Mjasiriamali kujijengea vitegauchumi tofautitofauti ndio
njia bora zaidi ya kujihakikishia mzunguko chanya wa fedha muda wote. Hata
hivyo mtu kujijengea vitegauchumi hivyo siyo jambo linaloweza kufanywa kwa siku
moja au mbili hasa kwa wale wajasiriamali vijana au wanaoanza na ambao
hawaelewi waanzie wapi. Mjasiriamali yeyote yule mdogo au mkubwa huna budi
kuzijua mbinu za kufikia malengo yako kifedha katika maisha.
Kabla mtu yeyote hajaanza kujikusanyia utajiri kwa njia
ya uwekezaji vitegauchumi anapaswa kwanza afahamu tofauti iliyokuwepo kati ya
rasilimali(asseti) na Madeni(liabilities). Watu wengi hutumia pesa zao kwa vitu
wanavyodhania kuwa ni rasilimali/mali na kwamba vinaweza hatimaye kuwafanya
wawe matajiri lakini kumbe vitu hivyo huzidi kuwadidimiza kwenye lindi la
umasikini kwa kuwabebesha mzigo mzito wa gharama na madeni. Watu hawa huishia
kukata tamaa kabisa ya kufanikiwa maishani.
Nitatolea mfano mmoja, mtu anaweza akaamini kwamba kwa
kujenga nyumba basi atakuwa ameshawekeza kitegauchumi au rasilimali itakayomhakikishia mzunguko chanya wa fedha
hapo baadae lakini ukweli ni kwamba kujenga nyumba itategemea ikiwa nyumba hiyo
umejenga kwa malengo gani. Nyumba unayojenga itakuwa rasilimali(asseti) endapo
tu itakuwa na uwezo wa kukuzalishia pesa badala ya kukumalizia pesa.
Nyumba unayoilipia kodi ya majengo na gharama nyinginezo
kama za ukarabati, umeme na maji pasipo kukuingizia hata senti tano hiyo siyo
asseti bali ni deni(liability).
Ikiwa utajenga nyumba na kisha ukaweka wapangaji
watakaokuwa wakikulipa kodi kila mwisho wa mwezi basi nyumba hiyo unaweza
ukaiita rasilimali(asseti). Hali ni hivyohivyo ilivyo kwa yule anayenunua kitu
kama gari. Gari lina gharama kama vile, gharama za bima, gharama za mafuta na
hata matengenezo inapotokea limeharibika. Ikiwa basi gari hilo haliingizi fedha
yeyote, hiyo siyo rasilimali bali ni deni kwani linakufanya utoe fedha
ulizokuwa nazo badala ya kukuingizia pesa. Tena mbaya zaidi ni kwamba kitu kama
gari lina tabia ya kupoteza thamani yake kidogokidogo kadiri muda nao
unavyosonga mbele.
Unapofahamu kitu hiki mapema, ndipo unapoweza kuwa makini
na katika nafasi nzuri zaidi ya kukwepa kuwekeza mtaji/pesa zako zote kwenye
vitu vinavyoweza kukugharimu zaidi siku za baadae. Utatambua ni kwanini
unatakiwa kujijengea rasilimali za kweli katika uwekezaji wako wa kifedha na
jinsi ya kutimiza malengo yako ya kujiongezea utajiri na mali zaidi.
Faida
za Mjasiriamali kujijengea Rasilimali.
1.Rasilimali
hukuongezea fedha zaidi.
Kitu chochote kile utakachokinunua na kikakuzalishia
faida(kuongeza mzunguko wako wa fedha) kitu hicho ni rasilimali. Rasilimali
inaweza ikawa ni hisa, hati za dhamana(bond), mashine, ardhi ama hata biashara
yeyote ile yenye uwezo wa kuzalisha faida inaweza kuwa rasilimali. Lakini ikiwa
biashara inakuongezea gharama na mzigo wa madeni hiyo haiwezi tena kuwa ni
rasilimali bali ni deni.
Njia rahisi zaidi ya kutajirika duniani ni kuhakikisha
unatumia fedha zako kununulia rasilimali. Hata rasilimali watu kwa mfano,
usikubali kukaa na mfanyakazi yeyote yule asiyeongeza chochote katika
kuhakikisha mafanikio makubwa kwenye biashara yako.
