Mnamo tarehe 14/06/2020 katika blog hii niliandika makala moja iliyokuwa na kichwa cha habari; JINSI YA KUTUMIA MAAJABU YALIYOPUNGUZA CORONA TANZANIA KUBUSTI UCHUMI WAKO UNAOSAMBARATIKA. Katika makala hiyo nilijaribu kwa kadri ya uwezo wangu kuchambua ni nini hasa kilichotokea mpaka Tanzania ikaweza kujijengea uwezo wa kustaajabisha wa kukaribia kuishinda corona.
Mbinu iliyotumika kwa wakati ule iliweza kufanya kazi vizuri sana lakini mara ghafla tukaja kujikwaa mahali fulani. Pamoja na kujaribu kujadili kile kilichosababisha corona kuibuka tena Tanzania(wimbi la pili la maambukizi ya corona) katika makala hii, lakini mimi lengo langu mahsusi leo si hilo, ila ni kutaka tu kuzidi kukusisitizia juu ya umuhimu wa kutumia mbinu zilizoweza kushinda wimbi la kwanza la Corona Tanzania zilizoasisiwa na viongozi wetu wa nchi hasa Rais wetu Dr. John Pombe Magufuli katika kupambana na kuyashinda matatizo mengine magumu likiwemo lile la mapambano ya kiuchumi kuboresha maisha yetu kifedha.
Ikiwa hukuweza kusoma makala hiyo au hukupata email
niliyotuma basi unaweza ukaipata hapa kwenye kiungo kifuatacho, JINSIYA KUTUMIA MAAJABU YALIYOPUNGUZA CORONA TANZANIA KUBUSTI UCHUMI WAKOUNAOSAMBARATIKA. Ikiwa wewe si mpenzi wa maoni, basi unaweza tu kuishia
hapa huna sababu ya kuendelea kusoma zaidi makala hii mpaka mwisho.
Sasa hebu tuendelee na mjadala wetu kama utapenda lakini,
kwani haya ni maoni yangu tu mimi binafsi kama Peter, nikiamini naandika kwa
nia njema kabisa kama mchango wangu kwenye mapambano ya janga hili
linaloisumbua Dunia nzima sasa hivi.
Sambamaba na mbinu ile iliyotumika katika wimbi lile la
kwanza la ugonjwa wa corona tokea mgojwa wa corona wa kwanza Tanzania
kugundulika, kila kiongozi kuanzia Rais wetu Dr. John Pombe Magufuli mpaka
Waziri wa Afya wakati huo Mama Ummy Mwalimu, wote walihimiza watu kutumia njia
zote za kisayansi na zisizokuwa za kisayansi katika kupambana na janga la
corona.
SOMA: Aina nne (4) za biashara zenye kinga ya majanga vikiwemo virusi vya corona (covid 19)
Tulishuhudia kauli hizo zikitekelezwa kwa vitendo kila
mahali kama vile, kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara, matumizi ya
vitakasa mikono(sanitizer), kudumisha
umbali wa mita moja mtu na mtu, kujifukiza na hata kutumia malimao, vitunguu
swaumu, tangawizi na ndimu kwa wingi ilimradi tu kila mtu alichukua tahadhari
zote zilizotakiwa.
Lakini chakusikitisha baada tu ya ugonjwa wa corona kudhibitiwa
kwa kiasi kikubwa, Watanzania wengi tulisahau na wengine kuachana kabisa na
tahadhari zile na ushahidi kila mtu anao mwenyewe, wengine hata tulitupa na
kuchoma barakoa, ndoo za maji tukafanya za kufulia nk. tukajidanganya kuwa
corona imetoweka Tanzania hivyo hatukuwa tena na haja ya kuchukua tahadhari
zilizowekwa na Serikali yetu pamoja na Shirika la Afya Duniani(WHO).
SOMA: Ebola: Tuachane na dawa za kizungu turudi kwenye asili, kikombe cha babu na muarobaini?
Karibu kila mmoja wetu ungemsikia akijisemea; “Mungu wetu ni Mkubwa ametuepusha na corona”
bila ya kukumbuka kuwa Dunia yote ni mali ya Mwenyezi Mungu na huwa habagui
watu wake kwa Taifa, Dini, wala Kabila mtu atokako, wote hupata magojwa au
kupona sawa kama vile ilivyo kwa mvua na jua, tena isitoshe yapo Mataifa
mengine athari za ugojwa huu ni kidogo kushinda nchi yetu.
