Ikiwa leo hii tarehe 5 Oktoba ni kilele cha wiki ya
huduma kwa wateja Duniani, wajasiriamali wale wadogo wanaochipukia au wale
wasiokuwa na mitaji mikubwa wanapaswa wajitathmini juu ya namna wanavyotoa
huduma zao kwa wateja wa biashara zao ikizingatiwa kwamba biashara ndogondogo
nyingi hujiendesha kwa kurudisha faida inayopatikana kwenye mtaji ikiwa
zitahitaji kukua na kuondoka pale zilipo.
Kinyume chake ni biashara nyingi ndogo kuendelea kufa
muda mfupi baada ya kuanzishwa kwake. Kitabu mahsusi cha biashara za rejareja
hususani duka la rejareja, (MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA), katika
sura ya 1 ukurasa wa 29 kimezungumzia miongoni mwa vitu vingine
vingi namna bora ambao muuzaji au mmiliki wa duka la rejareja na biashara zote
nyingine za rejareja anavyopaswa kuwahudumia wateja wake kwa weledi.
Mteja anahitaji kukaribishwa vizuri mara anapotokea tu
kwenye biashara hivi na si kuanza kuonyesha kukereka. Hata ikiwa ulikuwa
unakula kitu kwa mfano, acha mara moja, kwanza pale kwenye biashara kipaumbele
chako kikubwa siyo kula bali umekaa pale kwa ajili ya kuwahudumia wateja.
Mwonyeshe mteja tabasamu, kwa kifupi
kabisa ni kwamba ndani ya sekunde 5 mpaka 10 unatakiwa tayari uwe umemwonyesha
mteja kuwa unamjali. Mwisho mfungashie vizuri mteja kile ulichomuuzia kwa
kutumia kifungashio kizuri na siyo bora kifungashio.
Acha kumwekea mteja vipingamizi na figisufigisu zisizokuwa
na maana kama vile, “hamna chenchi” “sina kifungashio” “mkopo kasafiri”, “hili
siyo duka la walevi” nk. tafuta maneno ya busara ya kuwaelewesha wateja kile
unachotaka kuwaambia bila kuwakwaza ukizingatia kwamba mteja ni rasilimali
kwako anaweza kuja kununua tena siku nyingine au kukuletea wateja wengine na
hivyo kuihakikishia biashara yako ndogo mtaji wa uhakika. Hata ikiwa ni mlevi
au haendani na imani au itikadi yako mwelekeze kwa upole aelewe na wala si
kumdhihaki.
0 Response to "Jinsi ya kuendesha biashara ya duka, kwa mtaji wa kauli nzuri kwa wateja."
Post a Comment