Unaweza kushangaa nazungumziaje miwa jijini Dar es salaa
wakati maeneo kibao makubwa yapo sehemu mbalimbali nchini Tanzania kama vile
kule Morogoro, Mbeya, Tanga, Mwanza na Ruvuma ambayo mtu unaweza ukalima zao la
miwa tani kwa matani na kuisafirisha kuja hapa Dar es salaa kuiuza, sawa na
wafanyavyo wafanyabiashara wengi wa miwa wanaoleta miwa jijini kwa ajili ya
kutengeneza juis ya miwa ambayo hupendwa sana hasa nyakati za kiangazi kama
hizi.
Lakini lengo langu katika mfululizo wa makala hizi za
BIASHARA ZILIZOSAHAULIKA au ZISIZOPEWA KIPAUMBELE KIKUBWA LAKINI ZINA FURSA
KUBWA YA KUTENGENEZA FAIDA, lengo hasa ni kuibua fursa ambazo zinawezakuwa zipo
lakini watu wengi hasa wa vipato vya chini hawazifahamu. Ndiyo ni kweli kilimo
cha zao la miwa siyo fursa iliyojificha, maeneo kibao mikoani miwa hulimwa kwa
ajili ya kutengenezea sukari na mingine kusafirishwa kwenda maeneo mengine
wasiyolima kwa wingi kama jijini Dar es salaa kwa ajili ya kutengenezea juisi
za miwa.
Katika miradi au biashara ninazodai zimesahaulika ninachowakumbusha
watu ni kwamba biashara inaweza ikawa ni ya kawaida sana lakini wewe kwa
kuongeza ubunifu fulani ukaifanya kuonekana kama vile ni biashara iliyosahaulika.
Kwa hiyo mimi mantiki yangu kubwa hapa ni kuibua ubunifu ambao kwa mazingira ya
kawaida mtu unaweza ukadhani hakuna fursa yeyote ile. Mfano ni mtu mmoja
nilikuwa nikipiga naye stori kuhusiana na miwa hii hii, nikamweleza, unajua
bustani ya miwa inaweza ikamuongezea mtu kipato kwa urahisi sana akiwa hapahapa
Dar. Lakini yeye alinibishia na kusema hivi, “wewe si mzima, ukalime miwa dar
wakati hapo Morogoro mashamba ya miwa yamejaa mahekari kwa mahekari utamuuzia
nani?”
Nilijaribu kumueleza kwanini nilikuwa nasema vile,
nikamuambia kwamba, miwa ni zao ambalo soko lake halina mashaka, unapofika
sokono mara nyingi utawakuta wanunuzi wamepanga foleni wakisubiri kununua miwa
kwa ajili ya kwenda kutengeneza juisi ya miwa na hamna msimu wowote utakuta miwa
ikidoda sokoni iwe kiangazi au masika. Na nikamweleza pia kwamba ninaposema
bustani za miwa jijini Dar es salaam simaanishi mtu akaweke bustani ya miwa
maeneo kama kariakoo, posta, buguruni au hata Manzese hapana, haiwezekani.
Juisi safi na halisi ya miwa.
|
Dar ina maeneo kibao ambayo bado yanafaa kwa kilimo cha
bustani za mbogamboga na matunda. Watu wanaoishi kwa mfano maeneo ya Kiluvya,
Kimara, Mbezi, Chanika, Kigamboni, na maneo yote ya pembezoni mwa jiji wanaweza
kuwa na bustani ndogondogo za matunda na mboga au hata miwa kama
ninayozungumzia.
Kwanini
miwa? Pamoja na soko lake la uhakika jijini Dar, lakini miwa
haihitaji uangalizi mkubwa sana kama yalivyokuwa mazao mengine ya bustani kama
mbogamboga na matunda. Huhitaji mbegu ya kisasa sana kwani unaweza kuchagua tu muwa
mzuri ukaukatakata vipande na kupanda pingili zako. Tatizo kubwa katika kilimo
cha bustani ya miwa ni mchwa, lakini mchwa wanaweza kudhibitiwa kirahisi sana
kwa kutumia njia za asili kama vile majivu au kwa kununua dawa kidogo
inayopimwa katika maduka mengi ya pembejeo za kilimo ukachanganya na maji kisha
ukapaka pingili za muwa kabla hujazipanda ardhini.
Muwa hauhitaji maji mengi sana na unaweza, ukishaota
ukaweka matandazio kuzuia maji mengi ardhini kuchukuliwa na jua kama mvuke.
Ukishapanda wewe kazi yako kubwa labda ni kuja kupalilia tu siku moja moja
mpaka unavuna. Unaweza ukaweka mbolea kidogo ya kuku, ngombe au hata mbolea za
chumvichumvi kama vile UREA, CAN nk. Muwa hukomaa baada ya miezi 12, mwaka mmoja mpaka miezi 16 na utajua kama muwa umeshakomaa pindi majani yake yanapobadilika na kuwa rangi ya njano na muwa huwa na urefu wa mita 2 mpaka mita 4.
Mradi kama huu si kwamba ni biashara unayoweza ukasema
utaitegemea moja kwa moja kiuchumi, kama niliyotangulia kusema mwanzoni kwamba
biashara hizi naziita biashara zilizosahaulika na lengo
lake hasa ni kuongeza tu mzunguko wa fedha katika kaya au familia kwani katika
familia kunapokuwa na njia tofautitofauti na nyingi za kuongeza kipato mwisho
wa siku familia inaondokana na umasikini kuliko kutegemea chanzo kimoja tu cha
mapato.
Kama muwa hauhitaji muda mwingi kuukuza wala gharama
kubwa, lakini mwisho unapokomaa unakuwa na uwezo wa kupata hapo hata shilingi
elfu 5, sasa kwanini usijaribu kupanda kama una kaeneo nyumbani kwako? Licha ya
kupata pesa lakini pia muwa unaweza kuliwa na wanafamilia kama chanzo kizuri
cha madini na inasemekana pia maji yake yanasafisha figo.
Kumbuka pia kwamba mwaka huu niliahidi kuwa katika makala
zetu kwenye blogu hii na kampeni zetu
zote katika mitandao ya kijamii tutahamasisha zaidi njia za kuongeza mzunguko
wa fedha katia biashara zetu na mifukoni mwetu kwa ujumla katika kutimiza
malengo yetu.
Ndiyo maana hata katika GROUP LETU LA WHATSAPP LA
MICHANGANUO ONLINE kila siku pamoja na kuwa na masomo ya MICHANGANUO lakini pia
tunakuwa na somo la KUONGEZA MZUNGUKO WA FEDHA katika biashara zetu na
kujifunza nidhamu ya hali ya juu ya kutunza fedha.
0 Response to "BIASHARA NDOGO ZILIZOSAHAULIKA: BUSTANI NDOGO YA MIWA JIJINI DAR ES SALAAM"
Post a Comment