Safu yetu ya USHAURI leo tumepata swali la
msomaji mmoja kutoka kule Mkoani Mbeya na mimi kama kawaida nitaliweka swali
hilo hapa kama lilivyotumwa bila kuongeza wala kupunguza chochote isipokuwa tu
sitataja jina lake kamili kwani hajaniruhusu kufanya hivyo.
SWALI.
Kaka pole
na kazi naitwa HY ni mwalimu . Kwa sasa nipo mbeya nimeanzisha
biashara ya spare za pikipiki yaani duka la spare
za pikipiki. Ila ndani ya Muda mfupi mwalimu mwenzangu
kafungua biashara hiyohiyo mlango wa pili
ndani ya jengo hili hili. Sasa yeye amekua
na tabia ya kuhonga mafundi wangu na kuwaweka kwake hadi sasa mafundi watatu wamehamia
kwake. Na nimempata fundi mwingine ila nahisi nae
ataondoka maana ni rafiki na mafundi walio
toka kwangu. Naomba ushauri wako nifanye
nini ili niendelee??? Nakosa lugha nzuri ya
kueleza shida yangu ila kwa kuwa wewe ni mtaalamu
najua utanielewa.
MAJIBU
YA SWALI/USHAURI
Kwanza Pole sana ndugu yangu kwa mtihani huu
unaokusibu katika biashara yako. Ingawa hapa nitakupa majibu ama ushauri juu ya
namna ya kukabiliana na ushindani katika biashara kwa ujumla lakini kwa kesi
yako kuna vitu nitaongezea kidogo kutokana na sababu kuwa huyu jamaa(mshindani
wako) ambaye umesema ni mwalimu mwenzako anachokifanya siyo ushindani wa
kawaida wa kibiashara uliozoeleka bali ni HUJUMA(sabotage).
Hujuma hizi amezificha nyuma ya mgongo wa
ushindani na hujuma za namna hii wakati mwingine mtu anaweza hata akatumia
mbinu za aina mbalimbali mfano kumwaga kinyesi cha binadamu mlangoni pa
biashara yako usiku kusudi tu ikifika
asubuhi wateja wataharuki na kupaona kwenye biashara yako kama kituo cha polisi
vile. Tukio la namna hii binafsi niliwahi kulishuhudia mahali ila kwa bahati
nzuri mtuhumiwa alinaswa na kumtaja aliyemtuma ikagundulika kumbe alikuwa
mshindani wake kibiashara. Sasa huwezi ukasema eti mtu wa namna hii
anachokifanya ni ushindani wa kawaida wa kibiashara hata kidogo.
Kwanza kwenye hili la kuwahonga mafundi wako
napenda tu nikutie moyo kwamba, hebu kuwa mvumilivu kwanza, hafiki mbali huyu,
atahonga wangapi? Je, wakifika 10
atawalipa nini? Na hata kama atakuwa akiwafukuza wakishakuwa wengi, si mwisho
wa siku watamshitukia? Haki ni haki tu mwishowe wewe ndiye utakayeibuka kidedea
na kila mteja kuwa upande wako. Kwanza wateja huwa wana tabia ya kusimama
upande wa yule mwenye haki wakishagundua kuna mchezo mchafu kama huo. Atahonga
mafundi lakini hataweza kamwe kuwahonga wateja, wewe jifunze tu mbinu za
“kuwahonga” wateja kwani ndiyo kila kitu.
Akimhonga fundi wako au mfanyakazi na yeye
akakubali wewe wala usiwe na hofu ingawa inaweza kukuuma sana kwani wateja
wengine humfuata mtu kulingana na ujuzi alionao, afterall watafuta kazi ni
wengi kuliko kazi zenyewe, wewe jipange tafuta mwingine na mwisho atagundua
mbinu anayoitumia si endelevu ataachana nayo. Wewe cha kufanya ni ‘kustiki’
kudumu na mbinu nitakazokwenda kukushauri hapa chini ambazo ndizo zinazotumiwa
duniani kote na makampuni yaliyobobea katika biashara za aina mbalimbali.
Narudia tena, mbinu yake hii chafu itakuumiza kwa muda mfupi tu na kama malengo
yako ni ya muda mrefu utashinda!
