Katika makala yetu ya USHAURI leo kwa biashara ndogondogo zinazolipa Tanzania, tutajibu swali la msomaji wetu mmoja kwa jina Ahmad, (hapa huwa hatuweki utambulisho kamili wa msomaji anayeuliza swali pasipo ridhaa yake mwenyewe kwahiyo nitamuita jina moja tu hilo la, Ahmad).
Swali lake aliuliza kama ifuatavyo, nimeweka na
screenshot za meseji aliyotuma kwa wasap katika picha;
Habari Mwalimu?
Kwa
jina naitwa Ahmad...........,
Nimekuwa
nafuatilia sana Elimu za darasa unazonitumia asante sana.
Mimi
nina changamoto kubwa sina uzoefu wa biashara yeyote kazi yangu kuu ilikuwa
kilimo na kufundisha elimu ya Dini huko Mkoani
Natamani
sana nianze biashara ndogo tu ya mtaji wa elfu 80
Naomba
ushauri wako Mwalimu.
Nipo Dar es salaam, Majohe ya Gongo la Mboto
MAJIBU KWA SWALI LAKE NI HAYA HAPA;
Ahsante sana Ahmad kwa kufuatilia elimu yangu ya biashara
ninayotoa kwa njia ya email mara kwa mara, Na pia umesema ungetamani kutumia
elimu hiyo kwa vitendo sasa kuanzisha biashara hata ikiwa unao mtaji mdogo tu
wa shilingi elfu 80 (80,000/=).
Umeniambia unaishi Pugu Majohe ya Gongo la Mboto ila
sijajua kama kwa sasa hivi unajikimu vipi kimaisha nikimaanisha ikiwa kama
unaye ndugu yeyote au jamaa anayekusapoti katika mahitaji yako muhimu ya kila
siku ya chakula, malazi na mavazi ukiwa bado hujapata biashara au kazi ya kufanya kwani mimi kama
nijuavyo biashara ndogo nyingi huwa zinashindwa kupiga hatua ya maana kutokana
na kuzidiwa na mzigo mkubwa wa matumizi ya wamiliki wake.
Maisha ya biashara si lelemama hata kidogo, mmiliki huwa hana
namna nyingine ya kuishi zaidi ya mapato ya hiyo biashara ndogo na biashara
huwa bado haina uwezo wa kuzalisha fedha zinazotosheleza matumzi yake pamoja na
kumudu kuifanya biashara ikue. Matokeo yake unakuta biashara inakufa muda mfupi
na mmiliki kuona ugumu wa kila biashara ndogo nyingine yeyote atakayoanzisha.
Jambo la pili ambalo ningetamani kujua toka kwako ni ikiwa
kama tayari unayo familia mke na watoto/mtoto au la, hili nalo ni la kuzingatia
kwani ni sababu nyingine kubwa inayoweza kuiathiri biashara ikue ama izorote.
Familia inaweza ikaiongezea zaidi biashara mzigo wa matumizi usipokuwa
muangalifu au pia ikaipa biashara unafuu wa nguvukazi ikiwa tu mtajipanga vyema
wewe na mkeo na hata watoto ikiwa kama ni wakubwa wanaojitambua na haijalishi
wanasoma au hawasomi.
Suala la kutenganisha kabisa fedha za biashara na fedha binafsi
kwa mjasiriamali mdogo ni gumu na mtu asikudanganye eti ni kitu
kinachowezekana moja kwa moja pasipo kuwa na namna nyingine yeyote ile ya
kuijikimu kimaisha, kitu cha muhimu sana kufanya hapa ni kujitahidi kuongeza
kipato chako kwenye hiyo biashara ili pesa unayojilipa kama mshahara nayo iweze
kuwa nyingi inayokidhi mahitaji yako ya kila siku ;vinginevyo tutakuwa
tukidanganyana tu eti, usiguse kabisa hela ya biashara, je utakuwa ukiishi
vipi?
Ikiwa unaishi bachela / Single ni rahisi zaidi kuendesha
biashara ndogo ikakua kwa urahisi kwa kutumia mbinu kama zile nilizotumia mimi
mwenyewe wakati nilipokuwa nikianzisha duka langu la rejareja mtaa wa Msimbazi
Kariakoo, kisa hiki nimekielezea vizuri sana kwa picha halisi mnato za rangi
nilizopiga wakati huo katika kitabu changu cha Mafanikio ya Biashara ya Duka larejareja.
