SHILINGI MILIONI 5 ITATOSHA KUFUGA KUKU WANGAPI WA MAYAI? NAOMBA MCHANGANUO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SHILINGI MILIONI 5 ITATOSHA KUFUGA KUKU WANGAPI WA MAYAI? NAOMBA MCHANGANUO

kuku wa mayai
Katika safu yetu ya Ongea na mshauri au Uliza ujibiwe leo kuna mdau wetu mmoja katika Group la Michanganuo online aliuliza swali hili;

NINA MILIONI 5 NAWEZA KUFUGA KUKU WA MAYAI WANGAPI? NAOMBA MCHANGANUO

Na mimi nimeona niwashirikishe wasomaji wengine kwa lengo la kujifunza au kutoa mchango wowote ili kuboresha majibu hayo. 



MAJIBU.
Swali kama hili jibu lake unatakiwa kwanza ufahamu gharama zote za kumlisha kuku mmoja(1) kwa kipindi chote kabla hajaanza kutaga kisha ndipo ukisie kwa mtaji uliokuwa nao mkononi unaweza kutosha kulisha kuku wangapi na kiasi kingine kikabakia kwa ajili ya kulipia gharama zingine za kuanzishia na kuendeshea mradi kama banda, chanjo, madawa nk.

Gharama kubwa katika ufugaji wa kuku wa mayai ni hizi zifuatazo;
·       Chakula
·       Kuku wenyewe(vifaranga)
·       Chanjo
·       Dawa
·       Vyombo vya chakula/maji
·       Malazi(banda)

Katika mfano wetu huu ambao kuna mdau mmoja ameomba mchanganuo wake, amesema ana shilingi milioni 5 lakini alitaka kujua atajuaje idadi ya kuku anaopaswa kununua na gharama nyinginezo ili mtaji huo uweze kutosha hadi kuku watakapoanza kutaga.

Baada ya kuku kuanza kutaga ina maana kwamba mapato yatakayotokana na mayai hayo ndiyo yatakayokuwa sasa yakitumika kuendeshea mradi kwa kununulia chakula na mahitaji mengine hivyo tunahitaji gharama tu za kuanzia siku ya 1 mpaka wiki ya 18 ambayo ndiyo tunakadiria kuku wataanza kutaga mayai.

Na ni lazima ukitaka kufuga kuku wa mayai kama unataka usipate hasara basi uhakikishe unacho kabisa mkononi au benki kiasi cha fedha hizi za kugharamia mradi kutoka vifaranga mpaka watakapoanza kutaga. Ukitegemea kuja kubangaiza au kuungaunga mtaji utaweza kuhatarisha kuku wako wakafa au kudumaa kwa ajili ya kukosa matunzo.

Basi moja kwa moja hebu tuanze na gharama kuu kuliko zote ambayo ni CHAKULA.

Kifaranga cha mayai hula chakula kidogo kuliko cha nyama na pia kiasi wanachokula huweza kutofautiana kulingana na eneo, hali ya hewa na hata aina ya kuku(breed) hivyo ndio maana unaweza kukuta mahali pengine unaambiwa kuku 1 tangu kifaranga cha siku moja mpaka anataga hula kilo kadhaa na mwingine anakuambia hula kilo tofauti na hizo. Ni kutokana na mazingira tofauti.

Kwa mujibu wa chati ya ulaji wa kuku katika umri tofauti tuangalie kuku mmoja(1) tangu anaanguliwa mpaka anaanza kutaga hula kiasi gani cha chakula kisha tutaona katika mtaji wa sh. Milioni 5 tutaweza kununua vifaranga wangapi na hela nyingine ibakie kwa ajili ya gharama zingine.

Wiki ya 1-8 kifaranga mmoja hula wastani wa gr.2000 mpaka gr.3000 ila sisi tuchukue tu gr.2000
Wiki ya 8-18umri wa kutaga kuku mmoja hula wastani wa gr. 5000. Hivyo toka siku ya 1 mpaka kutaga atakula jumla wastani wa chakula gr. 7000 sawa na Kilo 7

Hizi kilo saba ni sawa na shilingi ngapi? Tuchukulie mfuko I wa kilo 50 wa chakula cha kuku bei yake ni shilingi 50,000/= ukigawa kwa kilo 50 utapata kilo 1 sawa na shilingi 1000 x 7 = sh. 7,000

Katika shilingi milioni 5 hebu tukisie kwamba asilimia 50% ya pesa zote zitatumika kwa chakula yaani milioni 2 na nusu na asilimia 50 nyingine ibaki kwa ajili ya gharama nyingine. Ili kujua milioni 2.5 itanunulia kiasi gani cha chakula gawa kwa shilingi 1000 bei ya chakula kilo 1 = 2500,000/ 1000 = kg.2,500

Kilo 2,500 zina uwezo wa kulisha kuku wangapi kwa muda wa wiki 18? Chukua kg. 2500 gawa kwa 7 = kuku 357. Kwahiyo makadirio yetu tunatakiwa tufuge kuku kuanzia angalao 300 mpaka 350. Lakini hebu tuamue kuchukua kuku 300 tu ili pesa kwa ajili ya gharama zingine ibakie nyingi kidogo zaidi ya milioni 2.5 tuliyokadiria mwanzoni.

Kwa hiyo tutakadiria gharama zote kwa kutumia kuku 300  tuone kama ile milioni 5 yetu itatosha au la.

