Katika makala iliyopita nilitaja sababu kubwa 14
zinazowafanya watu wengi kila mwaka kulalamika kwamba malengo ya mwaka
wanayojiwekea, pindi unapofika wakati kama huu wa kumalizika mwaka wanakuwa
hawajaweza kutimiza hata robo ya malengo hayo au yale mambo waliyokuwa
wameazimia kuyatekeleza mwaka ulipokuwa ukianza.
Watu wengine hudiriki hata kusema kuwa ni bora wasiweke
malengo kabisa kama hali yenyewe ndivyo ilivyo. Lakini swali moja la kujiuliza
ni kwamba, sasa kama usipoweka malengo utaishi vipi na wakati kila jambo
duniani ili liweze kutekelezwa na binadamu ni lazima kwanza aweke malengo?
Malengo yanahusiana moja kwa moja na namna tunavyofikiri, haiwezekani utekeleze
jambo fulani pasipo kwanza kuliwaza akilini na bila shaka yeyote ile kila mtu
ana malengo fulani akilini mwake kila kunapokucha. Ni baadhi ya wanyama na
viumbe wengine tu ndio hutenda mambo pasipo kuwa na malengo. Nasema baadhi ya
wanyama kwani hata Simba anapokuwa mawindon,akilenga kumkamata swala fulani
basi ujue atafukuzana na huyo huyo mpaka amemkamata, hivyo nao wana malengo
akilini mwao.
Kwenye makala hiyo iliyopita niliahidi kukuletea makala
nyingine tena ambayo ningekuelezea kinagaubaga sababu kubwa iliyonikwaza
binafsi mwaka 2017 nisiweze kufikia malengo yangu yote kwa asilimia mia moja
kama nilivyoyapanga mwezi Januari mwanzoni mwa mwaka 2017. Katika vikwazo vyote
14 na hata vingine unavyoweza kuongezea hapo kwani vipo vingi, kuna kimoja ambacho
baada ya kufanya tafakari ya hali ya juu kabisa nilibaini ya kuwa ndicho
kimekuwa sababu kubwa inayonikwamisha nishindwe kufikia kilele cha juu kabisa
cha malengo yangu kila ninapoyaweka.
Unaweza ukaamua kutaja sababu yeyote kati ya zile 14 kuwa
ndiyo kigingi cha kufikia mafanikio ya kweli katika malengo unayojiwekea,
sikatai kwani kama nilivyosema sababu zote zina uwezo wa kumfanya mtu akwame
kutimiza malengo yake kila mwaka mpya unapoanza mpaka unapokwenda kumalizika
kama ilivyokuwa kwangu menyewe mwaka 2017.
Unaweza ukazizingatia na kuziishi sababu hizo ukikwepa
kwenda kinyume nazo na kufuata yale yote yanayopaswa kufuatwa kama vile kubadilika na kuwa mtu wa vitendo zaidi, kuweka malengo makubwa,
kutokukata tamaa, kukaa mbali na watu wasiokuwa na malengo kama ya kwako,
kufanya mambo machache yenye tija kuliko utitiri wa vitu vinavyokupotezea
wakati wako bure, nk. kama ilivyotajwa
katika makala hiyo iliyopita, lakini bado ukashangaa pia malengo yako hayatimii
kama ulivyokusudia. Sasa bila kupoteza muda zaidi nakwenda rasmi kukutajia kile
nilichogundua.
KILELE CHA JUU KABISA CHA UBORA WA MAFANIKIO YAKO NI
MATOKEO YA MZUNGUKO MZURI WA FEDHA KATIKA BIASHARA/MFUKO WAKO.
Usije ukaninukuu vibaya tafadhali na pia naelewa fika
kabisa kwamba mafanikio ya biashara siyo fedha bali ni mawazo mazuri, hilo
karibia kila mtu analifahamu. Hii naweza nikaifananisha na simulizi kongwe ya Yai
na kuku ni kipi kilianza. Unapoanzisha biashara kwa wazo tupu bila ya
mtaji kwa maana ya pesa au rasilimali zingine maana yake ni kwamba unajaribu
kutengeneza mazingira fulani kusudi baada ya muda fulani mzunguko wako wa fedha
uwe mzuri na hatimaye uweze sasa kuifanya biashara hiyo kwa uhakika zaidi.
