KWANINI NI RAHISI ZAIDI KUTAJIRIKA UKIWA KWENYE AJIRA KULIKO KUJIAJIRI BINAFSI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KWANINI NI RAHISI ZAIDI KUTAJIRIKA UKIWA KWENYE AJIRA KULIKO KUJIAJIRI BINAFSI?


AJIRA VS KUJIAJIRI
Nadhani kauli hii inaweza kuwa imekushangaza kidogo kutokana na utamduni uliozoeleka kwamba mtu hawezi kutajirika kupitia ajira. Ni kinyume na mategemeo ya watu wengi kwani inadhaniwa kwamba kupata mafanikio makubwa kifedha kunatokana tu kwa kiasi kikubwa na mtu kumiliki biashara au kufanya uwekezaji kwenye vitegauchumi vilivyo na uwezo wa kuzalisha mapato.

Kabla hatujakwenda kutazama kile kichwa chetu cha habari kinachomaanisha, “Kwanini ni rahisi zaidi kutajirika kupitia ajira kuliko kujiajiri binafsi” hebu kwanza tutizme ule upande uliozoeleka zaidi wa “Kwanini ni vigumu mtu kupata utajiri akiwa katika ajira”


Si kama napingana tena na kichwa cha habari cha makala hii, ila ninachotaka hapa kieleweke ni mtazamo wa upande unaoamini kwamba kutajirika kupitia ajira siyo jambo rahisi. Ili kutajirika mtu atahitaji wakati fulani kuanzisha na kumiliki biashara/kampuni au kuwekeza mtaji aliokuwa nao. Ni vigumu sana kutajirika kupitia kuajiriwa peke yake. Hata hivyo jambo hili halipaswi kabisa kumfanya mtu aachane mara moja na kazi yake au hata kuachana na shule kwa lengo la kutaka kuanzisha biashara au kwenda kuwekeza.

Hili huwa naliandika mara kwa mara sana na hasa kwa rafiki zangu wanafunzi huwa simungunyi maneno kabisa wala kuwa mnafiki nawaeleza ukweli. Hupaswi kuchukua maamuzi ya kukurupuka. Kuwa mtulivu kwanza na ukishapata kazi au ajira ambayo itakuwa ni kama daraja kwako ndipo baadae utaweza kuingia katika ulimwengu wa kujiajiri mwenyewe. Njia hii ni rahisi kuliko kinyume chake au vile watu wengi wanavvyofikiria harakaharaka kwamba ajira si njia nzuri ya kumfikisha mtu kwenye utajiri. Leo tutaona kila kitu kilivyo hapa hapa hivyo vuta subira tuendelee kusoma hadi tumalize makala hii.


Makala hii nimelenga mahsusi zaidi kukuonyesha ni kwa jinsi gani kuajiriwa kunavyoweza kumfanya mtu akatajirika kinyume kabisa na ilivyozoeleka kwamba mtu kamwe hawezi kutajirika kwa kuajiriwa. Kwa kuwa kauli hizi mbili zinakinzana ni lazima tuelezee mazingira ya pande zote mbili ili kuweza kufahamu ni katika mazingira gani mtu anaweza akatajirika kupitia ajira na ni mazingira gani pia yanayofanya mtu asiweze kupata utajiri kupitia kuajiriwa.

SABABU ZENYEWE 4 NI KWANINI HUTAWEZA KUTAJIRIKA KUPITIA AJIRA.

1.Mwajiriwa kazi yake ni kutengeneza utajiri kwa ajili ya mwenye mali(Tajiri)
Wafanyakazi wapo pale kwa ajili ya kumfanya tajiri au wenye hisa katika kampuni au biashara kuendelea kuwa matajiri zaidi. Hawana tofauti na rasilimali(assets) ambazo kila mwisho wa mwezi hugharimu pesa ili kutengeneza pesa zaidi kwa tajiri na siyo vinginevyo.


