Katika safu yetu leo ya Ongea na Mshauri ama Uliza
ujibiwe tutamjibu msomaji wa blogu hii aitwae Edson, swali lake nitaliweka kama
alivyouliza kwenye “screenshot” hapo
chini lakini pia kama kichwa cha post kinavyosema. Alimaanisha hivi; MTAJI WA
BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA ANAWEZA AKAANZA NA MTAJI WA SHILINGI NGAPI?
Majibu:
Ingawa sijajua aina ya duka la rejareja unalotaka
kuanzisha kwani kuna biashara za maduka ya rejareja ya aina nyingi. Kwa mfano
unaweza ukawa unataka kuanzisha duka la rejareja la vyakula mchanganyiko
maarufu kama maduka ya mtaani/maduka ya kina Mangi nk. au hata duka la rejareja
la nguo, duka la dawa muhimu, duka la vifaa vya umeme, duka la vipodozi na urembo, biashara ya duka la vinywaji au laweza kuwa ni duka la rejareja la aina
yeyote ile zikiwemo biashara za supermarkets.
Zoote hizo ni aina za biashara za maduka ya rejreja kwa
mujibu wa kitabu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJREJAREJA, kitabu
mashuhuri Tanzania chenye uchambuzi wa kina kuhusiana na biashara zote za
rejareja duniani ikiwemo biashara ya duka la rejareja iliyojizolea umaarufu
mkubwa sana katika mitaa mingi ya miji na vijiji vya Tanzania.
Ukijaribu kuuliza
watu mbalimbali ni kiasi gani cha mtaji (fedha) mtu unachohitaji kuwa nacho ili
uweze kufungua duka la rejareja la kawaida mtaani, utapewa majibu mengi na
miongoni mwa majibu hayo hauwezi ukasema lipi ni sahihi zaidi ya jingine.
Ukweli ni kwamba hauwezi ukasema duka linatakiwa lianze na kiasi fulani cha
fedha kwani kila mtu anayeanzisha duka uwezo wake ni tofauti na mwingine, hivyo
watu hufungua maduka yenye ukubwa na hadhi tofauti. Kioski(kiduka kidogo) na
supermarket zote ni aina za biashara za maduka ya rejareja lakini mitaji yao
inatofautiana kwa kiasi kikubwa sana
Ndiyo maana tunasema
kwamba kabla haujaanzisha duka lako, tengeneza kwanza Mchanganuo mfupi wabiashara ya duka lako(Mpango wa biashara au kwa kimombo Business plan) kujua kiasi cha
fedha zitakazohitajika kama gharama za awali pamoja na gharama za uendeshaji.
Gharama za awali za
kuanzia zinajumuisha, pango la mwezi mmoja au miezi 6 ya chumba utakachotumia,
gharama za kumlipa dalali kama utamtumia, gharama za ukarabati wa eneo la
biashara yako ama matayarisho ya fremu yako ya duka, vitu kama mzani, makasha(shelfu
za duka), meza, viti n.k. ambapo gharama za kuendeshea zinajumuisha fedha za
kununulia bidhaa kwa ajili ya kuuza, mshahara kwa msaidizi /wasaidizi pamoja na
kulipia bili mbalimbali zikiwemo umeme, ushuru, wa taka na maji.
Kwa mfano una
shilingi zako laki tatu(300,000) tu na unataka kuanzisha duka dogo, je itawezekana? jibu ni ndiyo, kwani itakubidi kuhakikisha
katika mchanganuo wako gharama za vitu mbalimbali zilizotajwa hapo juu
unaziweka chini kwa kadiri inavyowezekana ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu za
aina mbalimbali ikiwemo, kuweka aina za bidhaa za duka zenye faida ndogo lakini hutoka haraka haraka, kutafuta mbia, kukopa kwa karadha (karadha maana yake ni kwamba unaazima vifaa mfano mafriji kwa mtu na kisha unamlipa riba ya
kuvitumia kwa muda mtakaokubaliana huku vifaa vikiendelea kubakia kuwa
mali yake).
Maduka mengine watu
huanzia nyumbani kwa kupanga baadhi ya bidhaa barazani, wanapopata mtaji wa
kutosha hufungua kioski au genge na mwishowe duka la ukweli lenye kila kitu
ndani yake. Kwa mantiki hiyo hauwezi ukasema eti kuna kiasi maalumu cha mtaji
unachopaswa uwe nacho kwanza ndipo uweze kufungua duka lako la rejareja.
Lakini kwa maoni
yangu binafsi mimi kama Peter Tarimo, kwa mfano ukitaka kufungua duka dogo la
kawaida lenye vitu muhimu karibu vyote kwa mahitaji ya kila siku ya watu ukiwa
na shilingi za kitanzania kuanzia Milioni moja mpaka milioni 6, au tuchukulie
wastani milioni tatu (3,000,000/= )
unaweza ukafungua pasipo kupata usumbufu mkubwa duka lako la wastani kwani
mtaji wa kutosha ni kigezo muhimu sana ingawa siyo lazima sana uwe na mtaji
mkubwa ndipo uweze kuanzisha duka la rejareja;
Mathalani tukichukua
hiyo milioni tatu(3) niliyopendekeza hapo juu tunaweza kufanya uchanganuzi wetu
kama ifuatavyo(huu ni mfano tu lakini
kulingana na mawazo yangu mwenyewe, wewe yaweza kuwa tofauti)
MAHITAJI
YA DUKA LA REJAREJA:
*
|
=
|
400,000/=
|
* Pango
miezi sita (6)
|
=
|
600,000/=
|
*Mzani
mmoja (1)
|
=
|
150,000/=
|
*Makasha
ya kupanga bidhaa (fremu)
|
=
|
150,000/=
|
*Vifaa
mbalimbali
|
=
|
200,000/=
|
*Bidhaa
za kuanzia
|
=
|
1,500,000/=
|
JUMLA.
