Kama kuna kitu matajiri wanachokijua zaidi
kuliko vitu vingine vyote basi ni PESA. Hali kadhalika masikini nao PESA ndio
kitu wasichokifahamu kuliko vitu vingine vyote. Ninapoyasema hayo simaanishi
kuijua pesa katika maana ya noti au sarafu hapana bali namaanisha kuwa na
uelewa wa ndani kabisa wa jinsi unavyoweza kuzalisha na kuzisimamia pesa zako
kikamilifu.
Kutimiza azma hiyo mtu anahitaji kitu kimoja
tu nacho ni mfumo utakaomwezesha kuingiza pesa na kuzisimamia, mfumo huo si
mwingine bali ni BIASHARA. Unaweza leo hii ukapata bahati ya kuwa na pesa
nyingi labda kutokana na kushinda bahati na sibu au vyovyote vile lakini
nakuhakikishia kama hautaziwekeza fedha hizo kwenye biashara na biashara hiyo
ukaiiwekea mfumo mzuri wa usimamizi, pesa hizo hata ikiwa ni bilioni moja
nakupa miaka michache tu utarudi palepale ulipokuwa mwanzo.
Hata kama utasema uzitumie ukizibanabana,
mwisho wake kama hazizai zitakwisha tu na hutakuwa na cha kuendelea tena kuweka
kama akiba. Kuna gharama mbalimbali za maisha na hizi hazikwepeki. Lakini
habari njema ni kwamba kupitia biashara uwezo wa mtu kuingiza pesa zaidi hauna
ukomo, ndio maana leo hii nimekuletea orodha ya biashara 7 unazoweza kuzifanya
mwaka huu mpya wa 2019 kama njia ya kujiingizia kipato cha ziada. Haijalishi unafanya
shughuli zako nyingine ajira ama biashara, unaweza kuchagua moja.
Kitu cha pekee sana katika orodha yangu hii
leo ni kuwa biashara hizi nimezichagua kulingana na urahisi katika kuzisimamia,
kwa maana nyingine ni biashara ambazo zinaweza kuanzishwa lakini mmiliki
usitumie muda wako mwingi kuzihudunia na zikawa zinakupa kipato kama kawaida.
1.Biashara
ya kuuza Bidhaa au Huduma Mtandaoni.
Sipendekezi njia ngumu sana ya kuanzisha duka
la mtandaoni hapana, nataka ufanye kitu kinachowezekana katika mazingira ya
kawaida kabisa. Unaweza kufungua blogu au tovuti lakini bado kwa mtu wa awaida
kabisa inaweza kuwa vigumu. Hivyo nitakutajia njia rahisi kabisa. Siku hizi
karibu kila mtu mwenye smartphone yupo pia kwenye mtandao wa kijamii kama siyo
facebook basi ni twitter, Insta, youtube au mtandao mwingine wowote ule.
Mitandao hii tunayoipenda sana katika
kuwasiliana kijamii unaweza ukaitumia pia katika kutangaza na kuuza bidhaa
yeyote ile au huduma unazozalisha mwenyewe au hata unazochuuza kutoka kwa watu
wengine. Tena unaweza hata kuuza kitu ambacho hunacho mkononi, ni mali kauli
tu, ukishampata mteja unamuunganisha na mwenye mzigo au unafuata mzigo na
kumpelekea kwa makubaliano ya kupata cha juu.
Kuna watu wengi sasa hivi wanauza simu,
vyombo vya ndani, madawa, ili hali hawana hata kioski, mteja akihitaji kitu
wanampelekea au kumtumia kwa njia ya mabasi. Siri kubwa ya biashara hizi ni
kujijengea jina(Branding). Kuna watu wanadili hata na ubuyu tu peke yake na
wanapata pesa kuliko mtu mwenye duka kubwa. Hakuna biashara iliyo na urahisi
kwenye usimamiaji kama hizi za kwenye mtandao kwani kila kitu una uwezo wa
kukidhibiti kiteknolojia, unaweza kupanga muda maalumu wa kuhudumia wateja wako
nk. Pia karibu kila kitu kinachouzwa katika maduka na magulio ya kawaida ya
jadi unaweza pia ukakiuza mtandaoni kuanzia vitabu, magari, vifaa vya
kielektroniki, vyakula, orodha ni ndfu unaweza mwenyewe kutaja chochote
unachokijua.
