Somo letu hili la leo linahusu USIMAMIZI MZURI WA FEDHA. Bila ya kujali kama ni fedha za mtu
binafsi katika mfuko wake mwenyewe au ni fedha za biashara, maana hasa ya dhana
hii ya elimu ya usimamizi mzuri wa fedha ni hii hapa chini;
Usimamizi
mzuri wa fedha ni kitendo au mchakato wa uendeshaji shughuli binafsi au zile za
kibiashara kwa kuzingatia bajeti, uwekaji malengo, uwekaji wa kumbukumbu za
mapato na matumizi, uwekaji akiba pamoja na uwekezaji katika miradi inayoleta
faida siku za baadae.
Lengo kuu la matumizi bora ya fedha ni kuhakikisha pesa
ambayo ni rasilimali muhimu sana duniani inaelekezwa kwanza kufanya mambo yale
yaliyokuwa muhimu zaidi katika maisha au biashara zetu badala ya kuzitapanya
katika mambo ya hovyo yanayosababisha hatimaye mtu au biashara kuishiwa fedha na
kuhangaika huku na kule (kufilisika)
SOMA: Pesa tuonazo ni makaratasi tu, jifunze njia ya kupata pesa za ukweli
Hivyo katika somo hili tutakuwa na sehemu kuu mbili; ya
kwanza ni usimamizi mzuri wa fedha binafsi mifukoni mwa mtu mmoja mmoja na ya
pili ni usimamizi mzuri wa fedha za biashara. Watu wengi wanajua kwamba kuna muongozo
katika usimamizi wa fedha lakini kitu wasichokijua sana ni ikiwa kuna aina
mbili za usimamizi na matumizi bora ya fedha.
Ijapokuwa aina hizi mbili za elimu ya matumizi ya fedha zinafanana sana katika vipengele vingi kama tutatakavyoenda kuona lakini ipo tofauti kubwa pia na tutakwenda kuiona huko mbele katika makala hii ya jinsi ya kusimamia vizuri pesa zako na zile za biashara. Mtu huhitaji kuwa mhitimu wa chuo cha usimamizi wa fedha ili uweze kusimamia vizuri fedha zako mwenyewe au za biashara yako.
Kitu cha msingi kuliko vyote ni kujifunza tu namna ya
kutengeneza fedha na njia bora za kuzidhibiti zisitumike vibaya basi, ndio
maana utakuta hata wazee wetu zamani ambao hawakusoma hata darasa moja wengine
walikuwa matajiri vilevile, wewe unadhani walitumia mbinu zipi kutajirika? Leo
tunaenda kuzijua mbinu hizo moja baada ya nyingine, so stay tuned.
SOMA: Biashara saba 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala
Kabla hatujaanza ni muhimu sana kuifahamu vizuri dhana
maarufu kwamba, biashara na mmiliki wake ni nafsi mbili tofauti zinazojitegemea
na hivyo pia fedha kutoka kwa nafsi hizo mbili ni vitu viwili tofauti na mahali
pekee vitu hivi 2 vinapohusiana au kukutana ni kwenye faida na mtaji ambapo
mmiliki ndipo hupata gawio lake kama malipo kwa mchango wake katika hiyo
biashara au kutoa mtaji kama uwekezaji kwa biashara husika.
SEHEMU
YA KWANZA (1) : Jifunze Usimamizi wa fedha binafsi
Umuhimu wa kujifunza usimamiaji mzuri wa fedha binafsi za
mtu mwenyewe mfukoni mwake unatokana na sababu kwamba vipato vya watu
mbalimbali havitokani na biashara tu peke yake bali pia hutoka vyanzo vingine
mbalimbali mfano, ajira, ruzuku, sadaka, zawadi, mikopo nk. Kwa hiyo ni muhimu
pia watu wawe na uwezo wa kusimamia vyema matumizi ya fedha zao binafsi
mifukoni kusudi ziweze kuwafanyia mambo makubwa zaidi na ya maana maishani.
SOMA: Njia 6 za kuondoa woga na stress za fedha katika maisha yako
Mambo
muhimu ya kuzingatia kwenye usimamizi wa fedha za mtu binafsi
Mtu binafsi haijalishi unafanya biashara, umeajiriwa au
unapata fedha zako kwa njia gani nyingine, ni lazima na ni muhimu kujifunza
elimu ya usimamizi na matumizi mazuri ya fedha unazozipata ili ziweze
kukusaidia kutimiza malengo mbalimbali muhimu unayojiwekea katika maisha yako.
