Kabla sijakwenda kukuletea muhtasari wa
mchanganuo mzima wa biashara ya genge la kisasa la matunda, mbogamboga na
vyakula la Duble M FRESH, hapa chini nitatoa maelezo kidogo kwanza kuhusiana na
sekta nzima ya biashara hii ya genge, faida, uanzishaji wake na wateja wa genge kwa
ujumla.
Matunda na mbogamboga ni mazao ya chakula ya
biashara yenye faida kubwa. Wengi hudhani ni biashara za vijijini lakini ukweli
ni kwamba watu wanaoishi mijini ndio wateja na walaji wakubwa wa mazao haya.
Katika mikoa inayokua kwa kasi kubwa kama vile mikoa ya Dodoma, Dar es salaam,
Arusha, Mbeya na Mwanza mazao ya chakula na hususani matunda na mboga mboga
yamekuwa ni biashara ya mtaji mdogo inayowaingizia wajasiriamali pesa nyingi na
ni tegemeo la watu wengi kuliko biashara za mtaji mkubwa.
Katika orodha ya Michanganuo ya biashara zilizopo
katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, tumeweka michanganuo
ya biashara ndogondogo za mitaji midogo kuanzia elfu 50(50,000), laki mbili(200,000)
mpaka laki tano(500,000) lakini pia kuna mipango ya biashara kubwakubwa za
mtaji kuanzia milioni 20, milioni 50 na kuendelea. Katika orodha hiyo kuna
biashara ya GENGE LA MATUNDA NA MBOGA iitwayo MMFRESH au DOUBLEM FRESH. MMFRESH
ni genge la kisasa lililopo katika Manispaa ya Kinondoni eneo la Sinza.
Uzuri wa biashara ya genge ni kwamba, mtaji
wa biashara ya genge siyo lazima uwe mkubwa sana na hauhitaji kukodi fremu ya
gharama kubwa kama ilivyokuwa kwa biashara zingine kama biashara ya duka la
rejareja. Kuna watu huamua kuanzisha duka genge na wengine huanzisha magenge tu
peke yake. Tofauti ya vitu hivi viwili ni kwamba, duka genge huuza mchanganyiko
wa bidhaa za matunda, mbogamboga, vyakula na bidhaa nyingine za madukani wakati
genge tu peke yake huuza matunda na mbogamboga au na vyakula kidogo.
Faida
ya biashara ya genge:
Biashara ya genge inalipa faida karibu nusu
kwa nusu ya mtaji ulionunulia mali. Hapa namaanisha kwamba unaweza ukanunua kwa
mfano tikiti maji shilingi elfu moja(1,000) na ukaja kuliuza kwa shilingi elfu
2(2,000) halikadhalika unaweza ukanunua ndizi shilingi mia ukaiuza shilingi mia
mbili, hapo watu husema umepata faida nusu kwa nusu.
Eneo
la kuweka biashara ya genge
Kama ilivyokuwa kwa biashara nyingine za
rejareja mfano wa biashara ya duka, eneo ndio kigezo muhimu kushinda kila kitu.
Jinsi ya kuanzisha biashara ya genge la matunda na mboga ni lazima genge lako
ulifungue katika eneo unalojua lina watu wengi au makaazi ya watu ili uweze
kupata wateja wa kutosha.
Usajili,
kodi, TIN namba na sheria mbalimbali
Biashara ya genge watu wengi huanzisha bila
hata ya kwenda TRA wala mahali pengine popote pale kujisajili au kukata leseni
na vibali mbalimbali kama zilivyo biashara nyingine. Si kama vitu hivyo
havihitajiki, la hasha bali ni kutokana na sababu kwamba biashara ya genge
inachukuliwa kama ni biashara ndogondogo isiyozidi mtaji wa shilingi milioni 4.
Biashara za udogo huu mara nyingi serikali huwa haihangaiki nazo kwenye suala
la kodi wala leseni ingawa pia kuna magenge mengine yanauza mauzo makubwa hata
zaidi ya maduka.
Kuna ushuru unaodaiwa na serikali za mitaa
pamoja na tozo nyingine mbalimbali mfano za usafi wa jiji nk..Lakini pia genge
lako likikua sana kutoka hatua ya genge la kawaida na kupita hatua ya genge
duka maafisa wa kodi na leseni wanaweza wakakutembelea na kukutaka ukakate vitu
hivyo.
Bidhaa
za genge:
Bidhaa za genge ni matunda ya aina zote kama nyanya,
maembe, machungwa, limao, ndimu, nanasi, ndizi mbivu mapeasi, tikiti, mabungo,
ukwaju, mapapai nk., mbogamboga mfano, mchicha, kabeji, spinachi, matembele,
karoti, pilipili hoho, pilipili kali, matango, bilinganyi nk. , baadhi ya
vyakula kama vile, ndizi mbichi, mchele, maharage, unga, viazi vitamu, viazi
mviringo, dagaa wakavu, samaki, dagaa wa kukaanga, viungo vya aina mbalimbali
kama iliki, mdalasini, karafuu na bizari.
