BIASHARA 7 NZURI ZA KUFANYA ZITAKAZOKUINGIZIA PESA HATA KAMA UMELALA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA 7 NZURI ZA KUFANYA ZITAKAZOKUINGIZIA PESA HATA KAMA UMELALA

KUTENGENEZA PESA WAKATI  UMELALA
Karibu kila mtu katika nyakati fulani hufikiria biashara za kufanya au njia za kutengeza pesa ambazo zitamletea pesa hata wakati wa usiku akiwa amelala. Hii maana yake ni kwamba biashara huingiza pesa hata kama mmiliki wa hiyo biashara hatakuwepo pale. Biashara nyingi humlipa yule mwenye biashara kulinganna na masaa anayotumia kuitumikia biashara husika. Unaweza kuona sasa kwamba biashara ya namna hiyo haina tofauti kubwa na ajira ya kawaida.

SOMA: Njia za kuingiza kipato nje ya  kazi yako.

Dhana hii ya kuingiza kipato ukiwa umelala inafanana sana au inakaribia kuwa sawa na dhana nyingine niliyowahi kuizungumzia katika kitabu nilichotunga kiitwacho MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA. Tofauti yake kubwa ni kwamba katika Mifereji ya pesa mtu unaweza kufanya biashara yeyote ile hata katika muda wako wa ziada itakayokupa kipato cha ziada wakati kuingiza pesa hata wakati  ukiwa umelala unatengeneza pesa kwa kutumia mfumo (AUTOMATION)

Kuna dhana iliyojengeka kwamba njia kubwa ya kuingiza pesa hata ukiwa umelala usiku wa manane ni kwa kupitia mtandao wa intaneti tu peke yake/biashara za mtandaoni au wengine mara nyingi huiita, njia ya kutengeneza pesa kupitia blogu. Lakini kiuhalisia mtu unaweza ukatengeneza pesa hata ukiwa umelala kwa kupitia biashara yeyote ile ilimradi tu umetengeneza mfumo(system) imara utakaowezesha shughuli kufanyika hata kama haupo pale. Hebu fikiria mmiliki wa mgahawa mkubwa wenye wafanyakazi kila idara kuanzia meneja mpaka mfagiaji, ana haja ya kuwa pale muda wote kweli?

SOMA: Biashara ya mgahawa wa chakula, mchanganuo na mtaji mdogo wa kuanzia.

Pamoja na kwamba kila biashara unaweza ukaitengenezea mazingira au mfumo wa kuiwezesha ikutiririshie noti hata ukiwa umelala usiku au ukiwa mapumziko wakati wa likizo, mapumziko wakati wa ujauzito, mapumziko baada ya kujifungua, mapumziko mwisho wa mwaka kama wenzangu kina Mangi wanapokwenda Moshi kuchinja ndafu wakati wa Krismasi nk. Huku nyuma ukiacha shughuli zako(biashara) zikiendelea kama kawaida na pesa ikiingia.

Haijalishi ukubwa wala udogo wa biashara, inaweza kuwa hata ni biashara ya mtaji wa laki moja, kinachozingatiwa hapa ni mfumo. Hata hivyo kumiliki biashara ya kukuingizia kipato hata ukiwa umelala siyo jambo rahisi sana lazima tuliweke wazi hili na nisingependa unafiki kuhubiri vitu visivyokuwa na uhalisia hapa ili kuwapa watu matumaini ‘feki’, kisa nisomwe na watu wengi.

Unatakiwa kufahamu ABC za biashara sawasawa kama  vile unavyoanzisha biashara yeyote ile nyingine, kuzingatia masuala nyeti kama vile suala la kufanya utafiti wa biashara husika pamoja na kuweka mpango wa biashara hiyo(mchanganuo), ni mambo ya msingi kabisa pamoja na kulijua soko lako vizuri.

SOMA: Jinsi mpango wa biashara unavyoweza kuongeza mafanikio ya biashara  yako.

Kabla biashara hujaigeuza kukuletea pesa hata ukiwa umelala, itahitaji uwekezaji wa pesa na muda mwanzoni, nyingine huchukua muda mrefu miaka 2-5, lakini mara tu mfumo unapokuwa umekamiilika basi kila kitu  hubadilika na kuonekana kana kwamba unaingiiza pea kiulaini bila jasho kumbe watu hawaelewi ulishawekeza muda na pesa nyingi  kabla.

