Heri ya Mwaka Mpya Ndugu Msomaji wa Makala hii !
Tunapoukaribisha mwaka 2022 kuna mambo mengi
tutanayoyaacha nyuma yetu lakini pia ni lazima tukubali kwamba kuna mengine
kamwe hayataweza kufutika kwenye mawazo yetu kwa urahisi siku za hivi karibuni
na moja kati ya matukio hayo ni kama vile kuondokewa na wapendwa wetu, kuugua
na hata kupatwa na majanga makubwamakubwa.
Kwahiyo nichukue nafasi hii kuwakumbuka hasa Wadau
wenzetu ambao siku kama ya leo mwaka jana waliweza kusoma ujumbe wangu wa mwaka
2021 lakini kwa bahati mbaya leo hii hatuko nao tena, Mwenyezi Mungu
awapumzishe kwa Amani Amina.
Wiki inayoisha nchini kuna habari ‘ilitrendi’ (kushika sana kasi) kuhusiana na deni la Taifa, huku
kila mtu akisema lake. Ijapokuwa si nia yangu kuonyesha upande ninoegemea
lakini pia kama haki yangu ya msingi na kama Mwananchi siyo vibaya nami nikatoa
maoni yangu kidogo katika mtazamo wa Kijasiriamali.
Siyo siri Watanzania wengi tunaogopa sana mikopo na
sababu kubwa ya hofu hii si nyingine bali ni UKOSEFU WA ELIMU YA KUTOSHA YA FEDHA. Wanaoujua utamu wa kukopa na
kufanyia kazi mikopo kwa malengo waliyokusudia huwa siri hii wengi hufa nayo
mioyoni, katu hawamdokezei mtu mwingine kirahisi.
Unapokuwa unatumia rasilimali za watu wengine kukuingizia
pesa zaidi ni sawa na kuwatumikisha watu wengine bila ya wao wenyewe kujua kama
unawatumikisha ilimradi tu unatumia akili. Wakati wa utumwa wajanja (Mabwana)
waliwatumia watumwa kama mitaji, lakini leo hii unaweza kuwatumikisha watu
wengine kwa kutumia rasilimali na nguvu zao kwa akili bila ya kuwashurutisha.
Dhana ya kukopo haipo kwa mtu mmojammoja tu peke yake
bali hata katika ngazi ya Nchi(Mataifa). Tatizo kubwa linalotuponza Mataifa
maskini ya Afrika na kuonekana kila mara kutiwa kitanzi na mikopo tunayopokea
Magharibi na Mashariki ni tatizo la matumizi ya mikopo hiyo. Kama tu ilivyo kwa
mtu mmojammoja, Mataifa hayo nayo baada ya kuchukua mikopo, fedha hizo huwa
haijulikani bayana zinakokwenda wala zinachofanyia ni nini.
Tena isitoshe hakuna ufuatiliaji wa nguvu na
uwajibishwaji kwa wahusika kwa upotevu wa hizo fedha, hata kukiwa na
uwajibishwaji kidogo wahusika hawalazimishwi kurudisha mali na pesa iliyopotea
zaidi ya kufungwa miaka miwili, mitatu na wakitoka jela wanakwenda kutafuna pesa
walizoiba kama kawaida.
Kachunguze Wamarekani na Wachina mikopo ndiyo
iliyowafikisha pale walipo leo baada ya kuitumia kwa nidhamu katika miradi
yenye tija. Badala ya sisi kuanza kulumbana eti ikiwa tukope au tusikope, mimi
nafikiri ulikuwa ni muda muafaka kujiuliza tutumie mbinu na mikakati ipi
kudhibiti mianya ya wizi wa fedha tutakazokopa ili zisipotee kirahisi,
zizalishe na mwishowe zirejeshwe kule zilikokopwa.
Kama
tunakopesheka na fursa ya kukopa tunayo kwanini tulaze damu wakati mzunguko wa
fedha ndani ni kidogo kiasi hicho?
Tukiachana na hayo ya deni la Taifa, mimi napenda zaidi
kudili na mtu mmojammoja katika suala hili. Kwanza ikiwa kama wewe ni
mjasiriamali mdogo, mwaka 2022 funguka kabisa, toka nje ya ‘miboksi’ uliyojilundikia miaka yote ! Tambua
kuwa kwa mtaji wako mwenyewe kidogo biashara haitaweza kupiga hatua yeyote ile
ya maana. Unahitaji rasilimali kubwa zaidi.
