SEMINA: MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUSAGA NA KUUZA UNGA SAFI WA DONA (USADO MILLING)-1 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SEMINA: MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUSAGA NA KUUZA UNGA SAFI WA DONA (USADO MILLING)-1


SEMINA SIKU YA -1: 

KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA YA KIWANDA CHA UNGA WA DONA (USADO MILLING) -HATUA KWA HATUA


UTANGULIZI:

Mpango wa biashara ni nini?
Kabla hatujaenda kuanza rasmi kuandika hatua kwa hatua mpango wa biashara hii ya USADO Milling kwanza ni vizuri kujikumbusha maana hasa ya Mpango/Mchanganuo wa biashara ni kitu gani.

Mpango wa biashara unaweza ukaulezea kwa namna nyingi tofauti lakini kwa mujibu wa Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI mpango wa biashara maana yake ni;

Maandishi yanayoelezea kila jambo kuhusu biashara unayotaka kuiendesha, mambo hayo ni, malengo, mikakati, bidhaa/hudumu utakayouza, soko (wateja), shughuli mbalimbali za masoko na uongozi, gharama, mahitaji, na masuala yote yanayohusiana na fedha.

Au pia unaweza ukasema hivi;

Mpango wa Biashara ni jumla ya maelezo yote yanayoihusu biashara, kuanzia malengo ya biashara mpaka mbinu mbalimbali zitakazotumika kufanikisha biashara husika. Ni dira au ramani inayokuongoza katika biashara yako kujua unatoka wapi na unaelekea wapi.

                           
NUKUU MUHIMU

“Mpango wa biashara ni andiko linaloishi, unachokiandika leo siyo lazima kiwe kile kitakachotokea kesho na ndiyo maana unaitwa utabiri/makisio. Cha msingi ni kufanya marejeo mara kwa mara wakati wa utekelezaji wa mpangowako ukilinganisha hali halisi na makisio yako, uongeze nini au upunguze kitu gani kusudi biashara yako iweze kufanikiwa zaidi. Na hii haimaanishi kwamba mpango wa biashara hauna maana hapana, kwani hakuna mtu yeyote yule duniani anayeweza kudai ameanzisha biashara bila kwanza ya kupanga kichwani mwake ataifanyafanyaje”Peter Augustino Tarimo


MAMBO MAKUBWA MATATU (3) AMBAYO KILA MTU ANAYEANZISHA BIASHARA DUNIANI HUYAFANYA

Kila mtu duniani anayetaka kuanzisha biashara, iwe anajua au hajui, ni lazima kwanza afanye mambo makubwa matatu 3 kabla hajaanza kuifanya biashara yenyewe.

1.   Ni lazima afikirie katika akili yake ni biashara gani anayotaka kuifanya.
2.   Akishapata wazo la biashara aitakayo, kitu cha pili ni kulifanyia utafiti wazo hilo
3.   kitu cha tatu ni kuweka mpango wa utekelezaji wa biashara hiyo akilini au katika maandishi.

Katika semina yetu hii, nitakwenda kushughulika na namba 2 na namba 3. Na hasa hasa nitakwenda kujikita zaidi na namba 3. Basi bila ya kupoteza muda mwingi hebu tuanze na namba 2 tuone jinsi ambavyo wamiliki wa Biashara hii ya USADO Milling walivyofanya utafiti wa biashara yao kabla hawajaandaa Mpango wa biashara.



UTAFITI (Upembuzi yakinifu)
Jambo la kwanza kabisa wamiliki wa kiwanda hiki cha USADO Milling, Maurine na Isabella walichokifanya baada ya kupata wazo la biashara yao ni UTAFITI, na katika utafiti wao walichunguza kila kitu kinachohusiana na biashara hii ambapo waliugawanya utafiti huo katika sehemu kubwa 3 kama ifuatavyo;-

1.  Ufafiti  wa soko na bidhaa wanazotaka kuuza.

2.  Utafiti wa maswala ya kiufundi na Utawala.

3.  Utafiti wa maswala ya fedha.

Katika vipengele hivyo 3 vyenye vipengele vingine vidogovidogo ndani yake unaweza kuona vinafanana na vile tutakavyokwenda kuona kwenye mpango wa biashara kwa kuwa kimsingi mambo yanayotakiwa uyachunguze katika utafiti ndiyo yaleyale tutakayokuja kutumia majibu yake wakati tukiandika mpango wa biashara.

