Ili
uweze kuandika vizuri mchanganuo wa biashara ya ufugaji wa kuku wa nyama kwa
ajili ya kuombea mkopo benki ama taasisi yeyote nyingine ile ya fedha, huna
budi kufanya utafiti wa kina kuhusiana na biashara nzima ya broilers.
Kufahamu
muongozo kamili wa jinsi ya kufuga kuku wa nyama nayo ni sehemu ya utafiti huo
kwani kutakuwezesha kujua vipimo mbalimbali, bei na hata gharama utakazohitaji
kwa ajili ya kutekeleza mradi wako kwa mafanikio makubwa na hivyo kurahisisha
kazi ya kuandika mpango wenyewe.
Kabla
hatujakwenda kuandika mchanganuo wetu wa kuku wa nyama hebu kwanza tuone
muongozo wenyewe upoje;
BANDA
/ MALAZI YA KUKU
Katika ufugaji wa kuku aina
zote iwe ni kuku wa nyama, kuku wa mayai, kuku chotara au kuku wa kienyeji,
banda/nyumba kwa ajili ya kuwahifadhi kuku ndiyo kitu muhimu zaidi
kitakachoamua ufugaji wako ufanikiwe ama usifanikiwe. Kuku wanahitaji nyumba au
banda bora kwa ajili ya kuwakinga na hali yeyote ile inayoweza kuwafanya
washindwe kukua vizuri au kudhurika kwa namna yeyote ile.
Inaweza kuwa ni hali ya hewa ya joto, baridi, upepo,
mvua, jua kali, unyevunyevu nk. Pia banda husaidia kuwakinga kuku na hatari
mbalimbali mfano wezi, wadudu na wanyama wabaya kama nyoka, mapaka, vicheche,
kunguru na mbwa. Banda la kuku linatakiwa liwe na uwezo wa kudumisha hali ya
hewa inayohitajika pasipo kutegemea hali ya hewa ya nje ya banda.
Kuna mifumo mikuu mitatu ya ufugaji wa kuku na hii ndiyo inayoamua banda lako la kuku liwe
la namna gani;
1. Mfumo huria
ambao kuku wanajitafutia chakula wenyewe hasa kuku wa kienyeji na huhitaji
banda kwa ajili ya kulala usiki tu
2. Mfumo wa Nusu huria –
huu kuku wanafungiwa ndani lakini wanajengewa uzio eneo wanaloweza kuzunguka na
kula
3. Mfumo wa ndani:-
Kuku hasa wa kisasa kama broiler na layers hufungiwa ndani moja kwa moja na
sakafu hufunikwa kwa matandiko/matandazio au katika cages
Vipimo
vya banda kwa ajili ya kuku 2000 wa nyama (broiler)
Kitaalamu kuku mmoja wa nyama katika mfumo wa kufugia
ndani anahitaji nafasi ya futi moja ya mraba ambayo ni karibu sawa na upana wa
rula moja ya sentimita 30 x urefu wa sentimita 30. Kwa vipimo hivyo maana yake
ni kwamba mita moja ya mraba(mita 1 x mita 1) inakadiriwa kutosha kuku wa nyama
10. Wengine huweka mpaka kuku wa nyama 12 katika eneo la mita moja ya mraba.
Hivyo utaona kwa idadi yetu ya kuku 2000 tutahitaji banda lenye ukubwa wa mita
za mraba 200 sawa na upana mita 20 x urefu mita 10. Urefu kwenda juu ni futi
saba sawa na mita 2
Unapoanzisha ufugaji wa kuku una machaguo mawili, la
kwanza uamue kujenga banda mwenyewe au ukodishe
mabanda yaliyokwisha jengwa tayari.
Banda
la kuku wa nyama linatakiwa liwe vipi?
·
Madirisha ya kutosha kuingiza hewa pamoja na mapazia
kwa ajili ya kuzuia upepo na baridi nyakati za usiku au hali mbaya ya hewa.
