Kukuza biashara
kutoka chini kabisa ifike hatua ya juu zaidi kunahitaji juhudi kubwa na ubunifu
kutoka kwa mjasiriamali mwenyewe ambaye anapaswa kujifunza mbinu za kukuza aina
ya biashara anayoifanya. Aina za biashara mbalimbali huhitaji pia mbinu tofauti
za ukuzaji kulingana na vigezo mbalimbali kama vile mazingira biashara inapofanyika,
aina ya wateja, ushindani uliopo na fursa mbalimbali za kimasoko na kimauzo.
Ili biashara
iweze kupata mafanikio haraka na makubwa, mjasiriamali ni lazima afahamu jinsi
ya kukuza mtaji mdogo aliokuwa nao na kuigeuza biashara hiyo ya mtaji mdogo
aliyoanzisha kuwa biashara kubwa inayolipa vizuri. Hapaswi kabisa kuziogopa au
kuzikwepa changamoto za ujasiriamali bali kuzitumia kikamilifu kanuni za
ujasiriamali katika kuzipunguza au kuziondoa kabisa changamoto hizo.
Mwanzoni mtu
kweli anaweza akaona ugumu kwani itambidi kuvaa kofia zote peke yake
nikimaanisha, mjasiriamali kushughulika na mambo mengi mwenyewe kama vile
kufanya kazi za mauzo, maswala ya kodi, kuhudumia wateja na kufanya kazi zote
zinazohusiana na uendeshaji wa biashara bila msaada kutoka kwa mtu mwingine
yeyote yule. Hakuna wa kumsaidia na mwisho wa siku anajikuta yupo hoi huku muda
mwingi ukiwa umekwisha.
Lakini kando ya
ugumu wote nilioutaja ikiwa mjasiriamali ataamua kukaa chini akavuta hisia zake
na kutazama mambo kwa mapana anaweza kwa urahisi kugundua njia anazoweza
akazitumia kuikuza biashara yake haraka zaidi na kwa wepesi huku akitengeneza
pesa nzuri chapchap na kuwaacha nyuma hatua nyingi mamia ya biashara kama
yakwake.
Ingawa kuna
mbinu na mikakati mingi inayowezakutumiwa kukuza biashara ndogo haraka, lakini
mbinu hizi zifuatazo zinaweza zikaifikisha biashara yeyote ile hatua nyingine
kabisa na kwa wepesi. Pamoja na kwamba nyingi ya mbinu hizi mwanzoni zinaweza
kumgarimu mtu muda wake mwingi lakini mwishoni zinaweza kuleta mabadiliko
makubwa kwa maana ya mauzo na faida kwa ujumla. Ni kama tu ilivyokuwa kwa mambo
mengine yote katika maisha kwamba ni lazima mtu awekeze kwanza muda na hata
fedha ndiyo aje kuchuma matunda baadae. Mjasiriamali hapaswi kulenga sana
mafanikio ya muda mfupi, bali katika mafanikio ya muda mrefu huku akizingatia
zaidi faida anayoipata mteja kama msingi mkuu wa mafanikio yake.
Mbinu hizo ni
hizi zifuatazo;
1. Tengeneza faneli yako ya mauzo.
Natumaini Faneli
unaijua, umewahi kununua mafuta ya taa dukani? Basi kile chombo chenye mdomo wa
duara mpana juu halafu chini kinapoingia kwenye chupa ni chembamba. Biashara
yeyote ile inatakiwa kuwa na kitu kama hiki, mahali ambapo wateja huja na
kukusanyika wengi kisha baadae ‘kupenya’ taratibu na kununua bidhaa/huduma
zako. Na biashara yeyote ile iwe ni ya mtandaoni au hata zile biashara za
kawaida mfano biashara ya kuuza nguo za mitumba nazo zina uwezo wa kuwa na faneli.
Biashara kwa
mfano hizi za kwenye mtandao wa intaneti, faneli yako inaweza kuwa ni
tovuti(website), blogu, email list, group la wasap, nk. kote huko unavutia
wateja waje kujua ni nini unachotaka kuwauzia wakipendezwa nacho basi hujipenyeza
kwenye mdomo wa faneli yako na kuja kununua, wasipovutiwa huzungukazunguka
kwenye faneli na ‘kusepa’ zao kwingine watakaporizika kupenya.