(Kimsingi Utafiti wa biashara mtu unapaswa kuchunguza mazingira yote yanayoihusu biashara husika, kwa maana nyingine ni kwamba unatakiwa kuifahamu hiyo biashara nje ndani. Hivyo ukishindwa kufuata njia za kitaalamu kufanya utafiti usihofu, wala siyo jambo baya, kwani watu wengi hufanya utafiti wa biashara zao bila hata ya kujua kama wanachokifanya ni utafiti)

Kwenye utafiti wa soko na bidhaa waliongozwa na maswali yafuatayo;

1. SOKO.
·      Soko la bidhaa zao ni lipi?
·      Walengwa wao ni akina nani?
·      Tabia za wateja wao zikoje.
·      Wapo wateja wangapi kwenye hilo soko?
·      Kuna changamoto zipi zinazolikabili soko hilo?
·      Ni gharama kiasi gani itakayotumika kulifikia soko?
·      Ni nani washindani wao wa moja kwa moja na wsiokuwa wa moja kwa moja?
·      Bidhaa zao zinafanana au kutofautiana vipi na za washindani wao?
·      Ni nini siri yao kuu ya mauzo?
·      Je washindani wako wanaweza kukuiga kirahisi?
·      Washindani wao wanachukuliaje ujio wao katika soko?

2. Bidhaa /Huduma.
Katika kipengele hiki walitafiti maswali haya yafuatayo kuhusiana na bidhaa ya unga wa dona;

·      Sifa za bidhaa(Unga wa dona) utakaozalishwa
·      Jinsi unga utakavyosafirishwa,
·      Wapi unga huo utakapozalishwa
·      Mahitaji ya unga ni kiasi gani sokoni
·      Kiwango cha uzalishaji kwa siku/mwezi
·      Upekee wa unga wao.

3. Teknolojia /ufundi;
·      Ukubwa na aina ya mashine zitakazotumika ukoje?
·      Kukadiria mahitaji ya vifaa na malighafi katika biashara. 
·      Ni kina nani, watakaowapatia  teknolojia  itakayotumika
·      Je, teknolojia watakayotumia ni ya kisasa au imepitwa na wakati?
·      Je, ni teknolojia inayoweza ikaigwa kirahisi?
·      Je, soko linafikika kirahisi?
·      Malighafi zitatoka wapi, na je zinapatikana kwa urahisi?
·      Tathmini ya usambazaji utakavyokuwa.
·      Tathimini  upatikananji wa vitendea kazi kama vile umeme, gesi maji n./k
·      Tathimini ya uchafuzi wa mazingira.
·      Ni faida gani jamii itakayopata kutokana na huu mradi?
·      Kuangalia sheria na taratibu mbalimbali za nchi zinazohitajika kufuatwa.
·      Kutathimini mwitikio wa jamii inayouzunguka mradi juu ya kuanzisha biashara husika katika mazingira yao.
·      Kutafiti upatikanaji wa malighafi sasa na wakati ujao.
·      Kutathmini ubora na bei za malighafi na njia mbadala za kupata malighafi.

4. Uongozi/Organisation;
·      Jinsi muundo wa uongozi wa biashara utakavyokuwa?
·      Ni kina nani watakaounda menejiment?
·      Uwezo wao ni upi?
·      Uwezo wao utasaidiaje biashara?
·      Wana uaminifu gani?
·      Udhaifu wao utarekebishwaje?
·      Idadi ya watu watakaoajiriwa ni wangapi?
·      Je upo mpango wa kuwapeleka mafunzoni (course)?

5. Fedha/Financials
·      Mahitaji yote ya biashara ni shilingi ngapi?
·      Ni kiasi gani cha fedha zitakazotumika kuiendesha?
·      Fedha hizo zitapatikana toka wapi?
·      Matarajio ya mauzo kwa mwezi, mwaka, yatakuwa kiasi gani?
·      Faida itaanza kupatikana baada ya muda gani kupita?
·      Kuna uhitaji wowote wa kukopa mahali ili kuweza kutimiza malengo waliyojipangia?
·      Kuna haja ya kutafuta wabia zaidi?
·      Biashara itarudisha mtaji baada ya muda gani kupita?

