Baada ya kusikia minong’ono mingi mitaani kuwa mchele
umeanza kushuka bei katika masoko
mbalimbali jijini Dar es salaam, binafsi sikukubali nikaamua kufunga safari
mpaka katika maduka yanayouza mchele kwa bei za jumla na rejareja pale Mbezi
mwisho ili niweze kujionea mwenywe punguzo hilo na ikibidi nijinunulie hapo
kilo mbili au tatu za kwenda kula nyumbani.
Si mara yangu ya kwanza kwenda katika maduka haya kununua
nafaka mbalimbali hususan mchele, maharage, mahindi, ngano, choroko, kunde na
hata wakati mwingine karanga, hivyo mazingira na hata bei za nafaka hizo
mbalimbali nilikuwa na aidia nazo ijapokuwa bei hubadilika mara kwa mara
kulingana na soko lenyewe lilivyo katika wakati husika kama ilivyotokea wakati
huu inaposemekana mchele umeshuka bei kwa sababu ya msimu wa mavuno ya mpunga
kuanza katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Mbeya, Ruvuma Rukwa na maeneo
mengine mbalimbali ya nchi ya Tanzania zao la mchele linakolimwa kwa wingi.
Na hata maduka mengi pia nayafahamu vizuri. Kuna duka
moja huwa napendelea kununua mara kwa mara kutokana na bei zao kuwa rahisi, wahudumu
wenye kauli nzuri na huwa na karibu kila aina ya nafaka ninayoihitaji. Safari
hii dukani hapo nilipita tu kuuliza bei ili nizunguke na maduka mengine mawili
matatu kuhakikisha kweli kama bei zimeshuka kama watu wanavyodai au la.
Kweli baada ya kuzunguka maduka kadhaa niligundua mchele
kupungua bei kulingana na madaraja(grades) husika tofauti na bei nilizozikuta
siku chache zilizopita. Mchele daraja la
kwanza kabisa ule super badala ya shilingi mpaka elfu tatu ilivyokuwa zamani
sasa mpaka shilingi elfu mbili na mia nne(2,400) unapata mchele kilo moja.
Nilikuta pia mchele wa hali ya chini kabisa(chenga) uliokuwa umefikia mpaka
shilingi elfu moja na miatano(1,500) kwa sasa unauzwa hadi shilingi elfu moja
(1,000) mpaka 900 kwa kilo moja.
HATUUZI KABISA MCHELE KILO MOJA, MBILI WALA TATU ,
TUNAANZIA KILO TANO NA KUENDELEA…
Kauli hiyo hapo juu ndiyo iliyonifanya nipate wazo la
kuandika makala hii ya leo. Baada ya kuamua ninunue mchele kilo 3 katika duka
moja(siyo lile nililozoea kununua kila siku lakini) nilimuuliza mhudumu kijana
wa kiume niliyemkuta nje ya duka hilo huku nikikunjua hela, “Nipimie mchele ule pale kilo tatu tafadhali”
Kwa mshangao kijana yule alinijibu
pasipo kujali hata kidogo, “Mchele kilo 3 hapa hatuuzi, tunanzia kilo
5”
Kwa kuwa mazingira ya maduka ya nafaka pale mbezi karibu
yote nayafahamu vilivyo, niliamua kumsisitizia tena yule kijana safari hii kwa
ukali kidogo, “Nipimie mchele bwana, kwanini unataka kumrudisha tajiri yako kijijini
hivihivi?” Kijana akijua fika kuwa bosi wake angeliweza kuyasikia
malumbano yale akiwa mle ndani dukani, alijitahidi sana kushusha sauti chini na
kurudia kunisihi; “Nakuambia kilo tatu
hapa hatuuzi, mchele unaanzia kilo tano na kuendelea labda kajaribu kwingine”
Na mimi kwa makusudi niliendelea kupaaza sauti juu kusudi yule mama(bosi wake)
aweze kuyasikia malumbano yetu vizuri. Na kweli kumbe yule mama alikuwa
akitusikia kila kitu tokea mwanzo akajitokeza akiwa amejawa na aibu.
Alishuhudia nilivyokuwa nimegadhabishwa na yule mfanyikazi wake.
