NATAKA KUFUNGUA BIASHARA YA STESHENARI MTAJI MILIONI 1.5 NIFANYEJE? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NATAKA KUFUNGUA BIASHARA YA STESHENARI MTAJI MILIONI 1.5 NIFANYEJE?


STESHENARY

Kila siku tumekuwa tukiendelea kupokea maombi ya ushauri na utatuzi wa changamoto mbalimbali ambazo wajasiriamali hasa wale wadogo wanaotaka kuanza kufanya biashara mbalimbali hukutana nazo, nasi huwa tunawajibu na baadhi yake huwa tunaweka hapa katika blogu hii kwa manufaa pia ya wasomaji wengine. Leo hii kuna mwenzetu mmoja anataka kupata ushauri kuhusiana na changamoto anazozipitia kama mwenyewe alivyozieleza hapa chini;

Habari Rafiki,  
Natumaini hujambo na pole kwa majukumu,

Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 22. Najishughulisha na kazi ya uuzaji wa duka la Stationary, Pia kijana ninayependa sana kujali, kupata  taarifa mbalimbali za kibiashara, kuthamini na kuheshimu mawazo na ushauri wa mtu yeyote, wakubwa kwa wadogo, pia ninapenda sana na ninatamani kuwa na biashara yangu mwenyewe ila nina changamoto zinazonikumba katika ndoto zangu za kufanya biashara na kujiendeleza kibiashara, 

1.  Changamoto ya kwanza ni mtaji.
2.  changamoto ya pili ni Muongozo wa biashara.

Ambapo mimi napenda kufungua biashara ya Stationary.

Naomba ushauri wako mpendwa nifanyeje ili nipate mtaji wa kutosha kufanya biashara hii ambapo biashara hii inahitaji at list uwe na mtaji wa Tsh Milioni 5 ili uweze kufungua biashara hii. Nina kiasi cha Tsh M1.5

Na  kulingana na kiasi nilicho nacho hakiwezi kufungua biashara hii na ndoto yangu naona kama inaweza potea hivihivi.
mimi kama mtu ninayependa kupata taarifa na ushauri kutoka kwa watu mbalimbali leo nimewasilisha ndoto zangu kwako ili uweze kunisaidia japo wazo moja ama jingine.

Tafhadhali naomba ushauri wako.

MAJIBU.
Mpaka hatua uliyofikia kulingana na maelezo uliyoyatoa hapa, tayari unao uwezo mkubwa katika kufanya utafiti na mpango wa biashara yako ya steshenari unayotaka kuanzisha. Kwanza tu kitendo cha kutaka ushauri kinaonyesha kwamba upo kwenye hatua za utafiti au tuseme upembuzi wa kujua ni njia zipi zitakazokuwezesha kutimiza ndoto yako hiyo.

Na kuhusiana na changamoto ulizozitaja pia, zaidi ya asilimia 30% tayari umekwisha zitatua mwenyewe, hizo asilimia nyingine zilizobakia ni rahisi pia kuzifanyia kazi na kuzishinda endapo utatulia na kuwa na subira kwani hitaji muhimu zaidi tayari unalo ambalo ni uzoefu wa biashara ya stationery na pia unaonyesha unaipenda biashara hiyo.

SOMA: Kuanzisha biashara nikiwa chuoni bado nasoma, naomba ushauri nina wakati mgumu.

Hii changamoto ya mtaji isikupe homa sana kwani kila mtu anayeanzisha biashara mpya wakiwemo hata na wale unaoona wamefanikiwa sana, hakuna hata mmoja aliyeanza akiwa na mtaji wote kwa asilimia 100%. Sijajua kwa uhakika ikiwa hiyo steshenari unayofanyia sasa kama ni ya kwako au umeajiriwa lakini nadhani utakuwa umeajiriwa ndiyo maana umesema unataka kuanzisha ya kwako. Sasa ikiwa uliweza kudunduliza mshahara wako mpaka ukafikisha hiyo milioni moja na nusu, nakushauri endelea kutumia mbinu hiyohiyo ya kujiwekea akiba mpaka utakapohakikisha mtaji umetosha au angalao hata umefikia asilimia 70% kitu kama milioni 3 na laki tano hivi.

