Mamilioni ya watu kote dunani tangu kuumbwa
kwa ulimwengu huu wamekuwa na ndoto kila mtu na za kwake. Wapo walioweza
kuzitimiza ndoto zao na vilevile wengi walikufa na kuzikwa na ndoto zao kabla
hawajafanikiwa kuzitimiza. Hii inamaanisha kwamba kama ndoto au malengo
yangelikuwa ni vitu vya kushikika mfano wa magunia ya viazi, basi makaburi
yangelijaa siku nyingi na duniani pengine pasingelikuwa tena na mahali pa kuzikia.
Mamilioni ya watu wenye ubunifu na vipawa vya
aina mbalimbali wamekuwa wakiishi na
ndoto zao wanazotamani kuzitimiza lakini kuna kitu kinachowavuta nyuma na
kuwazuia kuzitimiza. Wana ndoto za kuanzisha biashara, kujenga nyumba, kununua
kiwanja, kutunga kitabu, kupata mafunzo fulani, kuimba, kujifunza upishi,
kwenda ulaya, kumiliki gari, kuoa, kuwa kiongozi wa siasa, kufanya hija maeneo
matakatifu nk.
Lakini cha kushangaza ni kwamba wakati
asilimia kubwa ya watu hao wakihagaika(wakistruggle) kutaka kutimiza ndoto zao
hizo bila mafanikio, wapo baadhi ya watu siyo wengi sana lakini tunaowaita
waliofanikiwa sana ambao wao huweza, tena kwa urahisi sana kutimiza malengo yao
wanayojiwekea. Kwa kweli kwa macho ya kawaida watu hawa huwa tunaona kama vile
wamepata mafanikio kirahisi sana. Hivi ni kweli hupata mafanikio kirahisi namna
hiyo? Na kama hivyo ndivyo basi wanatumia mbinu gani?
Katika makala hii ya leo nitakuelezea vitu vine
4 ambavyo watu wenye mafanikio makubwa
huwa wanaviamini ili hali watu wa kawaida huwa wanaviona kama havina maana
yeyote kwao. Vitu hivyo ndivyo huwapa nguvu ya kutimiza malengo yao haraka na
kwa urahisi na zaidi ya hayo nitakueleza pia namna mtu unavyoweza ukazitumia
siri hizo 4 kufikia malengo yako ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikukwepa.
Nadhani umewahi kusikia stori nyingi za watu
waliowahi kuhangaika na maisha na kisha wakati fulani wakaja kutoka kabisa
kimaisha . Mifano hata hapa nchini kwetu
tunayo, watu kama akina Mzee Reginald Mengi, Eric Shigongo, Diamond platnumz,
na wengineo wengi, hawa ni baadhi tu na nimetaja wajasiriamali lakini wewe
unaweza ukawa na mifano kutoka sekta nyinginezo kama vile siasa, elimu nk.
Kulingana na maelezo ya wajasiriamali hao nyakati mbalimbali katika safari zao
za maisha, kabla hawajafanikiwa waliweza kuanguka wakainuka tena, wakaanzisha
biashara hii na ile, wakaacha, wakaanzisha nyingine tena mpaka pale walipokuja
kugundua vitu hivi na kuviamini ndipo wakaweza kutoka moja kwa moja.
Siyo ajabu hata kidogo unakuta mtu
anakuambia, kabla hajafanikiwa alianzisha biashara hata zaidi ya 10 ambazo zote
zilikufa au kumletea hasara lakini moja tu au mbili zikaja kumletea mafanikio.
Watu wengi wa kawaida wamekuwa wakifikiria kimakosa kwamba mafanikio maishani
hutokana na kile mtu anachokijua kwa mfano watu hupima mafanikio ya mtu kwa
kutumia kigezo cha elimu lakini ukweli ni kwamba elimu ni njia tu ya
kufanikisha mtu aweze kupata mafanikio. Elimu isipotumika vizuri haina uwezo wa
kumfanya mtu aliye nayo kufanikiwa hata angelikuwa na digirii ngapi. Wala
mafanikio pia hayawezi kutokana na wale watu unaowajua au na kipaji
ulichozaliwa nacho ikiwa hujachukua hatua zozote zile za kukigeuza kipaji hicho
kuwa pesa.
