Makala hii ni majibu kwa mdau wetu mmoja kwenye Group la Michanganuo-online
aliyetaka kujua mbinu za kutumia kuweza kusimamia mpango kazi. Aliuliza kama
ifuatavyo;
Habari
za leo; Naomba mbinu za kutumia kusimamia mipango ya kazi
Majibu:
Maneno Mpango kazi, mpango mkakati, Malengo yana maana inayokaribiana
sana na Mpango wa biashara au Mchanganuo wa biashara. Kwahiyo swali hili
nitaenda kulijibu nikitumia muktadha wa mpango wa biashara kama ulivyoelezwa
katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI.
Mpango kazi au Mpango mkakati ni sawa na ramani ya
kuyafikia malengo fulani mtu au taasisi iliyojiwekea. Na malengo yenyewe
yanaweza yakawa ni malengo ya kiuchumi, malengo ya kielimu, malengo ya kiafya
au malengo mengine yeyote yale maishani.
Siri ya Utelekezaji na usimamizi mzuri wa mpango mkakati
wako utategemea vigezo muhimu vifuatavyo, lakini kabla sijavitaja vigezo hivyo
kumbuka kwamba mpango kazi/mapango mkakati unaweza ukatekelezwa na mtu binafsi
au taasisi, inawezekana ikawa ni shirika, kampuni, shule, hospital ink.
Vilevile kabla ya kutekeleza mpango kazi wowote ule ni
lazima kwanza ukae chini na kuanisha ni kazi zipi ama mikakati gani hiyo
inayopaswa kutekelezwa. Hpa ndipo utakuta watu wengi wakiweka malengo kadha wa
kadha mfano, nataka kumiliki kiasi fulani cha fedha mwaka huu, nakata kuwa na
gari, nataka nihitimu ngazi fulani ya masomo kielimu nk. na nitatumia mbinu hii
na hii na hii kuweza kutekeleza malengo husika. Ngoma sasa inabakia
kwenyeutekelezaji wenyewe ambao ndio tunaouangazia hapa leo.
Watu wengi wanayo mipango mikakati ya hali ya juu sana
lakini shida moja tu inakuwa ni kwenye utekelezaji au inatekelezwa kwa makosa.
Jinsi
ya kutekeleza Mpango kazi/Mpango mkakati
1. Tenga
rasilimali za kutosha
Usimamizi na utekelezaji wa mipango unahitaji rasilimali watu,
muda na fedha. Kumbuka kwamba kitu cha msingi zaidi kwenye mpango wowote ule ni utekelezaji wake na siyo kitu kingine
chochote kile, hivyo utekelezaji ni lazima uhusishe mtu/watu iwe ni wewe
binafsi au timu uliyo nayo katika taasisi yako. Katika kutekeleza mpango ni lazima
kuwe na mtu maalumu atakayefanya kazi fulani, muda utakaohusika na bajeti
itakayotumika.
Nitatolea mfano wa mpango kazi mmoja, tuseme labda una
duka lako la rejareja na umeamua kumuweka kijana pale kama mfanyakazi wa
kukuuzia duka lako kwa malengo ya kupata faida na muda wa kufanya mambo yako
mengine. Ni lazima kijana huyo umpatie sappoti ya kutosha ikiwa ni pamoja na
bajeti au chochote kile kitakachohitajika kusudi malengo yaweze kutimizika kama
ulivyoyapanga.
Ikiwa utekelezaji wa mpango kazi unaufanya wewe mwenyewe
pia hakikisha unajitengea rasilimali za kutosha na hasahasa muda kila siku ili
kutimiza malengo yako uliyojiwekea na isijekuwa unatekeleza leo, mara kesho
umeacha, keshokutwa tena umerudia, mtondogoo umeacha, mpango mkakati wako
hautaweza kuleta mafanikio uliyokusudia kwa mtindo kama huo. Hivyo ratiba ni
muhimu sana na ni muhimu zaidi kuifuata.
2.
Tenga muda wa kufanya Tathmini/Marejeo
Tathmini ya mara kwa mara ni muhimu katika utekelezaji wa
mpango mkakati wowote ule wenye mafanikio. Unaweza kupima maendeleo ya
utekelezaji wako kwa siku, kwa mwezi au muda mwingine wowote ule uliojiamulia
ila inapendekezwa muda usiwe mrefu sana kwani utapoteza malengo yako.
