Kwenye mfululizo wetu au kipengele cha biashara zilizosahaulika au kwa jina
jingine biashara ndogo ndogo zisizopewa kipaumbele kikubwa na watu kumbe zina
uwezo wa kuzalisha faida kubwa na nzuri, katika pita pita yangu mitaani wiki
hii nilikutana na habari za biashara hii ya makopo yaliyotupwa ambapo kwa kweli
niliwahi kuiandikia makala nyingine nikasema, Si kila muokota makopo ni kichaa, wapo wanaotengeneza noti kushinda
hata karani wa benki. Ila hii ya leo ina tofauti kidogo.
Unapotaja aina za biashara ndogondogo zinazotengeneza
faida nono kama wewe ni mtu unayezifahamu fursa huwezi ukaacha hata kidogo
kuorodhesha biashara ya kununua na kuuza kwa jumla vitu chakavu vinavyopatikana
katika mazingira na ambavyo huchafua mazingira ikiwa vitaachwa vitapakae ovyo
ovyo, lakini kwa kuvikusanya na kuvirudisha kiwandani unakuwa unaboresha
mazingira ili yaweze kuwa safi zaidi.
Biashara hii licha ya kuwa ni nzuri kifaida lakini pia ni
halali kwani serikali inaunga mkono kikamilifu watu wanaohakikisha mazingira
yanakuwa safi na kubakia katika hali yake ya uasili. Hebu fikiria ni kitu gani
kingelitokea katika mazingira ya nchi na Dunia kwa ujumla kama kusingelikuwa na
kurudishwa viwandani vitu chakavu. Kuna chuma, plastiki, mabati na vitu chungu
nzima vinavyotoka viwandani ambavyo vingesababisha bahari na nchi kavu kugubikwa
na takataka za kutisha ambazo siyo kero tu kwa binadamu bali hatari kwa afya za
wanyama na viumbe hai vinginevyo vyote ikiwemo mimea samaki na hata wadudu.
Tanzania inapoelekea katika uchumi wa viwanda vitu chakavu kama plastic
vitakuwa ni dili kubwa wakati ujao
Si nia yangu leo kuzungumzia takataka zote kwa ujumla,
japo karibu kila takataka duniani ni fursa mojawapo ya biashara. Wakati wewe
ukilia ni uchafu, wenzako wanazigeuza kuwa pesa kwa namna moja ama nyingine.
Kama ilivyokuwa ada mimi huwa napenda kuibua fursa mitaani ambazo watu wengi
hawajazishitukia lakini wale wachache waliokwishazigundua wanapiga hela kimya
kimya utadhani wanamfukuza mwizi aliyebeba fuko la noti vile.
SOMA: Biashara ndogo rahisi kwa wajasiriamali zinazoendana na wakati tulio nao.
SOMA: Biashara ndogo rahisi kwa wajasiriamali zinazoendana na wakati tulio nao.
JINSI BIASHARA YA KUNUNUA NA KUUZA CHUPA CHAKAVU ZA
PLASTIKI KWA JUMLA ILIVYO NA FAIDA NUSU KWA NUSU
Nilikutana na dada mmoja anayefanya biashara ya kuokota
chupa chakavu za plastiki na kisha kwenda kuziuza, kwa maana nyingine dada huyu
yeye hufanya biashara ya chupa chakavu kwa rejareja. Baada ya kuziokota maeneo
mbalimbali yeye huzipeleka kuuza kwa wafanyabiashara wanaonunua kwa jumla na
kisha kupeleka kuuza kiwandani. Katika mazungumzo yetu dada huyu alikuwa
akinisisitizia juu ya faida kubwa wanayopata wafanyabiashara wale wanaonunua na
kuuza kiwandani kwa jumla pamoja na urahisi uliopo katika biashara hiyo.
Alikuwa akijaribu kunishawishi kama ninao mtaji niingie katika biashara ile au
tuingie hata ubia.
“Kaka biashara ya kununua makopo na kuyauza kiwandani nimeshaichunguza
kwa muda mrefu ina faida kwani unapata kiasi mara mbili cha bei unayonunulia
unapokwenda kuwauzia kiwandani, isitoshe wewe huna gharama kubwa kwani wao
wenyewe kiwanda ndiyo wanaotuma watu wao na usafiri kuja kuchukua mzigo baada
ya kufikisha tani kadhaa.” Alinisimulia dada huyu anayependa kuvaa kama
mwanaume awapo kazini, huvaa kofia pama, Tshirt na suruali ya jeans
“Ukiwa na mtaji kama laki moja na elfu 90 peke yake
unatosha kwani utanunua mzani wa mtumba ambao hauwezi kuzidi shilingi elfu
arobaini (40), na mtaji wenyewe kwa ajili ya kununulia mzigo shilingi laki moja
na nusu tu ambao utanunua tani moja ya makopo. Kuhusiana na eneo, halina shida
kubwa, unaweza ukatafuta eneo lolote lile la wazi kwani serikali huwa
haihangaiki sana na kuondoa biashara za muda mfupi, makopo ya plastiki
ukishafikisha tani moja au mbili wanakuja kuchukua hayakai muda mrefu.