Ukweli ni kwamba maduka yote ya nafaka za jumla ya pale
Mbezi nilikuwa nikijua fika kwamba unaponunua kilo kuanzia tano kushuka chini,
na siyo mchele tu peke yake ni nafaka za aina zote, bei huongezeka shilingi mia
moja, maana yake ni kwamba unakuwa umeuziwa kwa bei ya rejareja hata ununue
kilo moja wanakuuzia hawawezi kumrudisha mteja hivihivi kiholela. Nilifahamu
kabia kwamba majibu ya yule kijana aidha alikuwa amechoka au tu kilikuwa ni
kiburi chake pengine alichozoea.
Sikumficha yule bosi, nikamwambia waziwazi, “Mama
angu kwanini usifanye utaratibu wa kuwapa vijana wako angalao mafunzo ya msingi
tu ya kutoa huduma nzuri kwa wateja?” Mama alicheka huku akinitaka
radhi kwa kutamka, “Kakangu msamehe mdogo
wako bure atajirekebisha” Kijana naye baada ya kuona mambo yameshaanza kumchachia,
alijitahidi kuonyesha anajutia kosa alilofanya na chapchap akakimbia kwenda
kunipimia mchele.
Sikumwacha hivihivi nikaendelea kumpa darasa, “Sasa
wewe kijana kwanini ulitaka kumnyima bosi wako na wewe mwenyewe mapato? Hujui
mimi mteja ndiye bosi wako namba moja niliyewaajiri bosi wako huyo na wewe pia?
Nisiponunua unategemea aje nani kununua? Bosi wako namba 2 hawezi kwenda kukopa
pesa aje akulipe wewe, ni lazima pesa za kukulipa zitokane na faida
inayopatikana baada ya sisi wateja kuja kununua, hivyo mdogo wangu wajali sana
wateja wanaokuja kununua hapa.”
Mwisho niliondoka pale dukani huku moyoni nikitamani sana
mama yule japo angepata nakala ya kitabu changu cha; MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA, kitabu kinachofundisha
pamoja na mambo mengine mengi jinsi ya kumfanya mteja arudi tena na tena katika
biashara yako bila kujali ni biashara ya jumla au ni ya rejareja, kauli ambazo
hupaswi kabisa kumtamkia mteja na matendo ambayo mhudumu au wewe bosi
unapoyafanya basi jiandae kumtafuta mchawi aliyekuloga ambapo hautaweza kumpata japo utamaliza waganga wote
nchini.
Ilikuwa kidogo tu nirudi kuja kumjulisha kuhusiana na
kitabu hicho lakini nikafikiri angeweza kuona labda nilianzisha zogo lile pale
kwa madhumuni ya kuuza vitabu vyangu, nikaghairi nikaamua kujiondokea
zangu mdogomdogo huku nikiwa mkononi
nimeshikilia kifurushi changu cha mchele.
Kwa hakika kijana yule nisingelikuwa nazifahamu vyema
desturi za maduka ya mchele ya jumla pale Mbezi mwisho, ni dhahiri kwamba
ningeliondoka mapema sana kabla hata bosi wake hajajua ni nini kilichokuwa
kikiendelea kule nje. Najiuliza ni wateja wangapi wanaojiondokea kwa kuambiwa
kauli za namna ile?
Alichopaswa kunijibu yule kijana ni kunielewesha hivi kwa
lugha ya upole; “Kaka hapa mchele unaponunua chini ya kilo tano, unalipa bei ya
rejareja, na kuanzia kilo tano na kuendelea unalipa bei ya kawaida ya jumla”
Hapo ningekuwa nimemuelewa na wala pasingekuwa na sababu ya malumbano
yasiyokuwa na msingi.
.........................................................................
Kama hukuwa umewahi kusoma moja ya vitabu hivi hapa chini ni wakati wako sasa wa kuagiza nakala yako toka SELF HELP BOOKS TANZANIA
SIMU: 0712202244
WATSAP: 0765553030
.........................................................................
Kama hukuwa umewahi kusoma moja ya vitabu hivi hapa chini ni wakati wako sasa wa kuagiza nakala yako toka SELF HELP BOOKS TANZANIA
SIMU: 0712202244
WATSAP: 0765553030
10,000/=
5,000/=
3,000/=
Asante sana
ReplyDelete