Hapa tofauti na biashara, chanzo cha fedha zako chaweza
kuwa ni gawio la faida kwenye biashara, ajira, kibarua, ‘pocket money’, mkopo,
ruzuku, sadaka, uuzaji wa mali binafsi, au njia nyingine yeyote ile
inayokuingizia fedha.
SOMA: Jinsi ya kukwepa mitego inayokuvutia kwenye matumizi mabaya ya fedha zako
Hata ikiwa labda umepata pesa zako kutokana na kucheza
bahati na sibu au michezo mingine ya kubeti nk. ni lazima utafute njia bora
kabisa ya kuzitumia fedha hizo vinginevyo zitaisha muda mfupi na kwa haraka
sana bila ya kuona manufaa yeyote yale ukabaki na stori tu (simulizi) kuwa
uliwahi kushika mabilioni ya pesa zikayeyuka.
1.
Weka malengo na mipango ya kifedha
Weka malengo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Malengo
yako kifedha huanzia pale unapofikiria akilini ni kitu gani hasa unachotaka
kukifanya, una malengo gani? Je unataka kujenga nyumba, kununua kiwanja?
Unataka kusoma chuo? Unataka kununua bajaji/pikipiki? Unataka kununua gari?
Unataka kufungua biashara mpya? Unataka kusafiri? Una mpango wa kununua TV,
redio na vyombo vya ndani?. Ili uweze kufanikisha jambo lolote lile zuri
maishani unapaswa uwe na wazo dhahiri la ni wapi unakotaka kufika na kisha
uweke mpango wa kufika hapo
SOMA: Kufanikiwa malengo yako, focus kwenye mfumo(utekelezaji) na siyo kwenye matokeo ya mwisho
2.
Tengeneza Bajeti.
Baada ya kuweka malengo, kinachofuata ni kutengeneza
mpango au bajeti. Bajeti ni sehemu muhimu sana katika mpango wowote ule wa
kifedha na ndiyo itakayokusaidia kuyafikia malengo uliyojiwekea pasipo
kuhangaishwa na vidakizi vingine mbalimbali. Bajeti kwa kifupi kabisa maana
yake ni kukisia mapato na matumizi yako katika kipindi fulani tuseme labda
siku, mwezi au hata mwaka na kisha kufanya ufuatiliaji kulingana na hali halisi
itakavyojitokeza.
*(Ikiwa upo katika
darasa langu la MICHANGANUO-ONLINE -MASTERMIND-GROUP-2022, nadhani somo la
bajeti utalifurahia sana kwani ndiyo sehemu muhimu mno kwenye maandalizi ya
michanganuo ya biashara/business plans)*
3.
Punguza matumizi na zidisha mapato
Baada ya bajeti ni wakati sasa wa kuhakikisha unachunga
vilivyo matumizi yako yasizidi kile unachokipata ikiwa ni pamoja na kutafuta
njia zaidi mbadala za kujiingizia kipato mfano kuanzisha biashara ya pembeni,
kufanya kazi muda wa ziada au biashara za mtandaoni zisizohitaji muda mwingi.
Huu ndio wakati wa kubana matumizi na kuondoa kabisa kila aina ya matumizi
yasiyokuwa na umuhimu kwako. Jifunze kila wakati jinsi ya kuwa na pesa nyingi
zaidi ya zile ulizokuwa nazo
SOMA: Njia 7 unazotumia kubana matumizi lakini kumbe zinakuzidishia umasikini.
4.
Weka Akiba, tumia kanuni ya 80/20
Katika kipato chako unachokipata, weka pembeni kama akiba
asilimia 20% ya fedha hizo na utumie asilimia nyingine 80% inayobakia kwa ajili
ya matumizi yako ya kawaida. Pesa hizi asilimia 20% ni kwa ajili ya dharura
ikiwa lolote litaweza kutokea katika maisha yako ambalo hukulitegemea mfano
majanga kama ugonjwa na mengineyo, na hutakiwi kuzigusa kabisa kwa jambo
jingine lolote lile. Kanuni ya 80/20 ni muongozo tu na siyo msahafu/sheria
kwamba ni lazima iwe asilimia hizo, lakini kiasi hicho cha akiba ya dharura
angalau kisiwe kidogo.