Ijapokuwa nimesema kwamba karibu kila biashara inaweza ikatengenezwa kuwa inayoweza kuleta pesa ukiwa umelala, lakini aina za biashara au orodha nitakayoitaja hapa chini ni zile aina za biashara ambazo ni rahisi zaidi kutengenezewa mifumo ya kuzifanya zijiendeshe zenyewe pasipo mmiliki wake kuwa pale masaa yote au zina tabia ya ukishazihangaikia mwanzoni basi, zinafika mahali zinajiendesha zenyewe na kuingiza pesa mithili ya mashine vile.

Ni zile biashara ambazo mara ukishazisimamisha basi, hutumii tena nguvu yeyote kuifanya iendelee au unatumia nguvu kidogo sana. Zinatofautiana biashara na biashara, zipo zinazoweza kuujiendesha zenyewe kabisa kwa asilimia zaidi ya 99 na nyingine angalao utatumia nguvu asilimia fulani, hazilingani.

BIASHARA ZINAZOJIENDESHA ZENYEWE WAKATI WEWE MWENYEWE HAUPO PALE HATA KAMA NI USIKU WA MANANE UMELALA

1. Biashara kwenye mtandao wa Intaneti.
Biashara za kwenye mitandao kama vile, blogs,tovuti na mitandao mbalimbali ya kijamii kama facebook, twitter, you tube, Instagram,  Linkedin, jamii forum nk. ndiyo zinazoshikilia namba moja au kuongoza duniani katika biashara zinazoweza kuzalisha pesa mtu akiwa anafanya mambo yake mengine katika zama tunazoishi sasa. Hapa nazizungumzia kwa ujumla wake lakini ukiamua kuzichambua mojamoja unaweza ukapata mamia kama siyo maelfu ya biashara hizo ambazo zinaweza zikafanyika mitandaoni.

SOMA: Kipi bora, kujiunga katika mitandao mingi ya kijamii au kubakia  katikka mtangao mmoja tu?

Kwa uchache tu nitajaribu kuziweka katika makundi kadhaa yafuatayo;
( A) Kutengeneza pesa kupitia blogu au website yako,
Hasahasa blogu siku hizi zimekuwa ni chanzo kikubwa sana cha pesa kwa watu wengi. Blog zina namna nyingi mtu anaweza akajipatia fedha kama vile;

·       Kuuzaa na kutangaza bidhaa zitokanazo na taarifa kama vitabu pepe(softcopies), DVD, semina nk. Bidhaa hizi zaweza kuwa ni za kwako mwenyewe au za watu wengine. Mfano mzuri ni blogu hii ambapo tunauza vitabu na semina za ujasiriamali.

·       Kuuza na kutangaza bidhaa za kawaida, mfano unaweza kuuza dawa za asili, nguo, urembo nk kupitia blogu yako.

·       Kuingiza pesa kama wakala (affiliate) wa makampuni/biashara nyingine kwa kupigia debe bidhaa zao, mteja akinunua unakatiwa kamisheni asilimia fulani.

·       Kuweka matangazo ya google, Google Adsense. Ikiwa blog yako inapata idadi kubwa ya watembeleaji kwa siku, unasaini mkataba na Google wanakupa matangazo unaweka na pindi mteja anapobonyeza tangazo hurekodiwa na google hukulipa baada ya kipindi fulani.

·       Kuuza nafasi za matangazo kama vile wafanyavyo watu wa magazeti, unaweka tangazo na kutoza kiasi cha fedha ulichopanga.

·       Kutafuta wadhamini watakaodhamini makala au kurasa zile zinazotembelewa na idadi kubwa ya watu. Mdhamini hulipa kiasi fulani cha pesa kwa kutajwa au kutangazwa katika ukurasa huo.

·       Kutengeneza blogu ya uanachama, ni wanachama pekee waliolipa kiingilio wanaoruhusiwa kutembelea blogu hiyo na mfano ni hii tunayoiendesha, ‘HAICHACHI SEMINA’ au blogu ya semina ya michanganuo ya biashara.

