Katika historia nzima ya mwanadamu tokea kuumbwa kwa
Adamu na Hawa pamekuwepo na ushindani karibu katika kila nyanja ya kimaisha,
biashara ikiwemo. Ushindani huu tangu zama hizo umekuwa ukijulikana kama
mpambano wa kujinusuru ambapo mwenye nguvu ndiye huibuka mshindi(Struggle
for the survival in which the fittest win). Historia inatuambia kuwa
watu walipambana wakigombea ardhi, rasilimali, njia kuu za kiuchumi,
wanawake,nk. na mara nyingi mshindi alipatikana baada ya mpambano mkali
uliosababisha umwagikaji wa damu, mauaji, udanganyifu na matumizi makubwa ya
nguvu.
SOMA: Mshindani wako kibiashara anapoanza kukuhujumu badala ya kushindana kihalali ufanyeje?
SOMA: Mshindani wako kibiashara anapoanza kukuhujumu badala ya kushindana kihalali ufanyeje?
Lakini Ulimwengu wa leo uliostaarabika katika karne ya 21,
ushindani wa namna hiyo umeshapitwa na wakati kitambo haupo tena. Ikiwa kweli
mtu umedhamiria kutengeneza pesa nzuri, unapaswa kusahau kuhusiana na kupambana
na washindani wako kwa “mapanga”. Mshindani wako mkubwa leo, kesho anaweza
akaja kugeuka kuwa mshirika wako mkubwa wa kibiashara mnayegawana faida na
ambaye bila ya yeye kuwepo basi na biashara yako haiwezi pia kushamiri. Kwa
hiyo ikiwa unapambana na wapinzani wako inamaana kwamba wewe bado unaishi
katika nyakati fulani hivi kwenye karne ya 18 au ya 19.
Teknolojia ya kisasa inamruhusu mtu yeyote yule kufanya
maajabu, inamwezesha kuzalisha bidhaa ama huduma za kipekee kwa namna ambayo
itazifanya ziwe za aina yake na zisizoweza kamwe kuigizwa kirahisi na mtu
mwingine. Siku hizi badala ya mtu kupoteza nguvu zako nyingi katika shughuli za
uzalishaji na za mauzo, nguvu hizo unapaswa uzielekeze zaidi katia kufikiria na
kubuni ni kitu gani mteja anachohitaji, na atakubali kutoa fedha yake shilingi
ngapi kukilipia. Unatakiwa pia ufikirie wewe ni nani, unafanya nini na ni kwa
jinsi gani unavyoweza kutengeneza fedha zaidi.
SOMA: Njia mpya za kufanya mambo, Dunia, biashara, ajira, vinabadilika kwa kasi ya ajabu!
SOMA: Njia mpya za kufanya mambo, Dunia, biashara, ajira, vinabadilika kwa kasi ya ajabu!
Sahau kabisa kuhusiana na mapambano na washindani wako
kwasababu kama utajiingiza katika mpambano inamaana kwamba unajiingiza katika
jambo lisilokuwa na faida wala halitakuingizia pesa. Sisemi uache kabisa
kuwafahamu washindani wako au kuwapuuzia hapana, wafahamu kama kawaida ni nini
udhaifu wao na nguvu zao ni zipi lakini acha kupambana nao, majirani kuchuniana
bila sababu, hata hamsalimiani na mpaka wakati mwingine mnaendeana kwa waganga
matapeli wanatafuna pesa zenu bure, ukiuliza kisa, eti unaambiwa ni ushindani
wa kibiashara. Tazama zaidi wateja wako wanahitaji nini.
Mfano mzuri nitakaokupa hapa ni hii mitandao ya kijamii.
Ilivyo ni kwamba haiwezekani kabisa mmoja, mfano facebook kumtoa nje ya ulingo
wa soko mwenzake kama ilivyokuwa kwa biashara nyingine za kawaida.
Kinachofanyika ni kwa kila mmoja anayo fursa sawa na mwenzake ya kujitanua kwa
kuvutia na kushawishi wateja wengi zaidi watarajiwa.