·
Lijengwe urefu wa banda uanzie Mashariki
kwenda Magharibi kwa ajili ya kuwakinga kuku na jua kali
·
Banda liwe imara
·
Sakafu ya banda la kuku iwe tambarare na
inaweza kuwa ya saruji, udongo au mbao
Sehemu
ya kulelea vifaranga (Brooder) / Kiota
Kuku wa nyama wa siku moja mpaka waote manyoya wanatakiwa
wakae katika mazingira ya joto lisilobadilika badilika na pia sehemu isiyokuwa
na upepo mkali kwani wanaweza kufa. Wanahitaji kiota ambacho ni mduara
unaotengenezwa kwa kutumia karatasi gumu, boksi au material yeyote ya mbao
pamoja na wavu wenye matundu madogomadogo. Mduara unasaidia vifaranga
wasibanane kwenye kona wala wasiende mbali na chanzo cha joto, unaweza
kuuongeza kadiri wanavyokua
Kiota kinaweza kuondolewa baada ya wiki moja mpaka mbili pale
kuku wanapokuwa wameshaota manyoya na kujitegemea kwa joto la kawaida.
Ikiwa banda ni dogo na hali ya hewa siyo mbaya unaweza tu
kuweka vyanzo vya joto vya kutosha bandani na vifaranga wakaendelea kulelewa
humo bila ya kuweka viota tangu siku ya kwanza mpaka siku ya mwisho kuku
wanauzwa au kuchinjwa.
Kiota
kwa ajili ya kulelea kuku wa nyama kiweje?
Chanzo
cha joto: chanzo cha joto hakina mjadala kwa vifaranga wa kuku wa
nyama kwani ndiyo mbadala wa mama yao ikiwa wangelikuzwa kwa njia ya asili ya
kuatamia mayai. Chanzo cha joto kinaweza kikawa ni balbu maalumu ya umeme iliyo
na watts 100 au 250, Jiko la mkaa au Taa ya chemli.
Kama unatumia balbu ya umeme itundikwe juu kwa waya sentimita 35 kutoka sakafu ya banda na
inaweza ikapandishwa juu au kushushwa chini kutegemeana na hali ya joto ilivyo.
Balbu ikingwe isiguse vifaranga au vitu vinavyoweza kushika moto kwa urahisi kama
matandazo.
Ikiwa utatumia jiko la mkaa au taa ya chemli basi iwekwe
juu ya tofali futi moja juu vifaranga wasifikie na hakikisha mkaa hautoi moshi
au taa haivujishi mafuta. Chanzo cha joto kiwashwe saa 1 mpaka 3 kabla
vifaranga havijaletwa.
Joto ndani ya kiota siku ya kwanza linatakiwa kuwa nyuzi
35 za sentigred ( nyuzi 95 F) na linatakiwa kupunguzwa nyuzi 2 za sentigredi(nyuzi
5 F) kila baada ya wiki moja. Tumia kipima joto na ikiwa hauna basi tazama
tabia na mwenendo wa vifaranga kwenye kiota. Wakikusanyika sehemu moja karibu
na chanzo cha joto ni dalili joto ni
kidogo hivyo ongeza nguvu ya joto kama ni taa ishushe chini kidogo nk.
Joto likiwa kali watakaa mbali na chanzo cha joto huku
wakitanua mabawa yao na kuhema harakaharaka. Punguza joto kwa kupandisha taa
juu pamoja na kuwapa maji mengi ya kunywa.
Sakafu/Matandazo: Kwa
siku ya 1 – 2 magazeti, gunia au mifuko laini hutandikwa juu ya matandazo,
isizidi siku 2 kwani miguu ya kuku wa nyama hutanuka na wanaweza kupata ulemavu hatimaye
kutembea kwa shida.
Matandazo
yanatakiwa kuwa na kina cha inchi 3 – 4 kwa ajili ya kunyonya
unyevunyevu wa mbolea na kuongeza joto kwa vifaranga lakini yasiwe na chembechembe
ndogo sana au vumbi jembamba kwani vifaranga wanaweza wakafikiria ni chakula na
kuanza kula makapi.