Jinsi Maurine na Isabella walivyofanya utafiti wao kupata majibu kwa maswali mbalimbali yaliyotajwa hapo juu iliwabidi kutumia njia hizi mbili zifuatazo,

1. Utafiti wa msingi.
Waliwauliza watu moja kwa moja ambao ni wadau mbalimbali wa biashara hii ya usagishaji nafaka wakiwemo wateja wanaonunua unga rejareja maduka mengine, wafanyakazi kakita viwanda vya unga wa dona na sembe, wafanyabiashara na wamiliki wa biashara kama hii, taasisi mbalimbali zinazojihusisha au kusimamia biashara hii zikiwemo zile za serikali na za watu binafsi.

 2. Utafiti wa Dawati
Walisoma pia machapisho nje na ndani ya mitandao pamoja na kufuatilia vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na biashara hii ya usagishaji na uuzaji wa nafaka hususan mahindi.

Katika vipengele vyote vikubwa 3 walivyochunguza, soko ndiyo kitu muhimu zaidi na kilichohitaji majibu yenye uhakika mkubwa kwani kuanguka au kushamiri kwa biashara yeyote ile kunategemea sana kitu hiki, soko. Ilikuwa ni lazima kulijua soko lao vizuri na kwa kina sana ili kujiridhisha ikiwa kama kweli biashara hii inao uwezo wa kuwaletea faida.

Majibu ya maswali hayo yote yatawawezesha hapo baadae katika kuandika mpango wa biashara hii kuweka mikakati mbalimbali ya kufanikisha biashara yao.

Kwa hiyo kutokana na majibu mbalimbali waliyoyapata kutoka vyanzo mbalimbali walivyouliza iliwabidi kufanya pia uchambuzi wa mazingira ya biashara wanayotaka kuifanya. Uchambuzi huo unaitwa NUFUVI au SWOT analysis kwa kiingereza na ni kulinganisha mambo mbalimbali yanayoizunguka biashara tarajiwa.

NUFUVI kwa kirefu ni, Nguvu, Udhaifu Fursa na Vikwazo na maana yake ni mazingira au vitu vitakavyoweza kuja kuiathiri biashara kwa namna moja au nyingine. Kuna mazingira ya ndani ambayo ni Nguvu na Udhaifu halafu mazingira ya nje ambayo ni Fursa na Vikwazo. Jedwali la tathmini ya NUFUVI linaweza likawekwa katika mpango wa biashara kwenye moja ya sehemu hizi; Kampuni, Soko au Uendeshaji kama tutakavyoliona hapo baadae. Katika mpango huu wa USADO Milling tathmini hii ipo katika sura ya 2 “Maelezo ya kampuni”.

NJIA ZA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA
Unaweza kuandika mpango wa biashara kwa kutumia moja kati ya njia 3 zifuatazo;

1.   Kwa kufuatisha vipengele/sura zinazounda mpango wa biashara
2.   Kwa kutumia Vielezo/Templates
3.   Kwa kutumia Programu/Software maalumu

Hapa kwenye semina hii nitatumia njia ya 1 ya kufuata mfululizo wa vipengele vinavyounda mpango wa biashara. Mlolongo wa vipengele hivyo ni huu ufuatao;


1.0 MUHTASARI

2.0 MAELEZO YA KAMPUNI / BIASHARA
2.1 Malengo
2.2 Dhamira kuu
2.3 Siri za mafanikio
2.4 Umiliki wa Biashara
2.5 Kianzio(kwa biashara mpya au historia kwa kampuni iliyokwishaanza)
2.6 Eneo la biashara na vitu vilivyopo

3.0 BIDHAA au HUDUMA
3.1 Maelezo ya bidhaa/huduma
3.2 Utofauti wa bidhaa/huduma na za washindani
3.3 Vyanzo vya malighafi/bidhaa
3.4 Kopi za matangazo
3.5 Teknolojia
3.6 Bidhaa au Huduma za baadae

4.0 TATHMINI YA SOKO
4.1 Mgawanyo wa soko
4.2 Soko lengwa
4.2.1 Mahitaji ya soko
4.2.2 Mwelekeo wa soko
4.2.3 Ukuaji wa soko
4.3 Tathmini ya sekta
4.3.1 Washiriki katika sekta
4.3.2 Usambazaji
4.3.3 Ushindani
4.3.4 Washindani wako wakubwa