MBINU
HALALI NA HALISI ZA KUKABILIANA NA USHINDANI MKALI KWENYE BIASHARA YAKO, SIYO
HUJUMA LAKINI.
1.Fanya
utafiti kujua Nguvu na Udhaifu wako na pia kwa upande wa washindani wako.
Njia halisi na halali mtu katika sekta yeyote
ile ya biashara anazoweza akazitumia katika kukabiliana na ushindani mkali wa
biashara na hatimaye kuibuka mshindi zinaanzia kwenye Utafiti wa biashara na
soko lako kwa ujumla, pale unapoanza kulijua vizuri soko lako ni lipi pamoja na
kuwasoma barabara Washindani wako wa moja kwa moja na hata wale wasiokuwa wa
moja kwa moja kwamba wanafanya kitu gani, Nguvu na Udhaifu wao ni upi. Kisha na
wewe pia unajichunguza Nguvu na Udhaifu wako upo katika vitu gani.
Kwa kifupi Nguvu ni yale mambo yote kwenye
biashara unayoweza kuyafanya vizuri na kwa ukamilifu zaidi kuifanya iende mbele
na Udhaifu ni vitu au masuala yote usiyoweza kuyafanya vizuri na ambayo
yanaweza kuirudisha biashara yako nyuma. Hapa chini nitakuorodheshea mifano ya vitu
hivi viwili, Nguvu na Udhaifu kwa ujumla ambavyo vinaweza kuwa katika biashara
yeyote na wewe sasa utaangalia biashara yako hii ya vifaa vya ujenzi nguvu na
udhaifu wake ni upi na kwa upande wa mpinzani wako pia Nguvu zake na Udhaifu
upo wapi. Kila biashara ni lazima iwe na vyakwake.
NGUVU.(Strength)
· Mtaji
mkubwa wa kutosha.
· Wafanyakazi
walio na ujuzi
· Uharaka
wakati wa kutoa huduma.
· Unafuu
katika bei.
· Huduma
tofautitofauti kwa mteja.
· Eneo
zuri lenye watu wengi.
· Thamani
zaidi kwa mteja.
· Kuwahi
kufungua biashara mapema.
· Kutoa
zawadi kwa wateja.
· Huduma
ya usafiri wa bidhaa za wateja
Nguvu kwenye biashara vinaweza kuwa ni vitu
vingi na unaweza ukataja hata elfu moja au zaidi ukipenda, itategemea ni katika
mazingira yapi au ni aina gani ya biashara unayoifanya ilimradi tu kitu
chenyewe ni chanya kinachoiongezea nguvu biashara yako ya kusonga mbele.
Udhaifu(Weakness)
· Udhaifu
unaweza kuwa ni kati ya vitu vyote tulivyotaja hapo juu kwenye Nguvu lakini
kinyume chake mfano;
· Mtaji
kidogo.
· Wafanyakazi
wasio na ujuzi au wachache.
· Kutoa
huduma polepole mno.
· Bei
kubwa inayowakimbiza wateja.
· Eneo
baya
· Kuchelewa
kufungua
· Huduma
mbaya kwa wateja
· Lugha
mbovu
· Mpangilio
mbaya wa bidhaa
· Kukosa
uzoefu nk. na vile vitu vyote vinavyoweza kuizorotesha biashara.
Ufanyeje
Utafiti kuvijua vitu hivi.
Uafiti wa biashara kama nilivyoelezea kwa
kina sana katika Kitabu cha Michanganuo ya Biashara na Ujasirimali siyo kazi
ngumu kuifanya na wala huhitaji mtaalamu
au kampuni ikufanyie kama biashara yako ni ndogo tu au ya kati. Wajasiriamali
wa kawaida mitaani pasipo wala kujua huwa tunafanya utafiti kwenye biashara
zetu kila mara.
Mfano mzuri ni dada mmoja anayefanya biashara
ya kuuza mihogo ya kukaanga alinifuata siku moja na kutaka nimshauri, kwamba
jirani na kwenye biashara yake kuna babu mmoja ambaye naye anafanya biahsra
kama yak wake ya kuuza mihogo. Lakini jambo la ajabu alisema kwamba babu huyo
kila siku anapoona tu hyu dada akimuuzia mteja macho humtoka pima utadhani
mjusi kabanwa na mlango, huwa hatulii atazunguka mpaka kwenye kona moja ambayo
anaweza kuona vizuri kabati la huyo dada kujua mihogo imeuzika kiasi gani.