Bado nitatolea mfano wa mpango mkakati kwenye duka la
rejareja ambalo umemuweka kijana pale wa kukuuzia. Ni lazima utenge muda
maalumu kila siku au muda utakaoupanga wewe ambapo utakuwa ukifika pale dukani
na kufanya tathmini pamoja na kijana wako, hii ni muhimu sana kwani itamfanya
kijana kwanza azingatie kwamba anawajibika kuhakikisha kila kitu kinakwenda
sawa kama mlivyokubaliana kuliko tu kuacha mambo yende holela. Atafikiri lile
ni shamba la bibi na anaweza kufanya
chochote apendacho kwani hakuna njia mahsusi ya kumuwajibisha.
3.
Weka vipimo
Mpango kazi wako ni lazima uweke vipimo/kipimo
kinachoonyesha kiasi cha utekelezaji / utendaji kwa kila lengo, kipimo kwa kila
mfanyakazi, kwa kila idara na hata kwa biashara nzima kwa ujumla wake. Tukirudi
tena katika mfano wa mpango kazi wetu niliochagua wa duka la rejareja,
unapofanya marejeo au tathmini na kijana wako wa kazi, hakikisha kuna vitu
unavyovipima kujua maendeleo ya duka lako na vitu hivyo vywaweza kuwa ni mauzo,
faida, ununuzi wa bidhaa, stoku ya bidhaa nk.
Ikiwa vipimo vitaonyesha hakuna maendeleo yeyote au kuna kasoro za hapa na pale na kwa kipindi kirefu mfululizo, basin ujue mpango mkakati wako una mushkeli mahali, ni wakati sahihi sasa wa kubadlisha mikakati uliyojiwekea au hata kuachana kabisa na biashara yenyewe kwani huwezi kufanya biashara isiyokuwa na faida wala maendeleo ya maana.
Vilevile Ikiwa hakuna vipimo vyovyote unavyoweza kuvitegemea basi ujue kabisa hapo unatwanga maji kwenye kinu au unatekeleza mpango kazi usiokuwa na matokeo chanya. Kumbuka ya kwamba duniani kila jambo linaloweza kutekelezwa basi ujue pia jambo hilo linaweza kupimwa na ukiwa hautakuwa na vipimo sahihi basi hakuna kinachofanyika cha maana.
Vipimo si kwa mfanyakazi tu uliyemwajri hapana bali hata
ikiwa ni wewe mwenyewe unayetekeleza mpango mkakati wako binafsi ni lazima
ujiwekee vipimo na tathmini ya mara kwa mara kuangalia pale unapokwama au
kufanya vizuri ni wapi.
4.
Utayari wa Kubadilika muda wowote
Hakuna mpango wowote ule Duniani unaoweza kwenda sawasawa
kwa asilimia 100% na hali halisi inavyokuja kujitokeza wakati wa utekelezaji
hata iwe ni ile mipango inayowekwa na Bunge la Congress kule Marekani. Huwa
tunatengeneza mipango mikakati mablimbali kila siku na hata Serikali yetu
Tukufu kila mwaka Wabunge hukaa kule Dodoma wakitengeneza mipango ya bajeti.
Lakini kwenye utekelezaji wake mbele ya safari kunaweza kuwa na mabadiliko fulani
na hilo haliepukiki.
Ikiwa mazingira hayaendani na vile ulivyopanga basi
unaweza kubadilisha mikakati yako kulingana na mazingira yaliyopo ilimradi tu
hupotezi lengo lako la msingi. Kumbuka Mpango kazi / Mpango mkakati ni andiko
linaloishi, siyo jiwe ndio useme labda halitabadilika kamwe.
Natumaini
ndugu yangu Simon na mdau katika MASTERMIND GRROUP LA MICHANGANUO-ONLINE utakuwa
umepata mawili matatu kutokana na majibu yangu. Asante sana
Peter Tarimo
Mobezi katika kuandaa Michanganuo ya Biashara za aina
zote.
SOMA PIA:
1. Jinsi mpango wa Biashara unavyoweza kuongeza mafanikio ya biashara yako
2. Nna mtaji wa shilingi milionio moja (1000,000) naomba ushauri nifanye biashara gani?
3. Chakula cha kuku wa kienyeji kina tofauti yeyote na cha kuku wa kisasa?
5. Biashara 5 za mtaji kidogo kuanzia elfu 2, kumi mpaka laki moja unazoweza kuanza zikakutoa
0 Response to "NJIA ZA KUSIMAMIA NA KUTEKELEZA MPANGO KAZI / MPANGO MKATATI"
Post a Comment