2.Kuanzisha
kiwanda kidogo.
Dhana ya viwanda ikiwa ndio inashika kasi
Tanzania sasa hivi, mtu yeyote anaweza akanufaika na fursa hiyo kubwa kwa
kuchukua hatua mbalimbali kama vile, kufungua kiwanda chenyewe, kuuza malighafi
mbalimbali za kutengenezea bidhaa mfano, sabuni za vipande, sabuni za maji,
dawa za chooni, batiki, unga wa lishe, juisi za matunda, nguo, keki, crips,
ubuyu, tambi nk.
Au pia unaweza hata ukaanzisha darasa la
kufundisha jinsi ya kutengeneza vitu mbalimbali kama una ujuzi kupitia mitandao ya kijamii kama magroup ya wasap na facebook,
blogs nk. Unaweza pia ukaanzisha darasa mahali ukajitangaza kuwa unatoa mafunzo
ya namna ya kutengeneza kitu fulani ilimradi tu uonyeshe watu kwa vitendo ule
utaalamu unaotaka kuwafundisha.
Urahisi wa usimamiaji katika biashara hii upo
katika uhuru wa kuchagua ni muda gani ufanye kazi zako, unaweza kuamua uzalishaji
uufanye muda wa jioni au usiku baada ya kazi zako. Mauzo nayo unaweza kuyafanya
kwa jumla na hivyo kutopata usumbufu wa kutumia muda mwingi, labda wateja
unawaambia waje siku maalumu kuchukua mzigo au unawapelekea walipo. Ni rahisi
pia kuajiri mtu wa mauzo kwani utakuwa na vitu vinavyohesabika baada ya kazi ya
uzalishaji kuifanya mwenyewe.
3.Biashara
za vyakula.
Biashara ya chakula ni sekta kubwa unayoweza
kuchagua eneo dogo linalokufaa kulingana na mazingira yako(a niche) na kujikita
kikamilifu. Na uzuri wa chakula ni kwamba ni bidhaa inayotumiwa kila siku na
kila mtu, mtu akila leo kesho ni lazima atakula tena, hivyo kama umemuuzia
chakula kizuri leo kesho atakutafuta tena.
Unaweza kurahisisha usimamizi kwenye biashara
ya chakula kutegemeana na ni eneo lipi umejikita. Kwa biashara ya ziada lenga
maeneo yale ambayo hayatakupa usumbufu kusimamia. Unaweza kwa mfano katika
biashara za chipsi au mgahawa ukatengeneza mfumo utakaokuwezesha wewe usiwe
pale muda wote na ukafungua hata matawi mawili au zaidi kupata faida kubwa
zaidi. Wengi hutumia mtindo wa “daladala”, kufungua ofisi na
kumkabidhi meneja kila kitu yeye akuletee hesabu maalumu tu usiku huku ukikagua
aseti zako pale mara kwa mara basi.
4.Usafirishaji
wa Abiria na mizigo.
Kama unao mtaji hii bado ni biashara
itakayolipa mwaka 2019 kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hizo nchini.Watu
kila siku wanahitaji kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, barabara
zinaongezeka na kuboreshwa katika awamu hii ya uongozi kuliko awamu nyingine yeyote.
Utahitaji usimamizi imara tu kutengeneza faida nzuri mwaka 2019 iwe ni
bodaboda, bajaji, daladala, basi au hata malori ya mizigo.
Urahisi hapa kwenye usimamizi unakuja pale
inapowezekana kumwajiri mtu akafanya kazi na kukuletea hesabu tu ingawa kunaweza
kuwa na changamoto za hapa na pale lakini, uwongo unaweza kuingiza pesa huku
ukiendelea na majukumu yako mengine pasipo kutoa jasho jingi.
5.Ufugaji
wa kuku, sungura, samaki na ndege wengine wafugwao.