Sasa huyu dada akawa anashangaa na kuhisi
labda huyu babu ni mshirikina na vile vituko vyote labda huwa ndio njia za
kumloga ili asiuze biashara idode. Jibu rahisi nililompa yule dada ni kuwa,
wala huyu babu siyo mchawi hata kidogo ila kile anachofanya ndiyo mbinu yake ya
kumtafiti mshindani wake na pengine hata masikini babu wa watu hajui kama
anachokifanya kuwa ni utafiti. Hii spirit ya kuwatafiti washindani wetu huwa
imepandikizwa katika akili zetu ni vile tu watu wengi hawajui kuitumia kwa
faida, wanatafiti bila kuchukua hatua.
Mfano mwingine ni katika mapenzi, hivi
ukigundua mpenzi wako ana mchepuko utafanya kitu gani kwanza kabisa kabla
hujachukua hatua yeyote ile ya kuukomesha? Cha kwanza si utafiti kumjua huyo
mwenzako yukoje, ana nguvu zipi na udhaifu wake upo wapi? Sasa biashara nayo ni
hivyohivyo, halikadhalika na kwenye vita ni hivyo pia.
2.Tambua
Siri yako ya Ushindi ni ipi(Competitive Advantage)
Siri yako ya Ushindi kwa maneno mengine,
Faida yako ya kiushindani si kitu kingine bali unaangalia tu katika ile orodha
ya Nguvu ulizopata pale juu, chagua ile unayoweza kuimudu zaidi na ambayo
mshindani wako/washindani wako hawaiwezi kama wewe. Hapa ni lazima ufahamu
kwanini mteja afanye biashara na wewe na kumuacha mshindani wako.Ukiweza kujibu
swali hili tayari unakuwa umeshapata siri yako ya ushindani na utaitumia katika
mikakati yako yote ya masoko
Mfano labda wewe katika duka lako hilo la spea
za pikipiki mtaji wako ni mkubwa kulinganisha na la mshindani wako. Sasa nguvu
hiyo ya mtaji mkubwa unaweza kuitumia kikamilifu pamoja na yeye kuhangaika
kukuibia mafundi.
Komaa na kuendelea kuleta spea tofautitofauti
ambazo yeye hana uwezo wa kuzileta mwishowe utakuta hata mafundi wake wakirudi
tena kwako kununua spea ambazo yeye hana. Japo wapo wateja watawafuata mafundi
waliowazoea kule, lakini wengine pia hawatajali kigezo hicho wao shida yao
kubwa ni upatikanaji wa spea bora kwa bei wanayotamani, na wewe sifa hizo unazo.
Fungua duka lako muda wote wa kazi kila siku
hutakosa kuuza. Wakati yeye akihangaika kutafuta fedha za kuwalipa kundi la
mafundi aliowanunua, wewe endelea kumpatia mafunzo huyo fundi wako mpya
uliyemleta, mlipe stahili zake vyema isijekuwa labda wanarubuniwa kutokana na
wewe kuwabana mno. Lakini pia hakikisha unaulinda mtaji wako kama mboni ya
jicho lako kwani biashara bila mtaji haiwezi kusogea mbele.
Huyu mshindani wako alishagundua kuwa udhaifu
wako mkubwa upo katika eneo hili la mafundi ndio maana akatumia mbinu hiyo sasa
na wewe inabidi uonyeshe kuwa udhaifu huo unaweza kuukwepa kwa kutafuta na
kushikilia nguvu nyingine unayoimudu zaidi.
3.Chagua
Eneo lako unalolimudu zaidi(Niche)
Kipengele hiki hakitofautiani sana na kile kilichopita
cha siri yako ya ushindi isipokuwa tu ni kwamba hiki ni kipana zaidi na
unaangalia eneo kubwa katika biashara siyo kipengele kimoja. Tuchukulie mfano
wa biashara nyingine ya kuuza vifaa vya ujenzi. Badala ya kuuza vifaa vyote vya
ujenzi wewe unaamua kudili na vifaa vya aina moja tu au mbili mfano unasema
mimi nitauza sementi tu au mabati tu au mimi nitauza vifaa vya umeme tu nk.
