Unajua katika mitandao hii ya kijamii kuna aina fulani ya uandishi
unaotokana na matumizi ya simu za kisasa smartphone kwa mfano utakuta penye “Z”
mara nyingi panawekwa ‘X’ kimakosa kutokana na ukaribu wa herufi hizo, lakini
ndio imekuwa kama kawaida mtu ukikuta hivyo mara moja unatambua mwandishi
alimaanisha ‘z’ na wala siyo ‘x’. Vilevile katika safu hii hatutaji jina la
muulizaji swali pasipo ridhaa yake ndio maana tunaamua tu kuweka herufi yeyote
kwenye nafasi ya jina.
Swali lake original aliuliza
hivi;
mimi ningependa kkufanya biashara ila shida
mtaji pamoja na hayo hata psa ya kununua vitabu vya kujifunzia juu
yaujasliamali sina nifanyeje. naomba ushauri
MAJIBU
KWA SWALI HILO NI HAYA HAPA;
Hellow
B ,
Kwanza nikushukuru
sana kwa kufuatilia makala zangu na nimefurahi pia kusikia kuwa unapenda sana
kuanzisha biashara ila tatizo ni mtaji na kukosa pesa za kununulia vitabu vya
ujasiriamali kwa ajili ya kujifunza na kujiendeleza zaidi. Nikutie moyo kwani mpaka
hapo ulipofikia ijapokuwa bado uwezo wako wa kuanzisha biashara ni mdogo,
umepiga hatua kubwa tu kwa kuweza kusoma makala katika blogu yetu hii ya jifunzeujasiriamali.
Usijikune usipofikia
kama ukweli huna fedha za kununulia vitabu zaidi, na inawezekana kuwa ni kweli
hauna kwani umesema hata biashara haujaanza bado kutokana na kuwa mtaji huna.
Huwezi ukanunua kitabu cha sh. Elfu 5 au hata elfu 10 wakati kipato hakiruhusu,
ni lazima kwanza upiganie mahitaji yako yale ya msingi kama binadamu.
Mimi ningekushauri
kama unapenda kuja kuanzisha biashara, endelea kwanza kusoma makala mbalimbali
kwenye blogu yetu ya jifunzeujasiriamali pamoja na kusoma makala tunazokutumia
kwa njia hii ya email, bado makala hizi zinaweza kuwa msaada mkubwa kwako kwani
nyingi zinalenga kumjengea mjasiriamali mdogo uwezo wa kupata mtaji kwa njia za
kawaida kabisa bila kukopa wala kumdhulumu mtu. Na habari njema ni kuwa makala
hizo hulipi hata senti tano zaidi tu ya kulipia bundle katika simu yako ya
mkononi au kompyuta unayotumia kusomea.
Ikiwa utakuwa
ukifanyia kazi kwa vitendo yale yote utakayojifunza ndani ya makala hizo,
taratibu utajenga uwezo wa kijasiriamali na kuanzisha biashara ndogo. Kidogokidogo
biashara yako hiyo ndogo itakua na utajikuta mwenyewe tu ukihitaji kujifunza
zaidi na wala hutajali gharama bali utanunua vitabu zaidi kwani utakuwa ndio
wakati wake umefika.
Na kwa sababu sasa
utakuwa ukiingiza kipato kidogo utaweza kugawa kipato hicho asilimia fulani kwa
ajili ya kujiendeleza kimaarifa, ubongo pia unahitaji kuendelezwa na kulishwa
sawa tu na kama ilivyokuwa kwa mwili wako au hata unavyozitunza nywele zako,
kucha, kope, na viungo vyote vya mwili kwa ujumla ili viendelee kupendeza siku
zote za maisha yako hapa duniani.
Hilo ndilo jibu nililompatia
msomaji mwenzetu huyu. Lakini kwa faida ya wasomaji wengine wote pia ningependa
kuongezea hapo mambo machache kidogo kuhusiana na suala hili la usomaji vitabu
hasa vitabu vya ujasiriamali, biashara na mafanikio kwa ujumla.
SOMA: Biashara ndogo za mtaji mdogo kuanzia elfu mbili 2, kumi mpaka laki moja unazoweza kuanza zikakutoa.
