Tunaendelea na maswali kutoka kwa msomaji wetu wa Songea mkoani Ruvuma na Swali lake la
pili aliuliza kama ifuatavyo;
Ahsante
na kuna kauli zipo mitaani kwamba wenye umri mdogo hawawei kufanya biashara
kubwa kwa mafanikio, ni kweli??
JIBU:
Siyo kweli kabisa na ni uzushi mtupu kwani duniani na
hata hapa Tanzania ipo mifano ya vijana wengi waliofanikiwa katika biashara
zao, kupata utajiri au kuwa mamilionea na hata mabilionea wangali hawajafikisha umri wa miaka 30.
Sula la ni umri gani mtu
anaweza akaanza kufanya biashara linategemea vigezo mbalimbali kikiwemo
kigezo cha masomo au shule, vinginevyo kama tutakavyoona katika makala
hii, mtu hata akiwa na umri wa miaka 15 anaweza akaanzisha biashara na
akafanikiwa kufika mbali.
Ikiwa kijana bado
anasoma si jambo zuri kujiingiza katika biashara ingawa pia kuna baadhi ya watu ambao waliacha shule
na kwenda kujiingiza katika biashara zilizowapa mafanikio makubwa. Lakini
ukumbuke watu kama hao ni wachache sana.
Katika watu 100 labda wanaopata bahati hiyo hawazidi 10. Elimu itabakia
kuwa muhimu daima. Ieleweke kuwa hata hao walioacha shule ‘drop outs’ siyo kama waliacha wakiwa mambumbumbu, hapana, wengi
huwa wanakuwa tayari wameshajitambua.
Tuchukulie mfano wa hapa hapa kwetu vijana walioanza
biashara na kufanikiwa wakiwa na umri mdogo, Mohammed Dewji alitajirika akiwa na
umri mdogo sana, ingawa utajiri huo
chimbuko lake ni baba yake lakini fedha za baba yake zilikuwa ni kama mtaji tu.
Mo akiwa na umri wa miaka 25 pekee baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu huko nchini
Marekani, alianza kazi katika kampuni ya baba yake kama mkuu wa idara ya pesa wakati huo ikiwa na mapato ya dolla za Kimarekani milioni 30 tu,
lakini baada ya kuchukua uthibiti wa kampuni hiyo aliweza kuifanya kampuni hiyo
kufikisha mapato yanayokadiriwa kufikia
dola bilioni 1.5 katika kipinddi cha miaka 15 pekee.
Hebu fikiria katika umri huo wa miaka 25 tu alivyoweza
kuifanyia mapinduzi makubwa na ya kushangaza kampuni ya baba yake iliyokuwa ikijihusisha
na uuzaji tu wa bidhaa katika maduka lakini kutokana na ubunifu wake mkubwa
sasa kampuni hiyo imejikita katika
biashara za aina mbalimbali zikiwemo viwanda vikubwa vya bidhaa za chakula na
sabuni.
Dunia nzima sasa inamtambua Mohammed Dewji, hata Jarida mashuhuri la
Forbes likamtangaza kuwa Mtanzania wa kwanza
kuwa Bilionea, jarida hilo pia lilimtaja Mo kuwa Mwafrika bilionea kijana zaidi mwaka jana 2016 akimiliki utajiri unaozidi
dola bilioni 1.
Kijana mwingine wa Kitanzania Patrick Ngowi muanzilishi
wa kampuni ya vifaa vya umeme jua solar(Helvetic group), alianza biashara akiwa
na umri mdogo sana wa miaka 15 na dola
za Kimarekani $50 tu. Alipofikisha miaka 18 alikopeshwa mtaji na wazazi wake wa
dola zingine $1,800 alizozitunza akiwekeza kwa uangalifu mpaka alipogeuka na kuwa milionea kabla hata
hajatimiza umri wa miaka 30.
Ladi Delano kijana wa Kinaigeria akiwa na umri wa miaka
22 tu na kampuni yake ya ‘Bakrie Delano Africa’ aliweza kuwa biilionea katika
umri huo mdogo kabisa alipokuwa akiishi nchini China mwaka 2004.
Mfano mwingine wa kuvutia kutoka nje ya Tanzania ni wa
mwanzilishi wa mtandao wa kijamii Facebook, Mark Zuckerberg mnamo Mwaka 2004 January
akiwa na wanachuo wenzake bwenini
katika chuo kikuu cha Havard Marekani walianzisha mtandao huo na kumbuka
alikuwa na umri wa miaka 20 pekee. Alikuwa bilionea kwa mara yake ya kwanza
kabisa akiwa na umri wa miaka 23 tu mnamo mwaka 2008.
Wengine waliokuwa mabilionea wakiwa na umri mdogo ni pamoja
na mwanzilishi wa mtandao wa snapchat
Evan Spiegel aliyekuwa na umri wa miaka 25 mwaka 2015, Mwanzilishi wa
Google, Larry Page aliyekuwa bilionea kwa mara ya kwanza mwaka 2004 akiwa na
umri wa miaka 30 pekee. Bill Gates alitangazwa bilionea kijana zaidi mwaka 1987
alipokuwa na umri wa miaka 31 tu.
Kwahiyo ndugu yangu kutoka Songea sasa wasiwasi wako
umepatiwa majibu na ikiwa wewe ni kijana basi angalia kama bado upo masomoni au tayari umekwishamaliza
masomo yako. Na hata ikiwa unasoma bado, hilo haliwezi kukuzuia wewe kuanza
kujiandaa kuwa mjasiriamali kisaikolojia. Anza kujijenga kimawazo pamoja na kuanza kujifunza namna ya kujiwekea akiba kwani akiba ni muhimu sana hasa pale
utakapokuja kuanza kufanya biashara au kuwekeza.
Ndugu msomaji, kama una swali au ungependa kupata ushauri wowote ule kuhusiana na ujasiriamali au kuanzisha biashara yako, usisite kutuma swali/maswali yako kwa njia z meseji au e-mail, tutakujibu na tunaweza pia kuyaweka hapa bloguni majibu kwa manufaa ya wasomaji wengine bila kutaja utambullisho wako labda iwe ni kwa ridhaa yako tu.
Usikose swali la tatu kutoka kwa msomaji huyu wa Songea Kesho.
Usikose swali la tatu kutoka kwa msomaji huyu wa Songea Kesho.
..................................................................................................
Kwa vitabu vyako vya ujasiriamali na biashara katika lugha ya kiswahili, tembelea SMART BOOKS TANZANIA
Mawasiliano ni 0712202244 au 07655533030, Peter Augustino
Good. Brother we hear you
ReplyDeleteNice information 🙏
Delete