Sasa basi ni vitu gani hivyo wanaofanikiwa
huamini na kuwatofautisha na watu wa kawaida? Kama nilivyotangulia kusema na
kuwataja baadhi ya wajasiriamali waliofanikiwa hapa nchini Tanzania, hebu wewe
mwenyewe wachunguze. Bila shaka utagundua kuwa, karibu kila mmoja wao alianza
taratibi, kidogokidogo mpaka akafanikiwa,
hakuna hata mmoja wao aliyelala tu usiku na kesho yake asubui kuamka akiwa
tajiri, tena basi cha kushangaza ni kwamba hakuna hata mmoja aliyekata tamaa njiani
licha ya vikwazo vingi walivyokutana navyo. Ni kitu gani kilichowapa nguvu
wasikate tamaa na kuachana na biashara zao?
Unapowafuatilia kwa undani utagundua kwamba,
kile kilichowapa nguvu ni kile WALICHOKUWA
WAKIKIAMINI, basi. Na kukosekana kwa kichocheo hiki ndiko kunakosababisha
makaburi au dunia kujaa mno ndoto na malengo yasiyotimizwa. Kile mtu
anachoamini au kwa maneno mengine MTAZAMO WA AKILI(Mindset) ndiyo “petrol” au nishati inayochochea
mafanikio kutokea, Wajasiriamali niliowataja na watu wote duniani walio na
mafanikio makubwa, mafanikio yao hayo yalitokana na kile walichokiamini akilini
mwao.
Kwa mfano Eric Shigongo katika historia ya
maisha yake aliwahi kusema kwamba, alianza kufanikiwa baada ya kufuta akilini mwake
mawazo aliyokuwa amepandikiziwa angali mdogo kwamba yeye ni duni na hawezi
kufanikisha jambo lolote lile la maana. Alibaini pia kwamba hata majina mabaya
aliyoitwa utotoni yalikuwa na mchango hasi katika maisha yake na hivyo alipaswa
kuyapuuzilia mbali ili kuwa na mtazamo chanya mpya uliomwezesha hatimaye kuja
kupata mafanikio ya maana kiuchumi na kimaisha kwa ujumla.
Ukiwa uliaminishwa tokea utotoni kwamba
umetokana na familia duni na hivyo huwezi kufanikiwa, na kweli ikiwa
hautachukua hatua za makusudi za kufuta imani hiyo akilini mwako, itakuwia
vigumu sana kufanikiwa. Basi bila kuzidi kuchelewa hebu twende sasa nikakupe
vitu hivyo vinne 4 wanavyoamini wale wanaofanikiwa katika maisha.
1. Hakuna
mafanikio ya ghafla,
Ni lazima uanze kidogokidogo ndipo baadae
uweze kumalizia na kikubwa. Ingawa kweli wapo watu wanaochukua muda mfupi
kuliko wengine kupata mafanikio, lakini kwa ujumla mafanikio yeyote yale
makubwa ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu. Hatari ya kuamini katika
mafanikio ya haraka ni kwamba utakata tamaa mara tu utakapokutana na kikwazo
hata ikiwa ni kidogo, hii tena ni sababu nyingine ya dunia kujaa ndoto nyingi
zisizotimia kwani watu wengi hujaribu mara moja, na wanapoanguka, huacha mara
moja wakiamini wazo lao halikuwa sahihi.
2.
Ukikosea mara ya kwanza hujashindwa bado kwani siyo jaribio lako la mwisho.
Kuna mfano mmoja maarufu wa mgunduzi wa taa
hizi za umeme tunazotumia mpaka leo hii (balbu) kufeli karibu mara 9999 na mara
ya elfu 10 ndipo akaja kufaulu. Angeachilia pale pale mara ya kwanza tu
alipofeli, leo hii pengine dunia ingelikuwa bado inatumia vibatari na taa za
mafuta ya wanyama kama zama hizo. Mbaya zaidi katika imani hii namba 2 ni pale
mtu unapokosea na kisha watu wengine kukubeza; “Hee! Ulishindwa kiangazi masika utaweza?”, “Umeshindwa na taa ya Mungu
mchana, utaweza na taa ya Mzungu usiku?”
nk. hayo ni baadhi tu ya maneno watu hutumia kuzidi kuwavuja moyo wenzao
wanaoshindwa jambo. Na wewe ukiwa na mtazamo potofu(negative mindset) utakata tamaa kweli na kujiona hufai, huwezi na
wala hutokaa uweze tena kitu maisha yako yote.
