Kuna semi na dhana nyingi kuhusiana na suala
la kuchukua mkopo wa biashara kwa mfano wapo wanaosema kwamba; “hakuna tajiri
asiyekopa duniani akafanikiwa kuwa tajiri”, “matajiri ndio wanaokopa tu,
masikini huwa hakopi bali yeye huomba tu misaada”. Misemo hii mingine ina
ukweli lakini pia mingine ni upotoshaji mtupu.
Duniani watu wamegawanyika katika makundi
mawili linapokuja suala la kukopa fedha kwa ajili ya kuendeshea biashara. Kundi
la kwanza ni wale wasioamini kabisa kama mikopo ina uwezo wa kumtoa mtu pale
mahali alipo na kumfikisha mahali bora zaidi kiuchumi. Lakini kundi la pili ni
wale wanaoamini kwamba mkopo wa biashara ndio nyenzo muhimu zaidi kwa
mjasiriamali yeyote yule ikiwa atataka kupiga hatua ya kuelekea uhuru wa kifedha.
Binafsi mimi ni mmoja wa kundi lile la pili
la wale wanaoutazama mkopo kwa jicho chanya na ndio maana katika kitabu changu
cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LAREJAREJA nimezitaja nyenzo kubwa mbili(leverage)
mtu anazoweza akazitumia kukuza biashara yake haraka sana hata kuweza kufikia
hatua ya kufungua maduka au biashara nyingine nyingi.
Katika kitabu hicho ipo nyenzo hii ya Mkopo
lakini pia ipo na nyenzo ya pili ambayo ni muhimu sana hata kushinda hii ya
kwanza. Ni watu wachache sana wanaozijua nyenzo hizi zinavyofanya kazi na hata
wale wachache wanaozifahamu vizuri huwa hawapendi kabisa kuzitajataja ovyo kwa
hofu ya kuibuka washindani kwenye biashara zao zinazoshamiri.
Tukiachana na hayo, hebu tuendelee kujadili
mada yetu ya leo ya mikopo midogomidogo ya biashara kwanini kabla ya kukimbilia
kufuga ngombe uanze angalao na kuku au bata kwanza. Ninachokimanisha hapa ni
kwamba, usikimbilie kuchukua mkopo mkubwa kwanza kabla haujapata uzoefu na
suala la mikopo. Na njia pekee ya wewe kuupata huo uzoefu na mikopo ni kuanza
kukopa kutoka katika taasisi ndogondogo kwanza na kisha baadae unaingia mikopo
mikubwa kwenye taasisi au benki zinazotoa mikopo mikubwa. Experience unayoipata wakati ukiwa na mkopo mdogo ndiyo ileile
unayoipata wakati ukiwa na mkopo mkubwa.
Zipo benki pia zinazotoa mikopo midogomidogo
kuanzia hata laki 3 na kuendelea lakini watu wengi bado hudhani kwamba benki
hizo zenye majina makubwa haziwezi kutoa mikopo midogomidogo yenye masharti
nafuu isiyohitaji dhamana za kutisha. Karibu benki na taasisi kubwa kubwa zote
siku hizi wana vitengo vinavyoshughulika na kuwakopesha wajasiriamali
wadogowadogo wasiokuwa na dhamana za uhakika za kuweka. Mara nyingi hutoa
mikopo kwa vikundi ambavyo ni wanakikundi wenyewe wanaodhaminiana. Mwanakikundi
mmoja akishindwa kurejesha marejesho ya mkopo basi wenzake ndio hubeba jukumu
la kumlipia au kumfuatilia ikiwezekana kumfilisi kwakuwa wao ndio
waliomdhamini.
Sababu
kubwa 5 ni kwanini uanze kwanza na mkopo mdogo kabla haujaomba mkopo mkubwa
1. Kwanza kabisa mkopo mdogo utakupa uzoefu
utakaokufanya ujijengee nidhamu ya hali ya juu ya fedha. Kitendo cha kujua
unawajibika kurejesha fedha za marejesho ya mkopo wako kila wiki au kila mwezi
kitaifanya akili yako kisaikolojia ichukue tahadhari kubwa kwenye matumizi ya
fedha.
