Kwenye group la masomo ya kila siku yenye maudhui ya pesa
na michanganuo ya biashara kuna mdau mmoja ameuliza swali kuhusiana na biashara
ya rejareja akaomba samahani akijua alikuwa nje ya maa lakini kumbe yupo sahihi
kwani tunakaribisha swali lolote lile ilimradi tu lihusu Biashara, ujasiriamali
au Michanganuo ya biashara yeyote
Aliuliza kama ifuatavyo bila kupunguza wala kuongeza
chochote;
Habari boss
Samahani
kiongozi
Naomba
kuuliza swali ambalo lipo nje ya mada
Naomba
kujua uliweza vipi kufanikiwa katika uuzaji wa vinywaji baridi?
Maana
kwa ninavyofahamu mim hii biashara faida yake ni ndogo sana
Faida
yake ni kuanzia elfu moja mpaka elfu mbili kwa kreti zima la soda
Ulifanikiwa
vipi katika hali hii??
MAJIBU:
Bila samahani na swali lako wala halipo nje ya mada hata
kidogo maanake humu kwenye group la Michanganuo-Online mtu unaweza ukauliza
swali lolote lile juu ya michanganuo ya biashara, Ujasiriamali na Biashara za
rejareja kwa ujumla wake
Tukirudi
kwenye swali lako ni hivi;
Kwa upande wangu binafsi, nadhani wewe ni mmoja kati ya
watu waliowahi kusoma kitabu changu kiitwacho MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA, kitabu chenye kila kitu
mjasiriamali wa biashara yeyote ile ya rejareja na siyo duka tu anachopaswa
kujua ili biashara yake iweze kupata mafanikio
Ni ukweli binafsi mimi nimefanya biashara ya duka la
rejareja kwa muda wa miaka 12 na hunidanganyi chochote kuihusu hii biashara. Nimeuza
vinywaji vya baridi hususani soda, maji na juisi lakini pia nimeuza bidhaa
nyingine mbalimbali za dukani kama vile mchele, unga wa sembe/dona, sukari,
chumvi, viberiti, sindano, uzi, mshumaa, mafuta ya taa, pini na orodha ni ndeee......fu,
siwezi nikavitaja vyote hapa patajaa sijamaliza.
Kuna vigezo vingi huamua faida katika biashara ya duka au
tuseme biashara za rejareja kwa ujumla, mtaji wa biashara ya vinywaji, eneo la
biashara, aina ya wateja watakaonunua kwako nk. Aina za biashara ndogondogo
nyingi zina tabia hii ya kuathiriwa na vigezo hivyo nilivyovitaja.
Kama ulivyosema mwenyewe faida katika vinywaji baridi kwa
rejareja siyo kubwa kivile na siyo kwenye vinywaji tu peke yake bali ni katika
karibu kila bidhaa ya rejareja faida siyo kubwa sana. Kwa uzoefu wangu vitu
vingi vya rejareja unaweza kupata faida kuanzia asilimia 5% mpaka 35% hivi ya
mauzo.
Hii inamaanisha kwamba kwa mfano ukiuza bidhaa ya
shilingi 100 basi utapata faida kati ya shilingi 5 mpaka shilingi 35 na si
zaidi sana ya hapo. Tuchukulie mfano wa soda, kwa soda zinazouzwa shilingi 600
rejareja kreti yake duka la jumla inauzwa shilingi 12,000/= hivyo ni sawa na
kusema jumla soda moja umenunua shilingi 500/= faida kwa chupani sh. 100/=
Ili uweze kujua ni asilimia ngapi ya mauzo chukua faida
igawe kwa bei ya kuuzia = 100/600 kisha jibu zidisha kwa 100 = asilimia 16.6% Ungepata
jibu hilohilo kama ukichukua jumla ya faida ya soda zote kisha ugawe kwa jumla
ya mauzo ya soda kreti lote; 2,400/16,800 x 100 = 16.6%
Kwa soda zinazouzwa shilingi 700 kreti lake jumla
utanunua sh. 13,500/= sawa na soda moja sh. 562.5/= Faida kwa soda moja ni sh.
137.5/= Kujua ni asilimia ngapi ya mauzo chukua faida gawa kwa bei ya kuuza
kisha zidisha mara 100 = 137.5/700 x 100 = 19.64% Pia nayo ukitumia jumla ya
faida ya kreti zima ukagawa kwa jumla ya
mauzo ya kreti zima x 100 unapata asilimia hiyohiyo 19.64%
Kwa hiyo unaweza kuona kwamba hizi asilimia 16.6% na
19.64% zipo katika ile ‘range’
tuliyosema ya asilimia 5% mpaka 35%
Ni kanuni inayofanya kazi kwa biashara za rejareja Duniani
kote na si hapa Tanzania tu. Hata ukienda Marekani sijui china ni hivyohivyo.