Kabla hujanunua kitu chochote hebu jiulize kwanza
mwenyewe ikiwa kama kweli kitu hicho kina uwezekano wa kuzalisha kipato au
kuchukua pesa kutoka mfukoni mwako. Lengo lako linapaswa kuwa ni kujilimbikizia
rasilimali zinazoweza kukutengenezea fedha za ziada kuliko kukukaushia fedha
kupitia gharama itakazokupa. Ikiwa utakuwa na uwezo wa kutengeneza kipato cha
ziada kila mwezi ni vizuri zaidi kwani mzunguko wako wa fedha utakuwa chanya.
Hii ni mbinu ya kufanikiwa katika biashara au uwekezaji wowote ule.
2.Rasilimali
huongezeka haraka zaidi unapojiwekea misingi imara ya utunzaji wa pesa.
Kwa wale wanaofanikiwa kujijengea rasilimali za uhakika,
utakuta pia kabla ya hapo walianza kwanza kujijengea misingi madhubuti ya kifedha. Wana nidhamu ya hali ya
juu kwenye pesa, ni wavumilivu katika kujiwekea akiba na wanafahamu vyema jinsi
ya kujiwekea malengo yanayoweza kutimizika
kama vile kujiwekea akiba ya kutosha kabla ya kuamua kuwekeza katika miradi na
vitegauchumi.
Siyo rahisi kuishi maisha pasipo kupitia matukio
yasiyotarajiwa kama vile majanga mbalimbali ya asili mfano mafuriko nk. Ni
hivyohivyo na kwa upande wa biashara au uwekezaji rasilimali, kuna vipindi
mambo huweza kuwa magumu na biashara
kushuka lakini kitu kikubwa cha kujiuliza, ni lini na ni kwa kiasi gani hali hiyo itaweza
kukugharimu. Hapa unatakiwa kuweka mipango ya kifedha(makisio) pamoja na kuweka
akiba ya pesa. Hii itakupunguzia sana hatari ya kuingia madeni yasiyokuwa ya lazima
hata kama majanga na vikwazo vitajitokeza.
3.Rasilimali
nyingi hukupa uhuru tofauti unaoutaka.
Kumiliki rasilimali zinazoweza kubadilishwa kuwa pesa
taslimu haraka kama vile hisa au vito vya thamani kunakupa uhuru mkubwa pale
utakapohitaji fedha haraka kwani hautapoteza muda mwingi kutafuta mteja. Lakini
kwa rasilimali mfano wa nyumba au ardhi, hizi ingawa zinaweza zikachukua muda
mrefu kuuzika lakini pia siyo mbaya kwani zinaweza kukupa uhuru mwingine wa
kifedha ambao utahitaji kuwa na subira kidogo.
Kwahiyo basi ikiwa una uwezo wa kumiliki rasilimali
tofauti tofauti na zitakazokupa uhuru tofauti pia unaweza kuamua kuziuza muda
wowote ule rasilimali hizo ikiwa utaona kama zitakupa faida nzuri na kuamua
kununua nyingine ukitaka.
HITIMISHO.
Ili kuweza kuwa mwekezaji uliyebobea, jielimishe vizuri
mambo mbalimbali kuhusiana na uwekezaji
kusudi uweze kuwa na mikakati sahihi iakayokuwezesha kufanya maamuzi
mazuri pale soko litakaposhuka au kupanda na mwisho utajikuta ukifanikiwa
katika kila uwekezaji utakaoamua kuufanya.
…………………………………
Ndugu msomaji wa makala hii,
Makala zinazohusiana na fedha na mzunguko wa fedha katika biashara
zetu nazitoa pia kila siku katika group la wasap la michanganuo-online. Ikiwa
unapenda kujifunza zaidi karibu uje ujiunge kwa mchango kidogo wa sh. Elfu 10.
Unapata pia masomo yote yaliyopita katika group hilo, semina, vitabu na
michanganuo kamili bunifu ya biashara tuliyowahi kuandika.
Somo la leo Septemba 21 2018 ni hili hapa chini;
"KWANINI WANAOSEMA NIKISHINDA MILIONI 100 BAHATI NA SIBU NITAFANYA HIKI NITAFANYA KILE NI WAONGO?"
Namba zetu ni:
0712202244 wasap: 0765553030
Asante sana
Peter A. Tarimo
0 Response to "Mbinu za kufanikiwa kufikia malengo katika uwekezaji wowote utakaofanya."
Post a Comment