Lakini wewe badala ya kuvunjika moyo, hebu
jaribu kutofautisha utendaji wako na uwezo mkubwa uliojificha ndani yako ambao
kama utaamua kuutumia kila mtu anaweza akashangaa. Jiulize tena, ni nani
aliyezaliwa akiwa anajua kusema, kuandika au kuhesabu? Vyote tulikuja kujifunza
siyo? Aliye na mtazamo sahihi wa akili huamini kuwa, duniani hakuna aliyezaliwa
akiwa anafahamu kitu, kila taaluma duniani inaweza kufundishika na mtu yeyote
yule ana uwezo wa kujifunza taratibu mpaka akawa bingwa kabisa katika fani
yeyote ile. Uwezo wa akili ya binadamu yeyote yule ni wa ajabu sana kiasi
kwamba hakuna asiloweza kujifunza akaelewa.
3.
Ili ufanikiwe fanya kile unachokipenda.
Huwezi kufanikiwa katika shughuli usiyoipenda
na usiweke malengo yako kwenye pesa kwanza bali fanya kwa uaminifu kile kitu
unachokipenda zaidi kiasi kwamba watu macho yao yote yakutazame wewe. Watu wa
kawaida hudhani kimakosa kwamba wanaofanikiwa hufanya kwa kujilazimisha vitu au
kazi wasizozipenda mpaka wanafanikiwa, kumbe ukweli siyo hivyo kabisa. Huwezi
kufanikiwa kwa kufanya kitu usichokipenda.
4. Mafanikio
siyo kupaa tu, kuna kuanguka pia.
Kwa mfano kwenye Ujasiriamali tunajifunza kwamba,
tunapochukua hatari katika biashara kuna mambo mawili, kupata faida au kupata
hasara, na vyote viwili kila kimoja kina
nafasi sawa ya kutokea. Hii inamaana kwamba unapopanga kufanikiwa vilevile
panga na kuanguka. Mara nyingi watu wanaoanguka na kuinuka wakaendelea na
safari ndio ambao huja kuibuka washindi mwishoni.
………………………………………………
Mpenzi msomaji wa blogu hii, tulikuwa kimya
kidogo kwa siku chache lakini sasa tumerudi tena na kampeni yetu ya kuhakikisha
MZUNGUKO CHANYA WA FEDHA KWENYE BIASHARAZETU UNADUMISHWA inaendelea kama kawaida hapa bloguni, ndani ya GROUP LA
WHATSAPP LA MICHANGANUO ONLINE, katika blogu ya private ya MICHANGANUO na
katika EMAIL LIST yetu.
Usajili katika group unaendelea na kuna offa
mpya zimeongezwa sambamba na maboresho au updates kadhaa katika offa za zamani
bila kusahau kile kifurushi maarufu cha michanganuo 3 ya kuku. Vile vile
nichukue fursa hii kutangaza kwamba kitabu chetu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA
DUKA LA REJAREJA kimefanyiwa maboresho makubwa kwa kuongezewa sura yenye mfumo
mpya wa usimamizi wa duka la rejareja usioruhusu kabisa msaidizi kumuibia
tajiri(2 IN 1 SYSTEM).
Aidha mfumo huo utatolewa peke yake (bila
kitabu) free katika GROUP LA WHATSAPP LA
MICHANGANUO ONLINE. Pia ikiwa uliwahi kununua kitabu hiki na ungependa
tukutumie softcopy ya mfumo huo bure, tuma anuani yako ya email kwenye namba
0712202244.
Ndani ya GROUP LA MICHANGANUO ONLINE tunaendelea
na ratiba yetu kama kawaida, makala za kila siku za Michanganuo pamoja na
Mzunguko chanya wa fedha.
0 Response to "WANAOFANIKIWA KATIKA MAISHA HUAMINI VITU HIVI (4) VINNE "
Post a Comment