Kiota kimoja kinaweza kuwa na kuku kuanzia 100 mpaka 250
kulingana na ukubwa au aina ya chanzo cha joto, vifaranga wanatakiwa wawekewe
vyombo vya maji na chakula watakavyoweza kutumia kwa urahis mfano kwa chakula
unaweza ukatumia mifuniko ya maboksi, matrei ya mayai au trei ndogondogo za
aluminium/plastiki mpaka watakapoweza kulia kwenye vilishio vya
kawaida(feeders). Vifaranga 25 watumie chombo kimoja cha chakula na maji idadi
hiyohiyo.
MAANDALIZI
YA KUPOKEA VIFARANGA
Siku kadhaa kabla ya kuwasili kwa vifaranga wako wa kuku
wa nyama fanya usafi unaohitajika kwenye banda zima na mazingira yote
yanayozunguka eneo la ufugaji. Tumia dawa ya kuulia vimelea wa magojwa kama
Dettol kupulizia maeneo hayo pamoja na kusafisha banda na vyombo vyote vya
kulia chakula na maji.
Siku moja kabla ya kuwasili kwa vifaranga andaa vyema
sehemu ya kulelea vifaranga/kiota (brooder). Tandaza matandazo na juu yake weka
magazeti au gunia kwa ajili ili vifaranga waweze kujizoesha kutembea na kula
juu yake kwa siku mbili au tatu kabla hawajaachwa watembee juu ya matandazo
matupu.
Matandazo yasiwe ni chembechembe ndogo sana wala vumbi
kwani yanaweza kuwasababishia vifaranga matatizo ya kupumua. Matandazo mazuri
ni randa za mbao zenye ukubwa wa kati, nyasi laini na makapi ya mazao kama
mpunga nk.
Washa kabisa chombo chako cha joto kiota kianze kupata
joto. Andaa pia vyombo vya kulia chakula, vinyweo vya maji, vitamini na
glucose.
VIFARANGA
WANAPOWASILI
Vifaranga wanatakiwa waletwe kwa kutumia maboksi maalumu
kutoka kwa mtotoleshaji anayeaminika na usiwaweke kwenye gari la kufunika au
buti la gari wasijekukosa hewa wakafa. Mara tu wanapowasili hivi wapelekwe moja
kwa moja katika sehemu maalumu ya kulelea(Brooder) na vifaranga wapewe maji
safi. Ikiwa wataonekana ni wachovu basi maji yachanganywe na glucose na vitamin
kuwaongezea nguvu kisha baada ya masaa 4 – 5 ndipo waweze kupewa chakula.
JINSI
YA KUWATUNZA VIFARANGA WA KUKU WA NYAMA BAADA YA KUWASILI
CHAKULA:
Kwa siku ya 1 –5 huwa hawali wala kunywa maji mengi sana
kwa sababu bado wanakuwa wakitumia virutubisho walivyofyonza kutoka katika ute
wa yai wakati wa kuanguliwa.
Zipo aina tatu za vyakula nya kulisha kuku wa nyama kulingana na kiasi cha virutubisho
vilivyokuwepo ndani yake hasa kiasi cha protini navyo ni;
1. Chakula
cha kuanzia – Starter
2. Chakula
cha kukuzia – Grower
3. Chakula
cha kumalizia – Finisher
Vilevile Katika ufugaji wa kuku wa nyama unaweza ukatumia
njia mbili za ulishaji wa chakula ambazo ni;
1.
Kuanza
na Starter – Grower – Finisher
Katika njia hii wiki mbili za mwanzo
unawalisha Starter, Wiki ya tatu Grower na wiki ya nne na kuendelea unawalisha
Finisher
2.
Kuanza
na Starter – Finisher
Katika njia hii, wiki mbili za mwanzo
unawalisha Starter kisha wiki ya tatu mpaka siku ya mwisho
utakapowauza/kuwachinja unawalisha Finisher
Kuku wakiwa kwenye kiota siku ya kwanza mpaka ya tano
wapewe chakula muda wote bila ya kupimiwa, baada ya hapo unaweza kuwapa chakula
kwa ratiba maalumu mfano kuwawekea chakula kwenye vilishio kwa muda wa masaa 18
na kuondoa chakula kwa masaa 6 au masaa 16 kwa masaa 8 nk.