Uzuri wa blogu kwenye kujiendesha yenyewe ni kwamba wewe baada ya kuweka maandishi yako na picha, ukahakikisha umeyafanyia utafiti wa kutosha (Search Engine Optimisation) SEO, kazi kubwa hubakia kwa mtandao wenyewe kwani wewe hutajua saa wala siku wateja watakapotembelea blogu yako. Utashangaa tu namba ya idadi ya watembeleaji ikipaa juu.

Tena unaweza pia ukaiongezea vitu vingine vitakavyoifanya blogu ijiendeshe yenyewe zaidi(Automation) kwa mfano vitu kama autoresponder au email list ambayo wasomaji na watumiaji wa blogu yako wanapata huduma mbalimbali kama kudownload vitabu vya bure au kupokea makala moja kwa moja ‘automatically’ hata kama wewe muda huo upo katika mihangaiko yako mingine.

(B) Kuingiza pesa kupitia mtandao wa You Tube
Kwenye intaneti pia unaweza ukatengeneza pesa nyingi kwa kuweka picha za video katika mtandao wa youtube ambapo watazamaji watakapofungua video zako, you tube huweka na matangazo yao pale hivyo kukulipa kulingana na ni idadi gani ya watazamaji wanaozifungua video hizo na kuzitazama. Ukiweza kuupload video zinazotazamwa na watu wengi sana kwa siku ndivyo hivyohivyo napo utakavyolipwa fedha nyingi.

SOMA: Njia 7 halali na nzuri za kupata mafanikio na utajiri wa haraka.

(c) Upigaji wa picha mnato(still pictures).
Wapiga picha hawakubaki nyuma nao katika hili, wanaweza kuingiza pesa mtandaoni wangali wamelala kwa kutundika picha zao kwenye tovuti zinazouza picha (stock pictures), mara zinaponunuliwa zitumike wanapewa kamisheni.

(D) Biashara ya kununua na kuuza Blogu.
Unaweza kuingiza kitita cha fedha kwa kufanya biashara ya kununua na kuuza blogu zilizokwishatengeneza na watu wengine ambazo zimeshapata idadi kubwa ya watembeleaji. Hii pia hufanyika katika akaunti za mitandao mbalimbali ya kijamii kwa mfano hata hapa Tanzania wapo watu wanaokuza akaunti mfano za Instagram na kuziuza kwa bei kubwa kwa watu wengine mara baada ya kuwa na wafuasi wengi.

2. Biashara ya bidhaa zitokanazo na ubunifu wa akili yako.
Kwanini ni bidhaa na wala siyo huduma au bidhaa na huduma?, asili ya huduma haiwezekani ukatengeneza mfumo unaojiendesha wenyewe kirahisi pasipo wewe kuwapo. Kwa mfano katika kitabu cha MIFEREJI 7 YA PESA nilizungumzia “biashara ya bidhaa na huduma zitokanazo na mawazo yako”, ndiyo maana mwanzoni nilitangulia kusema Mifereji ya Pesa siyo sawa na Biashara zinazoingiza pesa hata kama umelala.

Unapobuni bidhaa iwe inahusiana na mawasiliano au sanaa, kazi kubwa utaifanya pale mwanzoni tu, ukishamaliza pamoja na kuitangaza sasa kinachobakia kwa asilimia kubwa ni wewe kufaidi matunda ya kazi yako. Mifano ya biashara hizo ni hii hapa chini;

·       Utunzi wa muziki na filamu; Katika MIFEREJI 7 YA PESA sura ya 1 uk. wa 5 kuonyesha nguvu kubwa ya kuleta faida biashara hii iliyokuwa nayo niliandika hivi, “Kazi zao zina tabia ya kuzaliana mithili ya virusi au bakteria, na huwa hazina tabia ya kusubiri miezi 9 kama Binadamu au Tembo….” Mifereji 7 ya pesa. Katika kitabu hicho niliendelea kufafanua kwamba tofauti kubwa iliyokuwepo baina ya mkulima na msanii wa muziki au filamu ni hiyo tabia ya kazi za sanaa kuzaliana tofauti na shamba au bustani ambayo kwa mfano unapolima bustani au matuta yako manne ya matembele, haiwezekani kuzitoa kopi bustani hizo zikawa 8, 16 nk. kama ilivyokuwa kwa CD au DVD ya filamu na muziki. Ni ukweli mchungu kwa mkulima lakini ndivyo ilivyo. Hivi karibuni mwanamuziki nguli wa Bongofleva Tanzania Naseeb Abdul au Diamond platnumz akihojiwa na shirika la utangazajia la BBC alisema ni lazima aangalie ni vitu gani anavyoweza kuwekeza sasa vitakavyokuja kumtengenezea pesa hapo baadae hata baada ya kustaafu kazi ya muziki.

