Safu yetu ya Ushauri wa biashara leo tumepata swali kutoka kwa
msomaji wetu aliyeko Kibaha mkoa wa Pwani na aliuliza kupitia watsap kama
ifuatavyo;
Tafadhali
naomba kufahamu kwa kina hatua mbalimbali za kufuata ili niweze kutengeneza
chakula cha kuku kiitwacho hydroponic folder, pia kama mnajua ni wapi
yanakopatikana matrei ya aluminium kwa ajili ya kilimo hiki mnijulishe.
Asanteni
sana,
JL.
Martin
Kibaha.
MAJIBU.
Asante sana ndugu Martin kwa swali lako zuri kabisa,
kwanza kabisa chakula hiki, hydroponic fodder (siyo folder), au majani haya ya
kulishia mifugo huwa hayatengenezwi kama ulivyotaja hapo juu kwamba unataka
kujua jinsi ya kutengeneza hydroponic fodder, bali mbegu huoteshwa na kumea
kama mimea mingine yeyote ile isipokuwa tu hii huwa haioteshwi katika udongo
kama mimea mingine bali ni katika vyombo maalumu au matrei yaliyotobolewa
mashimo kwa chini.
Utaalamu huu wa hydroponikia hautumiki tu katika
kutayarisha chakula kwa ajili ya wanyama au mifugo bali pia hutumika katika
utayarishaji au uoteshaji wa mbogamboga na matunda mbalimbali pia kwa ajili ya
binadamu. Lakini kwa kuwa swali hili msomaji umetaka kufahamu zaidi juu ya
namna ya kutengeneza mfumo wa kuotesha hydroponic fodder za kulishia mifugo
basi majibu yetu tutajikita zaidi katika eneo hilo la mifugo ambao kwa kiasi
kikubwa ni Ng’ombe, mbuzi, kuku, sungura, ndege wengine wafugwao, kondoo nk.
Kilimo cha hydroponic nchini (hydroponic farming in
Tanzania) kama ilivyokuwa kwa kilimo cha azolla chakula kingine cha kupunguza
gharama za ufugaji, hakijazoeleka sana na wala hakijawa maarufu kutokana na
wakulima na wafugaji wengi kutokuwa na ujuzi wa jinsi ya kutengeneza mifumo ya
hydroponikia(hydroponic systems)
HATUA
ZA KUPITIA UNAPOTAKA KUTENGENEZA MFUMO WA HYDROPONIC FODDER.
Mfumo wa hydroponikia hujumuisha chanja zilizobeba trei
kwa ajili ya kuotesha mbegu za kuzalisha hydroponic fodder. Lakini pia kwanza
ikumbukwe kwamba kuotesha au kuzalisha majani ya kuliwa na mifugo bila kutumia
udongo, hydroponic fodder siyo lazima mtu atumie vifaa vya kisasa sana na vya
bei kubwa. Mkulima au mfugaji anaweza kuandaa hydroponic fodder zake kwa
kutumia vifaa vinavyoweza kupatikana kwa urahisi kabisa katika mazingira yake
anayoishi.
Hii itategemea pia na ukubwa wa kilimo cha hydroponic
unachotaka kufanya kwa mfano ikiwa unayo mifugo michache tu kama labda ni kuku
50 na ngombe wawili au watatu huhitaji gharama kubwa sana kutengeneza mfumo
wako wa kuzalisha majani mabichi ya hydroponic fodder. Faida za hydroponic pia
naamini unazifahamu na zinajulikana na watu wengi siku hizi lakini kwa kifupi
tu ni kwamba hydroponic fodder faida yake kubwa kati ya nyingi iliyokuwa nazo
ni kumpunguzia mfugaji gharama za uzalishaji hasa zile za chakula kwa zaidi ya
asilimia 50%
Sasa hebu tuone hatua zenyewe kamili, ni jinsi gani mtu
kwa kutumia tu maji bila ya udongo anavyoweza kuotesha mbegu kwa ajili ya kupata
hydroponic fodder au majani yanayoweza kutumika kulisha mifugo karibu aina zote
wanaofugwa na binadamu.