Simaanishi ukiwa na familia basi haiwezekani kuanzisha
biashara ndogo ya mtaji mdogo ikakua hapana, bali ninachotaka hapa ni kuelezea
mazingira mazima yanayozunguka hali zote mbili, ukiwa na familia na ukiwa
single ili kuweza kujua hatua sahihi za kuchukua kabla hujaanzisha biashara
ndogo, zipo mbinu mbalimbali za kufanya na nitazieleza hapa ikiwa unayo familia
na unataka kuanzisha biashara ndogo ya mtaji mdogo kwa mafanikio.
Ikiwa unaishi peke yako bado hujawa na familia
inayokutegemea ni rahisi sana kuanzisha na kuendesha biashara yeyote ile ndogo
kwa mtaji mdogo kutokana na sababu kwamba unaweza ukajibana kwenye matumizi
yako na mtaji ukakua haraka haraka hata kama unalala kwa kubahatisha au kwa
ndugu na jamaa zako wanaokusapoti kwa muda ili hali yako ikae vizuri. Kumbuka
katika hatua hii unafanya kila namna ili uweze kwanza kukuza biashara itengemae
na kusimama.
Ikiwa tayari unayo familia inayokutegemea hapa mjini,
unayo kazi ngumu kidogo ya kufanya tofauti na mtu asiyeanza familia bado lakini
hata hivyo kuna mbinu moja mbadala ya kufanya nitakayokushirikisha hapa chini;
1. Tumia
nguvukazi ya familia vizuri :
Mshirikishe mwezi wako katika kila hatua ya ujenzi wa
uchumi wa familia, kama ana chanzo cha kipato ni vizuri zaidi, ikiwa hana
kipato chochote kile basi itawabidi wote wawili mjikite kikamilifu kwenye
mradi/biashara mtakayoianzisha, acha wivu wa kijinga na fanya kazi bega kwa
bega na mkeo/mumeo.
Na hata ikiwa mna mtoto/watoto wakubwa kidogo hata kama
wanasoma shule washirikisheni kwa namna tofautitofauti ili na wao waweze kuchangia
kidogo katika biashara mnayofanya hata kama ni kwa kiwango kidogo wapatapo muda
wa ziada.
Kwa mfano kama mna kiduka au kigenge-duka hapo nyumbani
mtoto asaidie kazi pale muda wazazi mna majukumu mengine kwani mkikosa pesa
hata hiyo shule yenyewe atasoma kwa mashaka. Afanye hivyo muda baada ya masomo
tu na siku za mapumziko na pia mpime mtoto, akiwa mwepesi wa kudokoadokoa
usimruhusu kabisa kwenye suala hili.
Mama anaweza akawa amefuatilia dagaa na samaki feri huku
baba akienda soko la Mabibo kufuatilia ndizi na matunda mengine, na mtoto
akiendelea kuuzia wateja vitu katika kiduka ama genge mliloanzisha. Nasema
kiduka nikimaanisha biashara ndogo kabisa kwani mtaji wa elfu 80 ni kidogo sana
kuanza biashara unayoweza kuiita biashara ndogo au hata ya kati.
BIASHARA
YA MTAJI WA SHILINGI ELFU 80 (80,000/=)
Sasa hapa ndiyo najibu rasmi swali lako, kwingine kote
huko tulikuwa tukiangalia tu mazingira yako ili uweze kujua wewe umesimama wapi
hasa.
Kwa mtaji wa shilingi elfu themanini si kama nabeza
hapana, bali ndiyo ukweli wenyewe ulivyo kwa watu wengi waliowahi kuanza
biashara na kiwango sawa au kinachofanana na hicho cha fedha, kamuulize mtu
yeyote na wala si lazima awe mtaalamu au mshauri wa mambo ya biashara
atakuambia tu, bwanae elfu 80 ni hela ya mboga tu, kufungulia biashara ni sawa
na kutwanga maji kwenye kinu.
Lakini huo ndio mtazamo wa watu wengi, simaanishi kila
mtu anauona mtaji wa elfu 80 kuwa ni kidogo hauwezi kufungulia biashara
ikafanikiwa hapana, na mimi ni mmoja wa wale watu tutakaokuambia elfu 80
inatosha kabisa kuanzisha biashara ndogo ya mtaji kidogo na ukatoboa kwakuwa
nilishawahi kufanya hivyo na nikafanikiwa pia. Waliowahi kusoma kitabu changu
cha Mafanikio
ya Biashara ya duka la rejareja ni mashahidi wazuri wanaoweza kunitetea,
nilianza na karibu mtaji sifuri lakini bado niliweza.
