JE, BIASHARA YA KILIMO CHA MATIKITI MAJI NI HADITHI ZILEZILE ZA MAYAI YA KWARE, SUNGURA NA KUKU? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JE, BIASHARA YA KILIMO CHA MATIKITI MAJI NI HADITHI ZILEZILE ZA MAYAI YA KWARE, SUNGURA NA KUKU?


MATIKITIMAJI, SUNGURA, KWARE NA KUKU
Kuna vipindi huwa zinaibuka habari zinazoshika chati sana miongoni mwa jamii, katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo hata na mitandao ya kijamii. Habari hizo mara nyingi utakuta zinahusiana kwa namna moja ama nyingine na fursa mbalimbali, kama usipokuta ni fursa ya kiuchumi, biashara, kilimo au ufugaji basi utakuta ni fursa ya kiafya au matibabu ya magojwa yasiyotibika kwa urahisi.

Hata fursa hizo nyingine bila ya kuzitaja kwa majina hapa kama wewe ni mtu mzima nadhani utakumbuka matukio hayo yalivyovutia hisia za watu wengi miaka ya hivi karibuni, wasomi ha hata wasiokuwa wasomi, viongozi na hata wananchi wa kawaida kabisa. Mifano ya hivi aribuni kabisa ni mayai ya ndege aitwaye kware yaliyosemekana kuwa na fursa kubwa kiuchumi kutokana na kudaiwa kuwa na virutubisho vingi vyevye uwezo wa kutibu na kukinga matatizo mbalimbali ya kiafya ukiwemo hata na ugonjwa hatari wa ukimwi.

SOMA: Kilichokuwa nyuma ya pazia ufugaji wa kuku wa kienyeji.

Fursa nyingine iliyovuma sana ni ufugaji wa sungura, Sungura ilisemekana kuwa mtu anaweza akatajirika ndani ya muda mfupi sana baada ya kujiunga katika miradi ya makampuni fulani yaliyokuwa yakitoa uwezeshaji kwa watu masikini kwa kiingilio cha fedha ambazo mtu unashangaa ni kwanini mtu huyu masikini asianzishe hata genge lake mwenyewe la matunda au biashara nyingine yeyote ile ndogo. Unaambiwa kuanzishiwa mradi wa sungura pamoja na kuwa mwanachama wao uchangie kwanza kiasi kisichopungua laki 2 mpaka 5 na baada ya kuchanga unasubiri mradi huuoni au hata ukiupata sungura wakizaa na kukua, hupati wa kumuuzia wakati walikuahidi mwanzoni kuwa wao ndio watakao kuwa wakiwanunua kwa kilo kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi, kwenye mahoteli makubwa, china na kwingineko.

Ikaja hadithi nyingine ya ufugaji wa kuku, unachoambiwa ni kwamba wewe anza na jogoo mmoja na tetea mmoja au matetea yasiyozidi 10 kisha unapigiwa mchanganuo wa hesabu hapo inayokuaminisha kabisa kwamba utatajirika ndani ya mwaka mmoja tu au miwili. Hugusiwi kabisa kuhusu gharama za mradi wala vihatarishi vyake. Kwa ujumla hadithi hizi ni tamu ukisikia zikisimuliwa vijiweni au hata katika mitandao mbalimbali ya kijamii, zinasisimua kwelikweli na kumfanya mtu kuchukua hatua haraka ya kujiingiza katika miradi hiyo bila kwanza ya kufanya uchunguzi wowote. Hatima yake ni watu kuishia kupoteza mitaji kidogo waliyoipata kwa shida na majuto mengi.

SOMA: Njia 7 nzuri na halali za kupata mafanikio ya haraka.

Kuna ujanja mwingine hutumiwa, watu au kikundi cha watu kujifanya wanahitaji sana kitu fulani na mara nyingi huwa ni noti, sarafu za zamani au vito vya kale vya enzi za ukoloni hasahasa hudai ni ukoloni wa enzi za Mjerumani, wajanja hao baada ya kutengeneza mahitaji hewa ya vitu hivyo kwa njia ya matangazo ya mdomo(networking), huwaacha wananchi/raia wenye uchu wa pesa wakihangaika huku na kule kuvisaka vitu hivyo kwa udi na uvumba.