Mtaji
wa kuanzisha genge:
Ukiwa na eneo tayari iwe ni kibarazani kwako au
kandokando ya barabara, genge la matunda na mbogamboga unaweza kuanza hata
ukiwa na shilingi elfu kumi(10,000). Lakini kama ninavyoshauri mara kwa mara
kuanzisha biashara yeyote ile hakuna mtaji maalumu unaoweza kuambiwa na
mtaalamu au mtu mwingine yeyote kwamba mtaji kiasi fulani ndio unatosha kuanza.
SOMA: Nataka kuacha kazi nianze biashara kwa mtaji wa milioni 5 hadi 10, nishauri nianze biashara ipi?
Kitakachokujulisha ni mtaji wa shilingi ngapi
uanze nao ni malengo na maono yako uliyokuwa nayo kichwani. Na vitu hivi maono
na malengo ndio mpango wako wa biashara unayotaka kuifanya na wala siyo
makisio(projections) kama wengi
wanavyodhani ingawa makisio ni sehemu tu ya mpango wa biashara yako uandike
usiandike. Kwa urahisi kabisa ukitaka kujua unahitaji mtaji kiasi gani wa
kuanza biashara yako, orodhesha mahitaji yote(gharama) ambayo ungependa
biashara yako iwe nayo na jumla ya mahitaji hayo ndiyo mtaji unaohitaji, basi
hamna zaidi.
Soko/Wateja wa biashara ya genge
Biashara ya kuuza genge wateja wake wakubwa
ni ni kina mama wa majumbani walio na familia. Hata kama utamuona mtoto au baba
akija gengeni kwako kununua mahitaji basi ujue kuna uwezekano mkubwa nyuma yake
kaagizwa na mama(mwanamke) ambaye ndiye mpishi pale nyumbani vinginevyo basi
watakuwa ni wateja wachache wanaume wanaoishi ubachela au wanafunzi wa vyuo.
Hivyo basi katika mkakati wako wa soko ni lazima uwalenge kina mama zaidi kama
utataka kufaulu biahsra hii.
Wanawake ndio wateja wakubwa wa biashara ya
genge.
|
Baada ya kuona kwa ufupi biashara ya genge
ilivyo sasa tutakwenda kuona Muhtasari wa mpango wa biashara ya genge la
matunda na mbogamboga la MMFRESH, genge lililopo Sinza Kinondoni Dar es salaa.
Mchanganuo huu mzima unapatikana katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA
UJASIRIAMALI, kitabu kilichosheheni kila kitu mjasiriamali anachohitaji ili
kufanikisha biashara ya kisasa. Mbali na michanganuo ya biashara mbalimbali
kina masomo mengine yote ya biashara na ujasiriamali sehemu moja.
MUHTASARI
WA MPANGO WA BIASHARA YA GENGE (MMFRESH)
Genge la matunda na mboga ‘fresh’ maarufu kama
DoubleMfresh au (MMFresh) ni genge ambalo dhamiria yake kuu ni kuboresha afya
za watu wa Kinondoni kwa njia ya kuwauzia mboga mboga na matunda yenye ubora wa
hali ya juu na ambayo hutoka shambani muda mfupi.
DoubleMfresh hadi kufikia mwaka wake wa 4
litakuwa na matawi mengine matatu kila
moja katika kila tarafa zinazounda manispaa nzima ya Kinondoni, lengo likiwa ni
kila mwana Kinondoni aweze kufurahia huduma hizi karibu na nyumbani anakoishi
badala ya kuzifuata masoko yaliyokuwa mbali.
Genge litamilikiwa na Bwana Omar Masoud Othman
mwenye uzoefu mkubwa katika biashara
ndogondogo hususani biashara ya dagaa, samaki na mazao yatokanayo na
bahari, uzoefu huo aliupata kutoka kwa marehemu
wazazi wake ambao walifariki dunia kutokana na ajali ya meli ya MV Spice
iliyotokea Septemba 10 mwka 2011 huko Nungwi Visiwani Unguja.
Mwaka 2012 ndipo alipoamua kulifunga genge la
wazazi wake kisiwani Pemba na mtaji wote kiasi cha shilingi milioni 2 akauhamishia
jijini Dar es Salaam ambapo anatarajia kufungua Genge la kisasa katika kitongoji cha Sinza Kumekucha kilichopo ndani
ya tarafa ya Magomeni na baadaye katika Tarafa nyingine zote tatu za Wilaya ya
Kinondoni yaani, Kinondoni yenyewe, Kibamba na Kawe.
Bidhaa zitakazopatikana gengeni MMFresh ni
pamoja na mbogamboga na matunda karibu aina zote, nafaka aina mbalimbali pamoja
na bidhaa zitokazo baharini kama vile samaki waliokaushwa na dagaa.
