
yako ya kupata nafasi unayoomba.
8. Ufahamu wa biashara ya mwajiri wako
mtarajiwa.
Kabla hujaomba nafasi, fanya utafiti wa
kutosha kuhusiana na biashara ili kuijua vizuri biashara hiyo na kuonyesha
katika maelezo yako mafupi ujuzi ulioupata katika sekta hiyo. Hili litakuwa
jambo la kuvutia kwani itaonyesha kuwa unao ubunifu na mapenzi ya dhati katika
nafasi unayoomba.
Kumbuka kwamba wakili anayeshinda kesi siyo
yule anayeijua sana sheria, bali ni yule anayefanya matayarisho mazuri zaidi ya
kesi. Ikiwa kesi yako itaandaliwa vyema na kuwasilishwa, ushindi wako pale
mwanzoni utakuwa umepatikana zaidi ya nusu.
Usiogope kuifanya CV yako kuwa ndefu mno.
Waajiri nao huvutiwa kununua huduma za waombaji waliofuzu vyema kama vile na
wewe unavyovutiwa kupata ajira. Kwa kweli mafanikio ya waajiri wengi wenye
mafanikio hutokana zaidi na uwezo wao wa kuchagua wasaidizi waliofuzu vizuri.
Wanahitaji taarifa zote zilizopo.
Kumbuka kitu kingine; Unadhifu katika
matayarisho ya CV yako yataonyesha kwamba wewe ni mtu mwenye bidii. Nimesaidia
kutayarisha CV kwa wateja zilizokuwa bora na za kipekee kiasi kwamba
zilisababisha waombaji kupata ajira pasipo kupewa udahili binafsi.
Mara CV yako itakapokamilika, mpe mgundisha
vitabu mzoefu atie jalada kwa unadhifu na kuwekwa maandishi na mchoraji ama
mchapaji kama ifuatavyo:
MAELEZO MAFUPI YA SIFA ZA
Robert K. Smith
AKIOMBA NAFASI YA
Katibu Muhtasi wa Rasi wa
KAMPUNI YA THE BLACK, Inc
Badilisha majina kila wakati CV
inapoonyeshwa.
Mguso huu binafsi unao uhakika wa kuamsha
usikivu, ichape CV yako vizuri, au idurufu katika karatsi nyeupe unayoweza
kupata na ijaladie kwa karatasi ngumu ya aina ya jalada la kitabu, mchapishaji
abadilishwe na jina halisi la kampuni liwekwe ikiwa itaonyeshwa kwa kampuni
zaidi ya moja. Picha yako inatakiwa kubandikwa kwenye moja ya kurasa za CV.
Fuata malekezo haya kwa umakini, ukiyaboresha popote pale ubunifu wako
utakapoamua.
Wauzaji wenye mafanikioa hujitunza wenyewe
kwa uangalifu. Wanafahamu kwamba muonekano wa kwanza hudumu muda mrefu. CV yako
ndiyo mwakilishi wako wa mauzo, ivishe suti nzuri ya nguo kusudi iweze kusimama
mshindi kinyume na kitu chochote mwajiri wako mtarajiwa alichowahi kuona katika
mchakato mzima wa maombi ya nafasi hiyo. Ikiwa nafasi unayoomba inastahili,
basi pia inastahili kuendewa kwa uangalifu.
Zaidi, kama unajinadi mwenyewe kwa mwajiri
kwa namna ambayo itawavutia kwa sifa zako, bila shaka utapata pesa nyingi kwa
huduma zako kutoka mwanzo kabisa kuliko ambavyo ungeliweza kupata kama
ungeliomba kazi kwa njia ya kawaida iliyozoeleka.
Kama utaomba ajira kupitia chombo cha
matangazo au wakala wa ajira, mpe wakala ruksa ya kutumia CV yako katika
kutangaza sifa zako. Hii itasaidia kukupa kipaumbele , kwa wakala na pia kwa
mwajiri mtarajiwa.
Jinsi
ya kupata nafsi ile ile unayotamani.
Kila mtu hufurahia kufanya aina ya kazi anayoimudu
zaidi. Msanii hupenda kufanya kazi na rangi, makanika na mikono yao, mwandishi
hupenda kuandika. Wale wasiokuwa na vipaji maalumu mapenzi yao yapo katika
tasnia fulani za biashara na viwanda.
Kuna aina nyingi za kazi za kuchagua, kuanzia
uzalishaji, masoko na taaluma mbalimbali.
1. Amua
moja kwa moja ni aina gani ya kazi unayohitaji. Ikiwa kazi hiyo haipo tayari,
pengine unaweza ukaitengeneza
2. Chagua
kampuni au mtu ambaye unatamani kufanya naye kazi.
3. Jifunze
kuhusiana na mwajiri wako mtarajiwa juu ya sera, wafanyakzi, na nafasi ya
kujiendeleza.
4. Kwa
kujitathmini mwenyewe, vipaji vyako na uwezo wako, tafuta ni kitu gani
unachoweza kutoa, na panga njia na namna ya kutoa faida, huduma, maendeleo na
mawazo unayoamini unaweza kuyatoa kwa mafanikio.
5. Sahau
kuhusu ‘kazi’. Sahau ikiwa kama nafasi ipo au haipo. Sahau njia ya kawaida ya,
“Naweza kupata kazi” Elekeza nguvu zako kwenye kile unachoweza kutoa.
6. Mara
utakapokuwa na mipango yako akilini, panga na mwandishi aliyekuwa na uzoefu
kukusaidia kuiweka katika karatasi kwa unadhifu na kwa undani
7. Iwasilishe
kwa mtu sahihi mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi. Kila kampuni inatafuta watu
wanaoweza kutoa kitu chenye thamani, iwe ni mawazo, huduma au mawasiliano. Kila
kampuni ina nafasi kwa mtu aliye na mipango dhabiti ya kivitendo kwa faida ya
kampuni.
Mlolongo huu wa taratibu unaweza ukachukua
siku kadhaa au majuma ya muda wa ziada, lakini tofauti katika kipato, katika
maendeleo na katika kuongeza kutambulika itaokoa miaka mingi ya kazi ngumu kwa
malipo ya chini. Ina faida nyingi, kubwa ikiwa kwamba mara nyingi itaweza
kuokoa kuanzia mwaka mmoja mpaka miaka mitano ya muda utakaochukua kufikia
lengo ulilochagua.
Kila mtu anayeanza au kuingia kupitia njia
fupi kupanda ngazi hufanya hivyo kwa makusudi na mipango madhubuti(isipokuwa
labda mtoto wa Bosi)
0 Response to "MAKOSA MAKUBWA 10 YA VIONGOZI NA AINA MPYA YA UONGOZI MZURI UNAOTAKIWA"
Post a Comment