Kuchagua eneo kutakufanya wewe ubobee au uwe mahiri na wateja watakutafuta wewe
tu na kuwaacha washindani wako.
4.
Tengeneza Ushirikiano.
Kuwa na mtandao na wafanyabiashara kama ya
kwako lakini wasijekuwa ni washindani wako wa moja kwa moja. Kwa kesi hii ya
dula la spea za pikipiki, unaweza kujenga ukaribu na watu kama mafundi. Ili
kuwalinda wasirubuniwe kuwa mbunifu, tafiti kile kinachowavutia wahamie kwa
huyo mpinzani wako, lazima kipo ila ikiwa utapata uhakika kuwa ni kweli
anawarubuni kwa kuwahonga fedha nyingi wewe usijibu kwa kuwapandishia dau
endelea tu kuvumilia kama nilivyokushauri pale mwanzoni.
Kama ni sababu zingine basi jitahidi na wewe
kuzidumisha. Hakikisha hata kama na huyo fundi mwingine atarubuniwa dukani
paendelee kuwa wazi na mtu atakayekuwa anaendelea kuuza spea kama kawaida usifunge kwa kukosa fundi,
mapato yako hayatokani na fundi tu bali pia na mauzo ya spea.
5.Tengeneza
Mahusiano mazuri na Jamii inayokuzunguka.
Huu ni mkakati mzuri kwani utakujengea jina
na wateja zaidi wataambizana kwa mdomo mtaa mzima kuwa unauza spea nzuri kwa
bei wanayoimudu. Usionyeshe waziwazi chuki yako kwa huyo mshindani wala kutoa
malalamiko kwa watu kiholela, waache wateja na wanajamii watagundua wenyewe
6.
Dumisha chochote kilichokuwa na thamani na kuachana kabisa na vile
vinavyokuletea hasara.
Vitu vyenye thamani ni mambo yote yale
yanayowafanya wateja waje kununua. Mambo mengine yote unayoona hayana tija wala
kumfanya mteja kuja kununua yatupilie mbali kabisa zikiwemo fikra za chuki kwa
huyo mpinzani wako. Acha kufikiria kila mara jinsi utakavyolipa kisasi kwa
kurudisha mabaya kwa huyo mshindani na badala yake jikite tu katika mbinu za
kitaalamu za kukabiliana na ushindani huku ukiendelea kuwa mvumilivu. Nguvu
hasi hazitakusaidia kitu na zaidi zitazidi tu kukudidimiza.
………………………………………………………
Swali hili la msomaji wetu
wa Mbeya lingeweza kujibiwa kwa asilimia 100 kama angelisoma kitabu changu kiitwacho
MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LAREJAREJA. Kwa mfano katika sura ya 2 ukurasa wa 41 ipo mada isemayo, “Tathmini
siri yako ya Ushindi”, Katika ukurasa wa 41 ipo mada nyingine isemayo, “Mbinu
za kuwa juu kushinda washindani wao” na Katika ukurasa wa 47 pia ipo
mada, “Kushindana na Maduka makubwa” Mada zote hizi tatu hakuna
zilichoacha kuhusiana na namna ya kudili na Ushindani kwenye biashara.
Ikiwa unapenda kujifunza kuandika mpango/mchanganuo wa biashara yako kwa urahisi kabisa jiunge na programu yangu katika Wasap iitwayo Michanganuo Online ambapo tunajadili kila siku jinsi ya kuandaa michanganuo bunifu ya biashara zinazolipa hatua kwa hatua. Kiingilio ni sh. elfu 10 na tunakutumia pia masomo na kila kitu tulichojifunza katika kipindi cha mwaka wote wa 2018.Kujiunga tuma ujumbe wasap 0765553030 na ikiwa hutumii wasap tutakutumia masomo na vitabu kupitia email. Unaweza pia kupiga namba 0712202244
0 Response to "MSHINDANI WAKO KIBIASHARA ANAPOANZA KUKUHUJUMU BADALA YA KUSHINDANA KIHALALI UFANYE NINI?"
Post a Comment