|
=
|
3,000,000/=
|
Faida
ya biashara ya duka la rejareja
Kwa mchanganuo huo
mfupi wa gharama za kuanzishia duka lako la rejareja unaweza kuona kwamba, gharama
za manunuzi ya mali(bidhaa) zitakazouzwa ili kutengeneza faida dukani thamani
yake ni shilingi milioni moja na laki tano(1,500,000)
Ni kawaida kwenye
duka la rejareja karibu kila bidhaa utakayouza faida yake ni kati ya asilimia
25% mpaka asilimia 30% ya mauzo yake. Hii ni kusema kwamba ukinunua mzigo huo
wa shilingi milioni 1.5 ukafanikiwa kuuza wote pengine ukapata shilingi milioni
mbili (2) basi ujue hapo ni lazima faida yako itakuwa kati ya shilingi laki 5
mpaka laki 6 yaani asilimia 25% – 30% ya hiyo milioni 2
SOMA: Biashara ndogondogo za kufanya Dar es salaam kwa mtaji kidogo bila kulipa pango la nyumba(fremu)
Kwa hiyo ndugu yangu
Edson nikutie tu moyo kwamba mtaji wowote ule uliokuwa nao unaweza ukaanza,
ningependa kukupatia mbinu nyingine moja kuhusu mtaji wa duka la rejareja
ambayo haijalishi hata kama una mtaji kidogo kiasi gani lakini unaweza ukaanza
biashara ya duka. Biashara yeyote ile ukisema usubiri mpaka upate mtaji kiasi fulani
ndipo uanze unaweza usiianze maisha yako yote.
Unaweza kuanza
vyovyote vile ndio maana kuna mahali katika majibu yangu nimekuambia kwamba
wapo watu hata huanzisha maduka yao kwenye vyumba vya kuishi walivyopanga. Siyo
lazima uanzie kwenye fremu ya duka na mfano halisi naweza kukupatia ushuhuda wa
kwangu mimi mwenyewe nilivyoanzisha duka langu katika mtaa wa Msimbazi Kariakoo
nikiwa sina hata senti tano mfukoni.
Nimeeleza mkasa huo
mzima katika kitabu changu cha Mafanikio ya biashara ya duka la rejareja kwa
shuhuda za picha za rangi, zipo zaidi ya picha 8 katika ukurasa wa 10 wa kitabu
hicho toka wiki ya kwanza kabisa naanza mpaka duka linaonekana duka. Na zaidi
ya hapo nimeeleza kinagaubaga jinsi ya kuendesha biashara ya duka la rejareja.
Kuna jamaa yangu
mwingine mmoja pia alinipa ushuhuda wake wa jinsi alivyopata mtaji wa duka
nilipokuwa naandika kitabu hicho, yeye alikuwa akiishi Manzese. Staili
aliyoitumia kupata mtaji wa kuanzisha duka lake kwa kweli hata mimi iliniacha
hoi, jamaa hakuwa na hata mia mfukoni tena akiishi kwa kaka yake pale Tandale
Kwa Mtogole.
Alianza kwenda mjini kama
utani akatengeneza ukaribu na matajiri kadhaa wa maduka ya jumla na rejareja
wakawa wanamwamini(bila mtaji wa pesa) kiasi kidogo cha mali alizozisambaza katika
maduka ya rejareja maeneo ya Manzese na Magomeni. Bei alizowauzia ni zilezile
wanazouziwa wanapokwenda maduka ya jumla kufungasha mali hivyo yeye ubunifu
wake hapo ulikuwa ni kuwapunguzia gharama za kufuata mzigo.
Kwa kuwa maduka yale
ya jumla walimwachia asilimia fulani ya faida kwenye kila bidhaa za duka la
rejareja alizochukua, haukupita muda mrefu sana akaanza kumiliki mtaji wake
mwenyewe wa duka la rejareja alilomwachia mkewe asimamie pale Kwa Mtogole huku
yeye akiendelea kuwasambazia mzigo watu
wa maduka ya rejareja kwa pikipiki. Hatimaye yule jamaa ninavyoongea sasa
hivi anamiliki maduka kadhaa ya jumla na rejareja maeneo ya Manzese na Magomeni
na ni Tajiri wa kutupa!
.....................................................
Kujipatia vitabu vyetu mbalimbali wasiliana nasi kwa namba 0765553030
Masomo katika group letu la whatsapp & Telegramu pia yanaendelea kila siku na leo hii 28/5/2020 tutakuwa na somo lenye kichwa cha habari kifuatacho;
Chakula ya akili nzuri saana
ReplyDeleteElimu nzuri Sana hii hasa kwetu sisi vijana! Let's think beyond we can grow Rich! Thanks for brain's diet
ReplyDeleteElimu nzuri ya kufaliji ,naamini hata mm nitaweza tusikate tamaa na tumutangulize Mungu katika yote.
ReplyDeleteKwanini hakuna mtu aliefafanua upatikanaji wa eneo?
ReplyDeleteVp kuhusu biashara ya nguo
ReplyDeleteGoos
ReplyDelete