Ni jambo la kushangaza sana ukisoma au
kuelezwa ripoti ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu zinazohusiana na
suala zima la furaha ya waajiriwa katika kazi mbalimbali. Mambo yaliyokuwa
gumzo na yanayoonekana kubishaniwa zaidi miongoni mwa waajiriwa wenyewe na hata
wale waliokuwa nje ya ajira kwa ujumla ni ikiwa, ufanisi wa kazi kwa mwajiriwa
aliye na furaha kazini ni mkubwa kushinda ufanisi wa mwajiriwa yule asiyekuwa
na furaha kazini.
Jambo hili kuhusiana na furaha kazini limezua
sintofahamu kubwa hadi kusababisha wataalamu mbalimbali waliobobea katika fani
zao kuamua kulifanyia tafiti zilizopelekea kuibuka matokeo hayo ya
kustaajabisha. Nitakueleza matokeo hayo ya kushangaza taratibu kadiri
utakavyoisoma makala hii, hivyo tafadhali ‘stay
tunned’ hakikisha tunakwenda pamoma mpaka mwisho wa makala.
Tukiachana kwanza na huo utafiti kwa
muda, tuendelee kwanza na mada yetu hii ya ikiwa kama kuna ukweli wowote kwamba
walio katika ajira wengi hawana furaha……
Furaha ni kitu nyeti sana maishani, maono na
malengo ya karibu kila mwanadamu, vyote dhumuni lake kubwa ni kuwa na furaha
maishani au akhera, hivyo furaha ijapokuwa utaona katika somo hili tutaegemea zaidi furaha kwa
waajiriwa wawapo makazini lakini vilevile somo lina manufaafa makubwa hata kwa
wajasiriamali kwani uwe umeajiriwa, umeajiri au umejiajiri mwenyewe, wote
wanahitaji furaha, wanachokitafuta siku zote ni furaha katika nafsi zao, na si
hivyo tu bali wote pia wanahusika kwa namna moja ama nyingine katika mazingira
ya kazi nikiwa na maana pale shughuli au biashara zinapofanyikia.
Kwanza kabla hatujaingia ndani zaidi kwenye
mada yetu hii, hebu tutazame furaha ni nini? Furaha ni hali ya hisia au akili
inayomtokea binadamu pale anapojisikia vizuri aidha kiafya, bahati, kiusalama,
kiimani, kiuchumi au kwenye mafanikio mengine yeyote yale. Hii ndiyo
kusema kwamba furaha ni suala la mtu binafsi zaidi. Sasa tunapoongelea furaha kwa
mtu yeyote yule awe ameajiriwa au mjasiriamali hutegemea sana vigezo viwili
vkubwa, watu huweza kuwa na furaha kutokana na vigezo hivyo 2 ambavyo ni;
· Mazingira
wanayofanyia kazi
· Mazingira
yao binafsi
Mada yetu hii itakwenda kujikita zaidi katika kigezo cha
kwanza ambacho ni mazingira mtu anayofanyia kazi. Sasa basi Mwajiriwa au tuseme
mfanyakazi anawezaje kuwa na furaha? Zipo pia njia kuu tatu ambazo mwajiriwa
yeyote yule anaweza akaijenga furaha yake juu yake navyo ni hivi hapa chini;
1) Kwa
kutokufanya kazi!
2) Kwa
kujenga uvumilivu na mshikamano na taasisi/kampuni anayofanyia kazi pamoja na
watu waliopo pale.
3) Mahitaji
yake kuendana sambamba na malengo yake.
Hebu sasa tujaribu kuzifahamu vizuri zaidi
njia hizo tatu mtu aliye katika ajira anazoweza akapata furaha;
1.“Kutokufanya
kazi”
(Mtu kufanya kazi uipendayo ni sawa na
kutokufanya kazi)
Bila shaka kila mtu angependa kufanikisha
kitu fulani katika fani yake aliyochagua maishani. Watu wanataka kuleta tofauti
katika fani hizo huku wakikidhi mahitaji yao ya kimaisha . Jambo hili hasa
ndiyo kiini cha maisha yenye furaha kamili kazini(katika ajira).
Watu hulitumia neno KAZI A au AJIRA
wakimaanisha kile mtu anachokifanya ili kujipatia riziki au kuishi lakini
wakati mtu unapofanya kile kitu(kazi) unayoipenda unakuwa haufanyi tena ‘KAZI’
aslani, hapo ni sawa na hujaajiriwa, bali unafanya kazi hiyo kwasababu
unaipenda, UNA MAPENZI NAYO na inakufanya uwe na FURAHA.
