Huu ni mjadala uliofanyika kwenye Mastermind group la
MICHANGANUO-ONLINE 25/1/2022 na unaweza kushiriki kwa kutoa maoni yako wewe upo
upande gani. Hapa nimeweka hoja kutoka pande zote mbili, wanaosema pesa inaweza
kumaliza kila tatizo na upande wa wale wanaotetea kwamba Pesa ni chanzo cha
kila tatizo hapa Duniani. Mwisho kabisa tulipiga kura na kuona ni upande upi
ulioshinda mjadala.
1.
Upande wa ndiyo Pesa ni suluhisho la matatizo yote:
Mtu wa kwanza
Hebu
jaribu kufikiria labda umekumbwa na ugojwa mbaya na wa ajabu, unaofanana na
Corona ambao chanjo yake bado haijagundulika bado wala tiba, lakini ukasikia
mara kuna dawa imepatikana huko Marekani lakini bei yake ni milioni 10 na
unapona kabisa. Huoni kwamba kama huna pesa hapa tumekuzika?
Hebu
fikiria zaidi labda umeoa au kuolewa na mweza ambaye hayupo vizuri kifedha,
kila siku ugomvi hauishi ndani ya nyumba kisa pesa, kwanini pesa isiwe chanzo
cha furaha?
Unataka
kuwapeleka wanao shule nzuri na hupendi wapoteze muda wao bure kwenye zile
shule za kina kayumba kwa sababu watamaliza darasa la saba hawajui hata
kiingereza cha kuombea maji, sasa kwanini pesa isiwe mwarobaini wa matatizo
yote duniani?
Jaribu
kuvaa viatu vya ombaomba ambaye hana kabisa mahali pa kulala anazurura tu huko
mjini, hivi kama leo hii nitakupatia milioni 20 ukaweza kwenda kujinunulia
kiwanja cha 20x20 mbagala na bado ukabakiwa na pesa nyingine kwa ajili ya
kusimamisha banda lako la mabati (fullsuit), niambie ubaya wa pesa hapo uko
wapi?
Ni
nani duniani asiyependa starehe? Kutembelea vivutio mbalimbali duniani, miji na
majiji ukila bata na kunywa vizuri, ukinunua nguo kali pamoja na magari ya
kifahari ya bei mbaya. Vitu vyote hivu huwezi kuvipata ikiwa kama mfukoni huna
pesa.
Kwahiyo
tusifanye mchezo jamani na pesa kwani hakuna tatizo isilotatua, tunaisingizia
tu bure kuwa ni chanzo cha matatizo kwakuwa hatuna kitu mifukoni.
Mtu wa Pili
Pesa
inao uwezo wa kutatua matatizo ya mtu kwa asilimia 99% hii inamaanisha kwamba
inaweza kukuokolea muda wako kwa asilimia 99 huku ikikuachia asilimia 1% tu ya matatizo
yako uyatatue mwenyewe. Kwa mtindo huo unaweza kuona kwamba unamiliki asilimia
100% ya muda wako kutatua asilimia 1% tu ya matatizo yako. Hii haimaanishi
kwamba pesa imetatua mataizo yako kwa asilimia 100%? kwa sababu pesa imetatua
mataizo yako kwa asilimia 99% na kukufanya mwenyewe utatue asilimia 1%
iliyobakia.
Mtu wa Tatu
Ikiwa
utahitaji chochote kile pesa inaweza kununua, Chakula, malazi, elimu, afya,
usafiri, burudani nk. Na ikiwa utapenda kufanyiwa jambo lolote lile, mara zote
yupo mtu aliyeko tayari kukufanyia kwa bei stahiki. Ukiwa na pesa unaweza kujipatia
huduma ya daraja lolote lile la juu mfano kwenye ndege, gari moshi, Uba,
mwendokasi ama usafiri mwingine wowote ule, wewe utapanda first class kila mara
na siyo daraja la tatu ama la nne. Ikiwa mtu ni mgojwa karibu ya kufa anaweza
akalipia matibabu yeyote yale ya bei ghali kuokoa maisha yake tofauti na
mlalahoi wa kawaida.
Sikatai
kweli kuna mazingira machache sana pesa inaweza isiweze kutoa msaada lakini
tukubali tu ukweli kwamba walio na pesa za kutosha wanaweza kujiandaa vizuri
zaidi kabla majanga hayajawakuta na wanakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa
kukabiliana na madhara yeyote yatokanayo na majanga hayo. Kwa hiyo pesa bwana
inaweza kutatua kila tatizo asikudanganye mtu.
