Kwenye kipengele hiki cha Ongea na mshauri wako leo hii
tutajibu swali la msomaji wa blogu hii mwanadada(mama) kutoka kule mkoani
Kigoma na kama ilivyokuwa ada, swali lake nitaliweka hapa mezani pasipo
kuongeza wala kupunguza nukta hata moja na pia siwezi kutaja jina lake kwani
hakuniruhusu kulitaja hapa. Ujumbe wake alionitumia kupitia text meseji ulisomeka kama ifuatavyo;
Asante kwa majibu mazuri kwa ndugu yetu
anayetamani kuwa BILIONEA! But hata mm natamani .kaka naomba msaada kwa
haya machache nitakayouliza pia ushauri nini nifanye? Umri wangu miaka
29, mwaka 2014 nilianza lasimi kazi ya kusaka pesa, baadae ya kukaa
nyumbani miaka 4 kama mama Wa nyumbani nikihudumia familia yangu, Mume wangu
alinipa laki 9 akanishauri nifungue duka la chakula, nikafanya hivyo lakin
sehemu alionichagulia mwenzangu haukuwa sahihi kwa duka LA chakula kwan mauzo
yalikua chini sana,cku nyingine nilikua nauza hadi sh200/1000 ,hapo unatumia
nauli,ushuru na pango ya soko. Baadae ya mwaka nilifunga duka nikarudi
kuhudumia familia, baadae nikajifunza mambo ya ujasiriamali nikawa natengeneza
vitu vyangu na kuuza (Batiki & sabuni unga na za Maji). Ujuzi mkononi,
nikawa Fundi mzur sana, shida moja kwangu ikawa in soko huku kwetu Kigoma,
Mungu ameendelea kunitumia nikajifunza tena kupka ubuyu Wa Zanzibar na
Karanga za mayai, Mungu ni mwema nimeanza kupata wateja wazr. Naomba msaada kwa
hili Wazo langu. Nimekaa nikawaza je nitawajengea lin wazazi wangu maana
hizi Biashara haznilipi sana? Mungu akanipa Wazo nikalifanyia uchunguzi nikaona
ni bora, nikafanya survey nikaona hicho kitu kwa hapa Kigoma
anaetengeneza wote wanaouza wanatoa Dar, walifurahi sana kwa kupata
bidhaa karbu na makaz yao, nikawa nimeandika business plan yangu vzr tu ikawa
na mtaji Wa million 2, toka mwezi Wa 3 mwaka huu, nikamwonesha mume akaipenda.
Shida yangu ni kwamba nimekosa hiyo pesa ili nifungue mradi wangu ambao hata
nikikopa baada ya mwezi 1 narudisha hiyo pesa tena yote nabaki na faida yangu.
Nimejtahidi sana kumshawishi Mume wangu amesema niendelee kwanza na Biashara
hiz ndogondogo. Nifanyeje ili ndoto zangu zitimie ktk hili ikiwa na solo liko
waz?
MAJIBU.
Kwanza kabisa niseme
kwamba swali lako limenifurahisha na kunigusa kwani umetaja kuhusiana na azma
yako ya kuwajengea wazazi wako nyumba. Nadhani Duniani hakuna mtu hata mmoja
ambaye katika ndoto zake hajawahi kufikiria kuwafanyia wazazi wake jambo fulani
kama fadhila, na cha kufurahisha zaidi wewe ni mwanamke tena ambaye umeolewa
lakini bado katika nafsi yako una shauku ya kuhakikisha unawafanyia wazazi wako
jambo kabla muda haujazidi kuyeyoma. Unawakilisha karibu kila binadamu
aliyezaliwa na wazazi hapa duniani. Zipo baadhi ya jamii au makabila ambayo
mwanamke akishaolewa kuwajengea wazazi wake ama kuwafanyia jambo kubwa kama
fadhila ni mwiko.
Kasumba hii ni mbaya
haifai kabisa na inafaa itupiliwe mbali, mwanamke kama ana nafasi kiuchumi ana
haki ya kuwafanyia wazazi wake jambo lolote zuri bila kujali ameolewa ama
hajaolewa. Kwahiyo nakupongeza sana dada kwa mawazo yako mazuri, big up!