SOMA: Kubuni kitu kizuri ni hatari, watu ni lazima wakopi na kupesti, ufanye nini ili kuzuia hili?
SOMA: Kubuni kitu kizuri ni hatari, watu ni lazima wakopi na kupesti, ufanye nini ili kuzuia hili?
Hebu watazame Facebook, Twitter, Whatsapp, Instagram na
wengineo, kila mmoja ana uwanja wake wa kujidai na hakuna hata mmoja utamsikia akitoa
malalamiko kwamba eti kuna mwenzake anamzibia rizki au kumuibia wateja wake.
Ukishindwa kuvutia wateja ukatoka nje ya soko, hayo ni matatizo yako mwenyewe
huna wa kumlaumu, utakaa benchi ukiwaacha wenzako wakiendelea kupeta ulingoni.
Katika Dunia ya utandawazi hakuna “wanaoshindwa”
kwasababu zipo rasilimali za kutosha kwa kila mtu, tatizo moja tu lipo kwenye
jinsi ya kuzitumia rasilimali hizo kwa ufanisi. Tumezungukwa na Ulimwengu
uliojaa fursa zisizokuwa na mipaka, sasa ni kwanini upoteze nguvu zako bure
ukipambana na washindani wako?
Tazama Mataifa makubwa ya Magharibi na hata yale ya
Mashariki kama vile Uchina, zamani ili taifa limshinde adui yake ilikuwa ni lazima kwanza kulipua madaraja,
kuharibu barabara, viwanda na miundombinu mingine ya kimkakati, kisha majeshi huingia
na baada ya kuteka nchi yote sasa yanaanza tena kuijenga upya kama Tanzania ilivyofanya
kule Uganda enzi za Mwalimu Nyerere au Marekani kule Afghanistan na Iraq.
SOMA: Kila mtu anastahili kupewa tena nafasi ya kurekebisha maisha yake upya, Barrack Obama.
SOMA: Kila mtu anastahili kupewa tena nafasi ya kurekebisha maisha yake upya, Barrack Obama.
Leo hii Mataifa yamebadilika, hutoa pesa kama misaada/mikopo
na rasilimali nyingine nyingi kama teknolojia kwa Mataifa masikini, na nchi
hizo maskini kwa kukubali kwao misaada hiyo zinakuwa zimejitia kitanzi shingoni
zenyewe kwani hatimaye hujikuta zimekuwa tegemezi kila kitu kwa Mataifa hayo
tajiri kwa kuendelea kubakia kuwa chini yao daima baada ya kushindwa kulipa
mikopo hiyo.
Na watu wa nchi masikini tulivyokuwa wajinga, utakuta
baadhi yetu tukichukua pesa zilezile walizotupatia kwa njia za kifisadi na
kwenda tena kuwekeza katika mabenki yao kinyemela au kununulia vitegauchumi
katika majiji yao makubwa mfano huko London, New York, Paris, Monaco na
kwingineko.
SOMA: Mwaka 2019 hebu ishi kama Mbayuwayu.
SOMA: Mwaka 2019 hebu ishi kama Mbayuwayu.
Hivyo badala ya kufikiria mapambano hebu kuwa kama Nchi
tajiri, fikiria faida utakayoipata kwa kujenga ushirikiano wa kimkakati. Mara
utakapoanza kufikiria kuhusu faida na wateja wako, biashara yako itaanza
kubadilika, mauzo mapya yataibuka na utaona waliokuwa washindani wako wakubwa
wakigeuka kuwa kikundi kimoja na wewe cha kutengeneza faida.
Hakuna haja ya kuogopa mabadiliko na kushikilia tu njia zilezile za kizamani za kufanya mambo
sawa na mtu anayeng’ang’ania kuishi kwenye pagala linalokaribia kubomoka ili-hali
anao uwezo wa kuishi kwemye nyumba bora, imara na mpya ya kisasa.
…………………………………………..
TAARIFA
IFUATAYO NDUGU MSOMAJI WANGU SI MUHIMU SANA KAMA HAUHIFADHI DATA NYINGI KATIKA SIMU
& COMPYUTA YAKO, INGAWA UNAWEZA KUIPITIA KIDOGO KAMA MUDA UNARUHUSU.