Biashara ya mtaji mdogo nzuri sana ya kuanza na fedha isiyozidi
elfu 80 ni ile biashara ya kuuza vitu vidogovidogo vinavyotumika kila mara na
watu, mahitaji ya kila siku ya watu, vitu ambavyo binadamu hawezi kuishi hata
siku moja bila ya kuvitumia. Tena uzuri mmoja ni kwamba umeniambia unaishi
mjini Dar es salamaam, na mji wowote ule hata kama siyo Dar inafahamika watu
huwa hawana mashamba wala mazizi ya mifugo na hivyo kila kitu wao hukimbilia
kununua tu penda wasipende, sasa kwanini usitumie fursa hiyo vizuri
kujineemesha?
Kwa mtaji wa shilingi elfu themanini (80,000/=) nashauri
kama ifuatavyo; Ukikurupuka wiki haiishi utajikuta huna kitu mfukoni, tulia
kwanza kisha tafakari, tafuta eneo, ni vizuri zaidi eneo likawa ni hapohapo
unapoishi kwa nje kama kuna kibaraza kidogo au hata njia ya wapita kwa miguu.
Lengo langu hapa nataka ukwepe gharama za kulipia fremu/pango la chumba cha kufanyia biashara. Kwa kifupi kabisa tafuta biashara ya kufanya ukiwa nyumbani. Sikuambii ufungue biashara gani, sijui genge au duka ama genge-duka hapana maana kwa mtaji huo ukisema ufungue biashara rasmi maalumu utafeli. Mpaka mtaji uongezeke kwanza ndipo uweze kujibainisha unafanya biashara ya aina gani hasa.
Tafuta biashara za mtaji kidogo kuanzia elfu 2, kumi mpaka laki moja unazoweza kuanza zikakutoa na siyo lazima eti iwe ni biashara
ya mtaji wa laki tano na kuendelea huko juu.
Chunguza watu waliokuzunguka, majirani nk. ni vitu gani
vidogovidogo haipiti siku hata moja bila ya kuvinunua. Chukua elfu 80 yako
nenda kama ni maduka ya jumla, sokoni au hata kwa wauzaji wowote wale wa vitu
vya jumla kanunue bidhaa hizo kiasi kidogokidogo ilimradi ujue ukija kuuza
utapata hapo faida kidogo na fedha yako ya manunuzi itarudi.
Hiyo centre utakayofungua inabidi uwe mbunifu sana,
ukiona vitu vya kutafunatafuna vina uwezekano wa kutoka weka, kwa mfano miguu
ya kuku, vichwa vya kuku utumbo nk. Unaweza ukaweka maandazi, keki, vichipsi
kwa aji ya watoto wa shule, mihogo ya kukaanga nk.
Unaweza pia kuweka shelve kidogo ukapanga hapo chumvi
pakiti kadhaa, majani chai, nyembe, shaving machines zile za miamia au mia tano,
miswaki na dawa za mswaki, juisi, soda, kalamu, unga wa sembe na hata maji ya
chupa. Pipipipi kwa ajili ya watoto, chama, biskuti na ice cream (ice krimu)
Mbogamboga za majani na matunda yote muhimu kama embe, mananasi,
matango, mabungo, machungwa, kabeji, mchicha, spinachi nazi, ndizi na karanga za kukaanga
visikosekane. Viungo vyote muhimu kama vitunguu maji, vitunguu swaumu,
mdalasini, pilipili manga, pilipili za kawaida, ndimu nk. Chunga sana usiweke
vitu vinavyoharibika upesi kwa kiwango kikubwa kuepusha hasara.
Kila kitu kinapoisha nenda chap kachukue kingine mteja
asije kukosa kitu. Vile vitu vinavyoisha harakaharaka vitie alama uwe
unavizingatia zaidi na kwa kiwango kikubwa. Hakikisha una daftari lako kwa
ajili ya kumbukumbu zote za manunuzi ya kila siku, mauzo ya kila siku, madeni
ya wateja kama yapo na daftari la orodha ya vitu vilivyoisha vinavyotakiwa
kununuliwa siku ya pili. Ikiwezekana ni vizuri uweke mapema utaratibu wa
kuandika kila bidhaa inayouzwa katika daftari ili kujua kwa siku umeuza nini na
vya thamani gani hivyo pia iwe rahisi kwako kujua kwa siku umeingiza faida
kiasi gani.
Silaha yako kubwa ya mauzo inatakiwa iwe ni kauli nzuri
kwa mteja na wakati mwingine bei nafuu, jitahidi bidhaa zako uzipate kwa
gharama nafuu iwezekanavyo kusudi pia bei yako ya mauzo kwa mteja iweze kuwa
shindani ili uwateke wateja waliozoea kununua kwa washindani wako kibiashara
wanaokuzunguka. Au basi ikishindikana kuuza bei ya chini angalao bei zako
zifananae na zile za washindani wako na si juu ya zakwao.