Asilimia hii 20% wataalamu hupendekeza angalao mtu
uhakikishe inafikia kiwango cha matumizi yako ya miezi 3 mpaka 6. Hii
inamaanisha kwamba mtu unapaswa uwe na akiba ya fedha zitakazokutosha kutumia
kwa muda wa miezi 3 – 6 ukiwa huingizi kipato chochote. Tuchukulie kwa mfano
labda umefukuzwa kazi au umeumwa na kipato chako kukoma, basi akiba yako hiyo
itoshe kukuhudumia kwa miezi 3 – 6 badala ya kwenda kuingia madeni hatari ya
riba yatakayozidi kukudidimiza kwenye bahari ya umasikini
5. Jifunze
jinsi ya kusave pesa, Fungua akaunti benki.
Ile asilimia 20% ya mapato yako iweke katika akaunti ya
dharura ambayo ni tofauti na akaunti zako nyingine za kawaida za akiba ambapo
ukishaiweka, umeweka na hutaweza kuitoa kiurahisi tena labda tu itokee dharura.
SOMA: Sababu kubwa 9 duniani kwanini watu hukopa pesa, nne kati yake ni za kuogopa kama ukoma
Ikiwa una malengo mengine ya muda mfupi kwa mfano malengo
ya kununua vitu kama samani za ndani, kiwanja, gari nk., unatakiwa katika
mapato yako kutenga asilimia nyingine ya fedha kwa ajili ya malengo hayo mbali
na ile asilimia 20%. Kiasi hicho kulingana na malengo yako kinaweza kuwa kiasi
chochote kile cha fedha mfano asilimia 5%, 10%, 20% nk. na unaweza kufungua
akaunti nyingine ya akiba kwa ajili yake mpaka umehakikisha zimetosha kutimiza
kile ulichokusudia kukifanya.
6.
Wekeza fedha zako kwa malengo ya muda mrefu.
Wakati uwekaji akiba katika akaunti maalumu ya dharura na
ile ya kawaida ya akiba ni kwa ajili ya malengo yako ya muda mfupi, kwa upande
wa malengo yako ya muda mrefu itakubidi sasa uanze kufanya uwekezaji wa fedha
zako kwa njia mbalimbali kama nitakavyoeleza hivi punde.
Hivi unafikiria kama umeweka akiba yako ya dharura fedha
za kutosha miezi 3 – 6 na muda ukapita lakini hakuna majanga yeyote
yaliyokutokea unadhani fedha hizi utazifanyia kitu gani zaidi? Bila shaka
utaamua kutafuta njia nyingine mbadala zaidi ya kuziweka fedha zako hizo huku
zikiendelea kuzaa faida kubwa badala ya kukaa tu kama akiba benki.
Halikadhalika kutokana na mikakati yako mizuri ya bajeti uliyojiwekea ikiwemo ubanaji wa
matumizi na njia mbadala mbalimbali za kuongeza mapato yako, mzunguko wa fedha
zako utakuwa chanya kiasi cha kusababisha ongezeko kubwa la fedha za ziada
ambazo ni lazima sasa uziwekeze katika miradi mbalimbali ya muda mrefu
kutegemeana na ni shughuli gani za kukuingizia kipato unazozifanya kwa ajili ya
kuja kukutiririshia fedha nyingi zaidi wakati kipato chako cha kawaida
kitakapokoma na kukufanya uishi maisha yasiyo na stress.
SOMA: Stress za pesa zinavyoweza kuzima kabisa ndoto za mtu na hatua za kuchukua haraka.
Kwa mfano ikiwa wewe ni mwajiriwa katika sekta binafsi au
mfanyakazi serikalini unaweza kuwekeza fedha zako kwenye mifuko ya uwekezaji ya
pamoja(UTT), masoko ya hisa, Ununuzi wa dhamana za serikali(hati fungani),
Kufungua akaunti ya akiba benki, Kuanzisha biashara yeyote, uwekezaji kwenye
ardhi na majengo nk.
Ikiwa wewe unaingiza kipato chako kupitia shughuli za
biashara unaweza pia kutumia kipato chako hicho cha ziada kuwekeza zaidi kwenye
biashara unazozifanya au kuwekeza katika miradi mbalimbali kama tulivyoona kwa
waajiriwa hapo juu. Ni kwa njia ya uwekezaji pekee ndio utakaokuwezesha wewe
kupata uhuru kamili wa kifedha katika maisha yako na si vinginevyo.
7.
Ukikopa tumia busara.
