Niiahidi kumalizia maswali
yaliyoulizwa na wasomaji wetu siku chache zilizopita na maswali niliyokuwa
naendelea nayo yalikuwa ni maswali kutoka kwa msomaji wetu wa Songea Mkoani
Ruvuma. Tayari maswali yake mawili tulishayajibi na niliahidi kujibu swali la tatu
hapa, ila Swali hilo la tatu sitaweza kulijibu kutokana na kugundua kwamba
linafanana mno na lile la pili hivyo nadhani kwa kusoma majibu ya swali hilo la
pili lililosema, Kijana waumri mdogo anaweza akaanzisha
biaashara kubwa ikafanikiwa? Atakuwa
amesharidhika.
Leo nitajibu swali jingine la msomaji mmoja yeye hakutaja
anatokea wapi, aliuliza kama ifuatavyo;
“Habari
ya jioni, mimi ni mkulima nina heka 3 za matikiti maji. Yamebakiza siku 7
kukomaa na yako vizuri sana! Natafuta soko kwenye kiwanda cha Bakhresa cha
juisi za matunda ila nashindwa kwani sina mawasiliano na hichi kiwanda. Unaweza
ukanisaidia?”
Kabla sijaweka majibu niliyompa msomaji huyu kwanza
nitaelezea kidogo kuhusiana na dhana nzima ya utafutaji wa masoko ya biashara
zetu iwe ni bidhaa, ama huduma na bila ya kujali huduma na bidhaa hizo
zinatokana na shughuli za shamba, kilimo na ufugaji au biashara za kawaida tu
za uchuuzi, viwanda na biashara za jumla jumla.
Kumbuka pia kwamba shughuli yeyote ile unayoifanya ni
biashara ilimradi tu lengo lako liwe ni kukidhi mahitaji fulani ya wateja. Hii
ni kwa mujibu wa maelezo ya biashara katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA
NA UJASIRIAMALI. Katika kitabu hicho hicho pia, kinazungumzia mchakato mzima wa
biashara kuwa ni mchakato wa kutafuta soko au “Marketing” kwa kimombo.
Hivyo kwa kifupi tu niseme kwamba unapotaka kuyakidhi
mahitaji fulani ya wateja ni lazima tangia mwanzo mpaka mwisho wa mchakato wako
huo uhakikishe kwamba unalo soko la uhakika la bidhaa au huduma zako.
Vinginevyo biashara au mchakato wako huo utakuwa na uwalakini na hapo sasa
ndipo unakuta mtu unaanza kujiuliza mwenyewe, “Mungu wangu tu, ona nitauza wapi bidhaa zangu hizi, zinanidodea.”
Kitu ambacho ni muhimu sana kufanya kama mjasiriamali au
mfanyabiashara unayechipukia ambacho kitakusaidia sana kuhakikisha unalifahamu
barabara soko lako unalolenga kuwauzia bidhaa au huduma zako, ni kufanya
utafiti wa biashara yako au unaweza kufanya mchanganuo wa biashara yako.
Tafadhali vitu hivi visikuchanganye hata kidogo, unaweza kusema; “huyu
mtu anazungumzia utafiti mara mchanganuo wa biashara, sasa nishike kitu gani?”
Ndugu msomaji wangu wala visikuchanganye, utafiti wa
biashara na mchanganuo wa biashara au mpango wa biashara ni kitu kimoja
hichocho na tena unaweza ukakutana na majina mengine mengi mahali kwingine kama
vile, mpango mkakati wa biashara, andiko la biashara, andiko la mradi, upembuzi
yakinifu, business plan nk. ni majina tu,
na kitabu kimeyaelezea vyema pamoja na tofauti zake ndogondogo.
Hakuna tofauti na jinsi ulivyokuwa mchele, mchele baada
ya kupikwa unakuwa na majina meengi, utakuta kuna wali, ubwabwa, biriani,
pilau, mseto na majina chungu nzima lakini bado ni mchele tu uleule ambao lengo
la kuuandaa ni ili watu waweze kula na kushiba. Halikadhalika mchanganuo nao
lengo lake pamoja na mengine mengi ni kutathmini au kubaini soko lako kwa
uhakika kabisa kabla hata wateja wenyewe hawajagundua kwamba utawauzia kitu
gani.
MAJIBU
YA SWALI
Jinsi
mkulima huyu atakavyoweza kupata soko la kuuza matunda yake ya matikiti maji
katika viwanda vya kutengeneza juisi vya mwekezaji Said Salim Bakhresa.
Ndugu mkulima ni kweli kwamba Bakhresa Food Products imeanzisha
viwanda kadhaa vinavyozalisha juisi kutokana na matunda halisi yanayolimwa
hapahapa nchini kama vile maembe, mananasi, pera, passion, na nyinginezo ingawa
sina uhakika sana ikiwa kama wanazalisha pia na juisi inayotokana na tikiti
maji(water mellon). Nasema sina uhakika na juisi za matikiti kutokana na uzoefu
wangu binafsi kwani sijawahi kuziona zikiuzwa madukani hata aina kutoka nje ya
nchi.
Sababu kubwa inayotolewa kwanini juisi ya tikiti maji
isiwepo kirahisi sokoni kama ilivyokuwa kwa matunda mengine kama embe, nanasi
na passion ni kuwa, juisi ya matikiti maji ni vigumu kuihifadhi katika vifungashio
ikadumu kwa muda mrefu pasipo kupoteza uhalisia wake hasa ile hali ya urojorojo.