Wajanja hao huwa na vitu hivyo tayari au mawakala wao wanaojifanya wanavyo hata kama ni feki, wanachukua vyuma vya kawaida na kuvipaka udongo vionekane kama ni vya zamani sana. Watu wenye tamaa ya kupata pesa haraka huishia kuuziwa vitu hivyo kwa fedha nyingi wakitumaini kwenda kupiga hela nyingi lakini mwishowe hujikuta wa kumuuzia hayupo kwani wale matapeli wakishauza mzigo walionao hutokomea au ukiwapelekea hudai mzigo ni feki siyo halisi.

Kuna aina nyingi za utapeli wenye sura za namna hii, wahusika wake kujifanya wamekuja na fursa fulani itakayowakomboa watu kumbe wao wenyewe ndio wanaotaka kujikomboa. Kuna hata walioleta mtindo maarufu wa upatu ulioitwa “kupanda fedha kisha zinaota” Huku kwetu vitu hivi, “SCAMS” kama wanavyoita tunaweza tukaona kama vile ni kitu kigeni lakini kwa nchi za wenzetu ni vitu vya kawaida na wamewahi kulizwa watu wengi sana siku za nyuma, ni kama unavyoona karata tatu siku hizi watu wengi wameshaishtukia ndio maana huoni tena wengi wakiingizwa mkenge.

SOMA: Je wajua siri nyingi za mafanikio zimejificha kwenye mambo haya madogomadogo?

Wengine hutumia teknolojia za kisasa kabisa hata humu mitandaoni kwa kuanzisha upatu au pyramid schemes ambapo watu huhamasishwa kuchangiana mitaji mithili ya hisa, mwishowe wanaonufaika ni wale waanzilishi tu na wanachama wachache wa mwanzomwanzo wanaotumiwa kama chambo huku kundi kubwa la watu likiishia kulizwa. Miradi hii huja kwa mgongo wa biashara za mtandao, network maketing au multilevel marketing nk. ingawa pia biashara za mtandao zipo nyingine chache za ukweli na si rahisi kiasi kile kumtajirisha mtu kama wahusika wanavyozipigia madebe, ni biashara inayohitaji muda wa kutosha na uwekezaji wa fedha kama zilivyokuwa biashara nyingine zozote zile.

Kabla hatujaendelea zaidi na mada yetu hii kwa undani hebu kwanza nikupe kanuni 4 au mbinu ambazo kabla hujaidaka fursa, hujaikamata fursa yeyote ile na kuamua kwenda nayo, unapaswa kwanza kuitia kwenye mzani na kuipima kwa kutumia hizo kanuni moja baada ya nyingine. Kwa kufanya hivyo fursa zote feki zenye harufu ya kitapeli utaziengulia mbali na kubakia na fursa zile tu zitakazokuwezesha kusonga mbele kipesa.

UTAITAMBUAJE FURSA KAMA NI YA KWELI AMA NI UTAPELI(CHANGA LA MACHO)?
Ukitaka kujiepusha kabisa na kutapeliwa kwa aina yeyote ile ya utapeli nilioutaja hapo juu unatakiwa uhakikishe unazingatia mambo muhimu manne yafuatayo pindi tu utakapoambiwa kuna fursa iko mahali fulani au fursa inajitokeza yenyewe mbele yako;

1. Fursa unaitafuta na siyo kuisubiri.
Matatizo ya fursa za kusubiri au kuambiwa na mtu mwingine ndiyo kama hayo tuliyokwishayaona. Miaka kadhaa iliyopita mimi mwenyewe binafsi alinifuata ndugu yangu mmoja na kunishawishi kwa hamasa kubwa tuende ‘tukapande pesa’ katika taasisi moja iliyokuwa ikishika chati sana kwa kipindi hicho. Akanitolea mifano ya rafiki zake kibao aliokuwa akifanya nao kazi sehemu moja waliokuwa tayari wamepanda mbegu na kuvuna, wengine wakanunua mpaka na viwanja.

