I CAN, I MUST, I WILL-THE SPIRIT OF SUCCESS. Binafsi
nimefurahishwa sana na kuzidi kuhamasika kutokana na kitenndo cha Mhamasishaji
wangu mkubwa tangu nikiwa mtoto Dokta Reginald Abraham Mengi kuandika kitabu
kinachohusu jinsi alivyofanikiwa kimaisha na historia ya maisha yake tokea
akiwa mtoto mdogo akichunga mbuzi kijijini kwake kule Machame. Kitendo
alichokifanya Mzee Mengi kwa kweli hufanywa na watu matajiri wachache sana hasa katika
nchi zetu za Kiafrika.
Kwa kipindi kifupi ambacho nimekuwa nikiandika na kuuza
vitabu vya ujasiriamali hususani vile vinavyohusiana na maendeleo binafsi ya
watu kama kina Reginald Mengi kwa lengo la kuhamasisha umma uweze kuiga mifano
ya watu hao katika kujiondoa kwenye lindi la umasikini wa kutisha, nimekutana
na vikwazo kdhaa na kimojwapo ni baadhi ya watu au wateja wa vitabu hivyo kuwa
wazito kuvinunua kwa madai kwamba wangependelea zaidi vitabu vilivyoandikwa
moja kwa moja na watu hao waliofanikiwa na wala siyo kwa kupitia waandishi wa
vitabu au waandishi wa habari.
Kitendo cha Mzee Mengi ni jawabu maridhawa kwa kundi hili
la wateja na kwa kweli ingelikuwa ni jambo zuri kama angalao kila mtu ambaye
anatazamwa kwenye jamii kama kioo na kundi kubwa la watu basi akaandika
historia ya maisha yake au hata kitabu chochote kile ambacho kitaondoa kiu ya
wale ambao wangependa kusoma kazi zao moja kwa moja kutoka kwao. Ni kweli
kabisa hata mimi natamani sana kusoma kitabu hicho hata ikiwa historia ya Mzee
Mengi naifahamu, huwezi kujua kila kitu, kuna vitu ambavyo akiviandika mtu
mwenyewe ndipo unapoweza kupata uhalisia wa mambo.
Mzee Mengi amewataja watu mbalimbali wengi
waliomhamasisha katika safari yake hii ya mafanikio akiwemo Mzee Alli Hassan
Mwinyi(Mzee Ruksa) na wengineo wengi, metoa pia mfano mwingine wa kuigwa kuwa
ni Rais wa sasa Dr. John Pombe Magufuli kuwa ana ile roho ya kijasiriamali ya
kusema “NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA”.
Hakuna kinachoshindikana mtu ukijiamini, Dr. Mengi siri
yake kubwa aliamini kwamba anaweza hata pale ambapo kulijitokeza watu
waliomkatisha tamaa. Wakatishaji tamaa hata leo wapo na wataendelea kuwepo siku
zote hivyo kikubwa ni kuiga roho hii anayotufunza Mzee Reginald Mengi katika
kitabu chake hiki cha I CAN, I MUST, I WILL-THE SPIRIT OF SUCCESS(NAWEZA,
LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA)
SOMA: Bila wazo bora la biashara hata ukipata milioni 100 huwezi kufanikiwa kibiashara-DR.Reginald Mengi
Katika kitabu hiki bila shaka, ijapokuwa bado sijakisoma
rasmi lakini ni lazima nikisome, Mheshimiwa Mengi atakuwa hajaacha kugusia
kuhusiana na suala zima la kiafya kwani bila afya njema hata utajiri na
mafanikio sio kitu tena, nimefurahi alivyoelezea kilichomsukuma aandike kitabu
hiki kuwa ni pamoja na wosia wa mwanaye
kipenzi, Rodney ambaye kwa sasa ni marehemu aliyemsisitizia sana juu ya kufanya
mazoezi ya viungo kila siku. Mwanaye huyu alikuwa mtu makini sana kwani
alifahamu fika hatari za kiafya zinazoweza kumpata mtu mwenye uwezo kama baba
yake na hata wale watu wa kawaida yakiwemo magonjwa mengi yasiyoambukiza kama
magojwa ya moyo, unene kupita kiasi na mengineyo.
0 Response to "KITABU SIRI YA MAFANIKIO YA MAISHA YA DR. REGINALD MENGI: NAWEZA, LAZIMA NIFANYE, NITAFANYA"
Post a Comment