Kwa biashara ya
kawaida kwa mfano duka la mtaani la kuuza urembo na vipodozi, faneli yake ya
mauzo ni fremu yenyewe ya duka au eneo mjasiriamali anapotandaza bidhaa zake za
urembo na vipodozi ili ziweze kuonekana na wateja watarajiwa kabla hawajachukua
maamuzi ya kununua. Ikiwa mjasiriamali hatakuwa na sehemu kama hiyo inamuwia
vigumu sana kuuza bidhaa au huduma zake kikamilifu.
Faneli ya mauzo
inaweza ikafananishwa na sumaku yako ya kuvuta wateja waje kununua kile
unachouza na unaweza hata ukatengeneza faneli zaidi ya moja kulingana na uwezo
na rasilimali ulizokuwa nazo.
2.Tafiti washindani wako.
Unapoamua
kuingiza sokono biashara yako iwe ni bidhaa au huduma, unatakiwa kuwajua vizuri
washindani wako(wale wanaouza kitu kinachofanana na cha kwako) Nenda katika faneli
zao chunguza ni nini wanachokifanya na utagundua ni nini wanachokuzidi nacho
kisha na wewe utakitumia kitu hichohicho huku ukikifanyia maboresho zaidi. Hii
ni njia rahisi sana ya kuikuza biashara yako haraka.
3.Tengeneza mfumo wako imara wa huduma kwa
wateja utakaokuwezesha kuwa na wateja wa kudumu.
Kumpata mteja
mpya ni vigumu mara tatu(3) zaidi kuliko kumtunza mteja yule uliyekuwa naye
tayari. Halikadhalika kumuuzia mteja mgeni kitu ni vigumu zaidi kuliko kumuuzia
mteja ambaye tayari ulikwishamuuzia tena mara nyingine. Jitahidi sana kuweka
vivutio kwa wale wateja uliokuwa nao tayari ili mauzo yako yaongezeke mara dufu
na hivyo kukuza biashara haraka.
4.Vumbua fursa mpya katika biashara yako
Kwa kutafiti na
kulitambua vizuri soko lako(wateja wako) unaweza kubaini fursa za masoko zaidi
ambazo unaweza kuuza bidhaa au huduma zako. Kwa mfano tuseme ulikuwa ukisambaza
vifaa vya steshenari mashuleni, unaweza pia kubaini mahitaji ya bidhaa za
chakula kama mahindi, maharage, mchele, ngano, sukari na mafuta ya kula kwa
shule za kulala boarding au hata zile shule zilizokuwa katika maeneo ya
vijijini wanakokula mlo wa mchana.
5.Tengeneza orodha yako
ya wateja na mawasiliano yao(Email list)
Hasahasa orodha
ya baruapepe(email list) ni kwa zile biashara za mitandaoni zaidi lakini pia ni
jambo zuri likifanyika hata kwa zile biashara za kawaida. Kuwa na orodha ya
wateja wako na jinsi ya kuwasiliana nao iwe ni kwa email, facebook, watsap au
mtandao wowote ule wa kijamii kama tulivyoona kwenye faneli ya wateja au sumaku
ya wateja, ni njia moja ya kisasa kabisa na iliyokuwa bora zaidi ya kukuza
haraka biashara yeyote ile duniani katika nyakati tunazoishi sasa.
6.Tengeneza ushirikiano wa kimkakati.
Ushirikiano wa
kimkakati na wadau mnaoendana utakuwezesha kupanua zaidi wigo wako wa kupata
wateja kwani kushirikiana na makampuni na watu wanaofanya biashara zinazofanana
na ya kwako kutakufanya ujuane na wateja ambao isingekuwa rahisi kuwafahamu
mwenyewe. Siku hizi kuna makundi(magroup) mbalimbali mitandaoni ambayo
hurahisisha sana ushirikiano wa namna hii.
7.Tumia majukwaa, mbalimbali.
Kwanini usitumie
majukwaa yaliyojaa tele kutangaza biashara yako? Hapa kwetu kuna facebook,
watsap, twitter, Instagram, forums na blogs mbalimbali. Na mengi ya haya
majukwaa ni bure kabisa kujitangaza hawachaji hata senti tano.
8.Wape wengine leseni wakuuzie biashara
yako.