Mara nyingi baadhi ya watu wanaponunua vitabu kutoka
kwangu nikifanikiwa kuonana nao ana kwa ana huwa wananiuliza hivi, “Bwana Peter, hivi nikimaliza kusoma kitabu
chako hiki chote ndio nitakuwa nimekuwa mjasiriamali kamili?” Huwa nacheka
na kuwajibu,
“hapana ujasiriamali ni mchakato usiokuwa na mwisho na kila unapomaliza
hatua fulani mbele kuna hatua nyingine inayofuata cha msingi ni kujua kwanza
ABC za Ujasiriamali kupitia kitabu kama hiki cha kwangu halafu mbele ya safari
siyo lazima uendelee kujifunza kupitia vitabu peke yake, kuna njia nyingi za
kujifunza ikiwemo njia ya UZOEFU kwa fani au tasnia uliyopo.”
Hata walioandika
vitabu si kama kila kitu walipata kwenye vitabu hapana, vingine ni uzoefu
wao katika kile walichoandika.
USIWE MTUMWA WA VITABU!
Unaweza kunielewa
vibaya lakini hii napenda sana kuitumia kwa sababu ni watu wengi mno hulalamika
tokea wameanza kufuatilia vitabu hivi vya biashara na mafanikio miaka imekatika
mingi na maktaba zao zimejaa lakini cha ajabu hamna hatua zozote walizopiga
kiuchumi kama walivyotarajia. Kama uliwahi kusoma kitabu changu ninachotoa bure
kisemacho, “JINSI YA KUJIFUNZA ELIMU YAPESA NA MAFANIKIO KWA UFANISI” unaweza ukanielewa vizuri zaidi.
Vitendo ndio kila
kitu, mafanikio ya kiti chochote hayatajali umejifunza kwa kiasi gani kama
haujachukua hatua kutekeleza mchakato fulani, tuseme labda umejifunza jinsi ya
kutengeneza sabuni za aina mbalimbali, ikiwa ujuzi huo utaufungia kichwani bila
kuutia katika matendo, utaishia tu kumlalamikia mkufunzi aliyekufundisha
kutengeneza sabuni huku ukidai kala pesa zako bure, kumbe kosa ni la kwako
hukuchukua hatua za kufanya biashara ya kutengeneza sabuni.
WENGINE HUULIZA, “NITANUNUA
VITABU VINGAPI ILI KUWA MJASIRIAMALI KAMILI NILIYEFANIKIWA?
Sikinzani hata kidogo
na dhana ya kujifunza kila siku ila tu ninachosisitiza ni kwamba,
“Usikimbilie kununua zana mpya wakati zile
ulizokuwa nazo bado hujajua hata kuzitumia vizuri”
Ninashauri hivi, ikiwa
uliwahi kununua vitabu fulani vya ujasiriamali, hakikisha angalao unavisoma
vizuri na kujaribu kuweka katika vitendo haraka yale uliyojifunza humo kisha sasa
ndipo uamue kununua vitabu vingine vipya.
Kuna walio tayari na
uwezo wa kujifunza vitu vipya kila wakati, hawa sina shaka nao, lakini wapo
ambao inachukua muda kujifunza mada moja au tuseme somo moja, ni vizuri
wakajijengea uwezo taratibu kwa kujifunza material walizokuwa nazo kwanza huku
wakiweka kipaumbele katika utekelezaji na wakanunua kozi au vitabu vingine
hatua kwa hatua kusudi kuepuka hali ya kukata tamaa njiani baada ya kuona
hawaelewi au kufanikiwa jinsi vile ambavyo wangependa wafanikiwe.
Kwa mfano hauwezi
ukasomea kozi au somo la kupamba sherehe mbalimbali na keki za harusi wakati
bado hujajifunza hata jinsi ya kupika keki zenyewe za harusi. Anza na mambo ya
msingi kwanza halafu panda ngazi taratibu kwa vitendo ndipo utaweza kuona
matokeo bora kabisa katika kila unachokifanya.
0 Response to "Napenda kuanzisha biashara ila sina mtaji wala pesa za kununua vitabu kujiendeleza, nifanyeje?"
Post a Comment