Kaeneo ulikopata kanaweza kuwa kadogo sana kuenea kila
kitu unachotaka kuuza lakini unaweza kufanya chumba unachoishi kama stoo yako
ya kuhifadhi baadhi ya bidhaa huku zingine ukipanga kwenye hako kaeneo
ulikopata na kila kitu kikiisha unakimbilia ndani kwenda kuongeza kingine. Na
hii ndio sababu ya kukuambia biashara anzia palepale unakoishi kwa sasa kupunguza gharama na siyo
ukapange mbali na hapo. Wapuuze wale wote watakao kucheka eti kisa
unafanya biashara ukiwa nyumbani kwani ukiwaomba hata mia bado watakucheka.
Nashindwa hii senta tuiite genge, duka ama kitu gani
kwasababu ni mchanganyiko wa vitu vingi binadamu anavyohitaji kila siku,
ingelikuwa kubwa kidogo ningekushauri tuiite supermarket ndogo (mini supermarket) lakini kwa kuwa ni
ndogo tuiache tu hivyohivyo tusiipe jina. Wewe lenga zaidi kukidhi mahitaji ya
wateja wanaokuzunguka bila kujali unapata faida kubwa au ndogo kiasi gani kwenye kila
bidhaa lakini pia usikubali uuze kitu kisichokuwa na faida kabisa hapana.
Kwakuwa utapata faida ndogondogo kutoka katika kila
bidhaa utakayoiuza basi utajikuta jumla ya faida yote kwa siku inakupatia fedha
nyingi zitakazosaidia kuikuza zaidi na zaidi biashara yako hatimaye uweze
kuamua sasa ufanye biashara ipi rasmi kwa mtaji unaoeleweka.
Kuna kitu kimoja napenda ukifahamu mapema sana ungali
bado unaanza biashara ya mtaji mdogo, tengeneza mapema mazingira ya biashara
yako kukopesheka na taasisi za kifedha kwani kuna siku huko mbeleni utakuja kuhitaji kukopa ili 'kuiboost' zaidi biashara yako ikue kwa haraka na kwakuwa utakuwa umeshapata
uzoefu wa muda mrefu mkopo hautakushinda kurejesha.
Tafuta kikundi chochote kile cha VICOBA au SACCOS
kajiunge kule na kwa kuanza usikimbilie kuchukua mkopo wowote ule, wewe weka tu
akiba kidogokidogo kwa ajili ya masilahi ya baadae. Au unaweza ukafungua
akaunti benki yeyote unayojua baadae unaweza ukaja kukopa kama mjasiriamali
mdogo.
Aina za biashara ndogondogo nyingi zinahitaji vyanzo
tofauti tofauti vya pesa katika nyakati tofauti, hivyo usiipoteze fursa hii
adimu hata kidogo, ukiacha ukifikiri eti utaenda muda ukifika itakuja kuwa vigumu
sana kwako muda huo utakapofika. Nashauri ikiwezekana kajiunge hata leo kabla
huujaanzisha biashara yenyewe huku ukijifunza taratibu biashara kwani kujifunza
biashara ni mchakato unaochukua muda wakati ukiendelea kuifanya na wala siyo
jambo la siku moja tu.
Kwa leo naona niishie hapa Bwana Ahmad, bila shaka
ushauri wangu utakusaidia kwa namna moja ama nyingine katika kujikwamua
kiuchumi. Kila la Kheri.
Peter
Augustino Tarimo
Mshauri na Mtaalamu wa Michanganuo ya Biashara zote kubwa
na ndogo.
Kwa
ushauri mdogomdogo kama huu kwa mtu yeyote tunatoa bure kabisa, tuandikie tu
kupitia watsap au SMS, 0765553030 au email: jifunzeujasiriamali@gmail.com
SOMA NA HIZI HAPA;
1. Kuanzisha biashara nikiwa chuoni nasoma, nipeni ushauri nina wakati mgumu
2. Nina mtaji wa shilingi milioni moja (1,000,000) naomba ushauri nitafanya biashara gani?
3. Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha au benki?
4. Unajua biashara yenye faida kubwa na ya haraka mara 2 ya mtaji utakaowekeza?
5. Biashara ya vinywaji jumla, mtaji milioni moja (1) naomba ushauri
0 Response to "BIASHARA NDOGO YA MTAJI WA 80,000/= NIUZE NINI KUPATA FAIDA YA HARAKA?"
Post a Comment