Hili ni swali
alilonitumia mfuatiliaji wa blogu hii kwa kutumia njia ya wasap na swali lake
lilikuwa hivi bila kuongeza kitu wala kupunguza; (huwa hatuchapishi jina la muuliza swali kama hajatupa idhini)
Asante,
mimi naitwa ‘Y’. naomba unielekeze mbinu za kumtambua
mteja katika biashara ya
umachinga.
MAJIBU:
Wewe kama
mfanyabiashara unapaswa kabla ya kuanza kuifanya biashara yako kufahamu kwa
uhakika wateja wale unaotaka kuwauzia biashara yako. Kwa kifupi kabisa
unatakiwa kufanya utafiti ili kujua bidhaa au huduma utakazouza, wateja wake ni
kina nani. Kuna njia nyingi unazoweza kuzitumia ili kuweza kuwajua wateja wa
biashara utakayoifanya na kubwa ni ile ya kuangalia ni matatizo gani yanayosumbua
sana watu kisha wewe ukaja na suluhisho la matatizo hayo.
Katika biashara ya
umachinga unaweza ukawatambua wateja wako aidha kwa kuifanya biashara hiyo na
kupata uzoefu kidogo au pia unaweza kuwatambua wateja kwa kuwauliza
wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara ya umachinga kama unaotarajia kuifanya.
Kila biashara huwa ina
kundi fulani la wateja ambalo wewe mfanyabiashara ndiye unayepaswa kulijua
kulingana na biashara yako unayoifanya. Kwa mfano ikiwa unauza nguo za watoto,
basi wateja wako wakubwa watakuwa ni kina mama hasa wale waliokuwa na watoto
wadogo.
Ukitaka kutambua mteja
wako kwanza fahamu wewe unauza kitu gani na kitu hicho kitawafaa au
kuwanufaisha watu wa aina gani hasa. Hivyo utakapokutana na mtu wa kundi
hilo unalolilenga basi moja kwa moja utajua kuwa mtu huyo ana uwezekano wa kuwa
mteja wako.
Mara nyingi wateja wenyewe
huwa hawafahamu kabisa ni kitu gani wanachokitaka mpaka pale watakapogundua
kuwa kuna mtu mwenye suluhisho la tatizo fulani linalowakabili, kwa hiyo wewe
ng’ang’ana zaidi na kutambua shida za watu kisha watafutie suluhisho la shida
hizo na hapo moja kwa moja utakuwa umeshatambua wateja wako ni akina nani.
Ukiwajua wateja wako
itakuwa rahisi zaidi kuwauzia kuliko kubahatisha sokoni kama mtu anayejaribu
kukamata senene gizani. Kama mmachinga ukishawafahamu wateja wako vizuri
utakuwa ukifanya biashara yako kwa malengo na utakuwa tofauti na wamachinga
wengi wanaozunguka wakibahatisha wateja mitaani. Zunguka mtaani lakini ungali
ukijua kabisa unawafuata kina nani kwenda kuwauzia, si kila mtu ni mteja wako.
Asante sana ‘Y’, ni
matumaini yangu kuwa majibu haya yatakuridhisha, na ikiwa bado basi unaweza kuuliza zaidi
illimradi maswali yawe mafupi.
0 Response to "JINSI YA KUMTAMBUA MTEJA KATIKA BIASHARA YA UMACHINGA (NAOMBA USHAURI)"
Post a Comment