Leo ni siku ya 5 ya semina
yetu hii na tunakwenda kujifunza jinsi ya kuandika hatua kwa hatua sura
inayoitwa MIKAKATI NA UTEKELEZAJI. Sura hii pia ni muhimu kwani baada ya
kulijua vizuri soko lako ndipo sasa unapanga ni mambo gani utakayoyafanya,
mbinu mbalimbali utakazotumia ili uweze kuyafikia malengo uliyojiwekea
kibiashara.
Mathalani umelenga kuwa na
mauzo ya shilingi milioni moja katka kipindi cha mwezi mmoja, ni lazima ukae na
kujua utatangaza vipi biashara yako hiyo, utauza namna gani na hata utasambaza
kwa njia zipi bidhaa zako. Ili kufahamu
kinagaubaga sehemu hii ni vizuri zaidi ukawa na MCHANGANUO HUO WA usado Milling
pamoja na Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI.
Basi hebu moja kwa moja
tukaone USADO Milling mikakati yao waliiweka vipi;
5.0
MIKAKATI NA UTEKELEZAJI
Hebu kwanza kabla ya kufanya chochote tuweke mezani vipengele
vidogo vitakavyotuwezesha kuandika sura hii nzima, vipengele hivi ndio dira
yetu itakayotuongoza;
5.1
Nguvu za kiushindani
5.2
Mkakati wa soko
5.2.1
Kauli ya kujipanga katika soko
5.2.2
Mkakati wa bei
5.2.3
Mkakati wa matangazo/promosheni
5.2.4
Programu za masoko
5.3
Mkakati wa mauzo
5.3.1
Makisio ya mauzo
5.3.2
Programu za mauzo
5.4
Mkakati wa ushirikiano
5.5
Vitendo na utekelezaji au Uendeshaji
Katika kipengele
kidogo cha, “5.5 Uendeshaji” kwenye
mchanganuo huu wa USADO hakijawekwa hapo kilipo bali niliamua kukifanya kuwa
moja kati ya Vipengele vikuu au SURA inayojitegemea. Hili halina neno na
mchanganuo huu utakuwa na Sura 9 badala ya 8 kama ilivyozoeleka mara nyingi
kwenye michanganu mingine katika Kitabu chetu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI.
Mara nyingi sana
Vitendo na utekelezaji ama Uendeshaji katika baadhi ya michanganuo ya biashara
huwa hakipo au huandikwa aya chache tu kutokana na aina ya biashara hizo
kutokuwa na shughuli hizo au kutokuwa na umuhimu wa kuviweka. Lakini biashara
kama hii ya kiwanda ni lazima kipengele hiki kiwepo kwani uendeshaji ndiyo
shughuli mama na muhimu zaidi.
Basi kama kawaida tunaanza na Muhtasari mdogo wa Sura hii ambao
lakini huja kuandikwa mwishoni, kisha nitarukia moja kwa moja kipengele kidogo
kifuatacho;
5.1
Nguvu za kiushindani
Kwenye nguvu za kiushindani za USADO Milling nimetaja na
kuelezea jumla ya vitu vitatu ambavyo ni UBORA, ENEO na KAULIMBIU yao. Vitu
hivi ndiyo USADO wanavyofanya kwa uzuri kuwazidi washindani wao wote na ndivyo
wanavyojivunia sokoni.
Kauli ya WANAUME WA DAR
HULA DONA kwenye nembo na matangazo yao itakuwa ni ya kipekee na iliyo na
uwezo mkubwa wa kuwahamasisha wateja wao walengwa ambao ni wanawake walioolewa wenye
umri kuanzia miaka 25 – 60 kununua unga wao kama njugu. Hakuna mwanamke
anayependa mume au familia goigoi.
5.2
Mkakati wa soko
Kati ya mikakati mikubwa 2 kwenye sura hii, SOKO na MAUZO,
mkakati wa soko umegawanyika katika mikakati midogomidogo 4 ambayo ni mkakati
wa kujipanga kwenye soko (Positioning), Matangazo/promosheni,
mkakati wa bei na mkakati wa usambazaji. Na yote hiyo imeelezewa vizuri kabisa
kama unavyoona kwenye mchanganuo wako huo wa USADO Milling.
5.2.2
Kaulimbiu yetu ya kujipanga sokoni,
Hapa nilielezea jinsi USADO Milling ilivyojipanga katika soko la
unga wa dona
kama kampuni itakayotengeneza na kusambaza unga safi na salama wa dona kwa
lengo la kukidhi mahitaji ya soko lake lengwa. Kujua mahitaji hayo maalumu na
ambayo hakuna kampuni nyingine yeyote katika eneo zima la Mikoa ya Pwani na
Jiji la Dar es salaa inayoweza kuyakidhi kwa ufanisi kama wao soma kwenye
mchanganuo huu kipengele hiki. Hivyo ndivyo USADO ‘walivyojiposition’ kwa wateja wao wawaone na kuwachukulia sokoni.
5.2.2
Promosheni na Matangazo
Kipengele hiki kidogo
chini ya mkakati wa soko la USADO Milling nimeelezea kinagaubaga namna ambavyo
kampuni ya USADO itafikisha ujumbe kwa wateja wake walengwa kuhusiana na uwepo
wa bidhaa yao ya Dona. Nimetaja njia mbalimbali watakazozitumia kama unavyoona
lakini pia ningeweza kutaja njia nyingine nyingi zaidi kama wamiliki wangeona
zinafaa kulingana na utafiti wao jinsi walivyoufanya.