MAHITAJI
MAKUBWA WAKATI WA UTAYARISHAJI HYDROPONIC FODDER
1.ENEO/BANDA AU NYUMBA
Hapa ni mahali utakapopanga trei au vyombo vyako utakavyotumia kwa ajili ya
kuoteshea mimea(hydroponic fodder). Hydroponic fodder hazihitaji mwanga mkali kwani zenyewe hujitengenezea nishati
na chakula zenyewe kutokana na wanga uliojaa katika mbegu, kwahiyo ni vizuri
ukapanga matrei ndani ya eneo lililokingwa na mwanga mkali wa jua.
VITALU: Hiki
ni kichanja kinachotumika kwa ajili ya kupanga vyombo au trei zako za
hydroponic fodder. Unaweza kutengeneza kwa kutumia material zozote zile kama
mbao, mabati au chuma ilimradi kiweze kubeba matrei yako vizuri. Unaweza ukapanga
kama ‘ghorofa’ kwenda juu au ukaweka kichanja kimoja tu kulingana na nafasi au
ukubwa wa mfumo wako unaotaka kutengeneza. Siyo lazima iwe ni chanja matrei
unaweza kuyapanga juu ya kitu chochote kile likichoinuka hata juu ya meza au
stuli unaweza kuweka ilimradi tu uhakikishe maji yanapochuruzika hayatuami
mahali, yanakwenda moja kwa moja katika chombo au mfereji utakaoyaondosha
katika mfumo wako wa hydroponic fodder.
JOTO:
Joto nalo halitakiwi kuwa kubwa sana wala kidogo sana bali liwe la wastani tu
kuanzia wastani wa nyuzijoto 17 mpaka 25 za sentigredi. Joto linapokuwa kubwa
kupita kiasi mbegu huchachuka na kuharibika na likiwa kidogo sana pia mimea
huota taratibu mno.
2.
MATREI(VYOMBO VYA KUOTESHEA)
Vyombo kwa ajili ya kutayarishia hydroponic fodder vinaweza kuwa ni vya umbo lolote
lile ilimradi tu kisiwe ni chombo
kinachoweza kushika kutu au kutengeneza kuvu kwa urahisi. Kwa mfano unaweza
hata kutumia hata ungo au beseni kama lile la kuogea baada ya kulitoboa matundu
kama majaribio ikiwa ndio unataka kuanza kuona jinsi hydroponic fodder
zinavyokuzwa.
Lakini aina ya vyombo vinavyokubalika zaidi kitaalamu
kutumika katika uoteshaji wa mimea, hydroponic fodder kwa ajili ya kulishia
mifugo ni matrei ya aluminium au matrei ya plastiki. Trei la aluminiam ndiyo
bora zaidi kuliko hata la plastiki ingawa gharama zake ni kubwa kidogo,
halishiki kutu wala kutengeneza kuvu inayoweza kuharibu mimea yako na hatimaye
kuwadhuru mifugo na binadamu pia.
Vipimo na ukubwa wa trei la hydroponic fodder au chombo
chochote kile utakachotumia kuandalia hydroponic fodder zako itategemea ni
kiasi gani cha majani unachotaka kuzalisha na upatikanaji wa vyombo vyenyewe
kwa mfano ikiwa vifaa(matrei) ya aluminium unaweza kuyapata kwa urahisi basi
yatumie kwani ndiyo bora zaidi kuyatumia na ikiwa vyombo au matrei ya
plastic ndiyo rahisi zaidi kwako
kupatikana basi tumia hayo ukifuata taratibu zinazotakiwa kuyafanyia usafi.
Usafi wa trei za hydroponic fodder au vyombo vingine
vyovyote utakavyotumia ni lazima
uhakikishe unakuwa ni wa hali ya juu kabisa kabla ya kuotesha mbegu zako na
ikiwa utatumia trei au vyombo vya plastiki itakubidi uongeze umakini zaidi
katika usafi huo kwani plastiki hushika kuvu kwa urahisi zaidi kuliko
aluminiam. Ni vizuri vyombo vyako au matrei ya kutayarishia hydroponic fodder
ukayasafisha kwa kutumia mchanganyiko wa maji na dawa ya kuulia vimelea na
wadudu wa magojwa kama vile dawa ya chlorine au Hydrogen Peroxide.
Clorini ni kama vile dawa unayoona ya kutibu maji(water guard) au hata JIKI ya
kufulia nguo na hupatikana kirahisi sana madukani.