Unaweza kukuza
biashara yako kirahisi sana kwa kuamua kutoa idhini kwa watu wengine kuzalisha
au kuuza kile unachokifanya wewe. Kwa mfano umebuni bidhaa fulani ya urembo au
kipodozi na kuipa jina lako. Unaweza ukatafuta watu au mtu mwenye uwezo
atakayeweza kuzalisha bidhaa hiyo kwa wingi ikiwa ni pamoja na kuisambaza kwa wingi huku jina lako
lilelile uliyoipa mwanzoni likiendelea kutumika kisha mnakubaliana wewe upate
asilimia fulani ya faida itakayotokana na biashara hiyo.
9.Kununua biashara nyingine.
Unaweza ukaamua
ili ukue haraka zaidi ukanunua biashara zile zinazoshindana na ya kwako au hata
kuungana nazo mkatengeneza biashara moja kubwa. Nayo hii ni njia mojawapo ya
kukua haraka kibiashara.
10.Jitanue kimataifa.
Unaweza kuuza
hata nje ya mipaka ya nchi au mkoa wako ulipo. Kuvuka mipaka kunaweza kuonekana
ni jambo gumu na linalohitaji gharama kubwa lakini ukweli ni kwamba hakuna
biashara zilizo na faida kubwa na ya haraka kama biashara za masafa marefu,
cheki wanaokwenda China, Dubay au hata wanaosafiri kwenda kuchukua na kupeleka
bidhaa hapo Zanzibar wanavyofanya biashara za uhakika ukilinganisha na baadhi
ya watu wanaong’ang’ania tu kariakoo au Manzese na sehemu nyingine jijini Dar es salaam.
Mbinu hizo kumi
hapo juu ni kati ya mamia ya mbinu mbalimbali zinazoweza zikatumiwa na
wajasiriamali na wafanyabiashara katika kukuza biashara zao haraka na kwa
ufanisi mkubwa.
……………………………………
Ndugu msomaji
wa makala hii, naandika pia makala nzuri za kuelimisha katika group la whatsap
la Michanganuo-online kila siku. Mle tunazingatia zaidi makala zihusuzo mzunguko wa fedha
katika biashara na michanganuo ya biashara bunifu zenye fursa za kipekee.
Karibu sana jiunge nami huko kama ulikuwa hujajiunga.
Kiingilio ni
sh. Elfu 10 tu na unapata uanachama wa kudumu unaoambatana na offa ya kitabu
mashuhuri cha MICHANGANUO
YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, michanganuo maarufu 3 ya
kuku(MKOMBOZI
CHICKS PLAN 3PACK) pamoja na mfululizo wa masomo yote yaliyopita tokea
Januari mwaka huu.
Kujiunga tuma
kiingilio chako sh. Elfu 10 kupitia namba 0712202244 au
0765553030 jina hutokea Peter Augustino Tarimo, kisha tuma
ujumbe kwa wasap 0765553030 au meseji ya kawaida usemao, “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO” na nitakuunganisha muda huohuo pamoja na kukutumia kila kitu. Ikiwa
hutumii watsap hamna tatizo kwani masomo tunakutumia pia kwenye email
utakayotutumia.
Leo hii tarehe
13 Septemba 2018 usiku saa 3-4 katika Group tutakuwa na somo kubwa sana
lisemalo “KUKOPA
FEDHA ILI UKALIPE DENI KUNAWEZAJE KUBORESHA MZUNGUKO WAKO WA FEDHA KWENYE
BIASHARA? Mada hii muhimu tutazungumzia mambo mengi mazito
yanayowasumbua vichwa wajasiriamali wengi kuhusiana na kukopa fedha kwa ajili
ya kuboresha biashara zao.
Somo litajibu
maswali mengi magumu kama vile ni kwanini wajasiriamali wengi wanastruggle(wanahangaika kimtaji
mitaani) ili-hali mapesa yamejaa tele mabenki na katika taasisi nyingi za fedha
hayana hata wa kuzichukua.
Usikose mtu
wangu wa nguvu kama tayari umejiunga na group hilo, na kwa wewe ambaye bado haujajiunga
muda upo wa kuhakikisha unawahi mada ikiwa live motomoto, usisubiri kuja kusoma
kama makala iliyopita haipendezi sana japo ndio, unaweza kupata somo zima kama
lilivyo na mengine yote yaliyopita katika mpango(programu) yetu ya mwaka wote
wa 2018, lakini kupata kitu ‘Mubashara’ ndiyo mpango mzima.
Kuweza kupata
maelezo juu ya vitabu mbalimbali kutoka Self Help Books Tanzania ltd, bonyeza
maandishi haya yafuatayo; >>SMARTBOOKSTZ
Wow
ReplyDelete