Kuandikiana mikataba siyo kwenye biashara
ndogondogo tu peke yake bali ni jambo muhimu sana hata katika biashara kubwa za
mamilioni ya shilingi. Bila ya mkataba wa makubaliano biashara haziwezi
kuendelea mbele, migogoro na kutokuelewana kunaweza kuzuka baina ya wenye hisa,
wamiliki wa kampuni, wafanyakazi, waajiri, wateja, wasambazaji bidhaa au wadau
wengine wowote wale kwenye biashara.
Mkataba ni andiko muhimu linaloikinga biashara
dhidi ya migogoro isiyotakiwa inayoweza kujitokeza ndani ya kampuni /biashara
Vitu
vinavyounda mkataba baina ya wenye hisa au wabia wa biashara
1. Haki na wajibu wa kila mwenye hisa.
Mkataba ni lazima ueleze bayana kila mmiliki atakuwa na jukumu gani na wajibu
kwa niaba ya kampuni.
2. Utaratibu wa kutatua migogoro endapo
itatokea. Migogoro inaweza ikasababishwa na kukosa uzoefu, au
tofauti ya kimaono jambo linaloweza kusababisha wabia kushindwa kukubaliana
kwenye mambo kama vile ya usimamizi wa fedha, uongozi nk. Hapa mkataba wa ubia
utazuia yote hayo kutokea
3.
Mpango
wa kuondoka(Exit strategy)
Mwanahisa
anaweza asiridhike akaamua kujitoa njiani au biashara inaweza isiweze
kutengeneza faida ikavunjika nk. Je mtafanyaje-fanyaje? Ni lazima kuwe na
mpango wa mapema. Imeshuhudiwa makampuni mengi hata hapa Tanzania kampuni kama
ile ya Wasafi Classic chini ya mwanamuziki nguli na tajiri Diamond Platinumz (Naseeb
Abdul). Watu walimlaumu sana Diamond na kampuni yake kwamba ni wabinafsi,
hawapendi maendeleo ya wengine nk. pale wamiliki wa WCB Wasafi walipowataka wanamuziki
wake kulipa fidia ya mamilioni ya fedha walipotaka kuvunja mkataba na kampuni
hiyo.
Kitu
kikubwa kilichofanyika pale ni hiki ninachokizungumzia hapa leo. Hivyo unaweza
kuona kwamba mikataba kwenye biashara ina maana na umuhimu mkubwa sana vinginevyo
mtu anaweza tu kujitoa kienyeji baada ya kuona pengine alichokuwa akikitafuta
keshakipata na hii imewafanya waanzilishi wengi wa biashara hasa hasa hizi za
ubunifu kama Sanaa kuishia kuwa hohehahe au hata kufa wakiwa masikini wa kutupa
baada ya watu waliowakaribisha kwenye biashara zao kupata ujanja na kuota mbawa
kabla ya kurudisha kwenye kampuni kile walichokubaliana au kilichotazamiwa.
Wakati
huohuo wao wanakuwa wameshakipata kile walichostahili kama umaarufu au malipo
ya fedha. Mkataba wa wasanii ikiwa utawekwa kabla utasaidia sana kuondoa shida
kama hizi. Ni sawa na uonavyo kwenye mpira, mkataba wa wachezaji ni lazima
usainiwe kabla timu haijaanza ligi vinginevyo utakuta mchezaji mmoja kwa mfano
unaweza kukuta amesaini timu ya simba kumbe tayari alikuwa keshasaini tena timu
ya Yanga na hili linaweza kusababisha hata timu kupewa adhabu na chama cha soka
TFF
Mbali na vitu hivyo 3 nilivyovitaja hapo juu
mkataba unaweza ukawa rahisi tu au pia unaweza ukawa na vitu vingi kutegemeana
na ukubwa wa kampuni au biashara. Mkataba kwa undani unaweza pia ukawa na vitu
vya ziada vifuatavyo;
· Taratibu
za uendeshaji wa kampuni
· Sera
za uuzaji wa shea za kampuni
· Sera
za kulinda wale wenye hisa chache kwenye kampuni
· Aina
za shea kampuni inazotoa nk.
Tanzania watu wengi huogopa sana kuunganisha
nguvu kuanzisha kampuni au biashara za ubia kutokana na kutokuelewa umuhimu wa kuwekeana
mikataba. Kukiwa na mkataba wa makubaliano baina ya wenye hisa au wabia katika
kampuni au biashara hakuna kitakachoweza kuja kwenda mrama maana kila kitu
huwekwa wazi kabla biashara haijaanza kufanya kazi.
Kuunganisha nguvu za mitaji ni njia bora
zaidi ya kujinasua na tatizo la ukosefu wa mitaji na katika nchi za wenzetu
zilizoendelea kama vile China na nyinginezo watu baada ya kubaini umuhimu wa
mikataba kwenye makubaliano ya kujenga ubia wamepiga hatua kubwa sana na
hauwezi tena kuwasikia wakilialia kukosa mitaji ya kuanzisha biashara zao.
