Kufunga mkanda au kwa kimombo Bootsrapping ni njia
inayotumiwa na wajasiriamali wengi wadogo wanaoanza lakini pia ni njia ambayo
kila biashara inaweza kuitumia iwe ni biashara kubwa au biashara ndogo. Kufunga
mkanda kwenye biashara maana yake ni kitendo cha kuanzisha na kuendesha
biashara kwa kujitegemea kimtaji pasipo msaada wowote kutoka nje.
Unatumia mtaji na rasilimali za ndani peke yake huku ukijitahidi kushusha chini
gharama za biashara kwa kadiri inavyowezekana.
Dhana hii ya kufunga mkanda tumeweza kuona ikitumiwa hata
na serikali za nchi mbalimbali kwa mfano hapa kwetu sera hiyo ilitumika sana
kipindi kile cha awamu ya kwanza na aliyekuwa Rais na Baba wa Taifa la Tanzania
Mwalimu J.K Nyerere na sasa hivi tena tunaweza kuona ikitumiwa na Rais J.P. Magufuli
kwa kuhimiza kuanzisha na kuendesha miradi mingi ya kiuchumi kwa kutumia fedha
za ndani zaidi kuliko kutegemea misaada au mikopo kutoka Mataifa mengine.
Kufunga mkanda kunasaidia sana uchumi wa taasisi iwe ni
mtu binafsi, kampuni au nchi kuwa imara zaidi na unaojitegemea. Hujenga nidhamu
ya pesa na kuleta matokeo bora. Kwenye kufunga mkanda mjasiriamali anatakiwa
kuchunga sana upande wa matumizi ya biashara yasijekuwa juu sana hasa kipengele
cha gharama, lakini pia haishauriwi kupunguza kupindukia kila matumizi ya
biashara bali kufanya matumizi katika yale maeneo tu yanayohusika moja kwa moja
na uzalishaji wa faida.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema, tumia fedha zaidi
kwenye kuwekeza kuliko katika matumizi ya kawaida yasiyorudisha fedha
zilizotumika. Unatumia fedha ukiwa na uhakika kuwa itarudi. Matumizi katika
vitu au mambo yaliyokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mapato ya biashara
yanaweza yakawa ni ununuzi wa malighafi ya kutengenezea bidhaa, kulipia
teknolojia nzuri itakayoongeza wateja, kununua vifaa au zana za kufanyia kazi
nk. Lakini pia chunga sana mzunguko wako wa fedha usije ukanunua vitu ambavyo
itachukua muda mrefu sana kurudisha pesa.
Kwa biashara ndogo inabidi utumie zaidi pesa katika
kuwekeza katika vitu vitakavyorudisha pesa katika kipindi kifupikifupi ili
kuimarisha mzunguko wa pesa wa biashara. Matumizi katika kitu chochote kile
ambacho hakitaleta mabadiliko yeyote kwenye mapato ya biashara usikipe uzito
wowote, matumizi kwa mfano kununua usafiri binafsi, kula na kulala katika
hoteli za gharama kubwa ukiwa safarini kibiashara, kupanga katika eneo la
biashara la gharama kubwa isiyolingana na biashara, kutumia usafiri wa tax au
bodaboda unapofuata bidhaa zako za biashara wakati ungekuwa na uwezo wa kupanda
mwendokasi au daladala ya kawaida nk. Hizo zote ni gharama zinazoua biashara na
wala siyo uwekezaji unaoweza kuiletea biashara mapato.
Kufunga mkanda siyo jambo rahisi linaloweza kumvutia kila
mjasiriamali lakini ni jambo lililokuwa na manufaa mengi kwa biashara yeyote iwe
ndogo au kubwa iwapo tu mmiliki wake atataka kuongeza mapato yake zaidi bila ya
msaada kutoka sehemu nyingine yeyote ile. Na hasahasa kwa biashara ndogo hii
ndiyo silaha kubwa kuliko zote mjasiriamali anaweza kuitumia kuhakikisha
anakuwa na udhibiti mkubwa wa biashara yake.
...................................................................
Kwa vitabu vya ujasiriamali katika lugha ya kiswahili fungua self help books tz
Kwa masomo ya kila siku, vitabu bila malipo, michanganuo ya kuku, matikiti maji na semina za kila mwezi jiunge na kundi letu la whatsap la MICHANGANUO-ONLINE namba 0765553030
0 Response to "HUNA MTAJI WA KUTOSHA, HUKOPESHEKI? JARIBU NJIA HII YA KUFUNGA MKANDA(BOOTSTRAPPING)"
Post a Comment