5.0 MIKAKATI NA UTEKELEZAJI
5.1 Nguvu za kiushindani
5.2 Mkakati wa soko
5.2.1Kauli ya kujipanga katika soko
5.2.2 Mkakati wa bei
5.2.3 Mkakati wa matangazo/promosheni
5.2.4 Programu za masoko
5.3 Mkakati wa mauzo
5.3.1 Makisio ya mauzo
5.3.2 Programu za mauzo
5.4 Mkakati wa ushirikiano
5.5 Vitendo na utekelezaji
5.5.1 Uendeshaji

6.0 MAELEZO YA UONGOZI NA WAFANYAKAZI
6.1 Mfumo wa uongozi
6.2 Timu ya uongozi na wafanyakazi
6.3 Mpango wa mishahara

7.0 MPANGO WA FEDHA
7.1 Dhana/makisio muhimu
7.2 Tathmini ya mauzo ya kurudisha gharama (Break Even Analysis)
7.3 Makisio ya faida na hasara
7.4 Makisio ya mtiririko wa fedha
7.5 Makisio ya mali na madeni (mizania ya biashara)
7.6 Sehemu muhimu za biashara

8.0 VIELELEZO / VIAMBATANISHO
·      Taarifa za mahesabu ya fedha kwa undani
·      Mahesabu yako ya nyuma
·      Leseni, vibali ripoti za kodi, hatimiliki na alama za biashara
·      Mikataba mbalimbali
·      Orodha ya mali na vifaa mbalimbali(Dhamana)
·      CV za viongozi na wafanyakazi muhimu
·      Kopi za matangazo ya biashara.


Kwa siku ya leo semina yetu inaishia hapa, kesho tutaendelea na sehemu ya kwanza ya mchanganuo huu- hatua kwa hatua

                                        SEMINA SIKU-2 

Ili uweze kufuatilia vizuri zaidi masomo haya mpaka mwisho ni vizuri ukawa na Mchanganuo kamili wa USADO Milling. Mchanganuo huo unapatikana kwa gharama kidogo ya sh. elfu 10 tu. Nasema ni gharama kidogo kwa sababu kila anayenunua anapata pia na vitu vingine bure vilivyo na thamani zaidi ya mara 5 ya hiyo. Vitu unavypata ni hivi vifuatavyo;


1.   Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI -Kiswahili

2.   Kitabu cha Michanganuo ya biashara kwa kiingereza(Ndio hutumiwa zaidi na vyuo vikuu vingi duniani. -Kiswahili

3.   Kifurushi cha Michanganuo ya biashara za ufugaji wa kuku(MKOMBOZI CHICKS PLAN 3PACKS) -Kiswahili

4.   Mchanganuo na semina ya Biashara ya Mgahawa wa chakula(JANE RESTAURANT)Kiswahili & kiingereza

5.   Mchanganuo wa biashara ya matikiti maji(kibada watermelon Project) Kiswahili

6.   Kujiunga na Magroup ya watsap & Telegram ya Michanganuo-online ukitaka.

Kutumiwa mchanganuo kamili wa USADO MILLING pamoja na vitu vingine hivyo vyote 6 nilivyoorodheshwa hapo juu kama OFFA, lipia shilingi elfu 10 kupitia namba zetu zifuatazo, 0765553030 au 0712202244, kisha tuma ujumbe usemao; 

"NITUMIE MCHANGANUO WA USADO NA OFFA YA VITU 6"

Kumbuka hii offa ni ya muda mfupi na pia Group la whatsapp halikawii kujaa, hivyo ni vyema ikiwa unanufaika na masomo haya basi uwahi offa hii mapema kabla haijamalizika au group kujaa.

NAMBA ZETU NI, 0765553030  au  0712202244  jina ni;


Peter Augustino Tarimo


KARIBU SANA! na usisahau kufuatilia mfululizo wa semina hii hapo kesho tena saa 4 -5 asubuhi.


                                       SEMINA SIKU-2 
I

0 Response to "SEMINA: MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUSAGA NA KUUZA UNGA SAFI WA DONA (USADO MILLING)-1"

Post a Comment