Matrei pia yanatakiwa yawe na matobo upande wa chini ili
kupitisha maji unaponyweshea mimea yako maji. Matrei au vyombo hupangwa juu ya
vichanja au maumbo yaliyotengenezwa kwa ajili hiyo ndani ya chumba au eneo
ulilotayarisha.
3.MBEGU
ZA HYDROPONIC FODDER
Mbegu kwa ajili ya utayarishaji wa hydroponic fodder
zinaweza zikawa ni za nafaka aina yeyote ile imeayo lakini nafaka
zinazopendekezwa zaidi kitaalamu na zinazotoa kimea au majani bora yenye
virutubisho vingi kwa wanyama ni mtama, ngano na shayiri. Mbegu nyingine
zinazofaa ni Mahindi, Ulezi, Uwele nk.
Matayarisho
ya mbegu za hydroponic fodder.
Mbegu zinatakiwa zichaguliwe zile tu zilizokuwa bora kwa
maana ya mbegu ambazo hazijatobolewa na wadudu wala zisizokuwa na makapi .
Mbegu zilowekwe kwa muda wa masaa 2 katika maji ya dawa (chlorine) na zisafishwe vizuri kwa maji safi na kusuuzwa ili kuondoa kabisa
uwezekano wa kuota kwa kuvu au viini vingine vya magonjwa vitakavyoweza
kuathiri uotaji wa fodder zenyewe, au hata kusababisha magojwa kwa wanyama
watakaokula hydroponic fodder zako. Unaweza kutumia ndoo za kawaida za plastiki
au beseni wakati wa uoshaji au utakapoloweka mbegu zako.Hakikisha pia mbegu
zako hazina sumu yeyote wala kemikali hatarishi inayoweza kudhuru wanyama na
binadamu.
4.
MAJI
Maji safi na salama yatahitajika wakati wa kuziosha mbegu
na kunyweshea mimea ya hydroponic fodder. Maji yanayotiririka chini ya trei
siyo vizuri kuyakinga na kuyatumia tena kwa ajili ya kumwagilia mimea ya
hydroponic kwani yanaweza yakawa ni
chanzo cha mazalia ya viini vya magonjwa kwa mimea hiyo na mifugo pia kama
fangasi na bacteria kutokana na sukari inayotoka kwenye mbegu zinazomea.
Utahitaji pia kuwa na bomba dogo au hata kubwa kwa ajili
ya, unywesheaji wa maji kwani maji hayatakiwi kumwagiwa mengi kama vile
ufanyavyo katika bustani ya kawaida ya udongo bali ni matone madogomadogo juu
ya majani mithili ya mtu anayenyunyizia dawa ya kuulia wadudu.
5.
MBOLEA YA HYDROPONIC FODDER
Suala la kutumia virutubisho au mbolea ya hydroponics kwa
ajili ya kustawisha na kuongeza uzito wa majani yako ya hydroponic ni mjadala
ambao mpaka sasa hivi kuna watu wanaosema ni sahihi kutumia mbolea(virutubisho),
hydroponic nutrients na wengine hukataa kwa madai kwamba kwasababu hydroponic
fodder huchukua muda mfupi sana kuvunwa siku 4 mpaka siku 7 tu, mbolea za
chumvichumvi zinaweza zikawa na madhara kwa wanyama yanayoweza kusababisha
hatimaye matatizo kwa afya ya binadamu watakaokwenda kutumia nyama au mazao ya
wanyama hao.
Hivyo huamini kutokutumia kabisa virutubisho vya aina
yeyote ile kwa ajili ya kukuza mimea ya hydroponic fodder. Kwa wale wanaotumia
virutubisho hivyo sanasana hutumia mbolea za maji mfano ‘booster’ kupulizia
fodder mara zinapoanza kumea. Hata hivyo usipotumia virutubisho vyovyote vile
bado fodder zako zitaota vizuri tu na kukua kwani zinatumia chakula na nguvu ya
nishati kutoka katika akiba ya mbegu zinazooteshwa.
