Huwa tunawaona watu duniani wenye vipaji, akili na uwezo
wa wa aina mbalimbali kama vile wanamuziki, wanamichezo, wasanii, viongozi na hata watu waliobobea katika taaluma
mbalimbali kama sayansi, uchumi, sheria,
utabibu na saikolojia kiasi ambacho hata mtu unadiriki kutamani na wewe
ungelikuwa kama walivyo, lakini kuna siku hata moja umewahi kujiuliza kama watu
hawa wamejaliwa tu na Mwenyezi Mungu na kuzaliwa wakiwa na vitu hivyo au
walikuja kuvipata hapa duniani baada ya kuzaliwa?
Utafiti mwingi umekwishawahi kufanyika katika maeneo
mengi ya dunia kuhusiana na swali hili na majibu yake kwa kweli
yanastaajabisha. Hata kwa mtu wa kawaida unaweza ukaangalia nyuma maisha yako
ulikotoka, watu uliosoma nao na wale uliokua nao rika moja, utagundua kwamba
baadhi ya watu walikuja kubadilika na kuwa tofauti kabisa na vile walivyokuwa
awali, akili, vipaji na uwezo wao ulikuja kuonekana kuwa tofauti au kinyume
kabisa na vile ulivyodhania watakuwa.
Hebu tuchukua mfano mmoja wa mtu anayeaminika kuwa ndiye
mwenye akili nyingi zaidi duniani(IQ kubwa) . Mtu huyo anayejulikana kama
Christopher Michael Langan alipimwa na
kukutwa na kiwango cha IQ 195 karibu asilimia 30% juu zaidi ya IQ aliyokuwa
nayo mwanasayansi mkubwa zaidi duniani, Albert Einstai, IQ ya mtu wa kawaida ni
80 mpaka 120. Langan alipozaliwa alianza kuongea akiwa na miezi 6 tu. Akiwa
shule ya msingi ilibidi arushwe madarasa ya juu kutokana na uwezo wake wa akili
usiokuwa wa kawaida. Akiwa sekondari ilimbidi ajifunze peke yake kutokana na
kukorofishana na walimu wake waliodai hawawezi kumfundisha mtu anayewazidi
akili, na chuoni nako alliamua kuacha akidai kwamba alikuwa na uwezo wa
kuwafundisha Maprofesa wake vizuri zaidi kuliko wao walivyoweza kumfundisha
yeye.
Lakini pamoja na uwezo huo mkubwa kiakili aliokuwa nao Langan
unafahamu ni kitu gani kilichokuja kumtokea katika maisha yake baadae? endelea kusoma
nitakusimulia punde kidogo.
Tukirudi kwenye hoja yetu ya msingi kwamba vipaji, uwezo
na akili nyingi binadamu huwa wanazaliwa navyo?, jibu ni HAPANA. Kipaji kama
ilivyokuwa ujasiriamali watu hukikuza katika mazingira wanamoishi baada ya
kuzaliwa. Ni ukweli kila mtu huzaliwa na kiasi fulani cha vitu hivyo lakini ili
kuja kubobea kunahitaji juhudi na maarifa.
Ingawa mtu anaweza akazaliwa akiwa na fursa fulani
zinazochochea zaidi vitu hivyo kama vile mtu kuzaliwa IQ yake ikiwa kubwa,
umbile lililokaa kimichezo, mtoto anayezaliwa katika familia yenye uwezo wa
kumpa elimu nzuri au mtaji, wengine huzaliwa wakiwa na sauti nzuri, sura na
umbile zuri nk. Vyote hivi ijapokuwa vinaweza kumpa mtu fursa nzuri ya kufanya
mambo makubwa lakini mhusika ni lazima afanye kazi ngumu ya kuvikuza vinginevyo
atabakia tu vile vile kama watu wengine waliozaliwa hawana hivyo vitu.
Ili mtu aweze kufanya mambo makubwa ni lazima atambue
wazi ni kitu gani anachomudu kukifanya kisha kuanzia pale aanze kukuza na
kuendeleza kipaji au uwezo huo kwa njia za kujifunza, kujitoa mhanga, nidhamu
na kujitolea muda mwingi wa kutosha kukifanyia mazoezi kipaji hicho.
Kuna watu wengi tu duniani walizaliwa wangali hawana
fursa yeyote ile, hawakuwa na sauti nzuri, hawakuwa na akili nyingi darasani
IQ, hawakuwa na miili iliyokaa kimichezo, Wengine walizaliwa hata hawana baadhi
ya viungo mwilini lakini baadae walikuja kuwa wabobezi katika fani zao. Hii
inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba binadamu anaweza akawa chochote kile
anachotamani kuwa ikiwa tu atachagua kuwa hivyo.
Lakini ni kwanini watu wengi hushindwa kufikia viwango
vya juu katika vipaji au fani zao? Sababu mojawapo ni kwamba siyo jambo rahisi
mtu kuweza kufikia viwango vya juu, inahitajika juhudi nyingi na kwa asili sisi
binadamu tulivyoumbwa huwa hatupendi kufanya vitu vigumu.