Na hata ukiamua kununulia eneo hatarishi kama vile maeneo
ya mabondeni, unaweza ilimradi tu uhakikishe siyo msimu wa mvua na pia usalama
wa makopo yenyewe kwani wale waokotaji makopo wenyewe wanaweza kuja usiku au
muda wewe haupo wakayaiba na kuja kukuuzia tena kesho yake.” Alimalizia dada
huyo aliyeonekana kuijua vizuri biashara hiyo lakini anakosa mtaji wa kuweza
kuianza.
Kwa mujibu wa maelezo ya dada huyu, kilo moja ya makopo
chakavu ya plastiki wanauza shilingi 150/= kwa plastiki laini na plastiki ngumu
na PVC hufika mpaka shilingi 350/= kwa wanunuzi wa jumla wanaonunua kwa ajili
ya kwenda kuuza kiwandani. Bei wanayokwenda kuuza kiwandani anasema hufika
mpaka kiasi mara mbili ya bei wanayonunulia. Hii ni kusema kwamba ukinunua tani
moja ya makopo kwa shilingi laki moja na nusu utaenda kupata shilingi laki tatu
kiwandani, ukiondoa gharama za manunuzi na nyinginezo unabakiwa na shilingi
karibu laki moja na kitu hivi. Kwa hiyo ni biashara iliyokuwa na faida nzuri na
isiyokuwa na gharama nyingi wala changamoto za kutisha.
………………………………………………………………….
Mpenzi msomaji mwaka huu ndio unamalizika, hivyo katika
kampeni yetu tuliyoianza pamoja mwanzoni mwa mwaka huu iliyoitwa, MAKE YOURSELF GREAT AGAIN AU JIRUDISHIE UKUU WAKO TENA, tuliahidiana sote kwamba ifikapo
kipindi kama hiki kila mmoja wetu ahakikishe anapima ni kwa kiasi gani ameweza
kutimiza malengo yake aliyojiwekea hususani yale ya kiuchumi na maisha kwa
ujumla. Sisi kama Self Help Books Publishers tulijiwekea lengo la kumalizia
kutafsiri kitabu cha Think & Grow Rich katika lugha ya kiswahili na
tunashukuru lengo hilo tumeshalikamilisha, kilichobakia sasa ni kumalizia tu
kukichapisha katika blogu yenu hii ya jifunzeujasiriamali kazi inayoendelea.
Je, na wewe ni lengo lipi umeweza kulitimiza? Si lazima
uliweke wazi hapa unaweza kujijibu mwenyewe tu na malengo siyo lazima iwe kila
ulichoazimia kufanya basi umetimiza kila kitu hapana, unapoweka malengo kuna
malengo mahsusi na malengo yale madogomadogo(rejea kitabu cha Mifereji 7ya pesa uk. wa 16.), hivyo angalia yale
malengo yako makubwa ni lipi uliloweza kutimiza kikamilifu?
Kuna mambo mengi na makubwa tuliyokuandalia mwezi huu wa
Disemba mwishoni mwa mwaka huu wa 2017 kuelekea Januari mwanzoni mwa mwaka mpya
wa 2018 usikae mbali, lakini juu ya kila kitu nakusihi sana kama ulikuwa
hujasoma kitabu mahsusi kwa ajili ya mtu anayetaka kujiwekea malengo kikamilifu,
kitabu kiitwacho, MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA basi
utafute kitabu hicho kwani ni kizuri mno hasa nyakati hizi za mwanzo wa mwaka
watu wanapoweka malengo mbalimbali ya maisha.
Ukikisoma huwezi hata siku moja ukaja kujuta pale mwaka
unapoisha, eti hujatimiza malengo uliyojiwekea. Kitabu hiki ni shilingi elfu 3
tu softcopy na unatumiwa kwa njia ya E-mail unadownload kwenye simu au kompyuta
yako. Tuma pesa katika namba 0712202244
au 0765553030 jina: Peter Augustino Tarimo, pamoja na anuani yako ya email kwa njia ya
meseji, utatumiwa kitabu mara moja muda huohuo. Unaweza pia kuwasiliana nami kupitia
ujumbe wa Whatsapp kwa namba 0765553030
ASANTE SANA
Peter A. Tarimo
self help books Tanzania
0 Response to "BIASHARA HII WATU WENGI HUIDHARAU LAKINI INA FAIDA KUBWA NA NZURI,MTAJI LAKI 1"
Post a Comment