Nilisita kidogo kuafikiana naye moja kwa moja nikamtaka kwanza anipe muda kidogo wa kutafakari fursa ile ndipo niamue kujiunga nayo. Kabla hata ile wiki haijamalizika, nikasikia redioni tangazo la serikali  kuwa baadhi ya viongozi wahusika wa ule upatu wametiwa mbaroni,  wengine wakiwa hawajulikani walipo huku ofisi zao zikiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.

2. Ifanyie kwanza utafiti na kuielewa.
Hata uambiwe fursa yenyewe ni ‘hot cake’ kiasi gani, sijui ukichelewa chelewa utakuta mwana si wako nk. usikubali, fanya upembuzi yakinifu kwanza walao kidogo kujiridhisha ikiwa kama fursa hiyo ni ya kweli, ni halali kuifanya na ina uwezo wa kukulipa.

3. Hakuna Fursa rahisi duniani.
Fursa nzuri ni ile itakayokufanya wakati mwingine ukubali kuachana na mambo yanayokupa faraja, ujitese kidogo. Ukiona fursa inayokuahidi mteremko tu pasipokuwa na changamoto ya aina yeyote ile, hiyo ni ya kuiepuka kama ukoma vile.

4. Fursa nzuri ni lazima ionyeshe na kuthibitisha mahitaji ya kweli ya watu.
Hebu ichunguze kwa makini kama kweli kuna watu halisi walio na mahitaji na kile kitu/huduma inayotokana na hiyo fursa. Unapoambiwa mayai ya Kware ni dili, je kuna ukweli kiasi gani kuwa yanao uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali? Na je, mahitaji yake ni endelevu? Ukikuta maswali hayo unapata majibu kwamba ‘SIYO KWELI’ fursa hiyo ni ya kuiogopa kama njaa.

Kwanini nimeandika hayo?, Hapa kwetu watu wengi baada ya “fursa hizo feki” kutokea katika nyakati mbalimbali, siku hizi watu wameanza kufahamu ukweli, huwezi kuwadanganya tena kirahisi ingawa lakini bado kuna watu wataingia mkenge tu ikitokea matapeli hao wakaibuka kwa sura nyingine tofauti. Fursa nyingine ni za kweli lakini wajanja kupitia mgongo wake hupenyeza hila na kuwanasa watu mithili ya buibui amnasavyo nzi.

SOMA: Njia wajanja wanayoitumia kupata matokeo bora zidi kwa kila wanachokifanya.

Kusudi hasa la makala hii ni kutaka kuonyesha jinsi ambavyo wajanja wachache kwa kupitia biashara zenye fursa nzuri hujipenyeza na kuzigeuza fursa hizo kuwa chambo chao cha kujipatia fedha kirahisi na kusababisha watu kuwa na dhana kuwa biashara hizo hazifai. Nitaelezea kidogo biashara nilizozitaja katika kichwa cha makala hii pale mwanzoni.

KWARE NA MAYAI YAKE.
Kware kama walivyokuwa baadhi ya ndege wengine waliwao na binadamu, wanaweza wakafugwa kawaida kwa lengo la mtu kujiingizia kipato au kwa lengo tu la kitoweo lakini wajanja walichomekea dhana ya uwongo kuwa mayai ya kware ni dili kubwa, kwa kuzua mahitaji ya uwongo kwa watu eti, yanatibu magojwa mbalimbali. Kwa kuwa watu walishindwa kutumia zile njia 4 nilizozitaja za kutambua fursa basi wengi wao waliingia mkenge na kujikuta wakitumia muda na rasilimali zao nyingi kujiingiza katika biashara ambayo hatimaye soko lake si endelevu.


kware

Lakini mpaka hivi leo mayai ya kware na kware wenyewe ni chanzo kizuri tu cha protini kama walivyokuwa ndege wengine kama kuku na bata na wala hawana sifa za ziada kama ilivyodaiwa na wajanja hao. Tatizo lilikuwa ni kule wajanja kutengeneza mahitaji makubwa kumbe soko lenyewe halikuwa kubwa kivile. Utakuta wajanja hao walikuwa na makusudi ya kuuza mbegu kwa wingi au utaalamu wa kuwafuga ndege hao lakini kumbe soko halisi hakuna. Ni vizuri mtu kuwa na utaalamu wa kufanya utafiti wa soko kabla hujaingia kwenye biashara yeyote ile utaepukana na utapeli mwingi wa namna hii.