Ndugu msomaji, ingawa
binadamu hatuna uwezo asilimia 100% wa kutabiri ni nini kinaweza kutupata au
kutokea siku zijazo hiyo haiwezi kutufanya tuache moja kwa moja kupanga na
kubashiri mambo yajayo. Nasema hivi kutokana na mkasa uliotupata blogu hii siku
chache zilizopita yapata kama wiki 2 hivi wa kupotelewa na vitenndeakazi vyetu,
simu na kompyuta. Kwa kweli vifaa hivyo vilikuwa ndio kila kitu katika shughuli
hizi za kublogu na kupotea kwake lilikuwa ni mtihani mkubwa mno kwetu.
Nakumbuka siku chache kabla ya tukio lile nilikuwa nimeahidi hapa mambo mengi
ikiwemo semina ya mahesabu ya michanganuo na ujio mpya baada ya likizo yangu ya
mwezi Januari lakini haikuweza tena kuwa hivyo.
Namshukuru Mungu ingawa
vifaa(Hardware) vilipotea lakini taarifa(software) nyingi muhimu zilikuwa
salama kwani hapo kabla nilikuwa nikifanya back
up kwenye Google drive(Manually), na nyingine nilikuwa nazo katika flash
ingawa pia kuna baadhi ya vitu vingine vilipotea kabisa na itanichukua muda
kuvipata tena upya, kitu kimoja nilichopoteza kabisa ni pamoja na kazi
nilizokuwa nimezianza hivi karibuni pamoja na meseji au historia nzima katika
mtandao wa WASAP.
Hata hivyo majina ya wadau
wote whatsape yalirudi kama yalivyokuwa, na hili ni kosa moja kubwa
nililofanya, kumbe kuna option katika whatsap unaweza ‘kubackup’ kila kitu kwenye
google drive automatically simu ikija kupotea au kuharibika kila kitu kinarudi
upya kwenye simu mpya utakayotumia. Unaingia ktk settings, kisha Chat, kisha Chat backup.
Changamoto nyingine
niliyokutana nayo katika tukio hili ni katika kufuatilia urudishaji wa line na
kufunga simu iliyoibiwa. Kwenye kurudisha line hamna utata wowote ila kufunga
simu mwizi asiweze kuitumia. Wahudumu wa mtandao wa simu waliniambia
kinachohitajika ni ripoti ya polisi, kitambulisho, Risiti ya kununulia simu au
IMEI namba za simu iliyopotea. Nilikamilisha vyote lakini mhudumu akadai ile
karatasi ya polisi simu haijaorodheshwa, nikarudi tena polisi. wahusika
wakaniambia nikafungue kesi ya kuibiwa simu counter kwani, wao wanahusika na
line tu.
Nilifanya hivyo nikapangiwa
mpelelezi nikajua ataniandikia tu ripoti nirudi zangu ofisi za simu lakini
mpelelezi alikomaa na kudai yeye kazi yake ni kupeleleza kesi tu na wala siyo
kuandika ripoti.”Hawa wafanyakazi wa makampuni ya simu wanajifanya kutufundisha kazi
sisi polisi, kila mtu ni mtaalamu katika eneo lake la kazi, na sisi pia ni
wataalamu hapa ofisini kwetu, waambie wasitufundishe kazi hapa na hata wewe
kama una utaalamu wako ni hukohuko, unauacha pale mlangoni unapoingia hapa”
Aling’aka kwa ukali yule askari wa kike akionekana kukerwa sana na mimi kuomba
ripoti ya kupotea simu baada ya kupewa ya line tayari.