Uwezo wako wa kuaminika na kukopesheka utategemea sana
historia yako ya ukopaji na ulipaji madeni siku za nyuma. Huathiri pia moja kwa
moja fursa yako ya kuja kupata mkopo kwa ajili ya biashara zako siku za baadae.
Hivyo unapokopa mahali popote pale hata iwe ni kwa mtu binafsi licha ya benki
au taasisi nyingine za fedha, hakikisha unalipa kwa wakati na kwa uaminifu
mkubwa.
8. Weka
mapema lengo la kumiliki ardhi na makazi.
Moja ya ndoto muhimu zaidi ya binadamu yeyote katika
maisha yake ni kuwa na kwake kwa maana ya kumiliki kiwanja na hatimaye kujenga
nyumba yake mwenyewe ya kuishi na familia yake. Rasilimali hii ni muhimu mno siyo
tu kwa ajili ya kuishi bali pia itaweza kuwa kama dhamana pale utakapohitaji
kukopa mkopo kwa ajili ya kuongezea mtaji wa biashara zako au mkopo kwa ajli ya
malengo mengine yeyote yale ya kimaisha.
9. Usijinyime
kupita kiasi, jipongeze kidogo!
Kosa moja kubwa watu wengi wanalofanya pindi
wanapotekeleza bajeti walizojiwekea ni kujinyima kupindukia, kumbuka binadamu
sisi utashi wetu una ukomo, tunaweza tu kuhimili kiasi fulani cha majaribu
kabla hatujakata tamaa.
SOMA: Saikolojia ya umasikini: Sababu 9 kwanini hupati pesa za kutosha
Tafiti zimethibitisha kwamba ikiwa mtu atajinyima
mfululizo kitu akipendacho mwishowe atashindwa kabisa kuhimili na kujikuta
anafanya kosa la kurudi nyuma kulekule alikotokea mwanzoni. Dawa ya tatizo hili
ni kujipa zawadi au kujipongeza kidogo pale unapofanikiwa kupiga hatua fulani
katika malengo yako mfano hata kujipongeza kwa kinywaji murua, safari/picnic au
mlo mzuri baada ya kufikia lengo fulani dogo miongoni mwa malengo yako makubwa.
10.
Katu usiache kujifunza elimu ya fedha kila siku
Ulimwengu wa pesa ni tata na hubadilika kila siku lakini
kitu cha kustaajabisha ni kuwa pesa ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila
binadamu na kama nilivyotangulia kusema pale mwanzoni ya kwamba, mtu hauhitaji
kuwa na shahada, stashahada au astashahada kutoka katika chuo cha elimu ya
usimamizi wa fedha ndipo uweze kujua jinsi ya kutengeneza pesa, kuzitunza na
kuzisimamia ziwe nyingi mpaka kukufikisha kwenye uhuru kamili wa kifedha.
Lakini unahitaji kujifunza angalao elimu ya msingi ya fedha kupitia majukwaa
mbalimbali mitandaoni na nje ya mtandao. Mfano mzuri kabisa ni jukwaa letu la
MICHANGANUO-ONLINE SUPER-MASTERMIND GROUP-2022
……………………………………….
Mpaka kufikia hapo, mpenzi msomaji wa somo hili la
JINSI YA KUSIMAMIA, KUTUNZA NA KUTUMIA VIZURI PESA ZAKO BINAFSI & ZILE ZA
BIASHARA YAKO ndio tumemaliza sehemu ya kwanza iliyohusu Usimamizi mzuri wa
fedha binafsi. Kesho tutaendelea na sehemu ya pili na tutaangazia zaidi juu ya utunzaji na usimamizi mzuri wa fedha za biashara. Usikose kujua kuna tofauti gani kati ya
usimamizi wa fedha kwenye ‘nafsi’
hizi mbili yaani, BIASHARA NA MMILIKI
WAKE.
Masomo haya pia yanaendelea katika MASTERMIND GROUP MICHANGANUO-ONLINE-2022. mahali pekee panapopatikana masomo ya fedha yasiyopatikana mahali kwingine kokote.
……………………..
Pia Vitabu vyetu vyote hapo chini vinapatikana na ukiwa popote pale nchini Tanzania au nje tunakufikishia ulipo kwa uaminifu mkubwa.
Mawasiliano yetu: 0765553030 au 0712202244
0 Response to "BAJETI: JINSI YA KUSIMAMIA, KUTUNZA NA KUTUMIA VIZURI FEDHA BINAFSI NA ZA BIASHARA YAKO (KANUNI 80/20)"
Post a Comment