Kwanini nasema hivyo? Ukiwa hapo kwenye ajira, kumbuka ndio mahali pekee palipo na fursa kubwa zaidi kwa wewe kuweza kuongeza mtaji wako utoshe bila usumbufu mkubwa na kwa muda mfupi kushinda nje ya hapo. Utakapotoka hapo tu itakubidi uanze tena mchakato upya ambao si ajabu ndani ya mchakato huo na hiyo milioni 1 na nusu ikakatika njiani hujafanya chochote cha maana. Hakuna  kitu kigumu kama kuanzisha biashara ukiwa na mtaji usiotosheleza.

SOMA: Kuendesha biashara bila mtaji ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini.

Sikatai kwamba unaweza ukaanza tu na mtaji huohuo wa shilingi milioni moja na nusu lakini utajiweka katika hatari kubwa zaidi ya kuja kukwama na biashara kufia njiani kwani kama inavyojulikana biashara ya steshenari full yenye uwezo wa kuoperate bila shida inatakiwa angalao iwe na mashine ya fotokopi ya uhakika(photocopy mashine) na photocopy ya namna hiyo inatakiwa kuwa mpya au kama ni used basi iwe kwenye hali nzuri.

Mashine ya namna hiyo si chini ya milioni 1, mpaka milioni 2 na nusu, kwahiyo unaweza ukaona hapo kwamba hiyo shilingi milioni moja na nusu uliyokuwa nayo inaweza ikatosha kununulia mashine ya kutolea fotokopi tu peke yake, bado vitu vingine kama pango la chumba, kompyuta na hata usajili na maboresho ya msingi ya chumba chenyewe cha biashara ili kiweze kuwa na mvuto unaotakiwa.

Njia ya pili ambayo ungeweza kutatua changamoto hiyo ya mtaji ni kwenda kukopa, lakini nachelea kukushauri ufanye hivyo labda kama ikiwa tayari wewe unamiliki mali zisizohamishika kama kiwanja au nyumba, vitu ambavyo kwa umri wako uwezekano ni mkubwa bado hujawa navyo. Na mkopo pia itakuwia vigumu kupewa mkopo wa maana kwa biashara inayoenda kuanza labda tena uwashirikishe ndugu jamaa na marafiki endapo watakubali kukukopesha mkopo wenye masharti nafuu au kuingia nao ubia mkamiliki biashara hiyo kwa ubia.

Nikuambie tu kwamba ndoto yako unakaribia sana kuitimiza, ondoa hofu, hebu ongeza bidii zaidi kwenye kile kilichokuwezesha kukusanya hizo shilingi milioni 1.5, usiziguse kabisa kwanza kwa namna yeyote ile mpaka pale zitakapotimia kiasi cha kutosha kuanzisha mradi wako wa stationary, uweze angalao kukodisha chumba eneo zuri lenye watu wa kutosha na pilika pilika kama vile mashule au maofisi au tu watu wengi, kununulia baadhi ya vile vifaa na mashine muhimu kama photocopy mashine, kompyuta na printa na vifaa vingine utakuja kuongeza mbele ya safari kidogokidogo. Lakini hauwezi ukaanzisha steshenari bila kuwa na vifaa kabisa hasa vile muhimu. STESHENARI NI VIFAA!, hiyo ndiyo siri yake kubwa ya ushindi.

SOMA: Kufungua kiwanda kidogo cha kusindika & kufungasha nafaka naomba ushauri.

Kwa upande wa changamoto yako ya pili, muongozo wa biashara ya steshenari, wala sina shaka na wewe hata kidogo kwani tayari naona hilo umekwishalifanyia kazi kwa zaidi ya asilimia 70%. Kwa kuwa umeweza kuniandikia email hii tayari wewe siyo mtu wa kukosa maarifa ya kufanya biashara, wakati ukisubiri mtaji wako utimie endelea kusoma vitabu, makala na chochote kile kinachohusiana na uanzishaji wa biashara. Unaweza hata kujipatia moja ya vitabu vyetu hasa kile cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, ni kizuri na kina hatua zote mtu anazotakiwa kufuata anapotaka kuanzisha biashara na wakati wa kuiendesha.

Naamini siku si nyingi utakuwa umesimama ndani ya steshenary yako mwenyewe ukihudumia wateja, biashara ya ndoto yako uliyokuwa ukitamani muda mrefu kuimiliki.

Peter A. Tarimo
Self help Books Tanzania.

0 Response to "NATAKA KUFUNGUA BIASHARA YA STESHENARI MTAJI MILIONI 1.5 NIFANYEJE? "

Post a Comment