Nilijaribu kumwelewesha yule
askari kuwa mimi shida yangu haikuwa kuipata simu bali karatasi ya polisi tu
ili nikaifunge simu yangu isiendelee kutumiwa na mwizi aliyeiiba, akakataa kata
kata na kudai ni lazima nifuate taratibu za kipolisi. Baada ya kulumbana sana alinipa kijana askari mwingine mvulana
nifuatane naye kwenye stationary moja ili wakanichapie maelezo fulani aliyodai
ni kwa ajili ya kutuma Tume ya mawasiliano kusudi hatua za awali za upelelezi
wa simu ilipo zianze. Kutoka nje ya jengo la polisi yule askari akadai
steshenari ipo mbali tunatakiwa tupande bajaji, nikamwambia hamna shida
nitalipa bajaji, tukaenda. Tulifika mlango wa steshenaru yenyewe ulikuwa
umefungwa akachukua simu akijaribu kumpigia mhusika lakini sijui alimjibu nini,
akaniambia turudi tena kule polisi.
Kuona ile mizunguko na gharama
zimeshaanza, nikajisemea moyoni, “kwani simu yenyewe ni shilingi ngapi, nia
yangu kwanza ilikuwa kumkomesha tu yule mwizi tukose wote ili siku nyingine
hata akiokota smartphone ya mtu aone ni bora kumpigia mwenyewe waelewane ampoze
ili amrudishie simu yake”. Nilimshukuru yule askari na kumwambia ni
heri yule mwizi aendelee tu kuitumia ile simu kuliko usumbufu na urasimu ule
nilioanza kuuona pale, tukaagana akarudi ofisini kwa bosi wake na jalada langu
na mimi nikaondoka zangu mpaka kule kwa wahudumu wa mtandao wa simu.
Niliwaeleza kuwa nimefungua tu kesi lakini hawajanipa karatasi yeyote ya
maelezo lakini nao wakawa wagumu kunielewa. Waliniambia wataomba simu ifungwe
lakini ni 50 kwa 50 ifungwe au isifungwe kwani sijakamilisha vigezo vyote.
Niliwaachia vielelezo nikaondoka zangu
Kweli nilipokuja kusearch
mtandaoni, IMEI za ile simu mpaka leo hii zipo active bado yule mwizi anadunda
nayo kama kawaida simu haijazimwa wala nini, roho iliniuma lakini nifanyeje.
Serikali ilitakiwa kuweka utaratibu unaoeleweka na uliokuwa wazi kuwa mtu
akipoteza simu yake, iwe kama vile ilivyo kwa line, kusiwe na longolongo au
urasimu mkubwa kiasi hicho wa kufungiwa simu. Vinginevyo wezi na vibaka
wataendelea kuiba simu za watu bila woga kwani wanafahamu si rahisi mtu
kuifunga simu pindi inapokuwa imeibiwa. Kama IMEI namba ninazo hadi risiti ya
kununulia simu, na polisi nimetoa ripoti, kwenye mtandao simu inaonekana line
zilikuwa za kwangu tatizo lipo wapi simu hiyo kufungwa?
Ikiwa unafanya biashara za
mtandaoni kwa kutumia vifaa kama vile, kompyuta, simu nk. Bima kubwa zaidi
unayoweza kuiwekea biashara yako ni kufanya BACKUP ya taarifa zako muhimu kila mara. Unaweza kutumia
medium(vyombo) mbalimbali kama vile flash, cd, DVD, External hard disc, Google
drive ama cloud storage nyingine yeyote ile nk. Si lazma uwe unafanya biashara
za mtandaoni, hata taarifa zako tu mwenyewe binafsi zinapopotea zinaweza
kukuumiza kichwa mno hata kushinda simu yenyewe au kompyuta.
Mwisho niwashukuru tena sana
wadau wote mliotufariji na kutupa pole nyingi katika kipindi hicho kigumu hasa
kupitia email na group la wasap, na mimi kwa niaba ya timu nzima ya Blog hii
nasema ASANTENI SANA!
Peter Augustino.
*Yale Masomo ya kila siku katika Group la Michanganuo-online
yameanza tena, na leo hii tutakuwa na somo lisemalo hivi,
“UKWELI ULIOFICHWA JUU YA PESA: WATU HAWATAFUTI KAZI BALI
HUTAFUTA PESA”
0 Response to "PESA NI KILA KITU: USHINDANI KATIKA BIASHARA HAULIPI TENA UMEPITWA NA WAKATI"
Post a Comment