SABABU KUBWA KWANINI MWAKA 2017 SIKUFANIKISHA MALENGO YANGU YOTE NILIYOJIWEKEA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SABABU KUBWA KWANINI MWAKA 2017 SIKUFANIKISHA MALENGO YANGU YOTE NILIYOJIWEKEA


Sisi waandishi na hasa wale tunaoandika kuhusiana na malengo, maendeleo binafsi au hata mafanikio ya mtu binafsi mara nyingi tumekuwa na mazoea ya kupenda kuitumia nafsi ya pili, nikimaanisha kwamba huwa tunaandika kana kwamba sisi wenyewe hatuhusiki, tunajifanya ‘waalimu’ kupita kiasi, kumbe na sie kwa namna moja ama nyingine mambo mengi tunayohubiri yanatuhusu na tunatakiwa tuyaishi pia.

SOMA: Tayari malengo yako kiuchumi ya mwaka umeshayaandika mahali?

Waandishi, au hata mifano mingine tuseme kama waalimu, wachungaji, mashehe na viongozi wengine wa dini ijapokuwa wanawaasa waumini wao kuishi namna fulani ya maisha lakini na wao pia wanapaswa kila siku kujibidiisha kuishi aina hiyo ya maisha wanayohubiri na changamoto wanazokumbana nazo waumini na wafuasi wao ni zilezile wanazokumbana nazo wao wenyewe.

Ndio maana katika makala yangu ya leo nimeamua kuandika kuhusiana na nafsi yangu mwenyewe badala ya kuandika “ Kwanini mwaka 2017 HUKUFANIKIWA malengo yako yoye kama ulivyojiwekea” nikaandika, “ Kwanini mwaka 2017 SIKUFANIKIWA malengo yangu yote niliyojiwekea.

Kusema ukweli hakuna sababu moja unayoweza ukainyooshea kidole kwamba ndiyo inayohusika na watu kushindwa kutimiza malengo ya mwaka waliyojiwekea au hata ya muda wowote ule iwe ni ya saa, siku, mwezi au muongo. Sababu ziko nyingi isipokuwa tu kuna zile zilizokuwa kubwa kushinda zingine.

SOMA: Jinsi ya kupanga malengo ya biashara au maisha yanayotimizika kwa urahisi.

Na watu tofauti huwa sababu au changamoto hizo huwaathiri pia kwa viwango tofauti kulingana na mazingira yao yalivyokuwa tofauti. Kikwazo kilichonifanya mimi nishindwe kutimiza baadhi ya malengo yangu siyo lazima kiwe ndicho hicho hicho kilichokufanya na wewe kushindwa kutimiza malengo yako au mtu mwingine, mara nyingi hutofautiana.

Kama utakumbuka, kama wewe ni mfuatiliaji wa makala katika blogu hii ya jifunzeujsiriamali, wakati tunauanza mwaka wa 2017 tulianza na kampeni tuliyoiita, JIRUDISHIE TENA UKUU WAKO au Make Your Self Great Again, kampeni ambayo ililenga kumfanya mtu kuhuisha tena ubora wake aliokuwa nao zamani iwe ni katika nyanja ya kiuchumi, kiafya, kiimani na hata kimaisha kwa ujumla.

Niliandika kwamba ifikapo kipindi hiki kila mtu tuliyekuwa naye katika mwanzo wa kampeni hiyo basi aweze kuleta mrejesho wake ni kwa kiasi gani ameweza kufanikiwa malengo hayo ya kurudisha tena hali yake bora kama ilivyokuwa zamani. Hii inamaanisha ni kiasi gani umeweza kutimiza malengo uliyojiwekea ifikapo mwezi Desemba 2017.

SOMA: Uamuzi mgumu na muhimu kuchukua ili biashara yako izidi kukupa faida mwaka 2017.