Kumbuka tena kuwa wakati Tanzania tukisherehekea kuidhibiti
corona kwa kiasi kikubwa, jirani zetu hapo Kenya, Rwanda na Uganda walikuwa
bado wakilia na ongezeko la wagojwa kila uchwao wala hatukutilia maanani tena
kama kuna kina Mangi kibao waishio
Nairobi na Mombasa na pindi ifikapo Krismasi ni lazima “wakahiji” makwao Kilimanjaro.
Ni nani ajuae kama wimbi hili la pili limechangiwa na
safari za watu tokea huko mwishoni mwa mwaka 2020?. Kwa kauli za namna hii za
kumtupia Mwenyezi Mungu kila majukumu hata yale ambayo tayari amekwishatupa
nyenzo na uwezo tayari wa kushughulika nayo, kwakweli hatuwezi kuwa tofauti na
ndege Mbuni ambaye huficha kichwa chake mchangani wakati kiwiliwili na makalio
vyote vikiwa nje akifikiri anajikinga na hatari. Ni ukweli usipingika kwamba
janga hili hakuna binadamu anayeweza akalizuia isipokuwa Mungu mwenyewe kupitia
mbinu mbalimbali alizotujaalia.
SOMA: Mbinu na mikakati ya kuikwamua biashara yako kwenye hali ngumu kipesa
Tumeweza kuona hata huko Marekani baadhi ya wachambuzi
wanasema moja ya sababu kubwa zilizomfanya Rais Trump kushindwa Urais (ingawa pia kuna sababu nyinginezo) ilikuwa ni hasira za wananchi wale walioonja
machungu ya corona kwa namna moja ama nyingine wakajikuta wakielekeza hasira
zao hizo kwa utawala wa nchi bila ya kujua kwamba janga hili hata angelikuwa
rais Malaika asingeliweza kulishughulikia kama ilivyo kwa Malaria au Ukimwi. Rais Trump
pamoja na uzalendo wake wote wa kutaka kuifanya Marekani kuwa ‘Mkuu
tena’ akajikuta akilazimika kumwachia kiti Biden.
TUFANYEJE SASA?
Tumshukuru Mungu kwani Rais wetu na Serikali yake kwa ujumla wanaendelea kusisitiza matumizi ya mbinu iliyotuvusha lile wimbi la kwanza la janga la corona ingawa sasa hivi hatuna budi pia kuongezea na mbinu zingine ili kuleta ufanisi zaidi. Hata Malaria kuna kipindi chloroquine ilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana lakini ikafika kipindi ikaanza kupunguza ufanisi ndipo wataalamu wakaja na mbinu mbadala ya dawa mseto zikiwemo aina nyingine za dawa kama, SP, artmether nk.
Kwa maoni yangu mimi hapa, sioni haja ya kuanza kulumbana
wala kulaumiana. Kwenye vita mkishaanza tu kutupiana lawama adui ndio mnampa
nafasi ya kuwapiga vizuri zaidi. Cha msingi kila mmoja wetu tushirikiane kwa
kutumia mbinu na silaha zote tunazohisi zinaweza zikatusaidia ili janga hili
litoweke tena, haijalishi tunatumia mashine ya kujifukiza au chanjo,
lakini kila mbinu ikithibitika tu haina madhara mengine kiafya kama
alivyotahadharisha Rais wetu kwenye chanjo, basi mara moja na sisi tuagize hizo
chanjo kama ilivyo kwa wenzetu majirani waliotuzunguka.
Kimsingi Rais wetu hakusema chanjo haifai ila alitoa
maagizo kabla ya kuchanjwa watu wake ithibitike ni salama asilimia 100%.
Kwahiyo Wizara husika ingeongeza kasi ya kufanya tathnmini aliyoagiza Rais ili
tusije baadae kusema kwanini hatukujua mapema.