Kitu ninachoshauri hapa
si mtu akimbilie benki au taasisi kubwa kubwa za kifedha kiholela tu
hapana, hawatakukopesha kirahisi hivyo. Hebu kaa chini kwanza kisha jiulize
swali hili, “JE, HIVI MIMI
NINAKOPESHEKA”
Mtu kukopesheka haimaanishi kuwa wewe unamiliki sijui
nyumba au mali isiyohamishika hapana, Kukopesheka watu huangalia kwanza
UAMINIFU WAKO na hiki ndicho chanzo cha ule usemi kwamba, UAMINIFU NI MTAJI.
Siku zote mimi huwa nasema kwamba ili mtu kujenga hali ya
kukopesheka, anzia katika ngazi ya chini kabisa, usipende shortcut. Unaanzia
wapi sasa? Ukiona huwezi hata kumkopa jirani yako shilingi elfu mbili upatapo
tatizo dogo na ujue pia utapata shida sana kujaribu kukopa kwenye kikundi cha
VICOBA au hata vile vya upatu wa kienyeji -michezo.
Kuaminika kunaanzia huko. Na usipoaminika pia hukopesheki popote.
Ikiwa bado hujajijengea uwezo wa kukopesheka nakushauri
usisubiri anza hata kesho kwa kujiunga na mikopo ya chini kabisa ya vikundi
vidogovidogo, vicoba nk. bila kujali utakopa kiasi gani cha fedha kwa kuanzia
lengo lako likiwa ni kujenga kwanza uwezo wa kukopesheka na tabia ya kujiwekea
akiba. Wakati huo lenga kukopa katika taasisi kubwa zaidi au benki kadiri muda
unavyokwenda na uwezo wako wa kukopesheka unavyoongezeka.
Mara tu utakapofanikiwa kukopa benki au taasisi kubwa ya
kifedha mara moja, endelea kudumisha hali yako nzuri ya kukopesheka na uaminifu
bila kujali kiwango cha mkopo unachopata kama ni kikubwa au kidogo.
Kidogokidogo utaanza kuona mtaji siyo tatizo kubwa tena kwako kwa kuwa unao
uwezo sasa wa kuupata unapouhitaji. Lakini hali hii ni lazima iambatane na mtu
kujifunza siku zote elimu ya kifedha hasa matumizi mazuri, kujiwekea akiba na
kuwekeza katika bishara zenye faida.
HITIMISHO
Siri ya mikopo ipo kwenye matumizi yake, Ikiwa kwa namna
yeyote ile utashawishika kutumia pesa za mkopo nje ya lengo mahsusi la mkopo
wenyewe, kataa kabisa, ni bora ukaurejesha mkopo mzima mzima kama ulivyo bila
ya kuufanyia chochote huku ukibakia na deni la riba peke yake kuliko kuufanyia
vitu tofauti na vile ulivyoombea.
Waliofaulu na mikopo mara nyingi huungana na wale
waliofeli na mikopo kuwaogopesha wale wasiojaribu hata siku moja kukopa kwa
kuwaaminisha kwamba mikopo ni kitu hatari
sana wanachostahili wajanja wachache tu, badala yake wangeliwapa somo ni kwa
namna gani wanaweza wakakopa bila ya kuhatarisha rasilimali zao nyingine kwa
kuwa wote waliofeli na waliofaulu wanao uzoefu kwenye kukopa. Usiogope kukopa
bali ogopa majaribu ya kutafuna fedha za mkopo.
……………………………………
Niemeongeza muda kidogo kwa ajili ya OFFA ya vitabu vyote
5 vya SELF HELP BOOKS TZ na Michanganuo ya Biashara, mwisho utakuwa ni tarehe 10 January 2022
Pia Group letu la Watsap, MASTERMIND GROUP-2022 bado kidogo tufunge kuunganisha watu na kuanza masomo na semina rasmi.
Ukihitaji Vitabu tu na Michanganuo lipa sh. Elfu 10 kupitia 0765553030 au
0712202244 Peter Augustino, kisha tuma neno “NATAKA OFFA YA VITABU TU”
Na ukihitaji na kuungwa na kwenye group tuma neno “NATAKA OFFA YA VITABU NA GROUP”
Soma Hapa Baadhi ya Meseji za Shuhuda za Waliojipatia OFFA Hii
0 Response to "SIRI YA MIKOPO NA CHANZO CHA WATANZANIA KUOGOPA MNO KUKOPA"
Post a Comment