Soko la matunda na mbogamboga jijini Dar es
Salaam hususani maeneo ya Sinza ni kubwa na lina endelea kukua kadiri idadi ya
watu nayo inavyozidi kuongezeka. Wilaya ya kinondoni kwa mujibu wa tovuti ya
Jiji la Dar es Salaam idadi yake ya watu inakisiwa kufikia watu 1,900,000 Mwaka
2012 kwa ongezeko la asilimia 4.1% kila mwaka.
Mkakati wa soko wa MMfresh utalenga zaidi
katika kuwavutia wateja wale wenye kipato cha kati kwa kufanya mambo mbalimbali
yatakayowajulisha na kuwavutia ikiwamo, kutengeneza na kusambaza kadi maalumu
kwa majirani siku ya ufunguzi rasmi, kubandika matangazo mitaani pamoja na
kutoa zawadi na nyongeza kwa wateja na watoto wadogo katika zile siku za mwanzo
mwanzo.
Mauzo katika miaka mitatu ya mwanzo yanakisiwa
kama ifuatavyo, mwaka 2012 shilingi 10,800,000/=, 2013 shilingi 16,200,000/= na
shilingi 24,300,000/= mwaka 2014. Asilimia ya faida ghafi kwa mauzo ni 45%
miaka yote mitatu. Faida halisi katika kila mwaka inakisiwa kuwa 280,000/=,
2510,000 na 4,705,000. Chini ni chati inayoangazia kwa ufupi makisio hayo.
1.1
Dhamira
kuu.
Dhamira kuu ya DoubleMFresh ni kuboresha afya
za watu wa maeneo ya Sinza na Kinondoni kwa ujumla kwa kuwauzia mbogamboga na
matunda yaliyokuwa “fresh” kutoka shambani. Hatutauza mbogamboga na matunda
yaliyolala ili kuhakikisha wateja wetu wanapata bidhaa bora na safi. Hii
itawavutia wateja wengi waendelee kuja kila siku na kusababisha bidhaa
kutokulala ovyo.
1.2
Malengo:
MMFresh
linatarajia kufikia malengo yafuatayo baada ya kufungua genge lake la kwanza
pale kumekucha.
(1) Kufungua
magenge mengine yapatayo matatu ifikapo mwaka wa nne.
(2) Kufikisha
faida ya sh.4,705,000/= mwishoni wa mwaka 2014.
(3) Kufungua
duka la rejareja ifikapo mwaka wa tano.
1.3
Siri
za mafanikio:
Mambo
yatakayosababisha DoubleMFresh kupata mafanikio ni haya yafuatayo:
(i)
Kuuza mbogamboga na matunda yaliyokuwa na
ubora wa hali ya juu.
(ii)
Kutengeneza maumbo yanayovutia kwa ajili ya
kupanga bidhaa.
(iii) Kupanua
soko kwa kufungua matawi maeneo mengine.
(iv) Kutoa
huduma nzuri ambazo zitavuka matarajio ya wateja.
2. Maelezo
kuhusu Biashara:
DoubleMFresh litamilikiwa na Bwana Omar Masoud
Othman na litaanza rasmi na mtaji wa Sh. 2,000,000/= ambazo ni gharama pamoja
na bidhaa za kuanzia biashara.
2.1 Umiliki
wa Biashara:
DoubleMFresh litamilikiwa na Bwana Omar Masoud
Othuman. Bwana Omar amejifunza biashara ndogondogo kutoka kwa wazazi wake
kisiwani Pemba tangu akiwa anasoma. Mwaka 2012 ndipo alipohamia jiji Dar es
Salaam baada ya wazazi wake kufariki dunia. Aliendelea na uuzaji wa samaki na
dagaa mitaani aliowachukua feri mpaka sasa anapotarajia kufungua Genge la
kisasa katika mtaa wa Sinza kumekucha………………………………………….
Mchanganuo mzima wa biashara hii ya Genge la
matunda, mbogamboga na vyakula.(MMFRESH) pamoja na michanganuo ya biashara
nyingine nyingi zinazolipa unapatikana katika kitabu chako cha MICHANGANUO YA
BIASHARA NA UJASIRIAMALI.
JINSI YA KUKIPATA KITABU HIKI NA BEI.
KITABU CHA KARATASI(HARDCOPY) ni sh. elfu 22 kwa wateja walioko Dar es salaa na tunawapelekea mpaka walipo. Mikoani tunatuma kwa njia ya mabasi ila gharama ya basi huongezeka kutegemeana na basi na eneo mteja alipo.
KITABU NAKALATETE(SOFTCOPY)
Tunatuma popote pale mteja alipo kwenye simu au kompyuta yake na bei ni shilingi elfu kumi(10,000/=)
Kwa mawasiliano, namba zetu ni hizi;
Whatsap/Simu: 0765553030
au Simu/sms: 0712202244
Peter Augustino Tarimo
0 Response to "MCHANGANUO WA BIASHARA YA GENGE LA KISASA LA MATUNDA, MBOGAMBOGA NA VYAKULA "
Post a Comment