SEMINA: KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU 2000 WA NYAMA (BROILER)-KUOMBA PESA-1 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SEMINA: KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU 2000 WA NYAMA (BROILER)-KUOMBA PESA-1

 

Vifaranga wa siku moja wa nyama

UTANGULIZI:

Hatimaye leo ndiyo siku tunaanza rasmi semina yetu ya kuandika mpango/mchanganuo wa biashara ya ufugaji wa kuku wa kisasa 2000(broiler) kwa ajili ya kuombea mkopo benki au taasisi nyinginezo za kifedha. Semina hii itaendeshwa na Mtaalamu wa michanganuo ya biashara mzoefu Bwana Peter Augustino Tarimo ambaye kwa Takribani miaka 10 sasa amekuwa akiandika michanganuo ya biashara za makampuni mbalimbali mapya na yaliyokwisha anza kwa malengo tofautitofauti kama kuombea mikopo, kuendeshea biashara na hata kwa ajili ya kufanyia tathmini ya uwezekano wa kufanikiwa kwa biashara.

Semina hii tofauti na nyingine tulizowahi kufanya huko nyuma, tutakwenda taratibu kidogo kwa lengo la kutokumuacha mtu nyuma, watu wengi hulalamika, “Peter unakwenda haraka mno hatukupati vizuri” na mimi kwa kuwa lengo langu ni kufundisha watu waelewe nazingatia ombi hilo hata kama itachukua wiki nzima. Hivyo tafadhali kama lengo lako ni kujifunza haraka haraka tafadhali semina hii itakuwa haikufai subiri nyingine zijazo mithali upo kwenye group hilihili kwani tutakuwa na semina nyingine nyingi zaidi mwaka huu wa 2022.

 

KWANINI BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU WA NYAMA (BROILER)?

Dhamira kubwa ya kuanzisha group la Michanganuo-online ilikuwa ni kuchambua au kuchanganua mawazo ya biashara zile zenye fursa kubwa ya kutengeneza faida haraka kwa mtaji mdogo. Mawazo ya biashara hizo yanaweza yakawa ya biashara yeyote ile ya kawaida lakini iliyo na ubunifu wa kipekee utakaosababisha iweze kutengeneza faida harakana kwa urahisi.

Kwa hiyo biashara ya ufugaji wa kuku wa kisasa wa nyama ni moja kati ya biashara hizo mtu unazoweza ukatengeneza faida upesi ndani ya kipindi kifupi sana endapo tu utazingatia mbinu za kisayansi zilizodthibitishwa kote duniani.

Ninaposema mbinu za kisayansi simaanishi mbinu zile ya kurushia maroketi mwezini au kupeleka binadamu sayari ya Mars hapana bali namaanisha matumizi ya mbinu zinazoeleweka kila mahali dunia nzima na zenye kutoa matokeo mazuri yaleyale yaliyokusudiwa haijalishi zimetumiwa na nani au wapi.

Tatizo wabongo hatuamini sayansi tunapenda mno kuchomekea mbinu zetu wenyewe za kijadi zisizokuwa na tija yeyote mfano badala ya kulisha kuku chakula chenye mchanganyiko sahihi wa virutubishi ili watage mayai mengi makubwa kila siku, tunaamua kuwasukumizia mipumba mikavu ya mahindi kuku wanaishia kunenepeana tu na mayai hakuna, halafu tunaanza kutafuta “ni nani mchawi anayeloga kuku zangu zisitage mayai”.

Kuna mfano mwingine jamaa yangu mmoja alinishangaza sana alipokuwa akinisimulia jinsi anavyokabiliana na magonjwa hasa kideri(new castle) kuku wake wanapougua. Jamaa anasema yeye humpa kila kuku kidonge kimoja cha  rangi mbili  akimaanisha antibiotic , piritoni moja na panodol moja!

Nikamuuliza kuku wa umri gani? Akasema inategemea kuku ameathirika kiasi gani, hata awe kifaranga dozi ni hiyohiyo ikiwa ataonyesha homa imemkolea sana. …….Nilibakia kichwani nawasikitikia hao kuku….. Akaendelea kusema kwamba kwa tiba hiyo kuku wake huwa wanakufa lakini siyo wengi sana, wengine wanapona na ni shauri ya hiyo dozi vinginevyo wangepukutika wote.

Tukiachana na stori hizo hebu tuendelee na mada yetu. Kwa hiyo mpenzi mfuatiliaji wa semina hii ninachotaka ufahamu ni kwamba siyo ufugaji wa kuku wa nyama tu wenye fursa kubwa na ya kipekee hapa Tanzania bali sekta nzima ya ufugaji wa ndege hususani kuku Tanzania ni sekta inayolipa na inakua kwa kasi sana kama ulikuwa hujui kwa mfano sasa hivi Tanzania kuna uhaba mkubwa sana wa vifaranga hawa wa kuku wa kisasa, mtu ukawa na mtaji wako ukaanzisha biashara ya  kutotolesha vifaranga nakuhakikishia maisha yako hayatabaki kama yalivyo sasa kiuchumi.

Bado sijazungumzia biashara ya mayai yawe ya kisasa au ya kienyeji, hivi nikuulize swali moja, umewahi kusikia muuza duka yeyote jirani na wewe akikuambia mayai yamewahi kumdodea dukani kwake mpaka yakaharibika? Basi ujue kabisa biashara au sekta hii bado ni mbichi kabisa haijaguswa.

Bora hata ukaniambia wenzetu hapo Kenya wao wameigusagusa kidogo sekta hii ndio maana hata unaona nyama na mayai yao yakifika huku kwetu tunashangaa bei ipo chini, tunalalamika. Unaweza kujiuliza kwani wao wanapata wapi chakula mpaka bidhaa zao zinakuwa chini hivyo wakati mahindi tunawauzia sisi wenyewe?