5.2.3
Mkakati wa Bei
Kwenye soko bei ni kitu muhimu sana na ambacho inatakiwa
kuwekewa mkakati madhubuti ili kuweza kuwanasa wateja kwa urahisi. USADO nao
hawajabaki nyuma kwani wamehakikisha watatumia mbinu ya kutokupandisha bei
kupita washindani wao kusudi wateja waamue kuchagua kununua kwao kutokana na
zile faida za ziada wasizoweza kuzipata kutoka kwa hao wshindani wao. Hii yote
ni kuhakikisha wateja wasipate kisingizio chochote cha kuukataa unga wao wa
dona.
5.2.4
Mkakati wa Usambazaji.
Kwenye usambazaji kitu muhimu walichofanya ni kuhakikisha
wanakuwa na kituo kikuu cha usambazaji eneo la kimkakati la Mbezi Mwisho, Mbezi
mwisho ni stendi inayofikika kwa urahisi siyo tu kutoka kila kona ya jiji la
Dar es salaam na Pwani bali kutoka maeneo mengine yote ya Tanzania yanayolima
mahindi kwa wingi na Afrika Mashariki kupitia barabara kuu ya Morogoro.
5.3
Mkakati wa Mauzo.
Kama kipengele kidogo kinachojitegemea katika Sura hii baada ya
kile cha mkakati wa soko, mkakati wa mauzo nao una kipengele chake kingine
kidogo kinachoitwa, makisio ya mauzo. Katika mkakati wa mauzo kuna mambo
makubwa mawili yaliyotajwa pale ambayo yakitekelezwa vizuri mauzo yataongezeka
haraka zaidi.
5.3.1
Makisio ya Mauzo na Gharama za Mauzo.
Kama nilivyosema katika kipengele kilichotangulia, Makisio ya
mauzo ni kipengele kidogo cha Mkakati wa mauzo na huwa kipengele hiki basi
ndipo tunakutana tena kwa mara ya pili na namba baada ya pale mwanzo kama
utakumbuka kwenye sura ya 2 ya “Maelezo ya biashara” tulipoona kwa mara ya
kwanza namba katika jedwali la Mahitaji ya kuanzia biashara au Mtaji.
Jinsi makisio ya mauzo
yalivyofanyika;
Kwanza kabisa nilitambua mauzo yatatokana na vitu gani ambapo
kwa USADO Milling vitu vitakavyouzwa ili kuleta mapato vipo viwili 2, unga wa
dona pamoja na Mifuko (viroba) baada ya kutumika kubebea mahindi
Tulikisia mauzo ya
tani 1 mpaka tani 1.5 kwa wiki, hii inamaanisha kwamba makisio ya mauzo ya unga
kwa mwezi (wiki 4) ni tani (1 – 1.5 ) x 4 sawa na tani 4 - 6 kwa mwezi. Hivyo
miezi mauzo ni mazuri kabisa huweza kufikia tani 6 na kwa miezi ambayo mauzo ni
madogo kabisa tumekisia kuwa ni wastani wa tani 4 kwa mwezi. Bei ya
mfuko/kiroba kitupu kimoja ni shilingi 500.
Mauzo huambatana na Gharama za mauzo ambazo kwa USADO gharama za
mauzo ni zile zinazotokana na ununuzi wa mahindi kama malighafi, usafirishaji
wake pamoja na gharama za kuyahudumia kabla ya kusagwa mfano malipo kwa vibarua
wanaopeta mahindi, msagishaji, umeme wa kusagia pamoja na vifungashio.
Katika jedwali kwenye mchanganuo wetu Mauzo na gharama za mauzo
vyote vimeonyeshwa vizuri.
Kama chati ya mauzo kila mwezi kwa mwaka 2020 inavyoonyesha hapo
juu mauzo ya unga wa dona yanatarajiwa kubadilika kulingana na vigezo
mbalimbali mfano miezi ya Mei na Juni mauzo ni makubwa, Agosti yatashuka kidogo
na kupanda tena mwezi Januari na Februari. Tofauti hii itasababishwa na vigezo
vingi vikiwemo, misimu tofauti, wingi au upatikanaji wa mahindi sokoni, washindani
na bei ya unga inayobadilika kila wakati sokoni.
Baada ya kukisia mauzo na gharama zake kila mwezi sasa nahamia
mauzo na gharama zake kwa mwaka mzima wa kwanza wa 2020 kisha miaka mingine
miwili inayofuata, 2021 na 2022. Mwaka wa kwanza nilipata kwa kujumlisha mauzo
ya miezi yote 12 niliyopata pale juu lakini miaka 2 inayofuata nimefanya
makisio kwa kutumia asilimia 25% mwaka wa pili na asilimia 50% mwaka wa 3. Ili
kuelewa kwa uzuri zaidi nakusihi ufuatilie vyema majedwali na chati zote katika
mchanganuo wako kamili wa USADO Milling.
Kufikia hapo ndugu mfuatiliaji wa course hii, nimefika mwisho wa
Sura ya 5 iliyohusu Mikakati na Utekelezaji. Lakini kama ulivyoona kipengele
cha Utekelezaji au Uendeshaji sikukiweka hapa na nimekipa Sura yake chenyewe
kutokana na unyeti wake kwenye aina hii ya biashara ya kiwanda. Hivyo kaa
tayari kujifunza kipengele hicho katika Sura inayofuata. Asante sana.
0 Response to "SEMINA SIKU YA 4: MRADI WA MASHINE YA KUSAGA UNGA SAFI NA SALAMA WA DONA (MCHANGANUO HATUA KWA HATUA)"
Post a Comment