Lakini kwa bahati mbaya sana mara nyingi
mahitaji ya binadamu yale ya muda mfupi ya kila siku hufunika shauku
hiyo(mapenzi hayo kwa kazi) na hatimaye kufanikiwa kuizima kabisa ndoto nzuri
uliyokuwa nayo awali. Kutimiza mahitaji ya muda mfupi ambayo kwa kiasi kikubwa
hutokana na kuiga kutoka kwa watu wengine au rika kuna msukumo mkubwa na
mahitaji hayo huzunguka juu ya vitu hivi vikubwa vifuatavyo;
· Pesa
· Faida
· Ubora
wa maisha
· Cheo/nafasi
na malaka
Vitu nilivyovitaja hapo juu huonekana kuwa vya kuvutia
mno kiasi kwamba watu wengi hulazimika kuamini kwamba hivyo ndivyo malengo ya
ajira/kazi ambayo kimsingi hawaipendi au hawana furaha nayo, wanaifanya kwa
vile tu kazi hiyo inalipa vizuri. Hebu jaribu kufikiria inaingiaje akilini
kumkuta injinia au daktari akifanya kazi ya uhasibu? Au Mtaalamu aliyebobea
katika masuala ya kiuchumi akifanya kazi ya siasa?.
Matokeo au zao la ajira ndilo hugeuka kuwa lengo kuu la
ajira kwani pesa au cheo ni zao tu la ajira na siyo lengo. Na kwa namna hii
yale mapenzi na kazi yanakuwa tayari yamekwisha uwawa. Sasa watu wanaweza kuwa
na AJIRA zilizokuwa na FURAHA ikiwa tu wataacha kuruhusu haya mahitaji ya muda
mfupi kuwaendesha.
2. Kwa
kujenga uvumilivu na mshikamano na taasisi/kampuni anayofanyia kazi pamoja na
watu waliopo pale.
Tumezoea kuona kwamba mtu anapoajiriwa mahali au kujiunga
na taasisi fulani mwanzoni kabisa huonyesha heshima na kutoa sifa zote nzuri
kwa kampuni/taasisi na uongozi wake
mzima. Lakini taratibu huanza kuleta upinzani na kuonyesha kutokujali
tena. Na mwishhowe huanza kuonyesha chuki waziwazi na kuanza kusaka ajira
nyingine mpya.
Suala ni kwamba uongozi umebadilika? Au kampuni
imebadilika? Hakuna hata kimoja kilichobadilika kati ya hivyo 2, Sasa ni kitu
gani kilichobadilika? Jibu ni MTAZAMO! Hilo tu basi. Kila taasisi au binadamu sawasawa
na ilivyokuwa kwa mtu na mchumba wake wanapooana, mwanzoni kabisa wanapokutana
kila mmoja huonekana mzuri mbele ya mwenzake na sababu kubwa ni kwamba kila
mmoja kati yao anataka aonyeshe ubora wake wa kiwango cha juu kabisa mbele ya
mwenzake, lakini kadiri uhusiano huo unavyokua siku hadi siku kila upande
hujifunza kuhusiana na mwenzake na ikiwa mmoja kati yao tuseme labda ni
mwajiriwa atashindwa kuendana /kushikamana au kuvumilia mtazamo wa mwajiri,
taassisi au kampuni anayofanyia kazi basi ujue kutoridhika nako huanza kukua
taratibu huku furaha nayo ikitoweka.
Hakuna taasisi au kampuni
iliyokuwa kamilifu kwa asilimia 100% na wala pia hakuna mwajiriwa
aliyekuwa mkamilifu kwa kiwango cha asilimia mia moja 100%. Kikubwa
kinachotakiwa hapa ni kuvumiliana na kuchukuliana mitazamo tofauti. Ili kuwepo
na furaha katika kazi yeyote ile mtu anatakiwa kutazama mambo kwa jicho la tatu
au kuvaa viatu vya mtu mwingine. Kwa kufanya hivyo tunakuwa na uwezo wa kuelewa
mambo kwa kina zaidi na kuendana na
mitazamo ya watu wengine katika taasisi tunazofanyia kazi. Kuumizana mioyo na
kuchanganyikiwa kunaweza kuepukwa huku majadiliano yenye manufaa yakipewa
nafasi.
3.
Mahitaji kwenda sambamba na malengo.
Kwa mtu aliyeajiriwa kuna vitu hivi muhimu viwili
1) Maisha
ya kazini
2) Maisha
binafsi.
Ni utamaduni na tayari imeshazoeleka kwamba mfanyakazi
anapaswa kuvitenganisha vitu hivi viwili awapo kazini lakini kwakweli ili
mwajiriwa mahali aweze kuwa ni mtu mwenye furaha vitu hivi viwili havipaswi
kabisa kutenganishwa. Kwanini? Sababu kubwa ni kwamba waajiriwa hutafuta kazi
hizo kwa malengo ya kutosheleza mahitaji au malengo yao binafsi hivyo hakuna
umuhimu wowote ule wa kutenganisha kazi na maisha binafsi na ni jambo muhimu
malengo na mahitaji hayo kuendana sambamba na maisha ya kazi.