2.Ajira/kazi haina uwezo wa kudurufiwa.
(Dhana hii niliwahi kuielezea katika kitabu cha MIFEREJI 7 YA PESA kuhusiana na biashara ya kazi za sanaa vs biashara nyigine za kawaida kama vile kilimo.) Biashara za namna hii hukua kwa mtindo wa kujiongeza zenyewe mithili ya photocopy inavyofanya kazi(duplication). Unapomiliki biashara tuseme labda ni biashara ya mgahawa wa chakula, ukiongeza wafanyakazi maana yake ni sawa na kutoa copy mfanyakazi wa mwanzo uliyekuwa naye, kwani mfanyakazi mpya atafanya kazi kwa kiwango sawa na yule aliyekuwepo na kuongeza mapato kiasi kama cha kwake. Ikiwa mfanyakazi wa mwanzo alikuwa akiingiza faida ya shilingi elfu 50 kwa siku ukiongeza wafanyakazi wawili faida itaongezeka na kufikia jumla shilingi laki moja na nusu.


Lengo la mjasiriamali siku zote ni kuikuza biashara yake hadi mahali ambapo anaweza akaiacha mikononi mwa msaidizi/meneja au hata kuamua kuiuza kabisa kwa mmiliki mwingine. Kwa mtindo huo mjasiriamali anaweza akatoka na kwenda kufanya mambo yake mengine huku biashara ikiendelea kama kawaida lakini kwa upande wa mwajiriwa hilo haliwezekani kabisa. Mwajiriwa akijaribu kuwa nje ya kazi hata kwa nusu saa tu bila ya sababu za msingi anaweza kujikuta kibarua kikiota nyasi mara moja. Mjasiriamli hujipatia kipato chake kutokana na rasilimali alizojiwekea wakati mwajiriwa yeye hubadilishana pesa na muda wake anaotumia kazini.

3.Kila siku ajira zinazidi kuwa siyo kitu cha kuaminika tena.
Ingawa kutafuta ajira kuna hatari kidogo kuliko kunzisha biashara, lakini usalama na uhakika wa kuendelea kudumu kwenye ajira siku hizi unazidi kupungua tofutti na vile ilivyokuwa siku za nyuma. Jambo hili limechangiwa zaidi na maendeleo makubwa ya kiteknolojia na ongezeko kubwa la watu duniani kote, kila mtu aking’ang’ania ajira chache zilizokuwepo.


4.Waajiriwa ndiyo wahanga wakubwa zaidi wa kodi mbalimbali za Serikali.
Hakuna njia rahisi mwajiriwa anayoweza kupata unafuu kwenye kodi, ni lazima alipe kodi iliyopangwa na serikali na kwa wakati, tofauti na wafanyabiashara au makampuni ambayo kuna misamaha mbalimbali, wanaweza kuchelewesha kulipa, kuahirisha na hata kupunguziwa kodi kulingana na hali ya biashara zao ilivyokwenda. Lakini hili haliwezi kufanyika kwa waajiriwa.

SASA KAMA HALI NDIVYO ILIVYO, NINI KIFANYIKE IKIWA MTU YUPO KWENYE AJIRA AU ANATARAJIA KUAJIRIWA?

Itumie ajira yako kujipatia uzoefu na kutengeneza mtandao. Licha ya hasara zilizotajwa hapo juu kwenye ajira lakini kuna faida nyingi zinazoweza kupatikana kutokana na ajira ambazo mtu anaweza akazitumia kujitengenezea utajiri mkubwa. Unapokuwa kwenye ajira au hata unapokuwa unapanga kuingia katika ajira unapswa kuchagua kampuni au mwajiri ambaye atakuwa na uwezo wa kukupa mchanganyiko wa vitu 3 vifuatavyo;

1.UZOEFU KWENYE MAUZO.
Stadi za muzo kwenye biashara ndiyo kitu muhimu pengine kushinda vingine vyote. Mauzo ni kile kitendo cha kumtafuta mteja, kujenga naye mahusiano ya karibu na hatimaye kumuuzia bidhaa au huduma. Ndio uwezo wenyewe wa kutengeneza mapato(utajiri). Hivyo kujifunza stadi za mauzo ni jambo la kwanza kabisa kwa mtu anayetarajia kumiliki biashara yenye mafanikio. Ukifahamu vyema kuuza tayari unakuwa umekamilisha karibu asilimia 80% ya kile unachohitaji kwa ajili ya mafanikio ya biashara yako. Vigezo vingine kwenye biashara havina maana ikiwa hautakuwa na uwezo wa kutengeneza pesa(mauzo)