1.  Chakula wiki 1-18
kuku 300 x kg.7 = 2,100 x 1000 = sh. 2,100,000

2.  Vifaranga 300@ sh. 2500 = sh.750,000

3.  Vitalu, mkaa au umeme = 200,000

4.  Vyombo vya chakula 25@ 7000 = 175,000

5.  Vyombo vya maji 30@ 6000 =  180,000

6.  Chanjo, wiki ya kwanza kideri wiki ya 2 typhoid na Gumboro, wiki ya 3 kideri tena, wiki ya 4 Gumboro. Mwezi wa 2 ndui na minyoo. Mwezi wa tatu kideri tena na kila baada ya miezi 3. Wastani wa kila chanjo ni sh. 6000 kwa kuku 300 - 500 jumla ni sh. 70,000

7.  Glucose na Vitamini wiki za mwanzo mara kwa mara jumla makadirio ni sh. 60,000

8.  Dawa ya kusafisha banda (Disinfectant) 7,000

9.  Mtaalamu wa mifugo(ushauri) = 100,000


10.     Posho ya msaidizi miezi 4.5@50,000 =  225,000

JUMLA YA GHARAMA ZOTE = 3,867,000

Hiki ndio kiasi cha mtaji utakachohitaji ili mradi wako uweze kufikia hatua ya utagaji wiki ya 18 kwa kuku 300 kwahiyo katika ile milioni 5 utabakiwa na kama sh. Milioni 1.2 hivi.

Banda gharama zake hatukuziweka na hii ni kwa sababu mdau aliniambia anazo tayari Cages alizokuwa keshazinunua tayari lakini hata hivyo kwa kuwa kiasi cha fedha zilizosalia katika ile milioni 5 ni nyingi( unaweza kukisia ujenzi wa banda lolote la gharama ya shilingi laki 5 mpaka laki 8 au milioni kabisa na bado ukaendelea kubakiwa na fedha za dharura kama laki 1 hivi.

Baada ya wiki 18 Faida itakayopatikana kwa siku.
GHARAMA
Kuanzia wiki ya 18 na kuendelea kuku mmoja anakadiriwa kula wastani wa chakula gr. 130, kwa kuku 300 = gr. 39,000 au kilo 39. Ambazo  ni sawa na shilingi 39,000/= kwa siku

MAUZO
Mapato/mauzo ya mayai kwa siku.
Tukadirie asilimia 80% ya kuku wote ndio watakaokuwa wakitaga kila siku hivyo 80% x 300 = kuku 240 watakaotaga kila siku. Sawa na trei 8 za mayai.

Kila trei ukiuza kwa sh. 7000 kwa siku utapata sh. 56,000

FAIDA KWA SIKU  56,000 – 39,000 =  17,000

Kuku wana uwezo wa kutaga hadi miaka 2 sawa na wastani wa siku 504. Hivyo faida kwa kipindi chote cha utagaji ni wastani wa sh. 17,000 x 504 = 8,568,000 Hapo bado hatujaweka mauzo ya kuku waliozeeka na mbolea.

Halafu ukumbuke kuwa tumepiga hesabu tukitumia makadirio ya chakula kwa gharama ya juu sana, ukiamua kutumia mbinu za utengenezaji wa chakula mwenyewe au kununua chakula cha jumla au sayanzi ya utengenezaji wa vyakula mbadala kama mbinu zinazopatikana kwenye kanuni za ufugaji bora za Bwana FRANK MAPUNDA mtunzi wa kitabu cha Tajirika na ufugaji wa kuku unaweza ukapata faida mara 2 ya hii tuliyokokotoa hapa.

Vilevile mtaji wetu wa milioni 5 bado ulikuwa haujamalizika zilibaki kama laki 1 na kitu hata kama tutajenga banda la milioni 1 ambalo pia huja kutumika muda mrefu likizalisha faida.

Naamini mdau uliyeuliza swali hili utakuwa amepata majibu na kama utakuwa na swali la nyongeza au kuna mahali hukuelewa vizuri una dukuduku basi usisite kuwasiliana nami kwa ufafanuzi zaidi au unaweza ukauliza pia kwenye group wadau wengine wakachangia.

...............................................

Ndugu msomaji wa makala hizi za ufugaji wa kuku, karibu kwenye group letu kuna wadau walio na uzoefu wa muda mrefu na masuala ya ufugaji wa kuku pamoja na taarifa nyingi ikiwemo michanganuo mbalimbali unayoweza kuitumia kuanzishia mradi wako ukuletee faida badala ya hasara. Ada ya kujiunga na kundi hili makini ni sh. 10,000 utapata mambo mengi na kamwe hutojutia kiasi hicho cha fedha.

Kulipia tuma kupitia namba 0765553030  au 0712202244 jina litokee Peter Augustino Tarimo. Kisha tuma ujumbe wa wasap au wa kawaida unaosema "NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUOONLINE" Utaunganishwa papo hapo na kutumiwa masomo mbalimbali mengi utakayosoma kwa muda wako pamoja na updates za kila siku kwenye group. 

WASAP: 0765553030
SIMU: 0712202244


Unaweza ukasoma pia makala nyingine zifuatazo















0 Response to "SHILINGI MILIONI 5 ITATOSHA KUFUGA KUKU WANGAPI WA MAYAI? NAOMBA MCHANGANUO"

Post a Comment