2. Mkopo mdogo unakujengea kuaminika na
taasisi za fedha na kuwa mtu unayekopesheka kwa urahisi zaidi popote pale
utakapokwenda kukopa kwani siku hizi taasisi nyingi za kifedha hasa mabenki
wana utaratibu na mfumo maalumu unaobeba taarifa za kila mkopaji nchini, hivyo
ukikopa benki ‘A’ kisha ukazingua, benki ‘B” watakubaini pindi tu wakicheki
jina au kitambulisho chako cha taifa.
3. Unajijengea kidogokidogo rasilimali za
kutosha zitakazokusaidia hapo baadae kuwa kama dhamana ya wewe kukopa mkopo
mkubwa zaidi.
4. Kwa kukopa fedha kidogo kwanza unajipima
uwezo wako wa marejesho upoje. Utajua kama unao uwezo wa kupata shilingi ngapi
kwa siku, mwezi na hata mwaka.
5. Mikopo midogomidogo kwanza itakufanya
ujenge mazoea na watu wengi wa aina mbalimbali
kama vile wakopaji wenzako wajasiriamali, maafisa mikopo kwenye taasisi
za kifedha ambao hata unaweza kuomba kwao ushauri au msaada mwingine wowote ule
wa kibiashara kwa urahisi.
Mbali na mikopo midogomidogo ya vikundi kuna
taasisi na mabenki wanaotoa mikopo kwa mtu mmojammoja lakini mikopo ya namna
hii huwa ina tabia ya kuambatana na masharti magumu kidogo ya dhamana kuliko
ile ya vikundi. Mjasiriamali utatakiwa kuhakikisha unaonyesha dhamana za mkopo
wako kusudi ikijakutokea umeshindwa kulipa marejesho basi benki au taasisi
iweze kuziuza dhamana hizo na kulipia marejesho ya deni la mkopo uliobakia.
Dhamana yaweza kuwa ni mali na samani zako za
ndani, nyumba, kiwanja, kadi ya gari, pikipiki au mali yeyote ile
isiyohamishika. Mshahara wako wa mwezi pia unaweza ukatumika kukudhamini
ukachukua mkopo wa biashara au mtu mwingine yeyote yule anaweza kukudhamini
kuchukua mkopo wa biashara endapo tu mtu huyo atathibitisha kumiliki mali
zilizotajwa hapo juu. Yote hii ni mikopo midogomidoho kuanzia laki mbili, tano
mpaka milioni 5. Kwa mikopo mikubwa pia baadhi ya masharti ni hayohayo ya kuwa
na dhamana za uhakika.
Lakini ni vizuri ikiwa huna kabisa historia
ya kukopa na ndio unaanzisha biashara yako ndogo basi angalau uanze hata na
mkopo mdogo, laki mbili, tatu au hata tano kusudi mambo yakija kuwa magumu
njiani basi usipatwe na kiwewe au madhara makubwa kwani ikiwa utakuwa
umesharejesha kiasi fulani cha pesa bila shaka kiasi kitakachokuwa kimebakia
hakiwezi kuwa kikubwa sana wewe kushindwa kabisa kukilipa hata ikiwa biashara
yako ni ndogo kiasi gani.
Siku hizi hata kuna mikopo hii ya kwenye
mitandao (kukopa online), mikopo kwa
njia ya simu janja yako ya mkononi ama kompyuta ya mezani unaingia tu mtandaoni
unajaza fomu ikiwa ni pamoja na kupakia taarifa za utambulisho wako kama
kitambulisho cha Taifa au cha kupigia kura na kisha unapata mkopo wako fasta
bila dhamana wala vitu kama ada ya mkopo au sijui bima ya mkopo na mengine
mengi. Sifa kubwa ya mikopo hii ni midogomidogo sana wakati mwingine kuanzia
hata shilingi elfu 5, 10, laki, laki mbili mpaka milioni 1. Kuna mifano ya
taasisi nyingi zinazotoa mikopo online na moja ni iliyokuwa ikiitwa TALA
Tanzania na makampuni karibu yote ya simu za mkononi.
SOMA: Je, kukopa ili ukalipe deni la zamani kunawezaje kuboresha mzunguko wa fedha kwenye biashara yako
Ni bora mtu ukaanza kuchukua mkopo kama hii
ya Tala ya shilingi elfu kumi, laki moja, laki tatu na kuendelea ukapata uzoefu
wa mikopo kuliko kuomba moja kwa moja mkopo wa milioni kumi hata ikiwa una
dhaminika huku ukiwa huna historia yeyote ile ya kukopa mahali pengine na wala
hujui mikopo inafanyaje kazi.