SUNGURA
Ishu ya sungura nayo ilianzia huko Kenya kwa makampuni mbalimbali kujinasibu kuwa wanahamasisha wakulima kufuga wanyama hao kwa wingi halafu soko lake wao makampuni ndio watakaowajibika nalo. Makampuni hayo hukupa aina zote za utaalamu ikiwa ni pamoja na mbegu huku na wewe ukilipia gharama hizo zote. Cha ajabu gharama zao zilikuwa kubwa sana hazikulingana kabisa na huduma waliyoitoa. Makampuni hayo yalijipenyeza hadi nchini Tanzania wakaweka hata na mawakala wao humu. Mengine yalianzishwa na Watanzania walioiga kwa wenzao Wakenya.

SOMA: Soko la sungura Tanzania linakua kwa kasi.

Sungura hawajaanza kufugwa leo, ukienda kwa mfano  kule Uchaggani maeneo mbalimbali kama vile Uru, Rombo, Old Moshi na Marangu, utashangaa sana kukuta maeneo mengi wanyama hawa hufugwa sana hasa na watoto wa shule kutokana na urahisi wake kwani sungura chakula chake ni nyasi tu na majani mabichi kama matawi ya migomba, majani ya kunde  nk.

Wajanja walikuja na mbinu ya ‘Sungura wa kisasa’, wakawaambia watu kwamba sungura hao wana kilo nyingi kuliko wale wa kienyeji, kitu kingine walichotumia kuwaghilibu watu kiurahisi ni mkojo wa Sungura, walidai sungura hamna kinachotupwa kwani kuanzia manyoya yake, kucha hadi mkojo ni dili kubwa huko Uchina, walidai Wachina hutumia mkojo wa sungura kutengenezea viuatilifu vya mazao.

Iwe ni kweli au si kweli mkojo huo ni dili, lakini isingeliweza kuwa ndiyo sababu kubwa ya kumfanya mtu aingie kichwakichwa katika mradi wa malaki ya pesa pasipokujua pesa zake zitarudirudi vipi. Wakadai na hao sungura wa kisasa hula pellets huku wakianzisha viwanda vidogo vya kuzalisha pellets waendelee kuwakamua pesa vizuri.

SOMA: Ujenzi wa mabanda ya kisasa ya sungura. 

Lakini Sungura hawakuwa na soko kiasi kile kama ilivyowekwa chumvi na baadhi ya makampuni hayo na mawakala wao, ni kweli sungura wana soko la kawaida, kuna watu huhitaji wanyama hawa kwa kitoweo na hata wengine kwa ajili tu ya kuwafuga kama urembo lakini hayo masoko ya kimataifa bado hayakuwa yamefikiwa hata kama kuna baadhi ya mahoteli wanaohitaji nyama hiyo nchini. Soko la sungura nje ya nchi linawezekana lakini ni kwa utaratibu utakaoratibiwa na watu walio na nia njema, siyo wajanja wenye uchu wa kujitajirisha kupitia migongo ya watu masikini.

Miradi hii ilitakiwa wakulima ndio waianzishe na kuiendesha wenyewe lakini siyo kwa kusimamiwa na makampui ambayo huwatoza kwanza kiasi kikubwa cha fedha kama gharama za kuanzia wakati soko wanalidhibiti wao. Kulikuwa na teknolojia gani ya kipekee wakati sungura wanafugwa miaka kwa miaka kila mahali?

Sasa walioingia mkumbo huu walishindwa kutumia vizuri kanuni nilizozitaja pale juu hasa ile ya kuletewa fursa na mtu mwingine badala ya wao wenyewe kuitafuta hiyo fursa. Ufugaji wa Sungura bado ni miradi halali na inayoweza kufanywa na mtu yeyote yule kama ilivyokuwa kwa miradi ngingine ya ufugaji na wala haina kitu spesho sana zaidi ya kuzingatia tu kanuni sahihi katika ufugaji na masoko yake.