SIRI
YA KUFANIKIWA BIASHARA YA KUUZA VINYWAJI BARIDI VYENYE FAIDA NDOGONDOGO
Sasa basi kama hivyo ndivyo unawezaje kufanikiwa ama
kupata faida kubwa kwenye biashara hii ya vivyaji baridi rejareja?
1.
Kuuza kwa wingi (Mass selling)
Haiwezekani uone mafanikio kwa kuuza rejareja soda tu
peke yake mahali pasipokuwa na bidhaa nyingine yeyote ile labda iwe pale mahali
unapouzia basi soda zinatoka kwa wingi sana pengine unauza hata kreti 10 mpaka
15 kwa siku.
Naweza kukuambia kwamba mimi binafsi wakati nafungua
biashara yangu ya rejareja kwa mara ya kwanza kabisa pale maeneo ya Msimbazi
Karikakoo kipindi hicho mtu ukiwa na eneo pale ulikuwa na uwezo wa kuishi kwa
kuuza soda tu peke yake bila ya kuuza kitu kingine chochote kile kutokana na
wingi wa watu katika eneo lile na kumbuka kama nilivyoeleza na picha nikaweka
kwenye kitabu hicho uliona nilivyoanza na friji moja tu la kampuni ya Pepsi na
kikabati kidogo cha kioo tena nje bila hata fremu lakini uliona nini baada ya
mwaka mmoja?
Naomba nikuulize tena, kwanza unajua nini kuhusiana na
biashara za rejareja? Kama ulisoma vizuri kitabu changu hicho utakumbuka pale
mwanzoni kabisa nilizungumzia aina za biashara za rejareja nikataja kuanzia Kioski
mpaka Supermarket na Hypermarkets ambazo ndiyo ngazi ya juu kabisa ya biashara
hizi za rejareja duniani.
Sasa hebu tazama soda na maji huuzwa mpaka kwenye Masupermarket
na hayo Mahypermarkets, mbona usiwasikie wakisema kwavile soda na maji vina
faida kidogo basi wanaachana navyo wauze tu vitu vyenye faida kubwa? Wewe unazungumzia soda yenye faida
karibia asilimia 20%, kuna vocha faida haifiki hata asilimia 3% na bado watu
wanauza na tena wengine hata hutegemea mauzo ya vocha peke yake bila ya vitu
vingine kuishi mjini. Siri pekee hapa ni maajabu ya kuuza vitu kwa wingi (Mass sales) Kumbuka vinywaji baridi ni
bidhaa mtu anaweza kunywa kila siku hivyo wasiwasi wa kudoda ni mdogo sana
ikiwa eneo (location) lina watu wa
kutosha
2.
Mchanganyiko wa Bidhaa mbalimbali (Diversity)
Watu hawategemei faida kwenye bidhaa moja tu ya rejareja
mfano soda au maji, katika duka zima au kioski chako au supermarket yako au
hata genge lako, hutauza bidhaa moja tu hapana. Kama mimi nilivyofanya kwenye
kikabati changu siku ya kwanza kabisa pale mtaa wa Msimbazi Kariakoo, ukitazama
vizuri utaona mle ndani ya kikabati kulikuwa na boksi la Panadol, Hedex, mifuko
ya keki na Clips za viazi. Sikutegemea faida ya zile soda kwenye friji la Pepsi
tu peke yake. Faida kidogokidogo kutoka katika bidhaa zote nilizoziweka
hatimaye iliweza kunifanya nione faida niliyokuwa nikiipata ni kubwa.
HITIMISHO
Kwahiyo ndugu yangu Yassin biashara ya kuuza rejareja
vinywaji baridi vyenye faida ndogondogo siri yake kubwa ili ufanikiwe kuiona
faida kubwa ni kuhakikisha unatekeleza mikakati hiyo miwili niliyoitaja hapo
juu, wapo watu wametajirika kwa biashara hizihizi na wengine kupata mitaji
mikubwa ya kuanzisha biashara nyingine za mamilioni ya pesa kupitia kwanza
kuuza vinywaji baridi kwa rejareja.
Naamini majibu yangu yanaweza kuwa na msaada kwako.
ASANTE SANA,
PETER TARIMO
SOMA NA HIZI HAPA:
1. Jinsi ya kujua faida ya duka la rejareja kila sikujioni unapofunga hesabu
2. Mtaji wa biashara ya duka la rejareja: Nianze nashilingi ngapi ili nifanikiwe?
4. Mchanganuo wa biashara ya genge la kisasa la matunda,mbogamboga na vyakula
0 Response to "SIRI YA KUFANIKIWA BIASHARA YA KUUZA VINYWAJI BARIDI VYENYE FAIDA NDOGONDOGO"
Post a Comment