Mtu wa nne
Pesa
ni kila kitu bwana! Ingawa nakubali kwamba pesa ndio chanzo cha maovu makubwa
zaidi Duniani, lakini pia ndiyo chanzo kikuu kabisa cha furaha. Nina uhakika
pesa inaweza ikatatua kitu chochote kigumu katika maisha yangu, hata naweza
nikasema ina uwezo wa kutatua matatizo mengi ya kiakili yanayowakumba watu
wengi siku hizi mfano misongo ya mawazo, upweke na hata kuchanganyikiwa akili
kunakosababishwa na hali ngumu na duni za kimaisha.
Mtu wa Tano
Ndiyo
pesa inaweza kusuluhisha karibu matatizo yote. Katika nyakati za zamani
inawezekana haikuweza kutatua kila tatizo lakini kwa nyakati hizi za sasa pesa
unaweza ukaifananisha na hewa ya Oksijeni au Visa ya kusafiria, huwezi kuishi
bila ya pesa utakufa!
a) Pesa inakupa uhalali wa karibu kila kitu
b) Pesa inakupa nguvu
c)
Pesa
ni kitu kinachoongeza thamani kwenye utu wako
d) Ukiwa na pesa ni sawa na mtu aliyeketi
juu ya gari au baiskeli yenye zile springi za kuzuia mshtuko (Shock absorber)
gari ikiruka juu huwezi kuumia kamwe.
Na
kwa msaada wake unaweza ukatatua kila tatizo linalokuja mbele yako.
Mtu wa sita
Ndiyo
pesa inaweza kutatua matatizo yote. Watu wanaweza wakasema kwamba pesa inaweza
tu kutatua matatizo kama ya ulipaji wa madeni mbalimbali na kodi za serikali,
lakini pia hata unapokuja upande wa suala la mahusiano kwa kutumia pesa mtu
unaweza ukanunua urafiki na mapenzi kisha baada ya muda kupita hautaendelea
tena kulipa kwakuwa rafiki au mpezi anakuwa keshakuzoea tayari na mmekuwa
pengine mke na mume. Pasipo pesa pengine isingeliwezekana kabisa kumpata.
Pesa
inatatua kila kitu sema tu tatizo ni watu kushindwa kupata pesa za kutosha
kutatulia matatizo yao ndio maana wanatafuta sababu zisizokuwa na mashiko.
Binti mdogo mrembo hata wa miaka 17 atakubali kuolewa na mzee wa miaka 70 huku
wakiitana baby baby, lakini je, ikiwa mzee wa miaka hiyo asiyekuwa na kitu
kabisa kweli si hata wanawake wa umri wake watamkimbia? Tuache masikhara bwana
pesa inatisha!
2.
Upande wa hapana, Pesa ndiyo chanzo cha matatizo yote duniani:
Mtu wa kwanza
Pesa
ni ibilisi na chanzo cha kila aina ya uovu hapa duniani, ninachokubali tu ni
kweli pesa inaweza kukusaidia kulipia baadhi ya vitu fulanifulani lakini
linapokuja suala zima la mahusiano pesa imefeli kabisa, Unaweza kutumia pesa
kumnunua mpenzi na marafiki lakini hebu niambie mpaka lini utaendelea kuwalipa?
Mapenzi ya kweli kamwe hayawezi kudumishwa na pesa na ingelikuwa ni hivyo basi
Bill Gates Bilionea aliyewahi kushika namba moja kwa utajiri Duniani
asingetalikiana na mkewe na wakaachana mazima kila mtu na hamsini zake.
Mtu wa Pili
Wewe
unasema Bill Gates? Mbona huyo ni chamtoto tu, Bilionea namba moja (1) duniani
anayeongoza sasa hivi kwa utajiri mkubwa Bwana Elon Musk anaishi ubachela huu
mwaka wa 5 sasa hana mkemaalumu baada ya kuachana na mkewe na isitoshe si mke
mmoja keshataliki zaidi ya wake watatu katika nyakati tofauti, hivi kweli
mnaosema pesa ni kila kitu kwanini tusiwapeleke mirembe mkapimwe? Pesa itanunua
kila kitu lakini haiwezi kabisa kununua furaha, mapenzi wala urafiki. Pesa haiwezi kutatua matatizo yote bali inaweza tu kutatua baadhi ya matatizo.