Lakini vipi ikiwa unalo wazo bora na hapo hapo unao mtaji wa kutosha, biashara
yako haitashamiri?
Hakuna ubishi wowote kwamba watu wengi wameshindwa
kutimiza malengo yao mengi waliyojiwekea shauri ya ukata. Mtu unapanga
kuanzisha biashara fulani au kutimiza malengo kadha wa kadha lakini njiani
unakutana na mitihani lukuki ya kifedha inayokufanya ushindwe kutekeleza kile
ulichokusudia, halafu lawama mara nyingi tunazibebesha zile sababu zingine
miongoni mwa zile 14 tulizozitaja katika makala iliyopita. Ni kazi ngumu sana
kutimiza miradi ya maana ya kiuchumi pasipo kuwa na rasilimali(fund). Watanzania wengi wanashindwa kutoka
shauri ya kukosa mitaji ya maana kuliko sababu zingine. Sikatai pia kuna uzembe
na ukosefu wa elimu sahihi ya ujasiriamali lakini ni kwa kiasi kidogo kushinda
kukosa rasilimali za kutosha.
Kwenye biahara chochote kile utakachokifanya, mbinu
zozote zile utakazozitumia, lengo lake kubwa ni kufanya mzunguko wako wa fedha
uwe chanya au kwa maana nyingine kiasi cha fedha unazoingiza kizidi kile
unachoingiza. Ukifanikiwa kuvuka kipindi hiki kigumu katika safari yako ya
maisha au biashara ya kuhakikisha fedha unayoingiza ni nyingi kushinda ile
unayotoa basi hapo ndipo watu wengi hupaita majina mbalimbali, wengine watasema
umetoka, wengine umetoboza, wengine, umefikia mpenyo wako wa maisha, umetajirika,
nk.
Fedha unaweza ukaichukulia simple lakini ni kigezo kikubwa mno katika kuhakikisha unatimiza
malengo uliyojiwekea. Sizungumzi hivyo nikimaanisha kwammba bila ya fedha
huwezi ukafanya jambo lolote, la hasha, ila ninamaanisha kwamba hata ikiwa kwa mfano
unafanya biashara isiyotumia mtaji kabisa kama hizi nilizotaja hapa katika
makala hii, (biashara ndogondogo 7 unazoweza kufanya bila mtaji wa pesa kabisa), bado inapofika asubuhi ni lazima uende gengeni kununua
vitafunio na ikifika mchana au jioni ni lazima uende dukani utoe fedha taslimu
kwa ajili ya kununua chakula, unga au mkate ule ili uendelee kuishi.
Na hata ikiwa hutatoa fedha wewe mwenyewe ni lazima fedha
hizo zitoke mfukoni mwa mtu mwingine ili wewe uendelee kuishi. Hii yote
inadhihirisha kwamba katika maisha suala la fedha kuingia na fedha kutoka ni suala
nyeti kupita vile tulivyozoea kufikiri. Ni sababu ya kufanikiwa au
kutokufanikiwa kwa mambo yetu mengi.
Naamini kabisa kwamba ikiwa utafuatana na mimi katika
mfululizo wa makala hiozi nilizoziandaa kwa ajili ya mwaka huu mpya wa 2018, dhana hii ya MZUNGUKO WA FEDHA au CASH FLOW utaweza
kuielewa vyema kabisa na wala hautabaki na utata unaoweza kuwa unauona sasa
hivi, najua wengi hawatanielewa vizuri hapa mwanzoni lakini itafika muda
watanielewa vizuri tu.
Sababu niliyoahidi kukueleza ndiyo hiyo kwamba, ukata au mzunguko hafifu wa fedha ndiyo uliokuwa chanzo kikubwa kwangu
kushindwa kutimiza sehemu kubwa ya malengo yangu ya mwaka 2017, siwezi kujua
kwa upande wako ilikuwaje lakini naamini watu wengi bado watakuwa wakisingizia
sababu nyingine zile 14 kama na mimi nilivyokuwa zamani nikizisingizia.