Lakini mikopo hii ya kwenye mitandao kwa njia
ya simu ina hatari kubwa moja na ni lazima kwanza mtu ujiridhishe na uhalali wa
kampuni au taasisi inayotaka kukukopesha maanake pia kuna matapeli wengi
wanaotumia fursa hiyo hiyo kujipatia pesa kijanja mtandaoni.
Utakutana na matangazo ya kuvutia mfano; pata mkopo kwa simu chapchap leo, mikopo ya haraka bila dhamana nk. na
ukijiingiza kichakichwa tu unaambiwa utoe kwanza ada ya mkopo huo au chochote
kingine kinachohusiana na mkopo kama kiingilio na hapohapo ukikubali kutoa
unakuwa umeshalizwa.
Mbali na zile taasisi kubwa zenye majina na
mabenki vilevile kuna taasisi nyingine ndogondogo zinazofanya biashara ya
kukopesha pesa kwa riba kisheria kama vile Viccoba, Saccos na kampuni za mikopo
midogo za watu binafsi(Microfinance), taasisi hizi hazijumuishi vikundi vingine
vinavyokopesha mitaani kienyeji kama vile Michezo na upatu kwani huwa hazina
usajili wowote ule serikalini.
Kila aina ya taasisi ina taratibu na masharti
yake kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mfano kiwango
cha mkopo wanachotakiwa kutoa, ruksa ya kukusanya amana za wakopaji nk. Hata
riba za mikopo taasisi hizi kuna kiwango maalumu wanachotakiwa wasizidishe ili
kutokuwaumiza wakopaji. Taratibu na sheria hizi husimamiwa na Serikali chini ya
Benki Kuu ya Tanzania(BOT) na mamlaka nyingine zilizowekwa kisheria.
Kwa upande mwingine wa shilingi wakopeshaji
nao hulindwa na sheria dhidi ya wakopaji pale wanapokaidi au kushindwa
kurejesha pesa walizokopa. Sheria huwabana hata kufikia hatua ya mali zao
kufilisiwa ili taasisi au kampuni isiingie hasara.
HITIMISHO
Ili kujijengea mazoea na tabia ya kurejesha
mkopo bila usumbufu ikiwa ndio unaanza kukopa mkopo wa biashara, anzia mkopo
mdogo wa chini kabisa na kisha upande juu taratibu, usione kama unapoteza muda
kwani hii itakusaidia sana kujenga msingi wa uaminifu kwa taasisi unayokopa
lakini pia kujijenga taratibu kimtaji huku ukikuza rasilimali chache ulizokuwa
nazo ambazo ndizo zitakazokuja kuwa dhamana ya kukopa fedha nyingi zaidi hapo
baadae. Usikimbilie kufuga ng’ombe kabla hujajaribu angalao kufuga kuku au bata
kwani uzoefu unaoupata kwenye mkopo mdogo ndio uleule unaoupata unapochukua
mkopo mkubwa wa biashara.
……………………………………………
Je, unahitaji mpango wa biashara kwa ajili ya
uendeshaji wa biashara yako, kuombea fedha(mkopo) mahali kama benki na taasisi
yeyote nyingine au kwa ajili ya kumtafuta mbia?
Basi usisumbuke, tunaweza kukuandikia au tukakupatia
course nzima, vitabu, templates na sample za michanganuo ukaandika mwenyewe kwa
njia rahisi.
Gharama zetu ni nafuu sana na kazi yako
inamalizika ndani ya muda mfupi. Wasiliana na sisi kwa namba/watsapp:
0765553030
Kununua vitabu vyetu na Michanganuo ya
biashara mbalimbali tembelea duka letu, SMART BOOKS TZ
Ukitaka kitabu cha Biashara ya Rejareja toleo
jipya la 2020 lenye maboresho na vitu vipya bonyeza jina la kitabu, Mafanikio ya Biashara ya Duka la rejareja
Lajabu hasani mrisho
ReplyDelete0672966005
ReplyDeletelojahasani443@gmail.com
ReplyDelete