Katika kitabu changu nilichoandika kiitwacho “SIRI ZA
KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO KWA UFANISI”(nadhani wale wote waliojiunga
kwa email katika blogu ya jifunzeujasiriamali wanakifahamu) katika ukurasa wa
15 nikinukuu kutoka kitabu kingine kiitwacho Outliers nilisema kwamba, kitu
kinachowatofautisha matajiri waliofanikiwa na sisi watu wa kawaida ni
masaa(MUDA) wanayotumia katika fani au vipaji vyao. Mwandishi alitolea mifano
ya wanamuziki wa kundi la The Beatles, Steve Jobs na Bill Gates akisema
kwamba wote walitumia karibu masaa elfu
10(10,000) katika fani zao kabla hawajafanikiwa kufanya mambo makubwa yaliyowafanya
kuonekana wabobezi katika fani zao.
Sasa hetu tena turudi kwenye ile stori yetu ya
Christopher Langan, mtu mwenye IQ kubwa kabisa duniani na hatma yake.
Kilichokuja kumkuta mtu huyu ni kwamba alikuja kuishia tu kuwa mtu wa kawaida
akifanya kazi za kubeba mizigo, wakati mwingine aliajiriwa kama mlinzi, baunsa
na hadi hivi leo amebakia tu kuwa mtu maarufu kwa kuwa na akili nyingi lakini
hakuna cha maana alichoweza kukifanya maishani tofauti na watu wengine kama
kina Bill Gates Steve Jobs, Albert Einstain na wengineo ambao hawakuwa na
kiwango kikubwa cha akili kama alichokuwa nacho Langan lakini mambo
waliyoyafanya ni makubwa mno, waliweza kubobea katika fani zao. Siri yao kubwa
siyo nyingine bali ni kujitoa kikamilifu kwa vitendo, nidhamu, na kujifunza kwa
bidii.
Hii ni habari njema sana kwa kila mtu anaye ‘struggle’
kwani ni dhahiri kabisa kwamba hatuna tena kisingizio cha kuwa chochote kile
tunachopenda, visingizio kama vile; sijazaliwa na kipaji hiki, mimi darasani
sikufanya vizuri, sina uwezo, IQ yangu ni ndogo nk. Unachohitaji ni maamuzi na
kisha kujitolea kwa moyo wako wote kuwa kile unachotaka uwe.
Kwa mfano unataka kuwa mwandishi mzuri, huna budi kutumia masaa yako mengi kufanya mazoezi ya
kuandika bila ya kujali shuleni ulipata alama gani katika somo la lugha.
Ninao mfano mzuri mimi binafsi wa wanafunzi wangu
ninaowafunza jinsi ya kuandika mpango wa biashara katika Group la Whatsap la
MICHANGANUO-ONLINE, wengine ni wanafunzi katika vyuo mbalimbali na wengine
hunitumia kazi zao ili niweze kuwapa ushauria au kuzipitia na kuwakosoa pale
walipofanya makosa.
Mmoja alinitia moyo sana baada ya kunitumia mchanganuo wa
biashara yake aliyokuwa ameshasahihishiwa na mkufunzi wake, aliniambia chuoni
alichagua swali hilo la kuandika mchanganuo wa biashara baada ya kujiunga na
masomo yangu na kudai masomo hayo yalikuwa msaada mkubwa kwa yeye kufanya
vizuri assignment ile.Ijapokuwa alikuwa amepewa maksi nzuri tu na mwalimu wake
baada ya kuupitia nilikuta kuna baadhi ya sehemu alikuwa amefanya makosa na nikamshauri
alitakiwa kufanya kitu gani. Alinishukuru sana na kusema ule ndiyo uliokuwa
mchanganuo wake wa kwanza kuwahi kuandika.
Nilimpa siri ya kuwa bora katika uandishi wa michanganuo
kuwa ni kufanya mazoezi ya kuandika michanganuo zaidi kwani kwa kadiri
alivyojitahidi katika mchanganuo wake
huo wa kwanza bila shaka atakuja kuwa mbobezi hata kunipita endapo ataandika
michanganuo miwili mitatu zaidi.
Hivyo kubobea katika fani, kipaji au uwezo wa aina yeyote
ule hakuna uhusiano wowote na kile mtu anachozaliwa nacho kutoka tumboni mwa
mama yake bali hutokana tu na juhudi zako za makusudi na kujitambua kuwa ni
nini unachotaka kukifanya.
…………………………………………....
Ndugu Msomaji, napenda kukujulisha kwamba masomo ya kila
siku katika lile group letu la Whatsap yanaendelea kila siku na wiki hii
tutaanza tena semina za kuandika michanganuo ya biashara zinazolipa hatua kwa
hatua. Kama utapenda kujiunga basi lipia ada yako sh. Elfu 10 kupitia namba za
simu 0712202244 au 0765553030 kisha tuma
ujumbe wa “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO” na tutakuunganisha muida huohuo
pamoja na kukutumia vitabu, masomo na semina zote zilizopita.
0 Response to "VIPAJI, UWEZO, AKILI NI VITU WATU TUNAZALIWA NAVYO AU KUJIFUNZA?"
Post a Comment