SASA
BAADA YA KUBAINI SABABU ZILIZONIFANYA NISHINDWE KUTIMIZA MALENGO YANGU 2017
NIMECHUKUA HATUA GANI?
Kwa mtu anayeanza chini kabisa hakuna ubishi ni lazima
uanze hata bila ya kuwa na senti tano mfukoni, hilo linawezekana na hata
asilimia kubwa ya mabilionea na matajiri wakubwa unaowasikia leo hii walianza
hivyo wakiwa na mawazo yao tu. Lakini inafika mahali ni lazima uongeze
rasilimali zako na hususan fedha ikiwa utataka sasa utoke kiukwelikweli na hapa
ndipo panapokuwa na mtihani kwa watu wengi nikiwemo na mimi mwenyewe. Ukiweza
kutegua mtego huu uliojificha hapa basi jua safari yako ya mafanikio kifedha au
hata katika nyanja nyinginezo zozote zile za maisha imepata kibali.
Kuongeza mzunguko wa fedha katika mfumo wako wa biashara
au maisha kiujumla kunahusisha vitu vingi na kuna njia kadhaa tofauti ambazo
katika makala zijazo tutazizungumzia, lakini pia mimi binafsi ninazo njia zangu
mwenyewe(za kivitendo siyo nadharia)
nilizokwisha ziandaa mwaka huu mpya wa 2018 ambazo nitazitumia kusudi niweze
kuondokana na tatizo hili la kutokutimiza vyema malengo yangu niliyojiwekea
mwaka huu 2018. Baadhi ya njia na mbinu hizo nitawashirikisha wasomaji wangu kwenye
blogu hii kadiri mtakavyoendelea kusoma makala humu na katika blogu yetu nyingine
maalumu ya SEMINA ile ya kulipia
kiasi kidogo cha fedha sh. Elfu 10.
Baada ya kugundua
tatizo la ukosefu wa fedha za kutosha katika kutekeleza mipango yangu
mbalimbali, nimeamua kulitolea uvivu suala hilo na naamini mwaka huu wa 2018
mwishoni sitakuwa kama nilivyo hivi sasa. Nakusihi na wewe achana na njia zile
zile za kizamani ulizokuwa ukizitumia kila mwaka ambazo hazikuwa zikikupa
matokeo yeyote ya kuridhisha, hebu twende moja kwa moja kwenye mzizi wa fitina
tuache kumung’unya mung’unya maneno sijui.. oo…ooo… sijui nini..., twende tukazijue
moja kwa moja mbinu mbalimbali zitakazotuondolea tatizo la mzunguko hafifu wa
fedha mifukononi mwetu na kubakia kila siku tukiimba, vyuma vimekaza, vyuma vimekaza
mpaka tunamkwaza Rais wetu John Pombe Magufuli.
Kampeni zetu zote tangu ile ya mwanzo ya ‘Kuelekea utajiri’, ‘Jirudishie ukuu wako
tena’ au ‘Make yourself Great again’ na hii ya mwaka 2018 ya ‘Mzunguko mzuri wa fedha’ zote zitaenda sambamba zikiwa na lengo moja
tu la kukufanya wewe unayefuatilia programu zetu maisha yako kuwa bora, bora
zaidi kushinda vile yalivyokuwa hapo kabla.
.............................................................................
Vitabu vya Vya Self Hel Books Publishers sasa vinapatikana katika format zote, Hardcopy na pia Softcopy. Ikiwa unataka Hardcopy na upo Dar, piga namba 0712202244 au 0765553030 na utaletewa kitabu/vitabu mpaka ulipo. Mikoani agiza mtu au pia tunaweza kukutumia kwa njia ya mabasi.
Kama utataka softcopy ya vitabu hivi, tuma fedha pamoja na anuani yako ya email na tutakutumia kitabu/vitabu udownload kwenye email yako.
Vitabu zaidi na maelezo ya kina kuhusu vitabu vyote vya self help books fungua ukurasa ufuatao SMART BOOKS TZ
0 Response to "MZUNGUKO MZURI WA FEDHA NDIYO NJIA BORA ZAIDI YA KUFIKIA MALENGO YAKO MWAKA MPYA WA 2018"
Post a Comment