SOMA: Biashara ya mazao ya chakula, unga, mchele, sukari maharage na mafuta ya kula. 

·       Utunzi wa vitabu; Kama ilivyokuwa kwa filamu na muziki, vitabu navyo baada ya mtunzi kumaliza kazi yake na aidha kumpa mchapishaji mswada wake au kuamua kuuchapisha mwenyewe, kinachofuata ni kuendelea kupokea mrahaba kama malipo ya asilimia waliyokubaliana na mchapishaji ama faida itakayotokana na vitabu vyake. Kumbuka hapa dhana ya kujiendesha yenyewe au kuingiza pesa umelala inakuja pale ambapo vitabu vya mtunzi vitauzwa maeneo mbalimbali na mawakala wakati yeye hayupo. Vitabu vinaweza kuuzwa mtandaoni pia kama PDF au katika tovuti zinazouza moja kwa moja(automatically) kama Amazon, Lulu na nyinginezo.

SOMA: Kwanini vitabu na semina za elimu  ya pesa na mafanikio haviwasaidii watu wengi?

·       Kutengeneza Apps za kwenye simu au kompyuta na michezo ya kompyuta. Wakati nilipokuwa natunga kitabu cha MIFEREJI 7 YA PESA miaka kadhaa iliyopita ni kama nilikuwa nafanya unabii vile kwani maneno niliyoandika leo hii yamedhihirika kuwa kweli, Katika Mfereji wa kwanza kipengele kidogo kilichosema, ‘Tengeneza michezo ya kompyuta na simu’ uk. wa 5 nilianika maneno yafuatayo wakati huo ‘apps’ hazijaanza kuwa maarufu kama ilivyokuwa sasa;

“Siku hizi kuna kitu kinakuja kwa kasi ya ajabu na huenda baadae kidogo kikaja kufunika mambo mengi; “Mobile Apps” ni applications za kwenye simu za kisasa ‘Smart phones’ ukifanikiwa kutengeneza moja tu ikapendwa na watu, unaweza ukauza dunia nzima na watu kama kawaida yao wakaanza kudai umeingia kwenye biashara haramu”-Mifereji 7 ya pesa.

·       Ugunduzi au Ubunifu wa vitu. Unapogundua kwa mfano mashine, teknolojia au dawa fulani na ukawekea hati miliki ya ugunduzi wako, utakuwa na fursa ya kupata mrahaba au faida kila kitu au mashine hiyo itakapodurufiwa na kuuzwa na watu/kampuni nyingine hata kama wewe binafsi haufanyi kazi katika kampuni hizo.

3. Uwekezaji katika Ardhi na Majengo.
Kwenye MIFEREJI 7 YA PESA niliandika ‘Wakalaa wa Ardhi na majengo’. Wakala si rahisi sana kutengeneza mfumo unaojiendesha, lakini hapa ni uwekezaji, inamaana kwamba kazi ngumu ni pale unapowekeza tu, kwa mfano ujenzi wa nyumba ya wapangaji siyo mchezo, utahisi kutoa pesa hata usiku wakati umelala lakini baada ya kumaliza tu, kila kitu kitakwenda “automatically”.

4. Biashara ya kuuza bidhaa/huduma kwa kutumia mashine.
Unaweka friji lako lenye uwezo wa kuuza soda lenyewe eneo lenye mzunguko wa watu wengi, mteja anapoingiza pesa na kubonyeza kitufe linamfyatulia chupa ya soda bila ya wewe kuwa pale, jioni unakuja na kutazama zimeingia tu sh. ngapi. Zamani, sijui kama siku hizi bado zipo, kulikuwa na simu fulani za mezani zilizowekwa vituo mbalimbali vya umma na mtu ulipaswa kutumbukiza sarafu ndani ya kiboksi kisha inakuruhusu kupiga simu. Halikadhalika kuna mashine za namna hiyo za kuuza vitu kama pipi, nk.