Mimi binafsi nashukuru nimeweza kupiga hatua kubwa katika mambo yangu mbalimbali ingawa siyo yote kama nitakavyoeleza hapo baadaye, na nikiongea kwa niaba ya kampuni ya Self Help Books Publishers, tuliweza kufanikisha jambo kubwa kupitia kampeni hii, ya KUKAMILISHA kazi ya kutafsiri kitabu cha Think & Grow Rich kwa kiswahili.

Disemba, huu ni mwezi wa kutathmini na mara itakapoanza Januari kila mtu anatakiwa aanze na mambo mengine tena mapya au kufanya marekebisho kwa yale ambayo hakuweza kuyafanikisha kama alivyopanga. Unaanza mikakati mingine mipya na malengo mapya au kubadilisha mikakati kwa malengo yaleyale ambayo hukuweza kuyafikia.

SOMA: Malengo, Dira na Dhamira yako mwaka huu ni nini?, hujachelewa bado, jipange.

Sitaeleza sababu kubwa iliyofanya nishindwe kutimiza malengo yangu yote kwa asilimia 100% kama nilivyokuwa nimeahidi mwanzoni mwa makala hii na badala yake, kwanza nitataja tu sababu hizo kwa ujumla. Kumbuka sababu kama nilivyosema awali zipo nyingi na nitazitaja kwa wingi wake halafu sababu kuu iliyonifanya nishindwe na huwa inawazuia watu wengi wengine pia kufikia malengo yao kama wanavyotarajia nitaendelea kuicha kiporo.

Tafadhali nina sababu za msingi za kufanya hivyo kwa faida ya wasomaji wengi wa blogu hii, naomba uvute subira na ufuatane nami makala mbili au tatu zijao.

Kwa wiki hizi 2 kumalizia mwaka huu, nakuomba tuwe pamoja katika tathmini kubwa tunayokwenda kuifanya katika blogu hii, kuna mambo mengi tutashirikishana ili sote kwa pamoja tuweze kuuanza na kumalizia mwaka wa 2018 kwa mafanikio makubwa zaidi kushinda mwaka wowote ule huko nyuma.

SOMA: Usiogope mabadiliko ya maisha kwani ni kama plasta, ikishabanduka kidonda hupona chenyewe.


Ndani ya wiki hizi mbili ndipo tutaweza kujadili sababu kubwa kuliko zote inayowakwamisha watu mara kwa mara kutimiza malengo yao, sababu ambayo mimi binafsi sikuwa nimeigundua mpaka nilipokuja kuigundua rasmi wakati wa kampeni yetu ya mwaka 2017 baada ya kunikwamisha mara kadhaa pasipo kujua.

SABABU (14) KWANINI WATU HUWA TUNASHINDWA KUTIMIZA MALENGO TUNAYOJIWEKEA MAISHANI.

1. Kukosa utendaji.
Maneno matupu kamwe hayawezi kuvunja mfupa, anza kutekeleza mara moja kile ulichopanga kufanya kumbuka asiyeanza hawezi pia kumaliza!, jitume kwa moyo wako wote.

2. Kujiwekea malengo yasiyoeleweka
Kwa mujibu wa kitabu cha MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI ZA MATAJIRI, malengo yako yanapaswa kutimiza sifa kuu 5 mbazo ni haya; yaeleweke, yapimike, yatekelezeke, yawe ya uhakika na yawe na muda maalumu wa utekelezaji.

SOMA: Mambo 7 usiyoyajua kuhusu kitabu cha Mifereji 7 ya pesa na siri Matajiri wasiyopenda kuitoa.


3. Kuweka malengo madogo,
Malengo madogo madogo kila mtu anayaweza na hayawezi kukusisimua au kukupa motisha wa kuyatekeleza(always THINK BIG)

4. Kutokupanga mpango
Ukishindwa kupanga maana yake unapanga kushindwa. Mpango ni ramani inayokuongoza kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Unapanga vipi kukamilisha malengo yako? Orodhesha na kisha uwe na mikakati iliyokuwa wazi.