SOMA:
Taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini baada ya waumini
wake wengi kukumbwa na vifo isivyo kawaida vinavyohusishwa na changamoto ya
upumuaji tayari zimetoa mpaka takwimu za viongozi wao kufariki dunia kwa dalili
zinazofanana na zile za gonjwa la Uvico 19 ( Covid 19). Lakini bado watu
hatujaonyesha kwa dhati mwamko wa kujilinda tuliouonyesha katika lile wimbi la
kwanza la covid 19 mwaka 2020. Iko wapi tena ile amsha-amsha ya Mama yetu Ummy Mwalimu ambayo pengine ndiyo
iliyosaidia watu tukachukua tahadhari kwa kiasi kile tatizo likapungua?
Tofauti na viumbe wengine, Mwenyezi Mungu tayari ameshatupa
Wanadamu maarifa kwa makusudi ili tuweze
kuyatumia kukabiliana na mazingira yetu wenyewe, tukishindwa kufanya hivyo basi
Mungu hawezi kutusaidia kwa njia za kimiujiza ingawa pia anaweza kufanya hivyo
akipenda mwenyewe. Tuzidishe kumuomba lakini kamwe tusitegemee miujiza,
akipenda mwenyewe kutushushia miujiza basi ni vizuri wala hatuwezi kumhoji.
Kama Rais wetu John Pombe Magufuli alivyotuasa kuwa HOFU
ni hatari kuliko hata Corona yenyewe, hivyo badala ya kutiana hofu na woga huku
mitandaoni tujitahidi kuelezana ukweli kwa njia ambazo hazitatuzidishia HOFU, Hata
mtu anayejua atakufa muda mfupi ujao anapoambiwa ukweli wenye matumaini kamwe
hofu haina nafasi kwake.
…………………………………………………
Mpenzi msomaji wa
makala hizi, ikiwa wewe ni mpenzi wa makala na chambuzi za kina zinazohusiana
na Fedha, Ujasiriamali na Biashara nakukaribisha sana kwenye MASTERMIND-Group na Channel yetu ya MICHANGANUO-ONLINE, mahali ambapo
unaweza kupata kila siku masomo yasiyopatikana mahali kwingine kokote.
Kiingilio kwa mwaka
mzima ni sh. 10,000/= na unapata bure kitabu (Mashuhuri )toleo jipya la 2021
cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI. Unaunganishwa pia na Group la
Whatsapp kwa ajili ya masomo ya kila siku lakini pia Channel ya Telegram ambayo
unaweza kudownload bure masomo mengine yote ya fedha yaliyowahi kufundishwa katika
group hili siku za nyuma.
Katika group kila siku
pamoja na masomo ya fedha(exclusively)
pia tunafanya uchambuzi wa michanganuo ya Biashara zile zilizokuwa na uwezo
mkubwa wa kuzalisha faida haraka Tanzania. Michanganuo yetu ni halisi inayozingatia
kanuni zote za mlolongo wa biashara kuanzia muhtasari, Bishara, Bidhaa/Huduma,
Soko, Mikakati & Utekelezaji, Uongozi, Fedha, mpaka Viambatanisho muhimu. Kitabu
kina michanganuo 10 ya biashara za Kitanzania zenye fursa kubwa ya kutengeneza
faida.
Kujiunga, Lipia
kiingilio sh. 10,000/= kupitia namba zetu, 0765553030 au 0712202244 jina Peter
Augustino Tarimo kisha ujumbe usemao, “NIUNGE NA MASTERMIND GROUP LA
MICHANGANUO-ONLINE NA CHANNEL YA MASOMO” Utaunganishwa muda huohuo pamoja na
kutumiwa OFFA yako kisha masomo ya kipekee jioni saa 3 mpaka saa 4 usiku.
Nafasi katika group
zimebaki chache hivyo ni vizuri ukawahi mapema isijekuwa kama mwaka jana
nilipata lawama nyingi sana baada ya nafasi kujaa. Sisi huwa hatuendeshi magroup
zaidi ya moja la whatsapp kutokana na kujali zaidi ubora wa kile
tunachofundisha katika kutekeleza moja ya kaulimbiu yetu ya mwaka huu isemayo; “KUMJALI MTEJA KWA
KIWANGO CHA HALI YA JUU KABISA”
Asante sana,
na chukua tahadhari ya corona bila kuruhusu HOFU wala WOGA;
Ni mimi
Peter A.
Tarimo
Mwandishi
na Mhamasishaji wako.
0 Response to "TULIKOSEA WAPI TANZANIA CORONA IKARUDI TENA KWA KASI HII?"
Post a Comment