Wakati wa kubadilisha aina ya chakula usibadilishe ghafla
bali anza kuchanganya kila aina nusu kwa nusu au robo kwa robo tatu siku mbili
mpaka tano kabla hujabadilisha moja kwa moja.
Hakikisha chakula ni kile tu kilichotengenezwa kwa uwiano
sahihi wa virutubisho vinavyostahili au nunua kabisa vyakula kutoka kwa
watengenezaji walio na uzoefu na wanaoaminika.
Hakikisha chakula ni freshi, kisicho na unyevunyevu kwani
unyevu unaweza kulea kuvu na bacteria wanaosababisha magonjwa hatari kwa kuku.
Baada ya kuku kutolewa kwenye viota wiki moja mpaka mbili
watahitaji vilishio na vinyweo vikubwa zaidi ambapo kila kuku 100 watahitaji
vilishio 3.
KIASI
CHA CHAKULA KUKU MMOJA WA NYAMA ANAKADIRIWA KULA KILA WIKI MPAKA ANAUZWA / KUCHINJWA.
WIKI |
Gramu |
Wiki
ya 1 |
175 |
Wiki
ya 2 |
350 |
Wiki
ya 3 |
455 |
Wiki
ya 4 |
560 |
Wiki
ya 5 |
770 |
Wiki
ya 6 |
910 |
JUMLA |
2240g |
Kiasi cha chakula kuku wako watakachokula kitategemea ni
muda gani utawafuga kuku, kiasi kuku watakachokula mpaka wiki ya nne ni tofauti
na kiasi watakachokula mpaka wiki ya tano au sita.
MAJI:
Kuku wa nyama wanahitaji maji safi mara kwa mara. Safisha
vyombo vya maji kila siku kuzuia maambukizi ya magonjwa. Weka vyombo (vinyweo)
3 vya maji kwa kila idadi ya kuku 100
Kiasi
cha maji wanachokunywa kuku 100 kwa wiki
WIKI |
Kiasi cha maji kwa kuku 100 |
WIKI 1 |
14ltr |
WIKI 2 |
28ltr |
WIKI 3 |
47ltr |
WIKI 4 |
56ltr |
WIKI 5 |
70ltr |
WIKI 6 |
84ltr |
WIKI 7 |
98ltr |
Kulingana na jedwali hilo hapo juu kwa muda wa wiki 4
mpaka 4 na nusu kuku mmoja anakadiriwa kunywa maji lita 1.75 mpaka lita 2
kutegemeana na hali ya hewa itakavyokuwa. Kukiwa na joto kali kuku watakunywa
maji mengi kuliko majira ya baridi na mvua.
MWANGA:
Ili kuomgezeka uzito na uotaji manyoya haraka kuku wa nyama
wanatakiwa wawekewe taa usiku na mchana kwa saa zote 24 siku ya 1 mpaka 5,
baada ya hapo wapewe saa moja ya giza kwa siku ili kuwazoesha giza wasije
wakapatwa na msongo(stress) au kifo ikitokea kukatika kwa umeme ghafla au
dharura yeyote ya kuzimika kwa chanzo cha mwanga.
VITAMINI,
CHANJO NA MADAWA
·
Siku ya 1 – 5 vifaranga wawapo kwenye viota
wachanganyiwe glucose na vitamini kwenye
maji
·
Changanya dawa ya kuzuia mafua au Coccidiosis(Vigostat yenye Ridocox)
kwa wiki nne za mwanzo. Kilo moja inatosha mfuko mzima wa chakula
·
Endelea kuwapa Vitamini katika maji kwa siku
zinazofuata hadi wiki moja kabla ya kuwauza ndipo upunguze
·
Siku ya 7 wape vifaranga chanjo ya Kideri(New
castle)
·
Siku ya 14 wapatie chanjo ya Gumboro
·
Siku ya 21 rudia chanjo ya Newcastle
·
Tenga kabisa kiasi cha fedha kwa ajili ya
matibabu ya dharura ikitokea kuku wakapatwa na ugonjwa wowote ule utakaohitaji
daktari/mtaalamu na dawa
·
Wapatie kuku dawa kulingana na maelekezo ya
mtaalamu/daktari wa mifugo
MATANDAZO/USAFI
Epuka kulowanisha matandazo na endapo maji yatamwagika
eneo fulani eneo hilo libadilishwe matandazo mengine makavu mara moja. Kila
siku ondoa matandazo yalliyolowana au kugandamana kwa unyevu na kutifua yale yaliyopo ili yanyonye unyevu vizuri.