SOMA: Unajua biashara yenye faida kubwa na ya haraka mara 2 ya mtaji  utakaowekeza?

5. Biashara ya Ununuzi na uuzaji wa hisa.
Biashara hii hufanyika kwa kununua au kuuza hisa katika soko la hisa mfano la  Dar es salaam DSE na pia wakati mwingine watu huwekeza katika makampuni mengine au biashara kwa ajili ya kuja kupata gawio la faida pasipo kuhusika moja kwa moja katika shughuli za uendeshaji wa biashara. Ukishawekeza fedha zako unasubiri tu siku ya gawio.

6. Ukopeshaji pesa usiokuwa rasmi mitaani. Wale wanaofanya biashara hii hukopesha watu wasiokuwa na sifa za kukopa taasisi za fedha au waliokuwa na haraka sana kwa riba kubwa ajabu. Unaweza kukuta mtu hata anakopa kwa riba ya asilimia mia mbili ndani ya muda mfupi sana kama miezi 2 nk. huku akiweka rehani mali zake za thamani kama vile gari, TV au simu.

SOMA: Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha au benki?

7.Kumiliki akaunti ya benki inayolipa riba kubwa.
Kuna akaunti katika mabenki unapoweka pesa zako baada ya muda fulani kupita wanakulipa riba asilimia fulani ya pesa zako ulizoweka, na riba hii inaweza kuwa kiasi kikubwa cha fedha kutegemeana pia na kiasi kikubwa cha fedha ulizoweka benki.

Aina za biashara hizo 7 zilizotajwa hapo juu ni zile ambazo zina urahisi mkubwa kushinda zingine katika kuzifanya zijiendeshe, kuna aina moja ya biashara ambayo sikuitaja rasmi lakini unaweza kushangaa kama siyo kucheka kwani sidhani kama hapa kwetu inaweza ikaingia akilini.

Eti mtu kuingiza pesa kwa kazi ya kulala usingizi. Ina maana kuwa anaingiza pesa moja kwa moja akiwa amelala kitandani na hii inasemekana Shirika la anga za juu la Marekani NASA ndilo hulipa watu kwa ajili ya kazi za kitafiti ambapo mtu anaweza akapewa kazi ya kulala hata miezi 6 kitandani ili wafahamu tu ikiwa wanaanga wanaweza kupatwa athari gani wawapo anga za juu wamelala kwa muda mrefu.

Kutengeneza pesa kwingine kunakoshangaza mtu akiwa amelala inasemekana ni katika makampuni yanayotengeneza magodoro mfano wa magodoro ya Dodoma(Dodoma nimetolea mfano tu sidhani kama wanafanya hivyo). Mtu analipwa kwa kazi ya kufanya majaribio ‘test’ mithili ya vile mtu anavyolipwa kwa kazi ya kuonja vyakula jikoni katika mahoteli makubwa au makampuni yanayotengeneza vinywaji.

HITIMISHO.
Ili mtu uweze kutengeneza pesa hata ukiwa umelala, unahitaji biashara lakini biashara hiyo uifanye ijiendeshe yenyewe kwa kiasi kikubwa, hapa nimetaja tu aina za biashara lakini wakati ujao makala hii natarajia kuiendeleza hivyo usikose nitakuletea njia au ni jinsi gani mtu unavyoweza kuifanya biashara yako ijiendeshe yenyewe. Nitakuelezea ni kwa jinsi gani unavyoweza ukatengeneza mfumo(system) ambayo ndiyo siri kuu ya kutengeneza fedha ukiwa umelala, umepumzika au unafanya ishu zako zingine.

Juu kabisa ya yote ni kwamba ili uweze kufanikisha yote haya huwezi kukwepa kuzijua ABC za biashara, ABC za biashara maana yake mtu unapaswa kujua yale mambo yote ya msingi katika uendeshaji wa biashara na kwa uzoefu wangu mimi binafsi, kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI ndiyo kitabu bora zaidi katika lugha ya kiswahili kilichokuwa na kila kitu sehemu moja.

