Siku ya Kimataifa ya kutokomeza umasikini duniani
inayoadhimisha kila mwaka tarehe 17 Octoba, chimbuko lake au historia yake
huwezi ukaizungumzia pasipo kumtaja padre huyu wa Kikatoliki anayejulikana kama
Joseph Wresinski raia wa nchi ya Ufaransa aliyezaliwa na kukulia katika
umasikini wa kutisha.
Wresinski alizaliwa katika familia ya wahamiaji eneo
liitwalo Angers Ufaransa hapo mwaka 1917. Alikulia katika familia hiyo duni
iliyogubikwa na umasikini mkubwa pamoja na hali ya kutengwa na kunyanyaswa
kijamii. Mwaka 1946 alifanikiwa kupewa daraja la upadre ambapo alipangiwa kazi
na Askofu wake na kuhudumu katika parokia mbalimbali huku akionyesha kuzijali
sana familia zilizokuwa masikini zaidi.
Tofauti kubwa baina yake na watu wengine mashuhuri duniani
waliowahi kuguswa na umasikini wa watu kama vile kina Mama Teresa na wengineo ni
kwamba yeye ni wa kipekee zaidi kutokana na chimbuko lake kuwa ni familia
masikini. Ukweli huo ulimfanya akiri kwamba njia pekee ya kuimarisha haki
katika jamii ni kwa kuzitambua na kujenga juu ya nguvu, akili na kujitambua kwa
watu masikini.
Aliamini watu masikini wanaweza wakawa viongozi walio na
mtazamo muhimu wa Dunia ambayo watu wote wanakubalika na kuheshimiwa. Hata
miradi aliyoanzisha haikuhusisha tu watu masikini peke yao bali ilimvutia kila
mtu kutokana na upekee wa uzofu na uelewa wake.
Aliweza kutekeleza hayo kwasababu alifahamu kutokana na
uzoefu wake binafsi ni jinsi gani mtu anavyojisikia anapofedheheshwa, jinsi
gani kukata tamaa kunavyochanganyika na matumaini na ni kwanini baadhi ya watoto
hukata tamaa katika umri mdogo. Ujuzi huo Wresinski hakuupata akiwa shuleni
bali tokea utotoni.
Alifahamu fika kwamba kitu watu masikini wanachokitaka
siyo misaada wala zawadi balli ni kutendewa kwa usawa na kusikilizwa kwa
heshima. Aliwasikia watu masikini wakitamka, “Kwani mimi siyo binadamu? nataka
nitenddewe kama binadamu!”
Mwaka 1956 alichaguliwa na Askofu wake kwenda kuwa mkuu
wa “Chaplin”, makao ya familia zenye hali duni zipatazo 250 zilizowekwa katika mahema ya
dharura katika neo la Noisy–Le-Grand karibu na jiji la Paris. Familia hizo
ziliishi katika vibanda vilivyojengwa kwa tope na Wresinski alisema hivi
kuhusiana na miaka yake aliyokaa makazi hayo; “Familia katika kambi ile
zilinihamasisha kila kitu nilichokifanya kwa ajili ya kuwakomboa. Walinishika,
waliishi ndani yangu, waliniongoza, walinisukuma kuanzisha nao harakati”
Mwaka 1957 alianzisha chama(vuguvugu) lililoitwa ATD
Fourth World Movement, kikiwa na malengo ya kuziunganisha sekta zote za kijamii
zilizotengwa na umasikini uliokithiri. Kwa malengo hayo aliweza kukutana na
viongozi mbalimbali duniani wa nchi, makanisa na vyombo vya Kimataifa. Aliamini
kwamba vuguvugu la ATD Fourth World Movement lingeweza kubakia wazi kwa
tamaduni zote, imani na makabila.
Mwaka 1979 alichaguliwa kuingia katika Baraza la nchi ya
Ufaransa la Jamii na Uchumi, nafasi iliyokuwa hatua muhimu sana kwake katika
kutafuta uwakilishi rasmi kwa ajili ya familia zilizoishi katika umasikini
uliokithiri. Alichapisha ripoti yake mwaka 1987 iitwayo Wresinski Report na
kufanikiwa kwa mara ya kwanza kupata kutambuliwa kwa familia masikini kama
washikadau wengine katika jamii.
Ndipo sasa Oktoba 17 1987, mbele ya watu wapatao 100,000
kutoka kila kada za kiuchumi na kijamii na kila bara, Joseph Wresinski akazindua
rasmi jiwe la kumbukumbu katika jumba la haki za binadamu Paris(Human Rights
Plaza in Paris). Ujumbe wake uliowekwa katika jiwe hilo ulisema hivi;
“Popote
pale wanaume na wanawake wanapolazimishwa kuishi katika umasikini uliokithiri,
haki za binadamu huvunjwa. Kuja pamoja kuhakikisha kwamba haki hizi
zinaheshimiwa ni jukumu letu la dhati”
Joseph Wresinski alifariki dunia Februari 14, 1988, katika
hospitali moja jijini Paris miezi minne tu baada ya kutoa hiyo ripoti yake.
Mawe mengine ya kumbukumbu kama lile la Paris yalijengwa katika majiji yapatayo
44 kote duniani na mwaka 1992, Umoja wa Mataifa ukatangaza rasmi kuwa Oktoba 17
ni siku ya Kimataifa kwa ajili ya kuondoa umasikini.
Jana tarehe 17 Oktoba 2017 ikiwa ndiyo siku ya
maadhimisho hayo, kauli mbiu yake mwaka huu ilikuwa ni;
“NJIA
YA KUELEKEA JAMII ZENYE AMANI NA UMOJA”
Katika taarifa yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Antonio Guterres anasisitiza umuhimu watu wanaoishi katika umasikini
uliokithiri kujumuishwa na kusikilizwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo
Endelevu ya mwaka 2030, anasema kwamba dunia ina watu wapatao milioni 800
wanaoishi katika umasikini wa kutisha na ametaja sababu kuu kuwa ni ukosefu wa
ajira, usalama mdogo, kutokuwepo kwa usawa, vita na mabadiliko ya tabia ya
nchi.
...............................................................................................
Njia pekee ya wewe na mimi kuungana na Umoja wa Mataifa katika kutokomeza Umasikini uliokithiri duniani ni kwa kufanya shughuli za kiuchumi kwa bidii na maarifa hususani kilimo na biashara. Na mafanikio katika Kilimo au biashara yanategemea sana mtu kuwa na maarifa sahihi. Pendelea kupata maarifa hayo mara kwa mara kupitia vyombo mbalimbali kama vile redio, vitabu, television, mtandao wa intaneti, majarida na hata semina mbalimbali.
Unweza kupata vitabu vya biashara na ujasiriamali kutoka self help books Tanzania kwa gharama nafuu kabisa, fungua ukurasa huu kwa maelezo zaidi; SMART BOOKS TANZANIA.
0 Response to "HISTORIA YA SIKU YA KUTOKOMEZA UMASIKINI DUNIANI KIMATAIFA OKTOBA 17"
Post a Comment