MATIKITI MAJI.
Matikitimaji kama ilivyokuwa kwa kuku na sungura, yamekuwa ni gumzo kubwa kama kweli yana fursa kubwa kiasi kile watu wengi wanavyoyatangaza. Ukweli ni kwamba tikiti maji ni tunda linalopendwa sana na lina mahitaji makubwa kwa binadamu hivyo moja kwa moja kuna fursa kubwa katika biashara hii. Pamoja na kwamba kilimo cha tikiti kina faida kubwa siyo kila mtu anaweza akamudu kulima matikiti kiasi cha kumfanya atajirike kirahisi.

Kwa kawaida biashara zenye fursa ya kutengeneza faida kubwa ndani ya muda mfupi kama ilivyokuwa kilimo cha matikiti maji, kwa upande mwingine zinaambatana na hatari kubwa. Kwa mfano ukizembea kidogo tu katika pembejeo labda mahali unatakiwa uweke mbolea mifuko 3 wewe kinjaa njaa ukaamua kubana matumizi na kuweka kamfuko kamoja, tayari biashara ya kulima matikiti utaiona chungu na msimu huo utakuwa ndiyo msimu wako wa mwisho kulima matikiti maji. Utaishia kusema matikitimaji yana faida sana ukiyasoma mtandaoni lakini shambani hayalipi kabisa. Na wakati wewe ukisema hayo, utaendelea kuona watu wakitafuna matikiti maji yaliyokolea ‘wekundu’ kila kona ya stendi na katika migahawa na masupamaketi.


KUKU.
Hakuna mtu ambaye hajawahi kufuga kuku, hata kama kwa bahati mbaya yupo lakini hawezi kudanganya kwamba hajawahi kula nyama ya kuku, kuku hutoa kitoweo kitamu sana na kinachopendwa na watu wengi duniani kote kuanzia Amerika ya Kusini, Ulaya, Asia, Afrika mpaka Australia. Uzuri na utamu wa kuku umesababisha watu wengi kujihusisha na ufugaji wa kuku wa aina mbalimbali kuanzia kuku wa mayai, kuku wa nyama, kuku wa kienyeji na hata kuku chotara kama kroiller na wengineo.

SOMA: Kati ya kuku wa nyama na kuku wa mayai ni yupi aliyekuwa na faida zaidi?

Kitu kinachoshangaza sana katika dhana nzima ya ufugaji wa kuku ni kwamba watu wengi kwa kuwa wanapenda sana kitoweo hiki na mayai yake, basi huvutiwa sana pia na ufugaji wake wakiamini kwamba watakapofuga itakuwa rahisi sana kujipatia kitoweo na mayai ya kuku. Lakini kumbe siyo rahisi kiasi kile. Unaweza kufuga kuku na wala usiweze kula nyama ya kuku na mayai kadiri upendavyo kwani kuku wana mahitaji na gharama sawasawa tu na ilivyokuwa miradi mingine yeyote ile ya kiuchumi.

Pia kuna dhana kwamba ufugaji wa kuku ni biashara inayoweza kumtajirisha mtu haraka sana, dhana hii ni kweli endapo mtu atafanya biashara ya ufugaji wa kuku kitaalamu kama inavyotakiwa akiwa na mtaji wa kutosha kama ilivyo kwa biashara nyingine yeyote ile. Kuna urahisi wake katika maeneo fulani kama vile kuku huchukua muda mfupi kuzalisha faida, kuku soko lake ni la uhakika nk. lakini bado mtu utahitajika kuzingatia taratibu zote za ufanyaji wa biashara kama inavyohitajika zikiwemo utafutaji wa soko kikamilifu ili uweze kupata faida kubwa au kutajirika.

Ujanja ujanja kwa upande wa kuku upo zaidi kwa wale wanaotaka kuuza taarifa za mafunzo ya ufugaji wa kuku, mara nyingi huwa ni semina, vitabu au softcopies mbalimbali zinazohusiana na miradi ya kuku. Kosa kubwa linalofanyika hapo ni kwa baadhi ya wahusika kutokutoa taarifa za kweli wakati wa kufanya promosheni ya products zao.