SOMA: Njia mpya za kufanya mambo: Dunia, biashara, ajira vinabadillika kwa kasi ya ajabu!


Kumbuka hizi siyo aina mpya za ujasiriamali wala wazo la biashara kutoka sayari nyingine bali vitu ni vile vile lakini kama ujasiriamali wenyewe ulivyofafanuliwa kwa mapana kabisa katika kitabu hicho, haya yote ndiyo matokeo ya UBUNIFU ambao ndiyo kitovu chenyewe hasa cha UJASIRIAMALI, biashara bora kabisa 7 za ukweli na zilizokuwa na uhakika wa kutengeneza faida ya haraka huku ukiendelea na mishemishe zako nyingine. 

………………………………………………………………….

1. Sababu kuu 2  kwaninii ununue vitabu hivi 3  kutoka self help books Tanzania.






Tunaandika Michanganuo ya Biashara(Business Plans) kwa ajili ya mahitaji yeyote kwa gharama nafuu. Pia tunatoa mafunzo(course) kwa mtu yeyote anayehitaji kuandika Business plan yake mwenyewe kwa njia nyepesi; Mawasiliano yetu ni: whatsapp/simu: 0765553030 au simu/sms: 0712202244

Kutembelea duka letu la Vitabu na Michanganuo mtandaoni fungua hapa: SMART BOOKSTZ

11 Responses to "BIASHARA 7 NZURI ZA KUFANYA ZITAKAZOKUINGIZIA PESA HATA KAMA UMELALA"

  1. msaada ndugu nahitaj kufanya biashara ila sijajuwa biashara ipi ambayo itaweza nipatia mafanikio kwa haraka ambayo mtaji wako sio mkubwa kama laki 3 hivi

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wazo la biashara inayoweza kukupatia mafanikio ya haraka haiwezekani mtu mwingine zaidi yako wewe unayelitafuta akakupatia kwani mawazo karibu yote duniani ya biashara huwa yanalipa kutegemeana na mazingira ya mwenye hilo wazo. Cha msingi ni wewe kuchagua mawazo yale ya biashara unazozitamani au unazojua una uwezo nazo kisha ukachekecha ni lipi kati yake utakaloweza kulimudu zaidi ya mengine ukizingatia vigezo mbalimbali kama vile kiasi cha mtaji ulichokuwa nacho, aina ya wateja wanaokuzunguka, ujuzi ulionao na sera au taratibu mbalimbali zinazoihusu aina hiyo ya biashara uliyochagua.

      Hapo utaona mimi kwa mfano mazingira yako siyajui hivyo nikupa wazo linaloendana na mazingira yangu laweza lisifanye kazi kwa upande wako.

      ASANTE!

      Delete
  2. Naomba msaada wa kupata blog au tovoti

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ingawa specifically hatujihusishi na utengenezaji wa blog na tovuti lakini ni jambo rahisi sana kufungua blogu ikiwa lengo lako mwanzoni ni kuweka contents zako(maudhui) yaweze kuwafikia watu. Unaweza kusearch google, "How to start a blog" na ukifuata vizuri maelekezo utaweza kufungua blog yako ndani ya muda mfupi.

      Ukihitaji website au blogu yenye muonekano wa kipekee sasa na pengine jina la kipekee(siyo dotblogspot na dotwordpress) basi unaweza kuwatafuta wataalamu wa kazi hiyo na siku hizi Tanzania wamejaa tele hata ukisearch mtandaoni au katika magroup huwezi kuwakosa, bei ya blog wengi huanzia elfu 30 na kuendelea wakati website huanzia laki kwenda juu.

      Delete
  3. Hiyo biashara yabkukopesha bila riba mbn haina ufafanuz

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nadhani hukusoma vizuri, sijaandika "kukopesha bila riba" bali "ukopeshaji usiokuwa rasmi mitaani" Hii maana yake ni wale watu binafsi ama siku hizi wanajisajili kabisa rasmi katika mamlaka rasmi za serikali na kupewa vibali vya kukopesha kama taasisi nyinginezo za kifedha. Mitaani watu wengi wamezoea kuita "Mikopo kausha damu" wanatengeneza faida kupitia riba wanazotoza.

      Delete
  4. Msaaada nahitaji biashara ambayo nitatumia mtaji wa lakin3

    ReplyDelete