Matandazo yanaweza kubadiklishwa kwa wiki mara moja au kadiri utakavyoona
inahitajika.
KUMBUKUMBU
ZA BIASHARA
Kila siku hakikisha unaweka kumbukumbu sahihi za ulishaji
wa kuku, kiwango cha ukuaji, madawa, idadi ya kuku wanao kufa na tarehe ya
kuchanjwa kuku. Pima uzito kila wiki kwa kuchukua sampuli ya kuku wachache.
Kumbuka ufugaji wa kuku ni biashara kama zilivyokuwa biashara nyingine na
uwekaji mzuri wa kumbukumbu utakusaidia sana katika ulipaji wa kodi, kutathmini
faida au hasara ya mradi wako na kutambua ni wapi gharama ni kubwa ili upunguze.
MUDA
WA KUUZA/KUCHINJA KUKU WA NYAMA
Kuku wa nyama huwa tayari kwa kuchinjwa au kuuzwa kuanzia
wiki ya 4 na kuendelea mpaka wanamalizika Kuna watu huuza kuku wa nyama kuanzia
siku ya 25. Wanapokaa muda mrefu sana bandani gharama za kuwahudumia huongezeka
na hivyo bei pia inabidi iongezeke kufidia hizo gharama. Kuku mmoja wa nyama
katika umri kuanzia siku ya 25 mpaka ya 35 anakuwa amekula wastani wa kilo 2 za
chakula
KIWANGO
CHA KUFA KWA KUKU (MORTALITY RATE)
Kwa ujumla kiwango cha kufa kwa kuku wa nyama ni kati ya
asiliia 5% mpaka asilimia 12%, hii ina maanisha katika kuku 100 wanaweza kufa
kuku watano mpaka 12, zaidi ya hapo kutakuwa na tatizo aidha mlipuko wa ugojwa
au wanyama na wadudu walao kuku.
MBOLEA:
Kwa kuku wengi mbolea inaweza kuwa nyingi sana hasa ikiwa
unafugia eneo la mjini hivyo ni lazima uwe na njia ya kuihifadhi au kuiuza moja
kwa moja kwa wateja watakaoihitaji kama vile wakulima wadogo wa mbogamboga. Kiroba
cha kilo 50 cha mbolea ya kuku huuzwa kati ya shilingi elfu 2,000/= mpaka
2,500/=
HITIMISHO
Usije ukatarajia kuku wa
nyama kujitafutia chakula wenyewe kama kuku wa kienyeji au kuku chotara wafanyavyo,
hivyo kabla hujaanza kufuga kuku wa nyama(broilers) piga mahesabu kabisa ujue
zitahitajika kiasi gani cha fedha za kuwahudumia mpaka umri wa kuuzwa ufike,
umuhimu sawa na huo pia upo katika soko la kuku wako, tafuta soko kabla hata
hujaingiza vifaranga kwenye viota. Zingatia sana vitu hivi 3;- banda bora la
kuku wa nyama, ulishaji sahihi na maji safi na salama ya kutosha.
Pamoja na hayo lakini
usipuuzie pia mambo yanayoonekana kuwa madogomadogo mfano, idadi ya vifaranga
katika kiota, joto na mwanga, kwani vitu hivi vyaweza kuwa na athari kubwa sana
katika afya ya kuku na mradi wako mzima.
Haya maelezo yamejitosheleza kabisa, thanks for sharing this knowledge with us, unarikiwe sana.
ReplyDelete