Hakuna uchawi hapo ndugu yangu, ni mbinu tu za kisayansi wanazozingatia kupunguza matumizi/gharama na kuzidisha faida mara dufu. Sisi Tanzania mavyakula tunayo ya kumwaga still hatuwezi kuzalisha mazao ya kuku kwa tija inayostahili. Pana tatizo hapa tuzinduke Watanzania!

 

Ni nini hasa maana ya mchanganuo wa biashara?

Ni vizuri kabla hatujaanza rasmi tukafahamu kwanza maana ya baadhi ya maneno huhimu tutakayoenda kuyatumia kwenye semina yetu hii na tutaanza na maana yenyewe ya mchanganuo wa biashara au Mpango wa biashara ni nini.

Kwa mujibu wa Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI ambacho naamini wewe mshiriki katika semina hii unacho bila shaka yeyote kwani ndiyo nyenzo kuu kila anayejiunga na group letu hili ninayompa ya kwanza kabisa,

Mchanganuo wa biashara /mpango wa biashara (Business plan) ni;-

 

Maandishi yanayoelezea kila jambo kuhusu biashara unayoiendesha, mambo hayo ni, malengo, mikakati, bidhaa/hudumu utakayouza, soko (wateja), shughuli mbalimbali za masoko na uongozi, gharama, mahitaji, na masuala yote yanayohusiana na fedha.

 

Unaelezea kile hasa unachotaka kukifikia, namna unavyoweza kukifikia na gharama mbalimbali zitakazotumika katika kufanikisha malengo uliyojiwekea.

Kwa maneno mengine ni kwamba mchanganuo wa biashara maana yake unagusa kila eneo la biashara husika kifikra kabla hata hujaanza kuifanya. Hii inakusaidia kupunguza changamoto mbalibali zinazoweza kujitokeza kwenye biashara kwani unakuwa nyingi umeshaziona kabla hazijawa halisi.

Mchanganuo wa biashara pia unamwezesha mtu kujua mahitaji yote ya biashara yake yote kabla hajaanza. Benki na taasisi nyingine za fedha mara nyingi hudai waombaji wa mikopo kuwasilisha mipango ya biashara zao kwa ajili ya kutathmini ikiwa kama  muombaji mkopo amejizatiti vipi au amejipangaje kutumia kiasi cha fedha anazoomba kupata faida itakayomwezesha kurejesha mkopo na biashara iendelee mbele.

 

Kuku wa Kisasa (Hybrids)

Kama mbegu za mahindi ya kisasa au mimea mingine iliyozalishwa kitaalamu kuku wa kisasa pia ni Hybrid. Mbegu ya hybrid maana yake ni mchanganyiko wa mbegu mbili kutoka kwa wazazi wawili tofauti walio na tabia au sifa tofauti kwa lengo la kuziboresha zaidi au kupata sifa fulani inayolengwa kwa mfano sifa ya kuzaa sana, sifa ya kutokushambuliwa na wadudu/magojwa, sifa ya maumbile makubwa nk.

Kuzalisha mbegu za hybrid iwe kwa kuku au kiumbe kingine chochote kile siyo jambo rahisirahsi kila mtu anaweza kulifanya hapana, ndio maana unaweza ukashangazwa sana unaposikia kuku wazazi kwa ajili ya kuzalisha kuku wa mayai na kuku wa nyama ni aghali sana karibu shilingi elfu 15 kwa kuku mmoja tu na tena isitoshe kuku hao wazazi ni lazima waagizwe kutoka ulaya, Marekani au Nairobi.

Ni mchakato tata unaofanywa na wanasayansi ya kijenetiki na masuala ya aina za wanyama(breeds) kwa kupandikiza aina tofauti za kuku kwa lengo la kupata mbegu yenye sifa fulani kama kutaga myai mengi au kubadilisha chakula kuwa nyama kwa muda mfupi kadiri iwezekanavyo. Wakati mwingine watapandikiza mjukuu na babu, mama na mtoto, kuku aina hii na ile nk. ilimradi  tu wapate sifa fulani zinazohitajika na wala siyo wanatumia madawa kuwabadilisha kama watu wengi wetu tulivyokuwa tukidhania.

 

Kuku wa Nyama (Broiler)

Kuku wa nyama Broiler ni kuku waliokuzwa maalumu kwa ajili ya nyama tu kutokana na wazazi jogoo na mtetea walio na sifa tofauti kama nilivyoeleza hapo juu. Kuku hawa ingawa wanaweza kutaga lakini watataga idadi ndogo sana ya mayai kulinganisha na kuku wa mayai. Hufikisha uzito unaostahili katika kipindi kifupi sana kuanzia wiki4 mpaka 6. Wafugaji wa kuku wa nyama hununua vifaranga kutoka kwa watotoleshaji wenye vibali maalumu kutoka Wizara ya Mifugo.

Baada ya maelezo hayo sasa tutakwenda kuanza rasmi utafiti kwa ajili ya kupata taarifa zitakazotuwezesha kuandika Mchanganuo wetu wa biashara hii ya ufugaji wa kuku wa nyama 2000 kwa ajili ya kuombea mkopo benki au taasisi za fedha. Baada ya kumaliza semina nzima kila mshiriki atakuwa na nakala kamili ya mchanganuo huo katika lugha ya kiswahili na kiingereza ambazo tutashirikiana hapa sote kuandika hatua kwa hatua.

Tafadhali usikose siku ya kesho kufuatilia semina hii na mjulishe yeyote unayemjali ashiriki pia.

0 Response to "SEMINA: KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU 2000 WA NYAMA (BROILER)-KUOMBA PESA-1"

Post a Comment