Hili huhitaji mabadiliko makubwa ya kimtazamo kutoka kwa
waajiri au makampuni kuelekea maslahi ya wafanyakazi wao na vilevile pia kwa
waajiriwa wanatakiwa kuwa na muelekeo wazi usiokuwa na upendeleo kuhusiana na
vipaumbele vya kazi na vile vyakwake binafsi.
Ni rahisi zaidi kutamka kwa maneno kuliko kutenda, ingawa
ni jambo linalowezekana mwajiriwa kuwa na furaha lakini bado ni waajiriwa
wachache mno wanaokuwa na furaha kamili katika kazi zao. Hata ikiwa kama
waajiri wangependa wafanyakazi wao wote kuwa na furaha, lakini siyo jambo
rahisi kutokana na kushindwa kurekebisha mifumo yao ya rasilimali watu kumfanya kila mfanyakazi kuwa na furaha,
vilevile pia siyo rahisi kila mfanyakazi ataweza kuwa na mapenzi na kazi au
kuwa na uvumilivu kama ilivyotajwa katika vitu au vigezo vingine 2
vilivyotangulia hiki cha mahitaji.
Vigezo vyote hivi vikiwekwa pamoja hulifanya suala la
mwajiriwa mwenye furaha kuwa ni kitu adimu na hivyo kuibua mjadala mzito wa
ikiwa mwajiriwa anaweza akawa na furaha kazini. Lakini yote kwa yote ,WAJIRIWA WANAWEZA
KUWA NA FURAHA KAZINI pale vigezo hivyo 3 vilivyotajwa na kuelezewa hapo juu
vinapofikiwa.
Baada sasa ya kumaliza suala la ikiwa mwajiriwa anaweza
akawa na furaha kazini au la, turudi tena rasmi katika ule utafiti wa kustaajabisha wa wataalamu juu ya ikiwa kama MWAJIRIWA
MWENYE FURAHA KAZINI, UFANISI WAKE UNAZIDI WA YULE ASIYEKUWA NA FURAHA KAZINI.
Safari hii tunakwenda kuangalia matokeo yake, ni nini walichogundua
kilichowaacha midomo wazi watu wengi?
Tangu kale dhana kwamba mfanyakazi mwenye furaha ndiye
aliye na ufanisi zaidi kushinda yule asiyekuwa na furaha imekuwepo kila mahali
kote duniani, lakini ni ukweli wa kushangaza kwamba dhana hiyo siyo kweli,
MFANYAKAZI MWENYE FURAHA HAIMAANISHI KUWA NI MFANYAKAZI MWENYE UFANISI. Utafiti
huo kuhusu athari za furaha kwenye makampuni ulifanyika na watu wawili, Profesa
Andre Spicer wa chuo cha biashara London
Carl Cadestrom wa chuo kikuu cha Stockholm.
Katika matokeo yao Andre na Carl walisema tabia ya
waajiri/makampuni kuhimiza furaha kama njia ya kuzidisha ufanisi/uzalishaji hakuna
uwezo wa kuleta furaha halisi inayoweza kupatikana kutokana na vitu vizuri
tunavyotegemea. Utafiti huo walioufanya katika supermarket moja ulibainisha
kwamba kadiri wafanyakazi walivyokuwa na hasira ndivyo pia ufanisi wao
ulivyokuwa mkubwa.
Wanasema kwamba hasa mtu anapokuwa hana furaha kisha
ukajaribu kupandikiza furaha ndani yake ndiyo unazidi kufanya mambo kuwa mabaya
zaidi. Kutaka kuwa na furaha kwa kukusudia kutafanya kazi kinyume na
ulivyotazamia.
Pia walibainisha kwamba watu walio na furaha mara nyingi
huingia mikataba mibovu, wakati mtu anapokuwa katika hali ya hasira huingia
mikataba kwa ufanisi zaidi. Hivyo kuwa na furaha muda wote hakuwezi kuwa kuzuri
katika kila hali kwenye ajira zetu ingawa pia kuna wakati furaha inaweza
ikasababisha baadhi ya vitu kufanyika kwa ufanisi.
Walihitimisha kwa kusema kwamba waajiriwa hawatakiwi
kutegemea sana furaha kwenye ajira zao kwani wanaweza kuishia kujihisi kukata tamaa
zaidi pale watakapokuta hawaipati furaha hiyo na badala yake furaha ni kitu
kinachokuja chenyewe bila kukilazimisha.
0 Response to "WAFANYAKAZI KWENYE KAZI ZA AJIRA WENGI HAWANA FURAHA, UPO UKWELI WOWOTE AU NI UZUSHI MTUPU?"
Post a Comment