Mtu wa Tatu
Pesa
hutengeneza tu njozi za furaha lakini siyo furaha halisi, waliojaliwa kuwa na
pesa nyingi wanaweza tu kurahisisha maisha yao lakini pia hilo linaweza
kusababisha mataizo. Watu walio na furaha zaidi maishani hudai kwamba chanzo
cha furaha yao ukweli kimetokana zaidi na maswala ya kiroho, mahusiano imara,
kuweza kukabiliana na matatizo, kitendo cha kuwasaida binadamu wengine waliokuwa
na matatizo mablimbali pamoja na kujitoa nje ya ukanda wao wa faraja (step out
of their comfort zone)
Kuwa
na fedha nyingi sana hutengeneza tu njozi za furaha, na kama tujuavyo sote watu
wanaoishi kwa njozi ni hatari sana kwani wanahisi muda wote wao ni wakamilifu
wasiokuwa na makosa.
Mtu wa Nne
Pesa
siyo majibu ya kila kitu tunachohitaji katika jamii zetu, kwa mfano ukiangalia
miji mikubwa na tajiri duniani kama vile New York, London na Shangai kuna
kiwango kikubwa sana cha uhalifu, wakati katika miji yetu masikini mfano
Zanzibar, Dodoma, Bujumbura, Nairobi na Kampala jamii zimetulia na huwezi
kusikia matukio makubwa makubwa sana ya uhalifu na mauaji ya kutisha, watu wana
furaha pasipokuwa hata na pesa nyingi na wanafanya mambo ambayo watu matajiri
wasingeliweza kuwa na wazo la kuyafanya, mambo hayo ni mazuri kwasababu
wanayafanya kwa ushirikiano kama binadamu wa kawaida. Kama nilivyotangulia
kusema pesa siyo jibu la kila kitu maishani.
Mtu wa Tano
Pesa
ingelikuwa na uwezo wa kuleta furaha maishani Mastaa na watu mashuhuri duniani
wasingejiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya, pombe na bangi. Kwa kutumia
vitu hivyo wangali na pesa nyingi ni ishara tosha kwamba kuna kitu fulani
wanachokikosa katika maisha yao licha ya pesa nyingi wanazozimiliki, hivyo
wanajaribu kukitafuta kitu hicho kwenye hivyo vilevi. Kitu hicho si kingine
bali ni Furaha.
Mtu wa Sita
Kwa
kukazia tu msumari uliogongelewa na msemaji aliyetangulia kusema, ngoja
niwataje kabisa live watu mashuhuri waliokuwa na pesa zao hapa Bongo na nje ya
bongo lakini waliishia maisha ya kusikitisha. Michael Jackson alikufa mpweke
licha ya utajiri wote aliokuwa nao, watu tulitazamia labda kando ya kitanda
chake pangelikaa mkewe na watoto wake wawili wakati akikata roho lakini haikuwa
hivyo, niambieni huo uzuri wa pesa hapa uko wapi?. Mwimbaji mwingine mashuhuri
Whitney Houston na mwanaye wote waliishia vifo vya kusikitisha baada ya
matumizi yaliyokithiri ya mihadarati, niambie walikosa kitu gani? Mastaa wa
hapa bongo kwa leo nawaweka kiporo lakini wapo pia ambao pesa haikuweza
kuwasaidia kwa lolote.
Je, mpenzi msomaji na wewe
una maoni gani? Tafadhali usiache kutushirikisha tuongeze hapo walipoishia
wengine lakini pia kura yako ni muhimu ili tuweze kujua sote kwa pamoja ni
upande upi utakaoshinda mjadala huu.
Asante sana
Peter
Augustino Tarimo
0765553030
Tafadhali piga kura yako hapo chini;
SOMA NA HIZI HAPA;
1. Unahitaji kupata pesa kiasi gani kwa siku ili uweze kuwa na furaha maishani?
2. Saikolojia ya pesa na kanuni 10 za kufuata ili uwe mtu uliyefanikiwa kimaisha
3. Biashara 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala
4. Njia 6 za kuondoa woga na stress za pesa katika maishayako
5. Je, ipo kanuni ya mafanikio ya kifedha? Mtazamo wakisaikolojia
0 Response to "JE, PESA INAWEZA KUTATUA KILA TATIZO DUNIANI AU NDIO CHANZO CHA MATATIZO YOTE?"
Post a Comment