MUDA SAHIHI WA KUFANYA BIASHARA NI SASA, BADO TENA UNASUBIRI AWAMU YA 7? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MUDA SAHIHI WA KUFANYA BIASHARA NI SASA, BADO TENA UNASUBIRI AWAMU YA 7?

Mazingira ya kibiashara awamu ya 6 ya mama Samia Suluhu

Kwenye kila awamu ya Utawala wa nchi kuna mazingira tofauti ya kibiashara. Mazingira ya kibiashara….. (kama nilivyowahi kuzungumzia katika makala zangu hizi zilizopita, ile ya….. 

MAZINGIRAYA BIASHARA KUELEKEA MIAKA 5 IJAYO YA UTAWALA WA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI, JEUMEJIPANGA VIPI?

Na nyingine…..

NUFUVI(SWOTANALYSIS), TATHMINI MUHIMU KABLA HUJAANZA KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YAKO;)

…..ni jumla ya nguvu mbalimbali ambazo hubadilikabadilika, zinaweza kutoka ndani ya biashara yenyewe au kutokea nje ya biashara na pia huwa zinaiathiri biashara katika mlengo hasi au chanya. Kwa mantiki hiyo mazingira fulani ya kibiashara yanaweza yakaifanya biashara ikashamiri au mazingi mengine yanaweza yakaifanya biashara ikadumaa na hata wakati mwingine kufa kabisa.

*Angalizo! Si lengo la makala hii kuanza kulinganisha mazingira ya kibiashara kwa awamu mbalimbali za utawala wa nchi hii bali lengo kubwa hapa ni kumpatia mjasiriamali mtazamo sahihi wa ni nini cha kufanya katika mazingira yeyote yale ya kibiashara, yawe ni mazingira hasi au mazingira chanya kwake.

Mazingira ya biashara yaliyokuwepo enzi za utawala wa Hayati John Pombe Magufuli ni tofauti na yale yaliyopo kwenye Utawala huu wa Mama Samia Hassan Suluhu ijapokuwa dhamira na Malengo ya awamu zote mbili ni moja ya kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaboreshwa zaidi.

Lakini tukumbuke katika kila awamu inazo mbinu, mikakati na staili yake tofauti ya utekelezaji ambayo sasa ndiyo huja kuathiri biashara na sekta nyinginezo mbalimbali kwenye jamii na hivyo kuwa chanzo cha kubadilika kwa mazingira ya kibiashara.

UNACHOPASWA MJASIRIAMALI KUKIZINGATIA

Kwa Mjasiriamali haijalishi ni awamu ipi ya serikali iliyokuwepo madarakani wala ni mazingira ya aina gani yaliyokuwepo, hasi au chanya, kutokea nje ya biashara au ndani ya biashara, mjasiriamali wa kweli unatakiwa kuhakikisha unajirekebisha ili kuendana na mazingira yale yaliyokuwepo, kama ni hasi basi ujitahidi kwa kila hali kuyafanya yakupendelee badala ya kukuangamiza.

Nadhani unamfahamu mnyama kinyonga na nyoka, kuwa kama kinyonga anapobadili rangi yake ili aweze kuendana na mazingira aliyopo, halikadhalika kuwa kama nyoka kujivua gamba lake la zamani kusudi tu aweze kuendana na mazingira mapya aliyopo yamnufaishe badala ya kumpa hasara. Nadhani hapa umenielewa mjasiriamali wangu.

Nitatoa mifano michache hapa, Kipindi cha mpendwa wetu Hayati JPM ijapokuwa wapo watu waliokuwa wakilalamika mazingira kutokuwapendelea lakini bado kuna watu mazingira kwao yalionekana kuwa mazuri, hivi unafikiri wasanii kama kina Diamond Platnumz na Harmonize(Konde Boy) kipindi hiki mazingira kwao yalikuwa mabaya? kama hapana sababu ilikuwa ni nini?

Sidhani kama kuna awamu yeyote ile ya utawala tangu ile ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuna hata moja ambayo hakukuwa na malalamiko katika sekta hii ya biashara, wala hamna hata moja ambayo kulikosekana wajasiriamali walioneemeka na kutoboa katika mazingira yaliyokuwepo.

Hivyo nihitimishe tu kwa kusema kwamba Mjasiriamali haupaswi hata kidogo mazingira ya kisiasa na kiutawala yaathiri biashara zako katika mlengo hasi, wewe daima unatazama faida na hivyo siasa waachie wanasiasa wenyewe, wewe piga kazi kwani Wananchi wameshaamua wenyewe kuiweka serikali yao madarakani.

Serikali iwe mbaya au iwe nzuri hutaweza kubadilisha kitu hapo, cha msingi ni wewe kukubaliana na mazingira yaliyopo na kuangalia ni jinsi gani mazingira hayo yanaweza kukunufaisha na siyo kukudhoofisha.

Kuna wajasiriamali hata katika vipindi vigumu mno kama kile cha mdororo mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani miaka ya 1930 walitoboa mfano kina Henry Ford na wengineo, hawa walichokifanya ni kutumia fursa mbalimbali kubwa zilizoletwa na mdororo ule kutengeneza faida ya kushangaza katika biashara zao.

Pamoja na Mama yetu Samia Hassan Suluhu kujitahidi kurekebisha mazingira mbalimbali ya kibiashara yawe bora zaidi lakini Wajasiriamali tusipochukua hatua ya ‘kuadapt’ mazingira hayo yatunufaishe badala ya kutudhoofisha, tutaendelea tu kulialia tukitamani awamu ya sita imalizike haraka ili ije awamu ya 7 tukidhania labda inaweza kutupendelea kumbe tunajidanganya tu.

..............................................................

1. Kupata vitabu na michanganuo ya biashara tembelea duka letu mtandaoni hapa, SMART BOOKS TZ

2. Kujiunga na MASTERMIND GROUP letu na channel kwa ajili ya masomo ya fedha na semina za uandishi wa michanganuo ya biashara lipia ada sh. elfu 10 kupitia namba zetu 0765553030 au 0712202244 kisha tuma ujumbe wa "NIUNGANISHE NA MASTERMIND GROUP LA MICHANGANUO-ONLINE" Utaunganishwa muda huohuo na kutumiwa bure Kitabu na michanganuo.

3. Kupata kitabu cha Think and Grow Rich katika lugha ya Kiswahili, fuatilia blogu yako hii punde tutaweka taarifa za bei na jinsi ya kukipata.

0 Response to "MUDA SAHIHI WA KUFANYA BIASHARA NI SASA, BADO TENA UNASUBIRI AWAMU YA 7?"

Post a Comment