Kama sijakosea,
umetaka ushauri juu ya wazo lako jipya la biashara ambalo kulingana na utafiti
wako wa awali(survey) umebaini kwamba biashara hiyo inao uwezo mkubwa wa kuleta
faida na hata kama ungefanikiwa kupata mkopo mahali ungeweza kuurejesha mkopo
huo ndani ya kipindi kifupi sana huku ukibaki na mtaji uliokopa kama faida.
Kulingana na maelezo
yako inaonekana wazi kwamba tatizo lako kubwa ni mtaji mdogo na mumeo ambaye
angeweza kukuongezea mtaji huo tayari keshaonyesha kutokufanya hivyo kutokana
na sababu kwamba mtaji aliowahi kukupa mara ya kwanza wa kufungua duka la
vyakula la rejareja haukuweza kuzaa matunda yeyote yale ya maana.
Mimi wazo lako hili
jipya la bishara sina tatizo nalo hata kidogo kwamba lina uwezo wa kulipa,
inawezekana kabisa kweli likawa ni zuri na litakalolipa lakini ukumbuke pia
kwamba karibu kila mtu anayeanzisha biashara yake mpya mwanzoni huona kabisa
akilini kwamba biashara iliyoko mbele yake itamlipa na utafiti humuonyesha hivyo.
Lakini atakapoingia ‘field’ uwanjani, uzoefu huonyesha kuwa wengi hukutana na changamoto nyingi, hali
tofauti au kukuta mambo ni kinyume kabisa na vile utafiti ulivyoonyesha awali.
Sababu zaweza kuwa nyingi lakini kubwa zaidi hutokana na ufinyu wa mtaji, ushindani
mkali, ukosefu wa maarifa sahihi juu ya biashara husika au uzoefu na usimamizi
usio makini.
Ushuri wangu mimi
kwako hautakuwa tofauti sana na ule aliokupa mumeo wa kuendelea kuwa na subira
kwanza huku ukiendelea kwanza kufanya hizo biashara ndogondogo za batiki,
sabuni za unga & za maji, karanga za mayai na ubuyu wa Zanzibar, biashara
ambazo wewe unasema hazilipi au faida yake ni kidogo sana. Nasema hivyo dada
angu kwani nijuavyo mimi siku zote mtaji wa kukopa ni hatari sana kuutumbukiza
kwenye biashara mpya unayoianza na ambayo bado hukuwa na uzoefu nayo angalao wa
miezi kadhaa, au ungelikuwa tayari unao mtaji wako mwenyewe mkononi unaokwenda
kuanza nao.
SOMA: Kuendesh biashara bila mtaji au na mtaji mdogo ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini.
Ni afadhali pia hata
kama ungelikuwa na kiasi fulani cha mtaji huo kama nusu yake au robotatu
ningekushauri uanze tu any way, lakini midhali mtaji hauna kabisa unategemea
kuazima mahali au ni kidogo mno ni bora kabisa ukaendelea kudunduliza
kidogokidogo kutoka kwenye biashara ulizozizoea tayari na ulizo na uhakika nazo
mpaka angalao utakapoweza kupata nusu ya mtaji unaohitaji ndipo ufikirie
kutafuta kiasi kilichobakia mahali pengine.
Vinginevyo basi
ningekushauri pia ikiwa huwezi kabisa kujizuia kuianza ukihofia fursa hiyo
kupita muda wake au kunyakuliwa na watu wengine, basi ianze tu hivyohivyo kwa
mtaji uliokuwa nao mwenyewe hata ikiwa ni mdogo kiasi gani mpaka mtaji wako
utakapotengemaa pasipo kwanza kukopa mhali popote. Lakini angalizo hapa ni
kwamba lazima upime kwanza kwani zipo
biashara asili yake unaweza ukaanzia chini kabisa kimtaji na nyingine ambazo
asili yake ni lazima uwe na mtaji kiasi kilekile kinachohitajika ndipo
ziwezekane kuanza.