2.UZOEFU KATIKA SEKTA HUSIKA
Ni muhimu pia kufahamu nje ndani kuhusiana na biashara unayotarajia kuja kuifanya siku moja. Ajira pia ina uwezo wa kukufundisha mbinu mbalimbali za biashara kwa mfano ikiwa umepanga siku moja uje kuanzisha biashara ya usafirishaji wa abiria na mizigo, ni vizuri kwanza ukaomba ajira kutoka katika biashara ama kampuni inayojishughulisha na biashara za usafirishaji. Kama ni biashara ya ardhi na majengo basi tafuta kwanza kazi inayohusiana na masuala hayo. Kama unayo maono ya kuja kumiliki biashara ya aina fulani hapo baadae basi tafuta ajira/kazi itakayokuwezesha hatimaye kuja kuyafikia maono yako hayo.

3.FURSA YA KUTENGENEZA MTANDAO
Ajira inayokuwezesha kujenga na kutanua mtandao wako ni fursa kubwa katika maandalizi yako ya kuja kuanzisha biashara hapo baadae. Ikiwa utaamua kuacha kazi, mahusiano yako na watu wengine au wateja hayatakoma mara moja. Unaweza kuyatumia mahusiano hayo kuimarisha biashara yako mpya au uwekezaji utakaoanzisha baadae.


Vitu vyote hivi vitatu unaweza usiweze kuvipata kwa wakati mmoja kutoka kwa mwajiri wako lakini angalao unaweza ukapata kimoja au viwili na vingine ukawa na mategemeo ya kuvipata taratibu ukiwa hapo. Hata hivyo mwajiri mzuri ni yule aliye na uwezekano wa kuvitoa vitu hivyo hata kama siyo kwa wakati mmoja. Kampuni au biashara nzuri mtu kufanya kazi kwa lengo la kupata vitu hivyo inapaswa kuwa na sifa zifuatazo;

·       Isiwe ni kampuni kubwa sana kiasi cha uwezo wako kutokuonekana kwa urahisi.
·       Iliyo na uongozi shirikishi uliotayari kuwaelimisha wafanyakazi wake
·       Utayari wa kusonga mbele
·       Isiyokuwa na ukiritimba
·       Yenye kuhimiza tabia za kijasiriamali kwa wafanyakazi wake
·       Inayokua.

HITIMISHO.
Tumia ajira yako kujipatia stadi zitakazokuwezesha kujiajiri na hatimaye kutajirika, kiasi cha mshahara utakaopata hapa hakina umuhimu mkubwa sana kwani ni ajira chache mno zinazoweza kumtajirisha mtu moja kwa moja kupitia mshahara wa mwezi peke yake, labda iwe mtu huyo anamiliki hisa katika biashara au kampuni anayofanyia kazi.


Kwa mjsiriamali au mwekezaji mtarajiwa, kazi nzuri ni ile inayomuwezesha kujijengea stadi stahiki, mazingira ambayo ubunifu unahimizwa, stadi za masoko na mbinu mbalimbali katika sekta husika zinafundishwa. Ajira ni rasilimali(asseti) siyo kwa maana ya mshahara unaoupata kila mwezi hapana, bali ni asseti kwa maana ya uzoefu na stadi unazozipata. NI JIWE LA KUVUKIA KUELEKEA UHURU KAMILI WA KIFEDHA.

.....................................................................

Ndugu msomji, unaweza kupata mafunzo ya ujasiriamali  kwa kina zaidi kupitia vitabu kutoka kwetu au semina na masomo ya kila siku katika Group la watsapp la MICHANGANUO-ONLINE. Unaweza kuona majalda ya vitabu vyetu hapo chini au ukatembelea ukurasa wetu wa vitabu wa;  SMARTBOOKSTZ. 

Ili uweze kujiunga na group la masomo la watsap kuna kiingilio cha shilingi elfu 10, unapewa na vitu mbalimbali vikiwemo vitabu, masomo na semina zote zilizokwishapita. Kwa mawsiliano;

SIMU: 0712202244
WHATSAP: 0765553030








0 Response to "KWANINI NI RAHISI ZAIDI KUTAJIRIKA UKIWA KWENYE AJIRA KULIKO KUJIAJIRI BINAFSI?"

Post a Comment