MCHAKATO MZIMA WA KUPANDA HYDROPONIC FODDER ULIVYO
Mchakato huanza na usafi wa matrei au vyombo
vinavyotumika kwa kuviosha na maji ya dawa (sterilization) ili kuzuia kuvu na
wadudu wanaoweza kusababisha magojwa. Tumia chlorine au hydrojen peroxide. Mbegu
baada ya kusafishwa kwa maji ya dawa hulowekwa kwenye maji masafi kwa muda wa
masaa 12 mpaka 24 ili kuzizimua ziweze kumea kwa urahisi . Usiloweke zaidi ya
masaa hayo kwani zinaweza kuanza kuharibika au kuoza.
Baada ya kuzitoa kwenye maji uliyolowekea, zisuuze na
kuzitandaza moja kwa moja katika trei ulizoandaa kwa makadirio ya kina cha robo
inchi kutoka sakafu ya trei au chombo unachotumia. Funika kwa kutumia mifuko,
magunia au kitambaa kwa muda wa siku
moja zitakapokuwa zimeanza kumea kisha zifunue ziendelee kuota.
Mwagilia maji kwa njia ya kunyunyizia kila siku mara 3
mpaka 4 ukitumia bomba linalotoa matone madogomadogo kama lile la kunyunyizia
dawa ya kuulia wadudu. Umwagiliaji wa hydroponic fodder ufanyike mchana tu na
wala siyo usiku kuepusha umande na ubaridi unaoweza kutengeneza kuvu.
UVUNAJI
WA HYDROPONIC FODDER
Ikiwa umeotesha hydroponic fodder kwa ajili ya kulishia
kuku(aina zote) basi utavuna baada ya siku nne 4. Na ikiwa umetayarisha kwa
ajili ya kulishia ng’ombe, mbuzi, kondoo, sungura nk. utavuna mimea yako baada
ya siku 7 mpaka 9.
Wastani wa uzito wa hydroponic fodder baada ya siku 7
mpaka 9 ni mara 7 ya uzito wa mbegu zilizotumika kuotesha. Hii ina maana kwamba
ukiotesha kilo moja ya mbegu utavuna hydroponic kilo 7 baada ya siku hizo 7
mpaka 9. Uvunaji wa hydroponic fodder
hufanyika kwa kuviringisha ‘mkeka’ wenye mchanganyiko wa mizizi na vimea vya
mbegu za hydroponic tayari kwa ajili ya kulisha mifugo wako. Mifugo kwa kawaida
hula kila kitu kuanzia mizizi, mabaki ya mbegu na majani(vimea) hawaachi kitu
chochote kile.
Naamini ndugu yangu Martine wa Kibaha Pwani majibu haya
yatakuwa yamekuridhisha na unaweza sasa ukafanya majaribio ya kutayarisha
hydroponic fodder hata ikiwa ni kwakutumia sinia, beseni au ungo na mbegu za
mahindi, mtama au ngano kisha baadae ukaamua kuandaa kiasi kikubwa zaidi cha
mimea hii ya kulishia mifugo hasa kuku isiyohitaji udongo kabisa.
……………………………………………..
MKOMBOZI
CHICKS PLAN 3PACK
Kwa mahitaji ya michanganuo ya kuku aina zote, wasiliana
na sisi, tuna michanganuo ya kuku wa mayai, kuku wa nyama na kuku wa kienyeji. Kifurushi
kizima bei yake ni shilingi elfu 10 tu na tunakutumia kwa njia ya email kama
PDF files au softcopy. Pamoja na offa ya kujiunga na group la MICHANGANUO-ONLINE
bila malipo ya ziada.
SIMU: 0712202244
WASAP: 0765553030
I want you to thank for your time of this wonderful read!!! I definately enjoy every little bit of it and I have you bookmarked to check out new stuff of your blog a must read blog! Airco
ReplyDeleteI have read your article; it is very informative and helpful for me. I admire the valuable information you offer in your articles. Thanks for posting it. Aluminium ramen en deuren
ReplyDeleteI wish for the great of success in all of our destiny endeavors
ReplyDeleteTheir team presented helpful ideas for new features discuss that enhanced the quality of the product.
ReplyDeleteI am unable to read articles online very often, but I’m glad I did today. This is very well written and your points are well-expressed. Please, don’t ever stop writing. marquise diamond exporter
ReplyDeleteAhsante na nashukuru sana kwa mafunzo haya, ila nina swali kwenye mbegu. Swali langu ni unaoyesha aina moja ya nafaka katika trei au unachanganya nafaka tofauti tofauti kwenye trei unayooteshea.
ReplyDelete