Siku hizi biashara nyingi ni zile ndogondogo
na za kati, na ndizo zinazoongoza katika ubunifu, ukuaji kiuchumi na kuchangia
katika kuondoa tatizo sugu la ajira. Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 90%
ya makampuni yote Duniani ni kampuni ndogondogo na za kati(SME’s). Unaweza
ukafikiria kama hali ndiyo hiyo basi kuanzisha biashara ndogo ni jambo endelevu
na rahisi sana lakini kumbe siyo kweli hata kidogo kutokana na tatizo la
kukosekana mitaji ya kutosha kuanzisha biashara. Tatizo hili linahitaji mbinu
mbalimbali za kijasiriamali kulitatua ikiwemo hii ya kuunganisha nguvu watu
wawili au zaidi ambayo ndiyo njia rahisi na nyepesi zaidi ya nyingine zote ya
kupata mtaji wa kuanzisha biashara ndogondogo
Biashara inapokuwa inaendeshwa chini ya ubia
wa watu wawili au zaidi kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kuibuka kutokuelewana
kati yao hasa pale biashara inapoanza kutengeneza faida. Ni muhimu kuwa na
mkataba utakaowahusu wanahisa/wawekezaji kukubaliana jinsi kampuni
itakavyoendeshwa na mkataba huo unatakiwa kuandaliwa vizuri na mwanasheria au
mtu anayeelewa mambo ya mikataba vizuri.
Wajasiriamali ni wepesi sana kudai kuweka
mikataba kwenye mambo mengine mbalimbali mfano wanapotaka kupanga chumba au
eneo la biashara, wanapouziana mali kama kiwanja au nyumba na mtu mwingine au
hata pale wanapotaka kuajiri mfanyakazi / wafanyakazi lakini husahau mkataba
muhimu sana pale wanapounganisha nguvu kama wabia au wanahisa kwenye
biashara/kampuni. Pengine ni kutokana na Watanzania wengi kuhusisha ndugu wa
karibu, jamaa au marafiki pale wanapotaka kuungana kibiashara jambo
linalowafanya waone hamna haja ya kuwekeana mikataba kama watu wasiojuana.
Mfano mwingine ni ule wa wafanyakazi na
mabosi wao (waajiri) katika biashara ndogo mara nyingi sana watu wanakuwa
wakipeana kazi kienyeji sana bila ya kuwa na mkataba wa wafanyakazi wowote
unaoainisha namna mambo yatakavyokwenda na matokeo yake ni kuja kuibuka sintofahamu
kubwa, mfanyakazi anaweza kuihujumu biashara pasipo mmiliki kuwa na uwezo wa
kumwajibisha na wakati mwingine pia tajiri kumhujumu mfanyakazi wake bila ya
mfanyakazi huyo kuwa na chohcote kile cha kufanya. Lakini kama kunakuwa na
mkataba kabla ya kila kitu mambo yanaweza kutatuliwa kwa haki na usawa bila
manunguniko kutoka upande wowote.
Katika Ulimwengu wa biashara na ujasiriamali
kuna mikataba ya aina nyingi nyingine ukiacha huu wa wamiliki au wabia kwenye
biashara, kuna mkataba wa makabidhiano ya mali, mkataba wa wapangaji, makataba
wa ujenzi wa nyumba, mkataba wa ukodishaji mali au chochote kile.
Na hata mkataba wa wafanyakazi wa ndani ambao
watu wengi hudhania tu kirahisirahisi kwamba kwa vile mfanyakazi wa ndani
pengine kamtoa kijijini basi hamna haja ya mkataba wa maandishi naye, kumbe
mkataba huo unaweza hata kuja kumlinda mwenyewe tajiri, hebu fikiria kwa mfano
mfanyakazi anakuja kujanjaruka na kula njama na majambazi wanakuibia kila kitu
ndani, ikiwa ulikuwa huna mkataba wowote naye unadhani ni nani atakayekusikiliza
ukienda kulalamika huko kwenye vyombo vya sheria?
Si watakuhoji mkataba wa mfanyakazi uko wapi, ukikosa na wewe wanakupuuzilia mbali
kwa kuwa ulikuwa ukimtumikisha mtoto wa watu kinyume cha sheria akaamua na yeye
kukukomesha?
HITIMISHO
Ukitaka kufanya biashara ya kisasa katika
karne hii ya 21 iwe ni biashara ndogo au hata biashara kubwa, usikubali kamwe
kufanya makubaliano yeyote yale ya kibiashara hasa ukiwa wewe ndiye mmiliki wa
biashara au kampuni kienyeji bila ya kusini mkataba wa kisheria utakuja kulia,
na siyo lazima kumshirikisha mwanasheria au wakili, mikataba mingine inahitaji
tu mashahidi au ushahidi ili pindi mgogoro ukizuka basi kuwe na ushahidi wa
kile mlichokubaliana pande mbili. Ukiona upande wa pili hautaki mkataba basi
achana naye mapema.
………………………………………
Kwa vitabu na Michanganuo ya Biashara
mbalimbali tembelea duka letu mtandaoni la SMART BOOKS TZ
0 Response to "MKATABA WA WAMILIKI WA BIASHARA / KAMPUNI: UMUHIMU WAKE NA JINSI YA KUANDIKA"
Post a Comment