Matokeo yake mfugaji anaweza akafanya maamuzi kwa kutumia taarifa hizo potofu kisha baadae anajikuta hali ni tofauti kabisa. Unapomwambia mtu ukianza na jogoo mmoja na tetea watatu baada ya mwaka mmoja atakuwa na kuku zaidi ya elfu 2 ambao akiwauza wote moja kwa moja anauaga umasikini bila kumwambia ukweli kuhusiana na gharama na changamoto zingine mbalimbali unampotosha.

SOMA: Kilichokuwa nyuma ya pazia ufugaji wa kuku wa kienyeji

Ndio maana kwa mfano sisi tumeamua kutengeneza michanganuo ya miradi hii mbalimbali kama ya kuku, sungura, matikiti maji nk. ili kuonyesha mbivu na mbichi ziko wapi, mtu afahamu kabisa kama ataamua kufuga kuku 1000 aandae gharama kiasi gani, akiamua kulima matikiti maji heka moja, mbili nk. aandae fedha kiasi gani na atarajie kwa wastani anaweza akapata faida kiasi gani, nasema ni matarajio au makisio na wala siyo kiasi kamili atakachopata, inawezekana kukawa na tofauti kubwa au ndogo kulingana na vigezo mbalimbali. Michanganuo hii inamfanya mtu afikirie kwanza kabla ya kukurupuka kujiingiza katika mradi wowote ule wa kiuchumi kabla kwanza ya kuutafakari angalao kwa muda mfupi.

……………………………………………..

Tafadhali hii hapa chini ni kwa wale tu ambao bado hawajajiunga na Group letu la watsap(MASTERMIND GROUP) la MICHANGANUO-ONLINE. Kama tayari ulishajiunga usisumbuke kusoma.

Ukitaka kuzijua ‘ABCD’ zote za biashara, wala usije kuhangaika huku na kule ukakutana huko na wajanja bure, nimekutayarishia kitabu hiki maridhawa ambacho kitakuwezesha kufahamu njia bora kabisa za kufanya utafiti wa soko na biashara yako kwa ujumla kisha kuandaa mchanganuo wa biashara hiyo.
Mchanganuo huo siyo lazima uwe ni ule wa kitaalamu sana, unaweza kuandaa mpango wa biashara kwa levo(ngazi) yeyote uliyopo. Kitabu kinakupa uchaguzi wa kuandaa mpango rahisi au mpango wa kitaalamu, uamuzi  ni wa kwako kwani kila biashara huhitaji mipango iwe rahisi au ya kitaalamu, iwe unapanga kichwani tu au katika karatasi. Kitabu hiki kinakupa fursa ya kuamua mwenyewe ufanye nini kulingana na levo yako uliyopo.

Ukinunua kitabu changu hiki, nakupa offa kubwa ambayo baada ya mwaka huu kumalizika, offa hiyo nayo itakuwa imepita. Nitakupatia bure kabisa masomo, vitabu na semina zote zilizopita katika GROUP LETU(MASTERMIND GROUP) liitwalo MICHANGANUO-ONLINE tunalojadili masomo ya Fedha na Michanganuo kila siku. Nitakuunganisha pia na group hilo la whatsapp ikiwa utapenda. Hata kama hutumii wasap nitakutumia masomo, vitabu na semina hizo kupitia email yako.

Kitabu na vitu vyote hivyo utavipata kwa shilingi elfu 10 ambayo unalipa kupitia namba zetu hizi; 0712202244 au 0765553030 jina ni Peter Augustino Tarimo. Namba ya wasap natumia, 0765553030.  Baada ya malipo tuma kwa meseji anuani yako ya email ikiambatana na maneno, “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO”

Kifurushi(Package) cha offa nitakazokutumia sambamba na kitabu hicho ni hii hapa chini;


Kwa vitabu zaidi kutoka kwetu tafadhali tembelea, SMART BOOKS TANZANIA.


0 Response to "JE, BIASHARA YA KILIMO CHA MATIKITI MAJI NI HADITHI ZILEZILE ZA MAYAI YA KWARE, SUNGURA NA KUKU?"

Post a Comment