Urahisi kwenye usimamizi wa biashara hii ni
kwamba unaweza kuwashughulikia mifugo wako muda wa asubuhi na jioni tu na
ikifika wakati wa mauzo ukatenga siku maalumu ambayo haupo kazini au kwenye
biashara yako kuu. Pia kumwachia msaidizi ni rahisi kwani mifugo ni kitu
unachoweza kuhesabu kwa urahisi.
6.Kilimo
cha mbogamboga na matunda kama nyanya, pilipili hoho, bamia, kisamvu na
matembele.
Ukiwa na uwezo wa kufunga green house,
itakurahisishia sana katika usimamizi na uendeshaji kwani hautahitajika ukae
pale masaa yote kutokana na kazi kurahisishwa na mfumo wa umwagiliaji wa
matone(drip irrigation system). Pia hakuna uhitaji mkubwa wa kuondoa magugu kama
ilivyo kwa bustani za kawaida kutokana na kuwepo kwa matandazio ya kisasa ya
nailoni yanayozuia magugu kuota.
7.Biashara
za nyumbani.
Hapa kama ilivyokuwa kwa mtandao wa Intaneti,
nyumbani ni ukumbi unaoweza kufanya biashara za aina nyingi sana pasipo
kulazimika kulipa kodi wala kuingia gharama nyingine nyingi. Urahisi katika
usimamiaji wa biashara hizi utategemea ni nani utakayemwachia hiyo biashara
pale nyumbani unapoondoka. Ikiwa kwa mfano unayemwachia ni mwenza wako, mke au
mume inakuwa rahisi sana kwani wote mnakuwa na lengo moja. Lakini pia unaweza
ukamwachia mtumishi wa nyumbani kuangalia biashara kwani nyingi huwa ni
biashara ndogo zinazohesabika kirahisi.
Ifuatayo ni orodha ya biashara ndogondogo
unazoweza kuanzisha nyumbani, kibarazani au hata ndani ya ua wako.
· Vitafunwa
mbalimbali
· Ice
cream na lambalamba
· Kuuza
barafu
· Kukodisha
vitu kama viti, maturubai, vyombo nk.
· Uuza
mkaa na kuni
· Kuuza
pumba kwa ajili ya kulishia mifugo
· Kuuza
maji ya bomb/kisima.
Hitimisho.
Wakati biashara ya ziada inaweza kuwa ni njia
nzuri ya kuongeza kipato chako pia vipo vitu kadhaa nya kuzingatia;
1. Zingatia
malengo ya kuanzisha biashara yako ya ziada, ikiwa ni ya muda mrefu kama vile
siku moja kuja kuifanya ndio biashara yako ya kudumu basi ianze taratibu huku
ukiifanyia utafiti wa kina ili uifahamu nje ndani. Ila kama unalenga tu la
kupata pesa za kukidhi haja fulani ya muda mfupi huna haja ya kufanya utafiti
wa kina sana.
2. Kumbuka
pia kwamba biashara ya ziada haiwezi kukupa utajiri wa haraka, ingawa zina
uwezo wa kumtajirisha mtu lakini haziwezi kufanya hivyo kimiujiza kwa siku
mbili tu au tatu, ni lazima uwe mvumilivu, uweke juhudi kuhakikisha unatoa
thamani ya kutosha kwa wateja na wala siyo kujidanganya eti inaweza kukutoa
muda mfupi tu ujao.
.....................................................
Ndugu msomaji wa makala hii ikiwa unapenda kujifunza zaidi masomo yahusuyo fedha na michanganuo ya biashara, basi karibu kwenye group letu la wasap na email kwa kiingilio cha sh. elfu 10 upate masomo yote tangu mwezi Januari na pia nafasi ya kujifunza kwa mwaka wote wa 2019 bila kulipa zaidi.
Namba za kulipia ni 0765553030 au 0712202244 kisha tuma ujumbe, "NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO-ONLINE"
Ikiwa hutumii wasap masomo tutakutumia kwa njia ya email.
Mwisho wa offa hii ni Desemba 30, wahi kabla group halijajaa kwani zimebaki nafasi chache. Masomo ni kila siku saa 3 usiku.
Kwa vitabu bora kabisa na Michanganuo ya biashara iliyokwisha andikwa tayari tembelea; SMART BOOKSTZ
🙏🏼
ReplyDelete