Mawazo kwamba ukikopa
baada ya mwezi mmoja tu tayari utakuwa umesharejesha mkopo wa watu yaache
kwanza kwani yamewahi kuwapotosha watu wengi hatimaye wakajikuta wametumbukia
katika shimo refu la madeni wasiloweza kujinasua kirahisi. Ndoto zako zitatimia
tu suala hili ukiliwekea subira, usikurupuke, ni kweli muda unapita na fursa
hazisubiri lakini wakati mwingine kulazimisha mambo kwaweza kufanya hali kuzidi
kuwa mbaya.
Mumeo tayari
keshaonyesha ni mtu anayependa maendeleo na ndiyo maana mwanzoni alikubali
kukupa mtaji wa duka. Angekuwa hakutakii mema sidhani kama hata angekuruhusu
ufanye hizo biashara ndogondogo, tena ameendelea kukutia moyo uwe na subira
kwanza ukizifanya kabla hajakuongezea mtaji wa hiyo biashara inayolipa.
Usije ukafikiria
namtetea kwa vile ni mwanaume kama mimi hapana, yeye pia amepima na kuiona
hatari kubwa inayoweza kuambatana na maamuzi ya haraka ya kutumbukiza mtaji wa
kukopa katika biashara mpya isiyopata bado uzoefu wa kutosha. Nielewe vizuri
sana hapa, si kwamba tatizo lipo kwenye uzoefu hapana kwani uzoefu watu huweza
kuupata mbele ya safari, tatizo kubwa hapa ni MTAJI WA KUKOPA, ikitokea umezama utaurudisha kwa nji gani?
Hebu jikomaze kwanza
kidogo uwe na uwezo angalao wa mtaji kiasi nusu au robotatu wa hiyo biashara
halafu kile kiasi kitakachobakia shemeji naamini kabisa atakuwa tayari
kukuongezea bila shaka yeyote. Kumbuka ile ni biashara na haipaswi kuingilia
mahusiano yenu kwa namna yeyote kama mke na mume. Ndoa nyingi zimevurugika kisa
masuala haya haya ya kichumi na biashara.
Mumeo anaweza akakupa
fedha na kwa bahati mbaya kama ilivyotokea mwanzoni mtaji ukajakukata tena,
huoni anaweza akahisi pengine fedha kuna mahali unazipeleka, akaishia hata
kuhisi labda unacho ‘kidumu’(mwanaume wa
pembeni) mahali kinachotafuna pesa zako na huo ndio ukaanza kuwa mwisho wa
ndoa yako?
Huo ndio mwisho wa majibu ya swali letu la leo
kutoka kwa mwanadada wa kule Kigoma, mpenzi msomaji tunakaribisha maswali na
changamoto mbalimbali kwenye biashara ndogondogo, hatutozi chochote kwa maswali
mafupimafupi kama haya na huwa tunajibu kupitia meseji, wasap na email lakini
wakati mwingine majibu tunayaweka hapa kwa manufaa ya wasomaji wengine. ASANTE
SANA.
………………………………………………...........
Darasa letu la whatsapp bado linaendelea kila
siku na kuanzia mwezi huu wa 7,nusu ya pili ya mwaka tutahakikisha mazimio
tuliyojiwekea Januari yanakamilika hivyo kama ulikuwa hujajiunga bado
hujachelewa. Kiingilio ni shilingi elfu 10 tu, unapata vitabu, masomo mbalimbali
ya semina zilizopita, michanganuo ya kuku aina zote nk. pamoja na fursa ya
kuendelea kupokea masomo mazuri kila siku na kuungana na group la watu makini
katika biashara zao mbalimbali. Wasiliana nasi kupitia SIMU: 0712202244 au
WHATSAP: 0765553030
Vitabu pia vipo tazama hapa chini au unaweza kutembelea, SMARTBOOKS TANZANIA kwa maelezo zaidi.
0 Response to "NATAKA BIASHARA INAYOLIPA NIWAJENGEE WAZAZI WANGU NYUMBA, NILIYO NAYO HAILIPI"
Post a Comment