5. Kuahirisha mambo.
“Nitafanya kesho” ni sumu hatari sana kwenye malengo hata ikiwa yatatimiza vigezo vyote vitano vilivyotajwa hapo juu. Vunja vunja malengo yako katika sehemu ndogondogo ili yatekelezeke kwa urahisi.

6. Kukosa mtaji(pesa) au rasilimali za kutekeleza malengo yako.
Malengo na hasa yale ya kiuchumi au biashara au lengo jingine lolote maishani yanahitaji mtu uwe na rasilimali kiasi fulani ndipo uweze kuyatekeleza kwa ufanisi. Unapokosa mtaji huwa vigumu kuyafikia.

7. Kuwa na malengo mengi mno
‘Mfukuza kuku wengi huambulia manyoya mikononi’ fanyia kazi fanyia kazi malengo mchache au ikiwezekana moja kwanza mpaka likamilikeshani yanahitaji mtu uwe na rasilimali kiasi fulani ndip malengo mchache au ikiwezekana moja kwanza mpaka likamilike kwanza.

8. Kufanya vitu vingine nje ya malengo uliyojiwekea.
Kwa mfano kutumia muda mwingi kupita kiasi kwenye burudani kama vile kutazama TV, sinema, redio, mitandao ya kijamii nk.

9. Kusikiliza watu wengine wanaokukatisha tamaa.
‘Weka pamba masikioni’, usisikilize sauti hasi zinazokukatisha tamaa.

10. Kuwa na fikra hasi
Badala ya kupoteza muda mwingi ukilalamika, utumie muda huo na nguvu zako kujifunza mambo mapya yanayohusiana na malengo uliyojiwekea ili uyakamilishe kwa ufanisi.

11. Ubinafsi uliopindukia
Usifikiri kujijali mno mwenyewe kutakusaidia kitu, ili ukamilishe malengo makubwa na muhimu unahitaji msaada kutoka kwa watu wengine pia na ni vigumu watu kukusaidia ikiwa wewe huna tabia ya kusaidia wengine. Kama hujawekeza kwa watu wengine na wao hawawezi kuwekeza kwako.

12. Kuzungukwa na watu wasiokuwa na malengo.
Ndege wanaofanana huruka pamoja. Mara zote kaa na watu wanaopenda kutimiza malengo yao.

13. Kukata tamaa mambo yanapokuwa magumu.
Hakuna kitu chochote kile kizuri kinachopatikana kiurahisi (so NEVER GIVE UP)

SOMA: Kamwe Kamwe Usikate Tamaa(Never Never Give Up)


14. Woga, wa kufeli au hata wa kufanikiwa.

Woga humfanya mtu kuwa na visingizio vingi huku akishindwa kutimiza malengo yake sawasawa.

................................................................

Ndugu msomaji wa blogu hii, blogu yako ya jifunzeujasiriamali ina makala nyingi zinazoelimisha mbinu mbalimbali za biashara, ujasiriamali na maendeleo binafsi ya mtu, ukitaka kujifunza kwa kina zaidi, tunavyo vitabu vya kulipia na vya bure pamoja na semina katika blogu ambayo nayo ni ya kulipia.

Kupata vitabu tembelea SMARTBOOKSTZ au wasiliana nasi kwa namba 0712202244  au Whatsapp  0765553030

Kupata kitabu kizuri cha Jinsi ya kujifunza elimu ya PESA kwa ufanisi, pamoja na vitabu vingine 25 bure kabisa bila malipo yeyote jiunge kwa email ukishabonyeza maandishi yafuatayo, JIUNGE NA BLOGU HII HAPA.

Lipia DARASA LA SEMINA hapa, upate na kitabu cha MICHANGANUO free.

Asante sana nikutakie sikukuu njema za mwisho wa mwaka huu 2017 kuelekea 2018     


0 Response to "SABABU KUBWA KWANINI MWAKA 2017 SIKUFANIKISHA MALENGO YANGU YOTE NILIYOJIWEKEA"

Post a Comment