Binadamu wote hakuna hata mmoja anayeweza
akadai kutopitia vitu hivi katika muda wa maisha yake, sote tumepitia huko na
hata ikiwa bado basi ujue kuna siku. Mambo magumu maishani, mikasa ya kukatisha
tamaa na maanguko kwenye yale tunayopanga kuyafanya ni vitu ambavyo hata wale
watu wanaodhania kwa kuishi kwa tahadhari ya hali ya juu kupitiliza wanaweza
kuvikwepa huja kugundua kumbe hawako sahihi. Unaweza leo hii ukawa unafurahia
neema, lakini kumbe hujui kesho kuna janga gani litakukuta.
Ni nani aliyefahamu katika harakati za marudio
ya uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni msichana asiyekuwa na hatia
Ackwilina Ackwiline angefikwa na mkasa wa kifo akiwa ndani ya basi akielekea
kurudisha fomu za maombi yake ya kazi? Janga limetokea na kwa hakika maumivu na
uchungu walio nao ndugu wa huyu binti hasa wazazi wake hauwezi kupimika.
Wanaona ni kama vile hakuna tena njia yeyote ya kutokea, wanahisi hawana nguvu
tena ya kusonga mbele na maisha yao, kila kitu kimegeuka na kusimama kimya,
haviendi mbele wala kurudi tena nyuma!
Ukweli wa mambo ulivyo ni kwamba sisi
binadamu uwezo wetu wa kuzuia mambo mabaya au mikosi kutukuta ni mdogo sana,
ingawa yapo mengine yanayoweza kusababishwa na uzembe au kwa makusudi na
wanadamu wenzetu. Na huo ni upungufu ambao sisi kama binadamu hatuwezi
kuubadilisha kirahisi. Sasa binadamu bada ya kupitia magumu yote hayo na mikasa
anapaswa kufanya kitu gani?
Katika mazingira kama haya wapo wanaoshindwa
kabisa kukabiliana nayo wanaamua hata kujitoa uhai au wanapatwa moja kwa moja
na matatizo ya akili, msongo wa mawazo na wakati mwingine matatizo ya moyo au
kiharusi(stroke). Lakini kumbuka pia kwamba katika kila anayekumbwa na mikasa
ya kutisha namna hii, maanguko, ugonjwa usiopona, kutengwa na jamii kwa sababu
yeyote ile au njaa na majanga ya kila aina, kunakuwa na njia iliyojificha nyuma
ya majanga hayo ambayo kama utaweza kuiona basi unaweza tena kupona na kurudia
hali yako ya kawaida kama ulivyokuwa zamani, na hii ndiyo imekuwa ikisababisha
watu wengi hata baada ya kupatwa na mikasa ya kutisha maishani lakini baadae
hupona na kupata tena mpenyo upya wa maisha yao huku wakisahau kama waliwahi
kukumbwa na mikasa hiyo.
UNAPOKUMBWA
NA MIKASA AU MAGUMU YEYOTE MAISHANI.
Fahamu kabisa ya kwamba sisi binadamu
tulivyoumbwa tumewekewa uwezo wa ajabu ndani yetu wa kupona tena taratibu
kutoka janga lolote lile na kurudia hali zetu za kawaida kama vile minyoo wa
ardhini walivyo, unapomkatakata kwa jembe ukidhani tayari umemmaliza kabisa,
vile vipandevipande huenda tena kujikuza upya na kuwa minyoo kamili inayoweza
kutembea kama zamani. Pamoja na maumivu yote anayoyapata unapokuwa
ukimkatakata, lakini kumbe ndiyo njia yake ya kujiongeza.
Ili kuondokana na hali ya magumu, mikasa na
maanguko ya kimaisha, jiulize maswali yafutayo;
1. Najifunza
nini kutokana na mkasa/tukio hili?
2. Nitatumia
mbinu gani au njia gani kukabiliana na tatizo kama hili wakati ujao kama
litanitokea tena?
3. Kuna
njia/fursa au mpenyo wowote unaoweza kujitokeza katika mazingira ya tukio hili?
Kwa kadiri utakavyojitibu mapema(kukubaliana)
na hali halisi iliyokuwepo mbele yako ndivyo na uwezekano wa kurudia hali yako
ya kawaida au kupona nao utakavyoharakishwa. Uwezekano tena wa kurudia hali
yako ya kuishi kwa furaha, mafanikio, afya na amani. Vitu vilivyotoweshwa na
giza nene la mikosi, dhuluma, maanguko, mikasa na roho mbaya ya binadamu
wanaojipenda wenyewe kuliko wenzao.
Wakati mwingine muda unahitajika, waswahili
husema “Muda ni dawa ya kila kitu”,
unahitaji kupata muda wa kupona majeraha hayo mabaya. Huhitaji wala mtu yeyote
kukushauri ni njia ipi uifuate zaidi ya ujasiri wako mwenyewe, kuamua uendelee
kuteketea katika maanguko haya yaliyokwishatokea kwa kuruhusu magonjwa ya moyo,
kiharusi na kujinyonga au uamue kupona taratibu njia pekee Mwenyezi Mungu aliyotupa
Wanadamu ya kujiondoa katika magumu, mikasa na maanguko ya kila aina
yanayotokea hapa Duniani.
Maisha yeyote mtu utakayoamua kuishi yawe ni
ya furaha, amani, mafanikio, utajiri, uchungu, magumu, kukatisha tamaa, yote
yataamuliwa na jinsi utakavyokabiliana na nyakati hizi chungu katika maisha.
Fahamu kuwa haupo peke yako, mimi, yule na hata mwingine tumewahi kupitia
nyakati ngumu kama hizi. JIPE MOYO
UTASHINDA!!!
0 Response to "UNAWEZAJE KUYAKABILI MAGUMU, MAANGUKO NA MIKASA YA KUTISHA MAISHANI KAMA HII?"
Post a Comment