Kwa kweli sijafanya utafiti kufikia hatua ya kuonana na
wahusika katika viwanda hivyo vya makampuni ya Bakhresa lakini kwa taarifa
nilizokuwa nazo, kampuni ya Bakhresa ina viwanda vya juisi za matunda maeneo mbalimbali
nchini yakiwemo Dar es salaam, Pwani na katika mikoa ya kanda ya ziwa. Kwa
mfano kuna kiwanda cha juisi kilichopo Mwandege Mkuranga katika mkoa wa Pwani
na kwa msimu ulioanza Novemba mwaka huu kwa mujibu wa afisa uhusiano wa kampuni
hiyo bwana Hussein Sufiani, kiwanda kina matarajio ya kununua matunda kutoka
kwa wakulima yenye thamani ya shilingi zipatazo bilioni 7 sawa na zaidi ya tani
70,000 za matunda mbalimbali.
Kama uonavyo ndugu msomaji, mzigo tani zaidi ya sabini
elfu siyo mchezo hata kidogo, hapa unahitajika utaratibu uliopangika vizuri
baina ya wadau wote wanaohusika yaani wakulima wenyewe, uongozi wa kiwanda
pamoja hata na serikali au vyama vinavyohusiana na maslahi ya wakulima katika
eneo husika na siyo tu suala la mtu mmoja au wawili kuamua wanataka kwenda
kuuza matunda katika kiwanda.
Si kama nabeza mkulima mmoja mmoja kuuzia kiwanda matunda
hapana, ila ninachotaka kueleza hapa ni kwamba, mahitaji ya kiwanda chochote
kile ni makubwa, huwezi kufungua kiwanda kikubwa ukategemea kubangaiza
malighafi, ni lazima ujipange aidha kwa kuzalisha malighafi zako binafsi za
kutosha au ukawa na wateja kabisa wanaoeleweka watakaoingia na wewe mkataba wa
kudumu kukuuzia malighafi kusudi kiwanda kisije kikakaukiwa malighafi njiani,
kwani itakuwa ni bonge la hasara huku ukiwa umeshawekeza mabilioni yako kibao
ya shilingi.
Ndugu yangu kama nilivyotangulia kusema sina nia ya
kukukatisha tamaa, ila kukueleza kile kilichokuwa wazi, ushauri wangu ni kwamba
kwa kuwa umechelewa sana kuhakikisha soko la matikiti yako mpaka yanafikia
kukomaa ndipo unaanza kutafuta soko, hata hivyo kiasi cha matikiti uliyokuwa
nayo ni kidogo sana kuogopa kuwa utashindwa kuyauza. Kwa heka mbili, tatu
unaweza hata kuyapeleka masoko mbalimbali yaliyoko Dar na yakaisha kwa muda
mfupi tu.
Kuhusiana na soko la makampuni tanzu ya Bakhresa, nadhani
ni vizuri zaidi ukatafuta mawasiliano nao kupata uhakika iwapo kama wananunua
au la, au pia unaweza ukawasiliana na chama cha wakulima wa matunda Tanzania
UWAWATA wakakupa ufafanuzi zaidi kwani mara nyingi viwanda vikubwa huwa
wananunua matunda kutoka kwa wakulima waliosaini nao mikataba maalumu.
Ulichokifanya ni sahihi kabisa, kufanya utafiti wa soko
la matikiti yako, ila kosa moja dogo ulilolifanya ni kuchelewa kufanya utafiti
wenyewe, kazi hii ulipaswa kuifanya kabla hata haujaanza kuandaa shamba kwa
ajili ya kuotesha mbegu za matikiti yako. Hata hivyo utakuwa umeshajifunza, wakati
ujao hakikisha kazi hii nyeti ya kufanya utafiti wa soko la bidhaa zako
unaifanya mapema iwezekanavyo na unaendelea kufanya hivyo katika kila hatua
utakayoendelea kuwa mpaka umeuza bidhaa zako zote. Na katika utafiti huulizi
sehemu moja tu, kwa mfano unakuja kuuliza kwangu, majibu nitakayokupa changanya
na mengine utakayopata sehemu nyingine na mwisho wa siku unakuwa na taarifa
zote muhimu zitakazokuwezesha kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa/huduma zako.
Kumbuka soko ni kitu muhimu pengine kushinda vigezo vingine karibu vyote kwenye
biashara na si zoezi la siku moja bali mchakato tangu unaanza wazo mpaka unauza.
……………………………………………………………......
Ndugu msomaji wangu, mwezi huu wa Desemba ni mwezi wa
kutathmini malengo yetu tuliyojiwekea katika mwaka huu unaomalizika wa 2017
kuelekea mwaka 2018. Nakuomba tuwe pamoja kwani kuna mambo mengi tutakumbushana
na mengine tutapanga hapahapa pamoja kama tulivyofanya kipindi kinachomalizika
hata kama ikiwa yalikuwa ni mambo machache lakini naamini sote tulikuwa
tukifanya mambo kwa malengo.
Kwa vitabu zaidi au maelezo kuhusiana na hivi tembelea; SMART BOOKS TANZANIA
0 Response to "SOKO LA TIKITI MAJI KIWANDA CHA BAKHRESA CHA KUTENGENEZA JUIS ZA MATUNDA"
Post a Comment